Hoja Nane za Mchinjita Kwenye Hotuba ya Nishati

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA NISHATI ACT WAZALENDO NDG. ISIHAKA MCHINJITA KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA NISHATI KWA MWAKA 2023/24.

Utangulizi
Jana Mei 31, 2023 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipokea na kuanza kujadili hotuba ya bajeti Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambapo leo itaenda kuitimishwa mjadala wake na kuidhinishwa na bunge. Wote tunafahamu kuwa bajeti ni nyenzo muhimu sana katika kugharamia huduma ya nishati na kuleta uhakika wa utekelezaji wa miradi, progamu na mikakati ya kisekta ili kuhakikisha upatikanaji wake.

Katika mwaka huu wa fedha 2023/24 Wizara ya Nishati imeomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi trilioni 3.08 ambayo Sh. tirlioni 2.9 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Shilingi bilioni 87. sawa na asilimia 2.9 kwa ajili matumizi ya kawaida. Kama ilivyo kwa bajeti zingine wananchi na wadau mbalimbali wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu vipaumbele vya bajeti.

Sisi, ACT Wazalendo kupitia Waziri Kivuli wa Nishati tumefanya uchambuzi wa mpango wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24. Katika uchambuzi wetu tumekuja na maeneo nane (8) yenye changamoto na tumeyatolea maoni ili kuhakikisha bajeti ya mwaka huu inayazingatia kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini.

Katika hoja hizi tumeangazia; uhakika wa upatikanaji wa huduma ya umeme, mafuta na gesi (nishati); Gharama za kupata huduma hizo; vipaumbele vinavyowekwa na Serikali kwenye kushughulikia changamoto, uanzishaji na utekelezaji wa Miradi; usimamizi wa matumizi ya fedha zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Katika hoja 8 tulizoziibua, chama cha ACT Wazalendo kinaona bado hakuna uhakika wa upatikanaji wa nishati hususani huduma ya umeme na bajeti ya mwaka huu haiendi kujibu changamoto hii kutokana na kutawanya vipaumbele. Aidha, bado kuna mkanganyiko wa taarifa za Serikali juu ya uwezo wa nchi kuzalisha umeme na mahitaji halisi ya huduma ya umeme.

Takwimu zinaonyesha uwezo wa nchi yetu kuzalisha umeme hadi kufikia mwezi April mwaka 2023 kuwa ni Megawati 1872.05 wakati mahitaji ya juu ya umeme kwenye Gridi ya Taifa ni Megawati 1431.39. Kutokana na takwimu hizi zinaonyesha tunazalisha umeme na kuwa na ziada lakini mara kadhaa wananchi tuumekuwa tukishuhudia mgao wa umeme nchini na majibu ya Serikali huwa ni uwezo mdogo wa kuzalisha.

Sasa kama takwimu za mahitaji zingekuwa sahihi kusingekuwa na kero ya uhakika wa upatikanaji wa umeme kwa watumiaji mbalimbali. Waziri mwenye dhamana anahitaji kuweka uhalisia wa mahitaji ya umeme kulingana na makadirio ya matumizi kwa mchanganuo wa watumiaji.

Zifuatazo ni hoja kuuu 8 (8) kuhusu mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwenye wizara hii kwa mwaka wa fedha 2023/24.

1. Utitiri wa miradi ya umeme na ufinyu wa upatikanaji wa fedha za utekelezaji.
Uchambuzi wa bajeti ya wizara hii kwa mwaka 2022/23 tulioufanya tulionyesha namna Serikali inavyotawanya nguvu kiduchu ya fedha iliyopo katika kutekeleza miradi mingi ya kuzalisha na kusafirisha umeme ambayo mingine kwa zaidi ya miaka saba sasa imekuwa ikitajwa kama miradi ya kipaumbele bila kutengewa fedha za utekelezaji wake au mingine kutengewa fedha kidogo.

