Hotuba ya rais wa zanzibar dk. Amani abeid karume

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,809
HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR DK. AMANI ABEID KARUME



HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR DK. AMANI ABEID KARUME

SALAMU ZA RAIS WA ZANZIBAR NA
MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI,
MHESHIMIWA DK. AMANI ABEID KARUME,
KWA WANANCHI BAADA YA KURA YA MAONI
JUMAPILI TAREHE 1 AGOSTI, 2010


Assalaam Aleikum,

Ndugu Wananchi,
Naanza kwa kumshukuru Mola wetu, Subhana Wataala, Muumba Mbingu na Ardhi, kwa rehema zake kwetu zinazotuendeshea mambo yetu kwa salama na amani.

Nachukua fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati na pongezi nyingi kwa wananchi wote wa Zanzibar walioshiriki katika Kura ya Maoni na kutumia haki yao ya kidemokrasia kutoa maamuzi au mapendekezo yao juu ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kushiriki kwao, kwa kupiga kura ya Ndio au Hapana, ni kuthibitisha kupevuka demokrasia na utawala bora nchini kwetu. Zoezi hilo ni la kihistoria ambalo limewapa wananchi wa Zanzibar haki ya kushiriki moja kwa moja katika maamuzi mazito yanayowahusu, na kila alieshiriki ameingia katika historia ya kuendeleza demokrasia, amani na utulivu inayotegemewa kuwa endelevu na msingi mpya wa maendeleo zaidi ya nchi yetu.

Matokeo ya kura hiyo yameshatolewa rasmi na nina wingi wa furaha kuwa kura ya NDIO imechukua nafasi ya juu ikiwa ni asilimia 66.4, karibuni thuluthi mbili ya kura zote zilizopigwa. Nawashukuru na kuwapongeza sana wananchi wote waliochukua uamuzi wa kupiga kura ya NDIO. Kufanya hivyo kumefungua sura mpya ya mfumo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kudhihirisha nia ya Wazanzibari kuishi kwa umoja, kupendana, amani na utulivu. Aidha, nawashukuru na kuwapongeza wale wachache waliokataa mfumo huo kwa kutumia haki yao ya demokrasia na kutoa uamuzi wao.

Kwa vile nchi yetu ni ya kidemokrasia na inafuata misingi hiyo, na kwa kua uamuzi wa wengi umeshafanywa na kauli ya wachache imesikika, sasa ni wajibu wetu sote kushirikiana kuendeleza gurudumu la maendeleo ya demokrasia chini ya mfumo mpya nchini mwetu. Katika hili, hakuna mtu alieshinda wala alieshindwa ila mshindi ni Zanzibar yenye amani, umoja na mshikamano.

Washindi ni wananchi wenyewe kutaka kukuza umoja, demokrasia, utawala bora, amani na maendeleo kwa pamoja. Huo ndio msingi hasa wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Baada ya kura hii ya maoni, wajibu sasa ni wa Baraza la Wawakilishi ambalo linatarajiwa kukutana hivi karibuni kufanya marekebisho ya msingi katika Katiba ya Zanzibar ya 1984. Sisi Zanzibar tutakuwa ni nchi ya kupigiwa mfano kwa chaguzi zitakazokuwa za amani na utulivu ikitiliwa maanani namna ya zoezi la upigaji kura ya maoni ulivyokwenda. Ni matarajio yetu sote kuwa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa umoja wao wataheshimu uamuzi wa wananchi wa Zanzibar na kufanya wajibu wao kwa faida ya kila mmoja wetu.

Ndugu Wananchi,

Zoezi hili la kupiga kura ya maoni ili kufanya uamuzi wa mabadiliko makubwa ya mfumo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuliwachia Baraza la Wawakilishi kupitisha Mswada wa Mabadiliko ya Katiba, litaingia katika historia ya maendeleo ya demorasia nchini kwetu na Afrika nzima kwa jumla. Mara nyingi nchi zetu za Afrika zinakutwa na majanga na mizozo kufuatia harakati za uchaguzi. Hali hiyo haipaswi kupuuzwa na ni vyema ikaepukwa kadiri inavyowezekana.

Kwa msingi huo, wananchi wa Zanzibar wameamua kubadilisha sura hiyo kwa kuweka mfano mzuri wa kuigwa na nchi nyengine ili demokrasi iendelezwe kwa kuendesha chaguzi kwa amani na kuwashirikisha wananchi wote katika utawala wa nchi yao.

Ndugu Wananchi,
Bado tuna wajibu wa kuthibitisha kuwa mshindi wa zoezi hili ni Zanzibar na Wazanzibari wote, kwa kuhakikisha kwamba sote kwa pamoja tunaendesha uchaguzi mkuu ujao katika hali ya amani, salama na utulivu, tarehe 31 Oktoba mwaka huu. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kudumisha utulivu na ushirikiano tulionao hivi sasa.

Baada ya hapo tutaingia, Inshaallah, katika kipindi kipya cha kuleta maendeleo makubwa katika nchi yetu katika hali ya umoja na mshikamano. Matokeo yatakuwa ya manufaa kwa wananchi wote na tutakuwa tumejenga Zanzibar Mpya yenye umoja na mshikamano tukiwa sote ni Wazanzibari.

Kwa kumalizia, napenda kutoa shukurani zangu za dhati, kwa mara nyengine tena kwa wananchi wote walioshiriki katika Kura ya Maoni, kwa utulivu na ustaarabu mkubwa. Natoa pongezi za pekee kwa Kamati ya Watu Sita ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Utekelezaji wa Azimio la Baraza kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ambayo Waheshimiwa Wajumbe wake wamefanya kazi kubwa na nzuri ya kuelimisha jamii Unguja na Pemba juu ya mfumo mpya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo tutaiunda baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Navishukuru vyama vyote vya siasa kikiwemo chama changu CCM, chama cha upinzani CUF, viongozi wa dini, wahadhiri na wanafunzi wa vyuo vikuu, NGOs waliounga mkono hoja hiyo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika kura ya maoni na kuikubali.

Naipongeza na kuishukuru Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), na wafanyakazi wake wote kwa kuendesha zoezi zima vizuri na kwa mafanikio, hasa ikizingatiwa kutokuwepo kwa uzoefu wa muda mrefu katika suala hilo. Tunalishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa – UNDP na washirika wengine wakiwemo Nchi za Jumuiya ya Ulaya na wengineo kwa msaada wao katika kuendesha zoezi hili. Aidha, natoa shukurani maalum kwa Switzerland, Uingereza, Norway na Sweden kwa kua tayari kutupatia uzoefu wao katika mifumo ya utawala wa umoja wa kitaifa na zaidi katika suala la uendeshaji wa kura ya maoni. Mchango wa Switzerland nchi yenye uzoefu wa miaka mingi umetusaidia sana.

Ndugu Wananchi,
Baada ya maelezo hayo, ni wajibu wetu sote kujipanga vyema na kuendesha uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, 2010 kwa ustaarabu na mwenendo huo huo mzuri tuliouonesha katika kura ya maoni. Kwa kufanya hivyo kwa uadilifu, tutapoza nyoyo za wenzetu waliokua na hofu juu ya jambo hilo na bila ya shaka mafanikio yake ni yetu sote. Tuhimizane sote mema na tukatazane maovu. Inshaalla Mwenyezi Mungu atatusaidia.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Mwenyezi Mungu awabariki wote.
 
Back
Top Bottom