Joseph Mihangwa Toleo la 355 28
<< Makala iliyotangulia
Abdulrahman Babu
Joseph Mihangwa
jmihangwa@yahoo.com
More information about text fo
JUKUMU la kuteka Kituo cha Polisi cha Malindi na
Magereza alipewa Amour Mohamed Dugheish;
wakati jukumu la kuteka Cable and Wireless ,
Kituo cha Redio na Uwanja wa ndege, alipewa
Hashil Seif Hashil na wengine kupewa maeneo
mengineyo muhimu.
Na huu ndio uhalisia wa mambo yalivyokuwa
kiasi kwamba duru za Kibalozi Visiwani wakati
huo zilinukuliwa zikisema, Afro-Shiraz ndio
wanaotoa askari, lakini UMMA Party ndio
wanaoratibu na kudhibiti mipango yote ya
Mapinduzi hadi ushindi (Smith, William, 1971).
Ni kwa sababu hii haishangazi kuona kwamba,
baada ya Mapinduzi hayo, wapiganaji wa UMMA
Party ndio pekee waliounda Jeshi la kwanza la
ukombozi la Watu wa Zanzibar Zanzibar
Peoples Liberation Army (ZPLA), likiongozwa na
Komandoo, Kanali Ali Mahfoudh.
Kwa kifupi, Mapinduzi haya yalianza kama
maasi tu ya walalahoi wa mjini waliokata
tamaa ya maisha kwa lengo la kuchoma moto na
kuteketeza mji wa Zanzibar.
Ni pale tu yalipoingiliwa na Wanamapinduzi
wenye taaluma hiyo, makada wa UMMA Party
waliofunzwa kisiasa na kijeshi, kwamba maasi
hayo ya walalahoi yaligeuka kuwa maasi ya
kimapinduzi. Na kama alivyosema Babu baadaye
kwamba,
..Mabadiliko hayo ambayo
hayakutarajiwa siku hiyo, yalifungua mengi:
kutoka malalamiko mlipuko kuwa maasi yenye
kuongozwa na itikadi ya chama (UMMA); kutoka
matarajio finyu ya utaifa kuwa mapinduzi ya
kijamii; na kutoka giza nene lisilo na matumaini
hadi kufunguka kwa taswira ya matumaini,
muhimu katika kujenga mfumo mpya wa kijamii.
Yote haya yalichochea ghadhabu ya mataifa ya
kibeberu
...
Nyerere, Uingereza wagoma kuyatambua
Mapinduzi
Nchi za Kisoshalisti hazikupoteza muda wala
nafasi katika kuyatambua Mapinduzi; Urusi,
China, Czechoslovakia, Vietnam na Ujerumani
zote mbili (Mashariki na Magharibi) ziliyatambua
Januari 13, na kuleta hima misaada mingi
mikubwa, ya kijeshi na ya kiuchumi. Zanzibar
ikakaribisha pia wataalamu kutoka China,
Ujerumani Mashariki na Urusi.
Urusi pekee ilileta meli iliyojaa magari, mizinga na
bunduki kubwa za kutungua ndege na vifaru
pamoja na silaha mzo mzo. Na mwishoni mwa
Februari 1964, Babu akatangaza kupokelewa kwa
msaada wa Shilingi za Kizanzibari 3,700,000/=
kutoka China akisema, Huo ni mwanzo tu wa
makubwa yajayo.
Majina ya kikoloni yalibadilishwa haraka, badala
yake yakawekwa majina ya Kikomunisti. Kwa
mfano, Uwanja wa Taifa ukaitwa Mao Tse-
Tung; shule moja ikapewa jina la
Mwanamapinduzi wa Cuba, Fidel Castro;
Hospitali ya Taifa ikaitwa V. I. Lenin na
Madaktari wa Kichina wakafurika; Vyuo viwili
vikaitwa Patrice Lumumba na kingine Kwame
Nkrumah, na mengineyo.
Kwa nchi za Afrika Mashariki, Kenya iliyatambua
Mapinduzi Januari 13, na Uganda Januari 14;
wakati Rais wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere,
alikataa kuyatambua Mapinduzi hayo akidai
hakuwa na uhakika kama kweli Karume alikuwa
ameshika madaraka; bila shaka kwa maana
kwamba hakupendelea Zanzibar kuwa mikononi
mwa Wakomunisti.
Katika kipindi hicho, wakati Serikali mseto ya
Mapinduzi ya UMMA Party na ASP ikijaribu
kusimama kwa miguu yake, Uingereza na
Marekani, kwa hasira, ghadhabu na hofu ya
Zanzibar kughubikwa na Ukomunisti, ilipanga
mikakati mbalimbali kukomesha hali hiyo,
ukiwamo mkakati wa kuivamia Zanzibar kijeshi;
kumuua Babu au kuunda Shirikisho la Nchi za
Afrika Mashariki (EAF) ili Zanzibar imezwe ndani
ya tumbo kubwa la EAF isifurukute. Na kama
yote hayo yakishindwa, basi, liundwe Shirikisho la
Tanganyika Zanzibar kwa madhumuni hayo
hayo ya kuidhibiti Zanzibar
Marekani na Uingereza zapata hofu
Tangu mwanzo, Serikali za Uingereza na Marekani
hazikufurahishwa na harakati za Kikomunisti
Visiwani Zanzibar, harakati ambazo hatimaye
zilizaa Mapinduzi, Januari 12, 1964.