Tulitahadharisha mwenendo huu wa uwekaji vipaumbele na usimamizi wa utekelezaji wake kwa kuonyesha mchanganuo wa miradi 10 ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme iliyotawanywa nchi nzima bila kukamilika kwa miaka mitano (5).

Aidha tulionyesha mwenendo na hali ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa miaka miwili mfululizo. Kwa mwaka wa fedha 2020/2021 wizara ilipanga kutumia Sh. trilioni. 2.197 lakini hadi kufikia Aprili 2021 ilipokea ShT. trilioni 1.35 sawa na asilimia 61.5 ya bajeti yote. Kwa mwaka 2021/22 wizara ilipanga kutumia shilingi trilioni 2.386 hata hivyo ilipewa shilingi Trilioni 1.820 sawa na asilimia 76.29 ya bajeti yote katika kipindi kama hicho.

Katika mwaka mwa fedha 2023/24 tumeona Serikali ikiendelea na utaratibu ule ule wa kuorodhesha utitiri wa miradi na kutawanya fedha bila kukamilisha malengo ya kuzalisha umeme ambao ungeweza kuendana na kasi kubwa ya ukuuaji wa mahitaji ya umeme ili kulihakikishia taifa kuwa na umeme wa uhakika. Kutokana na utitiri wa miradi tumeona kwa mwaka 2022/23 Serikali imeweza kukamilisha Mradi mmoja tu wa Kinyerezi I (MW185) ambao umechukua miaka 8 tangu 2015.

Huku ongezeko la uzalishaji wa umeme kwa mwaka huu umekuwa Megawati 177 kupitia Gesi asilia pekee. Orodha ya baadhi ya miradi ya kipaumbe iliyopo kwenye hatua ya utekelezaji na kutengewa fedha kwa mwaka huu ni kama ilivyo hapo chini;

i. Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) – MW 2,115; Umetengewa Sh. trilioni 1.5.

ii..Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Gesi Asilia – Mawe Project (MW 150); zimetengwa Shilingi bilioni 345

iii. Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Jua wa Shinyanga (MW 150); Jumla ya Shilingi bilioni 27.63 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji.

iv. Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezi I Extension (MW 185); Umetengewa Sh. bilioni 40

v. Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Kakono (MW 87.8); Shilingi bilioni 39.15 zimetengwa

vi. Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Ruhudji (MW 358); Umetengewa Sh. bilioni 6.27

vii. Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Rumakali (MW 222); Umetengewa sh. bilioni 5.25

viii. Ukarabati wa Kituo cha Kufua Umeme cha Hale Hydro Power Plant; Shilingi bilioni 6.4 zimetengwa.

ix. Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Malagarasi (MW 49.5); Jumla ya Sh. bilioni 15.52

x. Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Jua wa Shinyanga (MW 150); Jumla ya Shilingi bilioni 27.63 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji.

Kwa upande wa miradi ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nayo ipo miradi zaidi ya 15 baadhi ya miradi hiyo kama inavyoonekana hapa chini.

xi. Julius Nyerere Hydro Power Plant hadi Chalinze-kV 400 na Kituo cha Kupoza Umeme, Chalinze.

xii. Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa kV 220 kutoka Geita hadi Nyakanazi na Kituo cha Kupoza Umeme, Nyakanazi.

xiii. Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa kV 400 kutoka Singida-Arusha-Namanga na Kituo cha Kupoza Umeme, Lemugur.

xix. Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa kV 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma na Kituo cha Kupoza Umeme, Kidahwe

xx. Mradi wa Backbone Transmission Investment Project (BTIP)-Phase ll

xxi. Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa kV 220 kutoka Rusumo hadi Nyakanazi.

