May 3rd, 2011
Kamati Ndogo ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) imepongeza na kuunga mkono hatua zilizochukuliwa na Chama cha Mapinduzi na zinazoendelea kuchukuliwa katika kuleta mageuzi ndani ya CCM.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo hii iliyosainiwa na Mwenyekiti wake Hussein Bashe kamati hiyo ndogo ya UVCCM, ilisema imempongeza Mwenyekiti wa CCM Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa namna alivyosimamia mageuzi ndani ya Chama.
Taarifa hiyo ilisema kuwa kamati hiyo ndogo aidha inawapongeza Sekretarieti mpya na Kamati Kuu mpya iliyochaguliwa.
Katika taarifa hiyo ilisema ni vizuri kufanya mageuzi sasa wakati ambapo bado UVCCM kinakubalika kwa sababu kina wanachama 2.7 Milioni, kimeshinda chaguzi zote, kimetimiza miaka 32.
Taarifa iliongeza kuwa ni wakati muafaka kwa UVCCM kufanya mageuzi ili kuiimarisha kiuchumi na kifedha na hivyo kuifanya UVCCM iwe na rasimali zake zitakazokifanya kujitegemea na hivyo kuacha utegemezi.
Katika taarifa yake kamati hiyo ndogo iliongeza imepitia Hadidu za rejea za maeneo inayotakiwa kuyafanyia mageuzi ambayo ni Muundo wa UVCCM uliopo una ngazi sita za uongozi kwa upande wa Tanzania Bara yaani, Ngazi ya Shina, Tawi, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa na kwa Upande wa Zanzibar una ngazi 7 yaani Shina, Tawi, Wadi, Jimbo, Wilaya, Mkoa na Taifa.
Kamati ilifafanua kwenye taarifa yake je muundo huu unakidhi haja? Kuna mapendekezo gani toka kwa Vijana juu ya muundo huu.
Taarifa hiyo ilinukuliwa ikisema kamati itakuwa na wajibu wa kubuni na kutoa mapendekezo kutokana na maoni ya wadau, utaratibu mzuri wa kuboresha vyanzo vya mapato na hivyo kuimarisha UVCCM kimapato.
ili kutimiza malengo hayo hapo juu, kamati hii itafanya kazi na kukutana na makundi mbalimbali. Makundi hayo ni pamoja Viongozi na Wanachama wa CCM na UVCCM na Viongozi waastafu wa CCM na UVCCM, Makada mbalimbali kama vile wanamichezo, wasanii, wamachinga, wavuvi, wasomi, waandishi wa habari, makamanda wa UVCCM na asasi zisizo za kiraia zinazojishughulisha na vijana, ilisema taarifa hiyo.
Kamati hiyo ndogo itayokusanya maoni na Kuandaa mapendekezo ya mageuzi ndani ya UVVCM iliundwa na Baraza kuu la UVCCM Taifa lililokutana Dodoma tarehe 19/03/2011.