Hofu ya mataifa hayo ya Magharibi ilikuwa ni juu
ya Zanzibar kugeuka kitovu cha kueneza
Ukomunisti ukanda wa Afrika Mashariki enzi hizo
za vita baridi kati ya nchi za kibepari za
Magharibi, zikiongozwa na Marekani na
Uingereza; na nchi za Kisoshalisti za Mashariki,
zikiongozwa na Urusi na China.
Hofu hiyo ilizidishwa na Mapinduzi hayo ya
Kikomunisti, na jinsi Zanzibar ilivyofungua
milango haraka haraka kwa China na Urusi na
namna zilivyomwaga misaada ya kijeshi na ya
kiuchumi, huku Abdulrahman Babu, wakati huo
Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara,
akiitangazia dunia kuwa huo (ulikuwa) ni
mwanzo tu.
Alhamis, Januari 16, 1964, siku ya tano ya
Mapinduzi, Rais Karume, Hanga na Babu
walikwenda Dar Es Salaam kwa ndege
kumbembeleza Nyerere aitambue Serikali yao, pia
awape askari kwenda kurudisha amani na
utulivu.
Huku nyuma, Kiongozi wa Serikali, Field Marshal
John Okello, bila kujua juu ya safari ya Karume na
wenzake, akadai kwamba Karume hakushiriki hata
kidogo katika mapambano hivi kwamba
hakustahili kuwa Rais, japo Rais asiye na
madaraka.
Kwa hiyo jioni hiyo, Okello akafuta uteuzi huo na
yeye akajipa cheo cha Rais na Waziri wa Ulinzi;
na akamteua Karume kuwa Makamu wa Rais,
uteuzi ambao hakuutekeleza baada ya kupata
wazo la pili.
Haijafahamika bado walichozungumza Karume,
Hanga, Babu na Nyerere, lakini siku mbili
baadaye, askari polisi 300 kutoka Tanganyika
waliwasili Zanzibar kwa kazi iliyokusudiwa.
Itakumbukwa miaka mitatu kabla ya Mapinduzi
na miezi kadhaa kabla ya uhuru wa Tanganyika
Desemba 9, 1961, Rais Nyerere aliwahi kutamka
hofu yake kwa Zanzibar kuwa karibu na
Tanganyika, akisema, kama angekuwa na uwezo
wa kukitokomeza kisiwa kile hadi katikati ya
bahari ya Hindi, angefanya hivyo, kwa kuhofia
usumbufu na kutuumiza kichwa siku za
baadaye.
Hofu ya Mwalimu ambayo baadaye ilikuja
kujulikana kama The Zanzibar headache
(ugonjwa wa kuumiza kichwa kuhusu Zanzibar)
ilitokana, kwanza na harakati za uhuru za
Kikomunisti Visiwani zilizoongozwa na Babu enzi
hizo za vita baridi, kwamba huenda zingemtia
majaribuni juu ya msimamo wake kuhusu sera
zake za kutofungamana na upande wowote
Kimataifa iwapo suala la Zanzibar lingezua mzozo
kati ya mataifa makubwa, ikizingatiwa kwamba
yeye alikuwa mpenzi na kipenzi cha nchi za
Magharibi, hasa Uingereza.
Itakumbukwa pia kwamba mwaka 1957, wakati
harakati za Wakomunisti ndani ya ZNP zikichanja
mbuga kuelekea uhuru, Waingereza waliingilia kati
kwa kusaidia kuanzishwa kwa ASP ili kupunguza
kasi ya ZNP, pia Nyerere akiwa mmoja wa
waliosaidia. Kwa hiyo, hofu ya Mwalimu juu ya
harakati za Kikomunisti ilikuwepo tangu harakati
za uhuru hadi Muungano mwaka 1964.
Pili, Mwalimu aliogopa Zanzibar yenye migogoro
chini ya Sultani kama Mkuu wa nchi, kwamba
nchi hiyo ingeweza kutumika kama kituo cha
maadui kuishambulia Tanganyika. Hofu ya
Mwalimu juu ya Zanzibar kwa mambo hayo
mawili iliungana na ile ya Uingereza na Marekani
juu ya Zanzibar kuwa kitovu cha kueneza
Ukomunisti ukanda wa Afrika Mashariki, na kwa
sababu hiyo, Mwalimu akafunga nira na Mataifa
hayo.
Mazingira tangulizi
Kabla hatujatizama kuona namna mataifa ya
Magharibi yalivyojiingiza kudhibiti Ukomunisti
Zanzibar hadi shinikizo la Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar, ni vyema tuangalie
kwanza mazingira yaliyowezesha mchezo
kuchezwa na maandalizi ya mchezo wenyewe.