xxii. Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa kV 220 kwa Ajili ya Uendeshaji wa Treni ya Umeme (Standard Gauge Railway-SGR II, Lot I)
xxiii. Mradi wa Ujenzi wa kituo Kipya cha Kupoza Umeme Luguruni
Gharama halisi ya utekelezaji wa miradi yote hii ni Tsh. Trilioni 17 wakati wizara inaianzisha miradi hii ilijiwekea malengo ya kukamilika ifikapo mwaka 2025. Kwa mwenendo huu wa bajeti ambapo mpaka sasa wizara haijapata hata asilimia 30 ya fedha inazozihitaji kukamilisha miradi hii, ndoto ya kuzalisha MW 5000 za umeme ifikapo 2025 haziwezi kufikiwa huku baadhi ya miradi ikikumbwa na harufu za rushwa na uzembe unaoligharimu taifa kama tutakavyoainisha.

ACT Wazalendo tuna maoni kuwa Serikali ijikite kwenye miradi michache itakayotoa matokeo kwa kuzingatia uwekezaji ambao tumeshaufanya na ijikite kwenye uwezekano wa nchi kujitosheleza kwa nishati ya umeme kabla ya kufikiria kuuza umeme nje ya nchi. Kwa kufanya hivi tutaokoa fedha nyingi zinazolipwa kama riba ya kuchelewa kutekeleza mikataba kwa wakati na kuziba mianya ya wizi kwa utitiri wa miradi isiyojulikana itakamilika lini.

2. Ubadhirifu na usimamizi mbovu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
Shirika la umeme Tanzania TANESCO limebeba jukumu la kuzalisha, kusambaza na kuuza umeme. Katika nyakati mbalimbali tumekuwa tukishauri Serikali kuliimarisha na kulisimamia ili kukidhi mahitaji ya umma kwenye upatikanaji wa uhakika wa huduma za umeme. Hoja kubwa iliyokuwa ni shirika kuendeshwa kwa madeni na kupelekea kuwa na mtaji hasi.

Tulitoa mapendekezo ya Serikali kuyachukua madeni na kufanya kuwa mtaji wa shirika hilo ili kuongeza uwezo na ufanisi wa kiutendaji. Katika taarifa ya wizara imeonyesha imetekeleza ushauri kwa Serikali kubadili deni la TANESCO la Shilingi trilioni 2.4 kuwa mitaji wa shirika hilo.

Pamoja na kuchukua hatua hii muhimu, bado shirika hili linakabiliwa na hoja za ukaguzi zinazohusiana na ubadhirifu na uzembe katika Usimamizi wa majukumu yake.

Mosi, ongeze la riba kutokana na kuchelewesha kulipa madai ya watoa huduma. Kutokana na TANESCO kuchelewesha kulipa madai imepelekea kutumia nyongeza ya shilingi bilioni 148 (Sh, bilioni 113.84 kwa Panafrican Energy Tanzania na Sh. bilioni 37 wadai wengine).

Pili, mfumo wa mita za umeme kutoonyesha thamani ambayo kila mita imetoa na kuuza umeme. CAG amebaini kuwa kati ya mita 1803 za taarifa za mita 1638(90.8%) hazikuoneshwa katika mfumo wa usomaji mita moja kwa moja kwa mwaka mzima, mita 52 zilikuwa na taarifa za nishati iliyopokelewa pekee na mita 80 zilikuwa na taarifa za usomaji wa nishati iliyosafirishwa pekee. Hali hii imeligeuza kuwa njia inayotumika kusaidia wizi wa nishati ya umeme hasa kwa watumiaji wakubwa.

Tatu, Mita za umeme 874,019 kutothibitishwa na Wakala wa Vipimo. CAG ameonyesha ununuzi uliofanywa na TANESCO ambao haukufuata taratibu za vipimo na uzani. Bidhaa hizi zinathamani ya sh. Bilioni 115 kitendo kinachoweza kusababisha hasa kwa wateja au shirika.

Nne, TANESCO iliidhinishiwa bajeti ya shilingi bilioni 490.5 lakini ikatumia bilioni 594.755 hii ina maana kuwa ilizidisha bilioni 104.2187.
Tano, Tanesco kutofanya ukaguzi wa miradi, CAG ameonyesha kulikuwa na miradi 167 yenye thamani ya shilingi bilioni 39.7 ambayo haikutekelezwa kutokana uzembe wa watendaji wa shirika.

