Huu ni unyama wa hali ya juu

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Mtoto agongwa na gari, atupwa ufukweni Dar
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 26th July 2011
Habari leo

POLISI jijini Dar es Salaam wanamtafuta dereva aliyemgonga mtoto, Ally Shabani (7), kisha kumchukua akiwa hai na kudai kumpeleka hospitali, lakini mwili wake ukakutwa kichakani kwenye ufukwe wa Coco kando ya Bahari ya Hindi, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo iliyotokea Mtoni kwa Azizi Ally, wilayani Temeke, Dar es Salaam Ijumaa ya wiki iliyopita saa 11:30 jioni, dereva wa gari hilo Toyota Mark II nyeupe, aliomba kumkimbiza mtoto huyo hospitali.

Mashuhuda hao walidai kuwa dereva wa gari hilo ambalo namba zake za usajili kwa sasa tunazihifadhi, aliondoka na mtoto huyo akiwa hai baada ya kuwarubuni mashuhuda kuwa alitaka kumwahisha hospitali.

Mashuhuda hao waliozungumza na gazeti hili walidai waliandika namba za gari hilo, bila dereva kufahamu na kumruhusu kuondoka kwa amani katika eneo la tukio huku akiwa na majeruhi.

“Habari hizi zimetusikitisha watu wote. Tumesikia kutoka katika redio moja ikitangaza
kuhusu kuokotwa kwa maiti ya mtoto katika kichaka kilichopo Masaki kwenye eneo la Coco
Beach, huyo ndiye yule aliyegongwa pale Mtoni kwa Azizi Ally.

“Hakuna aliyekuwa akijua jina la mtoto, lakini kwa jinsi habari za Polisi zilivyoelezwa
na redio hiyo kuna ukweli kwamba ndiye yeye na hapa ninavyokuambia nyumbani kwao
wameweka msiba,” alisema shuhuda huyo.

Alidai dereva huyo mwanamume alidanganya kuwa anampeleka hospitali na kila mtu
aliamini, lakini ndugu walimtafuta katika hospitali mbalimbali bila mafanikio hadi polisi waliposema wamehifadhi maiti aliyeokotwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni ya Mwananyamala.

Gazeti hili liliwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela na kuthibitisha kuokotwa kwa maiti ya mtoto wa kiume anayekadiriwa kuwa
na miaka kati ya sita na saba na kusema kuwa hawakuwa na taarifa nyingine za ziada.

“Askari wetu wa doria wakiwa kazini usiku wa Julai 24, waliona alama za matairi ya gari
zilizoelekea kwenye eneo la vichaka vya Coco Beach karibu na Bahari ya Hindi na kupata
mashaka kutokana na ukweli kuwa haikuwa kitu cha kawaida kwa gari kuelekea kwenye
eneo hilo.

“Baada ya kufuatilia hadi mwisho wa alama ya matairi yale, waliukuta mwili wa Shabani
ukiwa na majeraha makubwa usoni pamoja na mikwaruzo tumboni na kwenye mguu wa kulia
kuashiria kuwa aligongwa na gari na kutupwa mahali hapo kuficha ushahidi,” alisema Kamanda Kenyela.

Kwa maelezo ya Kenyela, wao kama Polisi wa Mkoa huo wa Kinondoni taarifa yao ilirekodiwa kutokana na walichokiona na hawakuwa na maelezo mengine wala kuhisi gari iliyomgonga.

“Tunashukuru kwamba wewe sasa ndio unafungua masikio kwamba inawezekana aligongwa
nje ya eneo hili akaja kutupwa hapa, ninashukuru na naomba niwasiliane na mwenzangu
wa Temeke kuona kama kuna ukweli katika hilo,” alisema Kamanda huyo.

Kabla ya kutoa majibu, gazeti hili lilimpata Kamanda wa Polisi wa Temeke, David Misime
aliyethibitisha kugongwa kwa mtoto huyo.

“Kwa kweli tulikuwa hatuna habari hiyo siku ilipotokea ajali, lakini jana (juzi) asubuhi
alikuja mama mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mtoto wa shemeji wa marehemu aitwaye Salma Shabani na kutueleza kuwa alikwenda Mwananyamala hospitali kuangalia maiti na kugundua kuwa inamhusu,” alisema Kamanda Misime.

Alisema dada huyo aliwaeleza kuwa mtoto huyo aligongwa na dereva mwanamume aliyewadanganya mashuhuda kuwa alimchukua ili ampeleke hospitali, lakini akaenda kumtelekeza bila kujua kuwa namba za gari yake zilikuwa zimenakiliwa na walioona kilichotokea.

“Kwa kweli tunawashukuru mashuhuda walioandika namba na kuhakikisha zimetufikia
kupitia ndugu huyu wa marehemu (Salma). Ni tukio la kinyama na mauaji ya kikatili kwa
sababu kama mtoto alikuwa amezimia pengine angeweza kupona kama angewahishwa hospitali, lakini unyama wa dereva ndio nadhani umesababisha apotee kabisa…

“Alipo anapaswa afahamu kuwa hayupo safe (salama) hata kama atafungia gari lake tutamkamata tu. Askari wetu wameanza msako na tunawaomba mashuhuda wa ajali wajitokeze ili atakapokamatwa achukuliwe hatua kutokana na mauaji hayo. Huu ndio mwito wangu kwa sababu ushahidi utatoka kwa walioshuhudia ajali.”

Kenyela alitoa mwito kama huo akisisitiza mmiliki au dereva wa gari hilo kujisalimisha
Polisi mapema kwa sababu ni lazima atakamatwa tu.

Polisi katika mikoa yote miwili ya kipolisi haikutoa maelezo zaidi kuhusu wazazi wa
marehemu zaidi ya kusema kuwa mtoto huyo alikuwa bado hajaanza shule.

 
Unyama uliopitiliza!!!! Lakini polisi wamekosea kukimbilia kutangaza kwamba wanajua namba za hilo gari. Wangesema gari lililomgonga halijajulikana, jamaa angejiona ame-win na kuanza kutanua na gari lake then angekamatwa kwa urahisi kupita kiasi!!!

Tiba
 
Inatia uzuni sana serikali ingeangalia hizi sheria za madereva ziwe kama China dereva akigonga mtu akafa basi jela maisha
 
Endapo wakifanikiwa kumkamata mahakama itoe adhabu kali dhidi yake ili iwe fundisho kwa madereva wa hapa mjini sababu wengi wao wana tabia chafu kma ya uyo mwenzao. Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu.
 
Back
Top Bottom