Huu urasimu wa kutoa habari mpaka lini?

Ustaadh

JF-Expert Member
Oct 25, 2009
413
19
Sababu za kuchelewa ujenzi Barabara ya Mandela zatajwa

Kutokamilika katika muda uliopangwa kwa ukarabati wa barabara ya Nelson Mandela jijini Dar es Salaam kunatokana na sababu za kiutendaji ndani ya Wakala wa Barabara (Tanroads). Habari toka kwa mmoja wa maafisa wa kampuni iliyopata zabuni ya ukarabati wa barabara hiyo, Maltauro Spencon Strlying zimeeleza sababu mbili zinazochangia kuchelewa kukamilika kwa kazi hiyo ni kutolewa maelekezo yenye upungufu yanayotolewa na Tanroads ambayo yanaathiri ufanisi wa kazi wa kampuni hiyo.

Alisema kitendo cha wao kupangiwa kazi ya eneo dogo linalochukua saa chache na mhandisi mshauri badala ya kazi ya eneo kubwa itakayochukua muda kwa maelekezo ya Tanroads, kwa kiasi kikubwa inasababisha utendaji kuchelewa. "Tunapangiwa eneo dogo la kufanya. Tukishamaliza Injinia mshauri anakuja kukagua namna tulivyofanya, akisharidhika anatupangia eneo jingine ambalo nalo linakuwa dogo, tukimaliza anakagua tena…utendaji wa aina hii unaifanya iende taratibu," alisema.

Alisema kwa kawaida mkandarasi hupangiwa eneo kubwa la kufanya kazi yake na ndipo anakaguliwa tofauti na inavyofanyika sasa. Aidha, Ofisa huyo alikieleza kitendo cha kucheleweshwa kwa malipo yao toka Tanroads kama makubaliano yalivyo kwenye mkataba, kuwa kinawafanya waingie gharama.
"Mpaka sasa kuna fedha ambayo ilitakiwa tuwe tumelipwa, kutokana na sehemu ya kazi ambayo tumeikamilisha, lakini bado hatujalipwa pamoja na mfadhili ambaye ni Umoja wa Ulaya (EU) kuwa amekwisha zitoa fedha hizo," alisema. Alisema kuchelewa kulipwa fedha hizo kumeifanya kampuni yake kutumia Euro milioni nane kulipia gharama mbalimbali za mradi.

Gazeti hili lilipokwenda kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Ephraem Mrema, kutoa ufafanuzi wa madai hayo katikati ya Septemba mwaka huu, Katibu Muhtasi wake, aliielekeza mwandishi aandike maswali ili yapelekwe kwa Mrema.

Mwandishi aliandika maswali manne na kuahidiwa afuatilie majibu baada ya wiki moja. NIPASHE ilitaka kujua sababu zilizosababisha muda wa kukamilika kwa barabara hiyo uongezwe kwa kuwa ilipaswa kukamilika Desemba mwaka jana. Aidha, ilitaka kujua utaratibu unaotumika kwenye ukarabati au ujenzi wa barabara kama ile ya Nelson Mandela. Kadhalika, gazeti hili lilitaka kujua kwa nini mkandarasi hajalipwa fedha zake anazostahili kutokana na sehemu ya kazi aliyofanya mpaka akafikia kutumia fedha zake.

Kwa takribani zaidi ya mwezi mmoja, mwandishi amekuwa akifuatilia majibu na kuelekezwa amuone Afisa Uhusiano wa Tanroads, ambaye ameelekezwa kuyafanyia kazi maswali hayo. Hata hivyo, ofisa huyo amekuwa akimpa ahadi za uongo za kwenda kuchukua majibu, lakini kila anapokwenda anajibiwa kuwa maswali yake bado yanafanyiwa kazi. "Ameshakabidhiwa Injinia mmoja anayeyatafutia majibu. Anatakiwa atoe majibu na ayarudishe kwa Mtendaji Mkuu akayaone na kisha tutakujibu," alisema. Hata hivyo, baadaye alisema yameshapelekwa kwa Mrema ili ayaone na kisha tutakujibu lakini, mwandishi alipofuatilia alielezwa kuwa Mrema hajatoa majibu.
 
Back
Top Bottom