Ikulu na Utata Mpya wa Mwaliko Arusha!

Buchanan

JF-Expert Member
May 19, 2009
13,199
1,969
  • Ni mkanganyiko wa nne wa kiitifaki unaomhusu JK na mkoa huo!

MKOA wa Arusha umeingia tena katika “mzozo wa kiitifaki” baada ya mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mary Kisaka, kualikwa kimakosa kuhudhuria hafla ya kitaifa ya maadhimisho ya miaka 46 ya Muungano iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, jioni ya Aprili 26, mwaka huu.

Mary Kisaka anayekabiliwa na tuhuma kimaadili alialikwa badala ya Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda.

Arusha imekuwa ikiingia matatani katika suala la mawasiliano kati ya Mkoa huo na ofisi za juu nchini. Mkoa huo uliingia matatani miezi kadhaa iliyopita pale ulipomtuma Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Loliondo kwenda Ikulu, Dar es Salaam kukabidhiwa gari la wagonjwa na Rais Jakaya Kikwete, badala ya Halmashauri ya Wilaya ya Longido.

Kisaka, ambaye alikuwa diwani wa viti maalumu kupitia CCM katika Manispaa ya Arusha, anatuhumiwa kuhusika na uuzaji wa kiwanja cha wazi kilichopo jirani na soko la Kilombero la mjini Arusha mwishoni mwa mwaka 2005 na alivuliwa wadhifa wake mwaka 2006 baada ya kamati iliyoundwa kuchunguza kashfa hiyo kumwona kuwa ana hatia ya kuhusika na uuzaji wa kiwanja hicho.

Katika kashfa hiyo, ambayo iliutikisa uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha aliyekuwa Meya wa mji wa Arusha, Paul Lotta Laizer, pia alilazimika kujiuzulu na diwani mwingine Musa Mkanga wa Kata Sombetini pia alivuliwa wadhifa wake.

Viongozi hao waliokuwa wakiongoza kamati ya mipango miji walivuliwa nyadhifa zao baada ya kubainika kuwa walihusika kuuza kiwanja hicho cha wazi kwa kampuni ya EMOIL-Marketing ya jijini Dar es Salaam. Serikali ya Mkoa wakati huo ikiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Samwel Ndomba ilizuia ujenzi katika kiwanja hicho.

Baada ya kuvuliwa wadhifa huo, Kisaka alibakia kuwa mwanachama wa kawaida wa CCM hadi alipoibuka wiki iliyopita kwa kupewa mwaliko wa kuhudhuria Sherehe za Muungano katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na baadaye katika dhifa ya Kitaifa iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu akiacha maswali mengi hapa miongoni mwa viongozi na wanachama wa chama hicho kikongwe nchini.

Habari kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya CCM na Serikali mkoani hapa zilieleza kuwa mwaliko huo ambao unadaiwa kutumwa kutoka katika Kamati ya Maadhimisho na Sherehe za Taifa iliyoko ofisi ya Waziri Mkuu, ulikwenda kimakosa kwa Mary Kisaka badala ya kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda.

Habari hizo zilieleza kuwa Kamati ilituma mialiko ya watu watatu kwa Mkoa wa Arusha ambao ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, Onesmo Nangole, Mzee Yona Nko ambaye ni Mwenyekiti mstaafu wa Mkoa na Mary Kisaka ambaye ni mwanachama wa kawaida.

Hata hivyo, Nko hakuhudhuria sherehe hizo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa hakuwa katika hali nzuri kiafya lakini Nangole na Kisaka walisafiri pamoja kwenda Dar es Salaam kwa kutumia ndege ya Shirika la Precision Air Aprili 25 na walilipiwa gharama zote na Serikali.

