ISIS inavyotesa Wayazidi nchini Iraq

ISIS inavyotesa Wayazidi nchini Iraq

Herbalist Dr MziziMkavu

Platinum Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
43,106
Reaction score
34,926
waasi.jpg

Wapiganaji wa ISIS

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la ISIS wameyafanya maisha ya jamii ya Yazidi kuwa mabaya kwa kuwa wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Irbil, Iraq. Kipi kibaya zaidi: Kuwa mkimbizi au kubaki nchini mwako ufe kwa njaa na kiu?

Ni swali gumu lisilojibika kwa urahisi. Lakini pia ni vigumu kuipata picha halisi ya maisha ya raia wa Iraq wa jamii ya Yazidi ambayo imekuwa ikiyapitia katika kipindi cha wiki mbili baada ya kuwakimbia wapiganaji wa kikundi cha Islamic State of Iraq and Syria ( ISIS).

"Kwa macho yangu nilimshuhudia mbwa akila mzoga wa binadamu," Tariq kutoka jamii ya Kiyazidi alikiambia kituo cha televisheni cha CNN.

Alisema: "Huu siyo mgogoro. Ni maafa."

Inapofika usiku, kwa mbali huona mwanga wa taa kutoka katika mji walioukimbia. Wapo juu ya mlima unaowawezesha kuziona vyema nyumba zao, lakini hali ilivyo hawajui kama wataweza tena kurejea huko.

Mlima ambao wamejifadhi kwa sasa, upo karibu na mpaka wa Syria. Kama isingekuwa machafuko nchini humo, huenda ingekuwa kimbilio la Wairaq hawa lakini usalama sasa ni kubakia hapo walipo.

Wanachemsha chai katika kopo dogo, hivyo inawalazimu kurudia mara nyingi ili walau kila mmoja apate kitu cha moto tumboni.

Jua linapochomoza, sauti za ndege za kivita huunguruma juu ya vichwa vyao. Mawazoni mwao hudhani wakati wowote zitadondosha misaada ya chakula na maji, lakini mwishowe muungurumo huo hupotea na kurudi tena baadaye.

Siyo ndege za misaada kama wanavyodhani, bali zipo katika doria ya kulinda mali za wawekezaji katika miji mbalimbali nchini humo.

Inaelezwa kuwa ndege hizo ni za ulinzi wa mji wa Irbil ambao una miradi mingi ya wawekezaji kutoka nchi za Magharibi pamoja na hoteli za kifahari.

Katika mazingira ya nyuzi joto 45.7, wengi wameanza kuchoshwa na njaa na maji ya kunywa yamewaishia.

Maji pekee yanayopatikana ni ya mabaki yaliyonywewa na mbuzi na kondoo pia hayatoshelezi familia zilizokimbilia katika eneo hilo.

"Tatizo kubwa hapa ni ugonjwa wa kuhara hasa kwa watoto," anasema Dk Hussein Margat aliyekimbia na wakazi hao baada ya ISIS kuvamia mji wao siku kumi zilizopita.

"Hatuna tofauti na wanyama; tunalazimika kutafuna nyama mbichi," anasema Thasen Khalen mmoja wa watu waliokimbilia mlimani.

Maumivu ya jamii hiyo ya Yazidi yalianza Agosti 4 baada ya wapiganaji wa kikundi cha ISIS kuvamia mji wao wa Sinjar.

Alichokiona Khero Gaffal (44) ni kundi kubwa la wanaume wakiwa na silaha mbalimbali wakivamia mji wao.

Anasema wengi walikimbilia mlimani, lakini kundi hilo lilifanikiwa kuwakamata wanaume zaidi ya 60 kisha waliwapanga katika mstari mmoja na kuwaua wote kwa risasi.

"Walichimba shimo kubwa na kuwafukia wote nikishuhudia," anasema Gaffal huku akibubujikwa na machozi.

Baadhi ya miji watu wake wamekimbia kabisa na nyumba zimebaki tupu, wachache wamefanikiwa kufika mlimani kwani wengi wameuawa au kutekwa na wapiganaji hao.

