IPTL kwanini mnatutesa hivi Watanzania tunabaki tunadondoka Machozi ?

saggy

Senior Member
Nov 12, 2008
153
70
WAZIRI wa Fedha, Mustafa Mkulo, amelishambulia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kwa kuendelea kuchukua fedha za Serikali zitokanazo na kodi ya wananchi kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya mitambo ya kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) bila dalili yoyote ya kurudisha fedha hizo.

Hata hivyo, shirika hilo limesema tayari Serikali imetoa fedha za kununulia mafuta ya mitambo hiyo ya IPTL na hadi juzi jioni, mitambo hiyo ilifikia uzalishaji wa megawati 30 kutoka 10 baada ya mafuta hayo kuanza kutumika.

Akizungumza na HABARILEO kwa njia ya simu jana kuhusu fedha za kununulia mafuta hayo, Mkulo alisema, hafahamu chochote kuhusu mchakato wa kutolewa fedha hizo kwa kuwa yupo Dodoma.

Amesema, jambo la msingi linalotakiwa ni kwa Tanesco kuhojiwa kwanza namna ambavyo imetumia Sh bilioni 17 ambazo hadi sasa imepewa na Serikali kwa ajili ya kununulia mafuta ya mitambo hiyo na kiasi cha fedha walizoingiza.

“Mimi naomba mnisaidie, kwani Tanesco ni shirika linalofanya biashara au la nini? Serikali imekuwa ikilipa fedha ambazo ni za walipa kodi kwa ajili ya hiyo mitambo lakini hawaelezi zimetumika vipi na kama zitarudishwa au la,” alisema Mkulo.

Alisema fedha zinazotumika kununulia mafuta hayo ni za walipa kodi, hivyo haiwezi kuingia akilini fedha zao kutolewa kwa Tanesco bila kurudishwa wakati shirika hilo linajiendesha kibiashara, hali ambayo aliiita kuwa ni sawa na kuwabebesha mzigo wananchi.

“Je wameshaulizwa namna walivyotumia fedha hizo kuzalisha umeme? Kiasi gani wameuza? Fedha walizouzia umeme ziko wapi na kwa nini hazitumiki kununulia mafuta mpaka Serikali itoe tena fedha?” alihoji na kuongeza kuwa si jambo jema kuwaongeza mzigo wananchi kwa kunufaisha wengine.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando, alisema utaratibu unaotumika kuchukua fedha za Serikali kununulia mafuta, ni kwa njia ya ankara ya kudai malipo kutoka IPTL kwenda serikalini.

Amesema, baada ya hapo, kila mwisho wa mwezi IPTL huwajibika kupeleka ripoti Wizara ya Nishati na Madini ya jinsi mafuta yalivyotumika.

Kuhusu kurudisha hizo za fedha za mafuta ya IPTL serikalini, Mhando aliweka wazi kuwa suala hilo halitawezekana kutokana na ukweli kuwa shirika linajiendesha kwa hasara na linatumia gharama kubwa katika uendeshaji na kuingiza fedha kidogo.

“Kwa mfano tu, IPTL wao wanazalisha na kuuza umeme kwa senti 32 za Marekani kwa uniti moja, wakati sisi tunazalisha na kuuza kwa senti nane za Marekani, kwa kweli tunajiendesha kwa hasara, hatuwezi kulipa hizo fedha,” alisema.

Akizungumzia kuwashwa kwa mitambo hiyo ikiwa ni kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme katika bwawa la Mtera na hivyo kusaidia kupunguza makali ya mgawo wa umeme, alisema tayari fedha zimetolewa na Serikali kwa Wizara ya Nishati na Madini na mafuta yameanza kupakuliwa.

Alisema, kuwashwa kwa mitambo hiyo na kupewa mafuta kutasaidia kupunguza makali ya mgawo wa umeme nchini na megawati hizo zitakuwa zikipanda kulingana na mafuta na idadi ya mitambo itakayowashwa.

“Serikali ilitoa fedha tangu juzi kwa Wizara ya Nishati na Madini ambayo ndio wasimamizi kwa ajili ya kuagiza mafuta ya mtambo wa IPTL, na kwa taarifa nilizonazo tayari mafuta yameanza kupakuliwa na kupelekwa kwenye mitambo,” alisema Mhando.
 
Back
Top Bottom