Mwisho, changamoto ya mara kwa mara ya kusimama kwa mitambo ya ya kuzalisha umeme inayosababishwa na uzembe wa kutofanyika kwa matengenezo ya tahadhari ambapo matengenezo huchelewa kati ya siku 2 hadi 243. Hii imesababishwa na kutotekelezwa kwa sera ya matengenezo ya kuzuia hitilafu.
ACT Wazalendo tunataka hatua za uwajibishaji zichukuliwe kwa watendaji wazembe wote katika Shirika ili kuimarisha utendaji na ufanisi wa upatikanaji wa huduma. Pili, hoja zinazohusu ubadhirifu wa fedha za umma Serikali iwachukulie hatua za uwajibikaji na kisheria watu wote walihusika katika ubadhirifu.

3. Utekelezaji wa Miradi ya Bwawa la Kufua umeme la Julius Nyerere na Mradi wa kusindika Gesi Asilia Lindi (LNG)
Nchi yetu ipo kwenye mpango wa kuhakikisha inakuwa na nishati ya uhakika na ghrama nafuu. Hivyo, imekuwa ikiitaja miradi mikubwa miwili kama ndio injini ya kutufikisha kwenye ndoto ya kuwa na uhakika wa uzalishaji wa umeme. Changamoto kuwa za jumla katika miradi hii ni kuchelewa kutekelezwa kwake. Ndio hoja ya muda mrefu tuliyokuwa tunairudia rudia katika mapendekezo yetu. Lakini, kwa hatua kadhaa kila Mradi unachangamoto Mahususi kama tunavyozifafanua hapa chini.
3.1 Mradi wa kusindika Gesi Asilia wa Likong’o Lindi.

Katika hotuba ya bajeti Waziri amelieleza bunge kukamilika kwa mazungumzo na Wawekezaji, ya Mkataba wa Nchi Hodhi (Host Government Agreement-HGA) na Mkataba wa Uzalishaji na Ugawanywaji Mapato (PSA), kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi AsiliA kuwa Kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG) kwa thamani ya dola la Marekani bilioni 42 (Tsh.Trilioni 98.2). Ni wazi kuwa Mradi huu upo mbioni kuanza utekeleza wake kwa hatua za maandalizi (Pre-feeds).

Wakati tunaenda kwenye uwekezaji huu wa mradi mkubwa kuna changamoto ya kuwa na maandalizi madogo ya kuwawezesha wenyeji kushiriki na kufaidika na uwekezaji huu; malalamiko ya wananchi waliohamishwa kwenye ardhi zao kucheleweshewa na kupunjwa kwa fidia; pia, mfumo mbovu wa sera ya fidia ya ardhi kwenye maeneo ya miradi.
Kuhusu suala la fidia kwa wananchi wanaopisha Mradi, yapo malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walikuwa walipwe fidia na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi katika eneo la Mita 300 kutoka barabara kuu ya kwenda Lindi. Manispaa imekalia fidia hii kwa miaka 8 sasa wakati fidia ya TPDC imeshalipwa.

Pia, suala la maandalizi tunaona bado mji wa Lindi haujaandaliwa, vyuo vya ufundi stadi (VETA) kwa miaka yote havijafungamanisha kuandaa mafundi, wataalamu na wasaidizi kuupokea Mradi huu. Serikali inasema itaanza Kujenga Chuo cha wataalamu kuanzia mwezi Agosti na kukamilika mwaka 2024. Yaani kama jambo hili limekuwa la kustukiza vile.
ACT Wazalendo inatoa wito kwa Serikali kuwa na Sera mpya ya fidia kwa wananchi kupisha maeneo ya uwekezaji kama haya kwa kuanza kutumia mfumo wa ardhi kwa uwekezaji (Land for Equity) katika miradi kama hii. Ambapo ardhi ya wananchi itumike kama mtaji katika mradi na hivyo kuzipa Serikali za mitaa za maeneo husika umiliki katika miradi.

