mwanamwana
JF-Expert Member
- Aug 1, 2011
- 1,410
- 4,988
BODI YA ITHIBATI YA WAANDISHI WAHABARI UFAFANUZI KUHUSU WANAODAIWA KUWA WAANDISHI WAHABARI KUSHIKILIWA NAJESHI LAPOLISI MKOANIARUSHA
Dar es Salaam
12 Septemba, 2025
Kwa mujibu wa Kifungu cha 13(a) cha Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229, Bodi ina wajibu wa kutoa ithibati na vitambulisho kwa waandishi wa habari waliokidhi vigezo, pamoja na kusimamia uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya uandishi wa habari hapa nchini.
Aidha, katika kutekeleza majukumu yake, Bodi imebaini kuwepo kwa taarifa zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, zikidai kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu wawili wanaodaiwa kuwa waandishi wa habari kwa tuhuma za kuendesha televisheni za mtandaoni (Online TV) zisizosajiliwa kisheria.
Bodi inapenda kufafanua bayana kuwa watu waliotajwa kwa majina ya Ezekiel Mollel (Manara TV) na Baraka Lucas (Jambo TV) SIO waandishi wa habari kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229. Kifungu cha 19(1) cha Sheria hiyo kinaeleza wazi kuwa “mtu hataruhusiwa kufanya kazi za uandishi wa habari isipokuwa mtu huyo awe amethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.
Aidha, rekodi za Bodi zinaonyesha kuwa watu hao hawajawahi kujisajili katika mfumo rasmi wa usajili wa waandishi wa habari ujulikanao kama TAI HABARI kwa lengo la kuomba ithibati na kupata Vitambulisho vya Uandishi wa Habari (Press Cards) vinavyotolewa kisheria. Hivyo basi, hawana hadhi ya kisheria ya kutambulika kama waandishi wa habari.
Waandishi wa habari wote waliokidhi vigezo kisheria na kupatiwa ithibati wanaendelea kutambuliwa na kuruhusiwa kutekeleza majukumu yao kwa uhuru na heshima na kuzingatia Sheria. Wale ambao hawajakidhi masharti wanaendelea kuhamasishwa kujiendeleza kielimu ili waweze kushiriki ipasavyo katika taaluma hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Bodi inatoa wito kwa vyombo vya habari na wadau wote wa sekta ya habari kuendelea kushirikiana na Bodi ya Ithibati kuhakikisha kuwa sekta ya habari nchini inasimamiwa kitaaluma, ikizingatia maadili ya taaluma, maslahi mapana ya Taifa, na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi, kwa wakati na kwa uwazi.
Imetolewa na:
Patrick Kipangula Kaimu
Mkurugenzi Mkuu
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB
Patrick Kipangula Kaimu
Mkurugenzi Mkuu
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB