Wamebarikiwa wanaotendea wema wanyama!
Ndioo! wanyama wana hospitali tena mpaka za emergency. Saa tisa usiku mbwa wako akiumia unampeleka hospitali akatibiwe.
Wanyama wana polisi wao wanaitwa animal cops. Mnyama akikwama kwenye mtaro wanaitwa kuja kumtoa. Jibwa likileta noma mtaani wataitwa kulikamata. Ukipiganisha wanyama au kuwatesa hasa kwa kuwanyima chakula na kuwapa maisha duni polisi wa wanyama watakufungulia kesi.
Kuna kijiji kimoja jogoo alikuwa anaranda mitaani bila ya mwenyewe. Polisi waliitwa. Wiki mbili walimkimbiza na kumtaimu jogoo mpaka walimpata na kumpeleka nyumba ya wanyama ambako alikaa mpaka akatokea mtu wa kumchukua (kumuadapti) na kukaa nae nyumbani kwake. Bongo jogoo wako umemfungia anaibiwa na kuliwa itakuwa huyu asiye na mwenyewe.
Mbwa au paka akipotea mwenyewe anatangaza kwenye TV au redio. Sio siri nilishasikia tangazo kuwa eneo fulani kuna mbwa anazurura (stray dog) sasa mitaa yetu mbwa wazururaji ni wangapi?
Ni lini umepeleka paka wako hospitali. Lini umepeleka mbwa wako kuogeshwa. Umeshawahi kumlipia tiketi ya ndege mnyama wako ukasafiri naye kwa sababu huna mtu wa kumuacha naye nyumbani?
Lini umemnunulia paka wa nyumbani kwenu chakula. Au unaona ni halali kumpa miba ya samaki? Eti ukimpa chakula hatakula panya. Ndio maana paka wa Bongo wanafungua vyungu vya samaki jikoni.
Ni vitu vya namna hii vinavyofanya nchi za wenzetu kuneemeshwa hata kama watu wake si washikaji dini.