Huyu ndiye Kardinali Mteule, Protase Rugambwa

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
1688926494272.png

Leo Jumapili Julai 9, 2023 kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francisco amemteua Askofu Mkuu Mwandamizi Jimbo Kuu la Tabora, Protase Rugambwa kuwa kardinali nchini Tanzania.

Je, unaujua wasifu wa Askofu Mkuu Rugambwa aliyeteuliwa kuwa Kardinali wa tatu katika historia ya nchi ya Tanzania?

Rugambwa alizaliwa Mei 31, 1960 Bukoba mkoani Kagera, alisoma katika seminari ndogo za Katoke, iliyoko Jimbo la Rulenge-Ngara na Itaga mkoani Tabora.

Alipata daraja takatifu la upadri Septemba 2, 1990 ambapo alibahatika kupewa daraja hilo na aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki wakati huo, Papa Yohane wa Pili alipotembelea Tanzania.

Baada ya kupewa daraja hilo takatifu, alipangiwa kuwa Padri wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara.

Kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2008 alifanya utume wake katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu Vatican.

Januari 18, 2008 aliteuliwa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani wakati huo, Papa Benedikto XVI, kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma. Miaka minne baadaye Juni 26, 2012 aliteuliwa kuwa Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na wakati huo huo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu.

Utume wa Rugambwa uliendelea hadi Novemba 9, 2017 alipoteuliwa na Papa Francisco kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu alitumikia baraza hilo kwa vipindi viwili hadi muda wake wa kikatiba ulivyoisha.

Aprili 13, 2023 Baba Mtakatifu alimteuwa Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora.

Rugambwa anakuwa kardinali wa tatu nchini Tanzania akitanguliwa na Laurean Rugambwa aliyefariki dunia Desemba 8, 1997 na Polycarp Pengo aliyestaafu mwaka 2019.

Pia soma: Askofu Mkuu Mwandamizi Protase Rugambwa ateuliwa kuwa Kardinali
 
... Hongera kwake...Mungu amtangulie kwenye majukumu yake mapya.
 
Back
Top Bottom