Pili, katika mazungumzo yanayoendelea kati ya TPDC, Serikali na Wawekezaji wa Mradi wa LNG ni muhimu suala la Manispaa ya Lindi kumiliki angalau 2.5% ya Mradi mzima lizingatiwe na mchango wa manispaa uwe ni Ardhi yake kama Mtaji.

Tatu, Serikali iwalipe fidia wananchi 51 na wajengewe makazi mbadala maeneo yaliyopimwa na yenye huduma zote za kijamii na vile vile wapewe shughuli mbadala za kiuchumi kama vile ufugaji wa samaki, ufugaji wa kuku, kilimo cha mbogamboga.
3.2 Mradi wa Bwawa la kufua Umeme la Julius Nyerere- Rufiji
Mradi ulianza mwaka 2019 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2022. Mradi huu wenye thamani ya shilingi trilioni 6.5 bado haujakamilika na haujulikani kwa hakika ni lini utakamilika. Hoja kubwa katika Mradi huu ni ucheleweshwaji kukamilika kwa Mradi.

Ambayo inapelekea hatari ya kuongezeka kwa gharama za Mradi kwa uzembe wa Serikali ukadiriaji usio na uhalisia. Pili, ucheleweshaji wa manunuzi ya vifaa vya umeme na mitambo na kusababisha muda mrefu wa kukamilisha mradi na hivyo kuongezeka kwa gharama za mradi. Kuhusu hoja tatu CAG ameeleza kuwa

i. Kutosimamia mchango wa fedha za Wajibu wa kampuni kwa jamii (Corporate Social Responsibility) kwa ufupi huitwa CSR.
CAG ameendelea kuhoji uzembe wa Serikali kushindwa kusimamia utekelezaji wa wajibu wa kampuni kuendeleza jamii - CSR. Kampuni inayotekeleza Mradi huu ilipaswa kutekeleza mpango ulioandaliwa na Serikali wa miradi mbalimbali ya kijamii yenye thamani ya shilingi Bilioni 270. Hadi mwezi Disemba 2022, takribani miaka minne tangu Mradi uanze, mpango huo haujatekelezwa. Huku ni kukiuka makubaliano ya mkataba na kuwanyima wananchi wa Wilaya ya Rufiji na wilaya zinazozungukwa na mradi huu fursa za kimaendeleo. Ipo hatari ya kuzipoteza fedha hizi ikiwa mradi utakamilika bila ya hatua muafaka kuchukuliwa. Waziri Mkamba amesema Serikali itaanza Kujenga Chuo cha Utaalamu wa Nishati na Gesi huko Lindi, ni muhimu uamuzi huu ushirikishe wananchi maana eneo la Mradi linapatikana kwenye Halmasahuri za Rufiji, Kibiti na Kisarawe.

ii. Kuchelewa kukata tozo ya fidia ya ucheleweshwaji wa Mradi.
CAG pia amebainisha ucheleweshwaji wa kukata tozo ya fidia ya kuchelewa kwa Mradi yenye thamani ya shilingi Bilioni 327.9. CAG ameeleza kwamba kitendo cha TANESCO kutotoa tahadhari ya mapema kwa mkandarasi juu ya ucheleweshaji wa mradi na kusababisha kutokutoza tozo au fidia za ucheleweshaji kwa mkandarasi tangu kipindi cha kumaliza mradi kilipopita, yaani tarehe 14 Juni 2022, kimepelekea kupoteza fedha kiasi hicho. Hoja hii inarudiwa kwa mwaka wa pili mfululizo na hakuna hatua zilizochukuliwa.