Kama hatua ya kwanza ya kindumbwendumbwe
hicho, Marekani ilimteua na kumhamishia
Zanzibar kutoka Congo (sasa DRC), Balozi na
Jasusi beberu la Shirika la Marekani (CIA), Frank
Carlucci kufanya kazi za kibalozi na kijasusi
Visiwani.
Ndani ya Serikali ya Mapinduzi namo hali
haikuwa shwari kwa wanaharakati wa mrengo wa
kushoto kumtuhumu Karume kushindwa
kusimamia na kuendeleza Mapinduzi. Kwa
sababu hii, wanaharakati wa Chama cha UMMA
ndani ya Serikali Abdulrahman Babu, Khamis
Abdallah Ameir, Ali Sultani, Ali Mahfoudh, Salim
Rashid, Badawi Qullatein na wengineo,
walioanzisha uhusiano kuunda njama na wenzao
wa ASP wahafidhina wa sera za Kisoshalisti ili
kumpindua Karume.
Wanaharakati wa ASP walikuwa ni pamoja na
Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Ali Twala,
Hassan Nassoro Moyo na wengineo. Karume na
wenzake wenye siasa mgando, wakaogopa. Na ili
aweze kuendelea kudhibiti madaraka Visiwani
asipinduliwe, aligeuka kumtegemea Mwalimu
Nyerere na Jeshi la Tanganyika Visiwani.
Kwa kipindi chote, Chama cha UMMA kilishinikiza
Hanga ateuliwe kuwa Waziri Mkuu Mtendaji na
Karume abakie kama Rais asiye na madaraka.
Ukweli, mwanzoni Hanga aliteuliwa Waziri Mkuu,
lakini Othman Sharrif akamchochea Karume
abadili uteuzi kwa kumuogofya. Uteuzi ukafutwa
siku hiyo hiyo, Hanga akanywea.
Uingereza, Marekani zaingia kazini
Ili kuhakikisha Ukomunisti hausimiki mizizi Afrika
Mashariki kupitia Zanzibar, Marekani ilibuni
mikakati ifuatayo: ilikuwa, ama kwa Uingereza
kuivamia Zanzibar kijeshi kwa msaada wa
Marekani; au kuunda Shirikisho la nchi tatu za
Afrika Mashariki Kenya, Uganda, Tanganyika na
Zanzibar ambayo ingemezwa ndani ya Shirikisho
isiweze kufurukuta. Shirikisho la Tanganyika na
Zanzibar kuunda Tanzania lilikuja baadaye kama
ajali tu baada ya mikakati miwili ya kwanza
kushindwa.
Katika sehemu hii ya makala na kuendelea, kwa
kutumia vyanzo mbali mbali, zikiwamo simu za
maandishi ( telegraphs ) za kijasusi za Serikali za
Marekani na Uingereza kwa Mabalozi wao Afrika
Mashariki, na ambazo sasa zimeondolewa katika
orodha ya nyaraka za siri, tutaona namna
mpambano dhidi ya Ukomunisti ulivyoendeshwa
kufikia Muungano wa Tanzania.
Mambo yalianza Januari 13, 1964, siku moja
baada ya Mapinduzi na Okello akiwa tayari
ameunda Serikali yake kwa kumteua Karume Rais
wa Jamhuri ya Zanzibar na Pemba; pale Katibu
wa Jumuiya ya Madola na Waziri wa makoloni
wa Uingereza, Duncan Sandys, alipomwandikia
Rais wa Kenya, Jomo Kenyatta, kumwelezea hali
ya Visiwani akisema
.. Lakini Wajumbe wawili
wa timu ya Sheikh Karume, Bwana (Kassim)
Hanga na Bwana (Abdulrahman) Mohamed
(Babu) wanaaminika kuwa wafuasi wakubwa wa
Ukomunisti. Kama Serikali (ya Zanzibar), hatua
chache tu Pwani ya Afrika Mashariki itakuwa na
mwegemeo wa Kikomunisti, na pengine kuruhusu
vituo vya kijeshi kwa mataifa ya Kikomunisti,
litakuwa jambo hatari sana na la usumbufu
kwetu.
Barua hiyo ambayo nakala walitumiwa Nyerere na
Obote, ilieleza kuwa, tatizo kubwa lilikuwa ni
Babu na Chama cha UMMA; akamtaka Kenyatta
awasiliane na Nyerere na Obote ili angalau
walizungumze.
Wakati huo Uingereza na Marekani zilikuwa
zimekataa kuyatambua Mapinduzi, kama njia ya
kumshinikiza Karume ajiweke mbali na Babu.
Naye Karume, kwa hasira akawatimua Balozi wa
Uingereza na Kaimu Balozi mdogo wa Marekani
Visiwani, Februari 19, 1964. Mabalozi hao
waliruhusiwa kurejea baada ya nchi zao
kuyatambua Mapinduzi, Februari 23, 1964, huku
nafasi ya Kaimu Balozi wa Marekani ikichukuliwa
na jasusi Frank Carlucci.
Itaendelea