Imeelezwa kuwa katika mazingira ambayo bado hadi sasa hayajaeleweka, Kisaka alialikwa kama Katibu wa CCM Mkoa Arusha badala ya Katibu aliyepo (Mary Chatanda) hivyo kuzua malalamiko mengi kutoka kwa wanachama kuhusu mwaliko huo ikidaiwa kuwa maofisa husika walichanganya majina yao au walifanya hivyo kwa maelekezo maalumu kutoka kwa viongozi wa juu.

Akizungumzia kitendo hicho, Katibu wa Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, alithibitishia gazeti hili kuwa ni kweli kulitokea dosari katika mialiko iliyotumwa na mwaliko wake kama Katibu wa Mkoa wa Arusha ulitumwa Morogoro kimakosa. Morogoro ndiko kulikokuwa kituo chake cha kazi kabla ya kuhamishiwa Arusha mapema mwaka jana.

“Mimi sifahamu huyo mwingine alialikwa ni nani…..lakini mwaliko wangu ulitoka CCM Makao Makuu na ulitumwa kimakosa Morogoro na wa Katibu wa Morogoro ulitumwa Tabora….na watu wa Morogoro walinipigia simu Aprili 25 nikiwa Dodoma nilikokuwa nahudhuria kikao wakinieleza kuwa nipitie mwaliko wangu pale,” alisema Katibu huyo.

Hata hivyo, wakati Chatanda akieleza kuwa alialikwa na CCM Sherehe za Muungano zilikuwa za kiserikali na habari zaidi zinaeleza kuwa hakuhudhuria sherehe hizo kutokana na kukosa mwaliko rasmi.

Mmoja wa maofisa wa CCM Mkoa wa Arusha alieleza kuwa Katibu Chatanda alijibu kidiplomasia ili kuepusha zaidi fedheha iliyotokana na makosa hayo.

“Namfahamu vizuri Chatanda majibu yake ni ya kidiplomasia na kama kiongozi alitaka kuficha mapungufu yaliyotokea lakini kimsingi hata yeye ameumizwa sana na jambo hilo,” alisema mtoa habari wetu.

Mwanachama huyo aliongeza kuwa kimsingi Kisaka hakustahili kuhudhuria sherehe hizo kwa kuwa bado anakabiliwa na kashfa ya kuhusika na ufisadi uliotokea na bado alikuwa hajasafishwa popote na hadi sasa Manispaa ya Arusha wanadaiwa zaidi ya shilingi bilioni moja na kampuni ya EMOIL-Marketing kutokana na kashfa hiyo ya kiwanja.

“Baada ya kuzuiwa kujenga, EMOIL walifungua kesi mahakamani na kushinda ambapo Manispaa waliamriwa kuilipa kampuni hiyo shilingi milioni 250 na riba ya fedha hizo zimepanda na kufikia bilioni moja na hadi sasa fedha hizo hazijalipwa…..hicho ndicho wanachama wanacholalamikia kuwa inawezekanaje mwanachama ambaye ameitia hasara Manispaa na bado anaandamwa na kashfa hiyo kualikwa kwenda Ikulu wakati kuna wanachama wengi waadilifu na viongozi wao,” alieleza mwanachama huyo.

Kwa upande wake Kisaka alipopigiwa simu na gazeti hili alieleza kuwa hana la kusema na kuwashangaa wanachama wanaomnyooshea kidole kuwa hakustahili kuhudhuria dhifa ya Ikulu.

“Hao wanaolalamika wakueleze wao inawahusu nini”….. Sitaki kuzungumza chochote…wakueleze hao wao wanajua zaidi,” alisema Kisaka na kukata simu.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Nuru Milao alithibitisha kuwa ofisi yake ilipokea mialiko mitatu kutoka ofisi ya Waziri Mkuu na kuwapelekea wahusika lakini hawafahamu chochote kuhusu mialiko yenyewe wakati mialiko hiyo ikiwasilishwa alikuwa nje ya kituo chake cha kazi.