iii. Ucheleweshaji wa Manunuzi ya vifaa vya Umeme na mitambo na kusababisha muda mrefu wa kukamilisha mradi na hivyo kuongezeka kwa gharama za mradi
Ununuzi wa Mitambo Mikubwa ya kufua umeme pamoja na ile ya kielektro mekaniki na mekaniki vilicheleweshwa kwa miaka miwili kuanzia tarehe ya agizo la ununuzi la tarehe 30 Mei 2020. Hii sawa na miaka miwili kuchelewa baada ya kusainiwa kwa mkataba wa bwawa la Julius Nyerere yaani tarehe 15 Desemba 2018.
ACT Wazalendo inatitaka Serikali iweke wazi na iwashirikishe wananchi kuhusu mpango kutekeleza miradi ya jamii inayotokana na uwekezaji (CSR)

4. Matumizi ya nishati mbadala kwa ajili ya kupika
Serikali imekuwa kwenye mpango wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia (Clean cooking). Nishati safi ya kupikia ni rafiki wa mazingira na afya ya mwanaadamu inakadiriwa kwamba kila mwaka hekari milioni moja ya miti inakatwa kwa matumizi ya kuni na mkaa. Tayari matamko yametolewa yakisisitiza taasisi za umma na binafsi kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31 mwaka 2025.

Mjadala huu unaibuwa uhitaji mkubwa wa nishati mbadala utakaobadilisha utamaduni wa matumizi ya kuni na mkaa uliopo nchini.
Katika kutekeleza hilo tumeona Serikali imetenga Shilingi bilioni 10 kwa ajili kutoa Ruzuku ya mitungi ya gesi na vifaa zaidi 200,000 vijijini. Pamoja nia njema ya Serikali Mradi huu haujibu changamoto za msingi za kwa nini wananchi wanashindwa kumudu na kutumia nishati ya gesi. Changamoto kubwa ni gharama za gesi yenyeyewe unaotokana na kuagiza wakati tunao gesi ya kutosha ndani ya nchi.

Mwaka 2009, Kiongozi wa Chama na kwa wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya hesabu za mashirika ya ummah ndugu Zito Zubeir Kabwe aliiagiza shirika la maendeleo ya petrol nchini ifanye utafiti wa uwezekano wa kuzalisha gesi ya kupikia LPG hapa nchini badala ya kuagiza kutoka nje. Utafiti ule ulionesha kuwa kwa shilingi bilioni 87 tunaweza kuzalisha gesi ya kupikia inayoweza kuhifadhiwa kwenye mitungi ya gesi sisi wenyewe kama Serikali inataka kushiriki kwa ufasaha mapinduzi ya matumizi ya nishati ya kupikia inapaswa kuutekeleza mradi huu ili tuwe na gesi ya kutosha nchini inayoweza kusambazwa kwa bei nafuu.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali badala ya kuwa afisa masoko wa makampuni ya gesi ijielekeze kwenye wajibu wa kuhakikisha kuwa tunakuwa na miundombinu ya kusambaza gesi asilia iliyopo nchini majumbani.

5. Gharama za kutunza vyura nchini Marekani
Mwaka 2000 Tanzania ilisafirisha vyura 500 kwenda bustani ya wanyama ya Bronx na Toledo iliyopo Marekani ili kuepuka hatari ya kupotea kwa vyura ambayo ilitokana na utekelezaji wa mradi wa umeme wa maji wa Kihansi mnamo mwaka 1994. Ingawa haiwezekani kubainisha idadi kamili ya sasa ya vyura vinavyosimamiwa nchini Marekani, Shirika la Umeme Tanzania linagharamia dola za Marekani 130,000 kwa mwaka kwa ajili ya kutunza vyura hao, ambapo inakadiriwa takribani ya dola za Marekani milioni 2.86 sawa na Tsh. Bilioni 6.7 zilitumika kwa miaka yote 22 ya kuhudumia vyura. Katika mwaka 2020/21 na 2021/22 ilifanya malipo ya shilingi milioni 611.92 (sawa na dola za Marekani 260,000).