Watu wengi wa jamii ya Yazidi ni maskini na wanasumbuliwa na ugonjwa wa kifua kikuu. Madaktari wanasema hivi sasa wengi wameanza kuonyesha dalili za ugonjwa huo kutokana na uchovu na njaa.

‘Hatukuwa na kitu'

Maisha yaliyojaa dhiki kwa Tariq (33) yalianza Agosti 3 baada ya kupigiwa simu na rafiki zake waliopo vijiji vya jirani wakimwambia "Daish" neno ambalo kwa lugha ya kwao tafsiri yake ni kwamba wapiganaji wa ISIS walikuwa njiani kuelekea katika mji wao.

Taarifa ziliendelea kumiminika kutoka kila kona ili kuweza kujinusuru na wapiganaji hao.

Chaguo lilikuwa ni lake, abaki abadili dini na kuwa mmoja wa wapiganaji, abaki auawe iwapo atakaidi matakwa yao au akimbie.

Tariq na familia nyingine za watu wasiopungua 300 walichagua kukimbia kabla ‘jamaa' hawajaingia katika mji wao.

"Tulikimbia, njiani lita moja na nusu ya maji ilinywewa na watu 15, kila mmoja alikunywa funda moja na kumpa mwenzake, hatukuwa na kitu zaidi ya nguo tulizovaa," anasema Tariq.

Baba yake mwenye umri wa miaka 80 alikufa siku mbili baada ya kukimbia nyumbani kwao. Joto na njaa vilichukua uhai wa mzee huyo.

Hakuwa peke yake. Tariq anasema alihesabu maiti kati ya 500 na 1,000 ambazo nyingine ziligeuka chakula cha mbwa.

"Kuna zaidi ya familia 20,000 zimekwama milimani, kama hawatapelekewa chakula na maji kwa wakati, watafariki dunia wote, " anasema Tariq.

Wanga'ang'ania katika helkopta

Mtangazaji wa CNN, Ivan Watson anasema picha aliyoishuhudia katika mlima huo ni ya kutisha kwani kila helkopta inapokaribia kushusha msaada wa chakula na maji, watu zaidi ya 5,000 hukusanyika wote wakitaka kupanda ili waokolewe.

Anasema kwa nguvu zao itachukua mwaka mmoja na nusu kuweza kuwaondoa watu wote katika milima hiyo kwa kuwa kila tripu moja inaweza kubeba watu 20 tu.

"Kila helkopta inapokaribia kutua watu huvamia, wanawake wanawatupa ndani ya helkopta watoto wao wakitaka wawe salama, hakuna anayetaka kubaki kila mtu anataka kuwa wa kwanza kuondoka," anasema Watson. Anasimulia kuwa mwanamume mmoja alidandia katika bawa la helkopta, lakini kadri ilivyozidi kwenda juu alichoka na kuachia…alidondoka na kufa wakimshuhudia.

ISIS ni nani

Ni kundi la kigaidi ambalo inadaiwa limechipua kutoka katika lile la Al Qaeda. Lilianza kushamiri katikati ya mwaka jana.

Hata hivyo kiongozi wa kundi hilo, Abu Bakr al- Baghdad anakanusha kundi hilo kuwa na uhusiano na Al Qaeda.

Kiongozi huyo ambaye alikuwa mstari wa mbele katika vikundi vya waasi tangu nchi hiyo ilipovamiwa na Marekani mwaka 2003, anasema hakuna uhusiano wowote kati yao.

Baghdad anaaminika kuwa imara katika mapigano na kwamba kundi lake sasa hivi limevutia vijana wengi katika matukio ya kujitoa mhanga tofauti na Al Qaeda. ISIS inaendesha shughuli zake katika nchi za Iraq na Syria.

Inaelezwa kuwa kundi hilo linasaidiwa na matajiri kutoka Kuwait, Syria na Iraq. Mpaka Juni mwaka huu kundi hilo lilidaiwa kuwa na pesa taslimu Dola 900 milioni za Marekani.

Source
:Mwananchi

http://www.mwananchi.co.tz/habari/habari-ya-ndani/-/1724700/2418898/-/item/0/-/1lgi6gz/-/index.html
 
Back
Top Bottom