“Ni kweli mialiko ilipita kwetu kama ilivyo kwa sherehe nyingine zote za kitaifa na sisi tuliwafikishia wahusika na hatuhusiki na kingine zaidi, naomba uwasiliane na maofisa wa ofisi ya Waziri Mkuu ambao watakuwa katika nafasi nzuri ya kueleza vigezo wanavyotumia katika kuwaalika watu, ” alisema Milao.

Tukio hilo sasa ni la nne kwa mkoa wa Arusha kuingia katika “mzozo wa kiitifaki”. Katika matukio mengine, Rais Kikwete alialikwa kugawa pikipiki zilizotolewa msaada na wafadhili wa CCM kwa ajili ya shughuli za chama hicho Wilaya ya Arusha mwaka 2008 lakini ikabainika kuwa kati ya wafadhili waliochangia ni mfanyabiashara na mtuhumiwa katika kesi ya fedha za Akaunti ya madeni ya nje EPA, Japhet Lema.

Viongozi hao wa wilaya ya Arusha wanadaiwa kujaribu kumsafisha mtuhumiwa huyo kupitia msaada wa pikipiki hizo kwa kumtumia Rais Jakaya Kikwete kwa kuchomeka jina lake kuwa miongoni mwa wafadhili waliokuwa wapewe vyeti na aonekane pia kuwa ni mmoja wa wafadhili muhimu wa CCM.

Lakini katika hali isiyotarajiwa Rais Kikwete aligoma kugawa pikipiki hizo na kuwaeleza kuwa wazigawe wenyewe kwani wanajua walikozitoa, baadaye viongozi waliohusika walipewa karipio na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho.

Katika tukio la la pili Rais alialikwa kufungua hoteli ya kitalii ya Snow Crest, Desemba 18 mwaka jana, lakini uzio wa hoteli hiyo ulivunjwa na Wakala wa Barabra (TANROADS) baada ya siku moja tu na kuzua maswali mengi miongoni mwa wananchi.

Katika sakata hilo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Deudetis Kakoko, alikaririwa akieleza kuwa ukuta wa hoteli hiyo ulikuwa umejengwa ndani ya hifadhi barabara na ofisi yake ilikuwa imekwishakumwandikia mmiliki wa hoteli barua iiliyokuwa inaelekeza uzio kuvunjwa. Pamoja na maelezo hayo Meneja huyo alijikuta katika mgogoro wa chini kwa chini na baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali mkoani.

Na katika tukio la tatu mapema mwezi Januari mwaka huu katika viwanja vya Ikulu Rais kikwete ambaye alikuwa akabidhi magari ya kubebea wagonjwa kwa Wakurugenzi wa Halmshauri za Wilaya za Mbozi mkoani Mbeya na Longido mkoani Arusha alikataa kukabidhi gari kwa Mkurugnezi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Kayange Jacob ambaye ndiye aliyekuwa amealikwa. Alifanya hivyo baada ya kugundua kuwa aliyetakiwa kukabidhiwa gari hilo hakuwapo.

Rais Kikwete alisikika akihoji: “Wewe ni …(huku akitambulishwa na Kaimu Mnikulu) ahaa, umetokea Loliondo, ahaa hii gari si ya kwako bwana, sikupi….si yako…hii ni ya watu wa Longido si Loliondo,” alisema Rais Kikwete na kuwageukia maofisa wa Ikulu, “Hii ni nini? Hii ni kashfa, waombeni radhi hawa mliowaalika bwana (waandishi wa habari).”

Kikwete alimgeukia Mkurugenzi huyo “Gari hili moja ni kwa ajili ya watu wa Longido, si wa Loliondo, wewe ni nani kakutuma?”alikaririwa akiuliza Mheshimiwa Rais.

Baadaye Ikulu iliomba radhi kutokana na utata uliojitokeza na msaada huo wa magari aina Landrover 110 yaliyotolewa na Mkurugenzi wa kampuni ya CMC Automobiles Limited, Abdul Haji na yaligawiwa kwa wahusika.


Source: Raia Mwema
 
Back
Top Bottom