ACT Wazalendo tunaitaka serikali iache mara moja kuchezea fedha za Watanzania katika miradi ambayo utekelezaji wake unagharimu uhai wa taifa hili ambalo linaishi kwa mikopo na kuwa ombaomba.T ANESCO inayoendeshwa kwa madeni na mikopo inabebeshwa mzigo ambao ukiwaeleza Watanzania wanashindwa kugharamiwa matibabu yao kwa kukosekana fedha, wanashindwa kuunganishiwa umeme bure au kwa bei nafuu kwa kukosekana fedha na kuwa kutunza vyura hawa ni bora kuliko huduma hizo muhimu watabaini kuwa serikali yao inawadharau kwa kiwango kikubwa.

6. Udhaifu wa kiutendaji wa Shirika la maendeleo ya petrol nchini TPDC unaligharimu taifa
TPDC imekuwa ikiendeshwa katika namna ambayo inagharimu taifa letu mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali amebainisha mapungufu mengi ya kiutendaji katika shirika letu la maendeleo ya petroli katika maeneo anuai kama nitakavyoa ainisha hapa chini
i. TPDC inaiuzia TANESCO gesi kwa gharama kubwa kuliko makampuni binafsi yanayouza gesi na hivyo kuongeza gharama za umeme kwa wananchi.

Mnamo tarehe 17 Januari 2019, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji iliandika barua yenye kumbukumbu namba: EWURA/60/TR.1/16/2/019/Vol III/51 kwenda Wizara ya Nishati ikirejea ripoti ya utafiti wa gharama za Shirika la Umeme Tanzania ambayo ilipendekeza mambo mawili ili kupunguza bei ya gesi, na kufanya bei ya umeme kuwa nafuu kwa Watanzania. Pendekezo la kwanza lilikuwa kubadili mikopo ya Serikali kwa Shirika la Umeme Tanzania kuwa Ruzuku na pendekezo la pili lilikuwa kutekeleza pendekezo la kwanza pamoja kubadilisha mkopo wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania kwenye bomba la gesi kuwa Ruzuku.

Iwapo Serikali itafanyia kazi mapendekezo hayo bei ya gesi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania inaweza kupunguzwa kutoka dola za Marekani 5.19 kwa mmBTU hadi 4.359 kwa mmBTU ambayo itapunguza gharama ya kuzalisha umeme kwa Shirika la Umeme Tanzania. Ukaguzi wa CAG wa Mikataba ya mauziano ya gesi pamoja na ankara za madai ya kila mwezi ulibaini kwamba bei iliyotozwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania bado ni kubwa ikilinganishwa na wauzaji wengine wa gesi kama vile kampuni ya PAET licha ya mapendekezo yaliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji mwaka 2019.

Serikali isimamie TPDC ili ikiwezekana yenyewe ndiyo iwe na mauzo ya chini kuliko makampuni mengine. Haitokuwa na mantiki kwa wananchi kuongezewa gharama ya umeme kwa kuwa tu inauzwa na shirika ambalo limeanzishwa na kuendeshwa na kodi zao.

Jambo hili linatufanya tuhoji umakini wa waziri mwenye dhamana kusimamia mashirika haya kwa maslahi ya taifa lakini ni kwa nini tusione kuwa hii ni hujuma kwa shirika la umma ambapo likiingia kwenye ushindani litashindwa kwa sababu ya kuwa na bei kubwa huku mashirika binafsi yakiimarika.

ii TPDC imetekeleza mradi wa kutumia gesi katika mradi wa mabasi yaendayo kasi bila ya kuwapo mkataba kati yake na kampuni ya UDART.

Mwaka wa 2018/19 Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania lilianza mazungumzo na Wakala wa mabasi yaendayo kasi Dar-es-salaam kwa ajili ya ujenzi wa kituo maalumu cha kuuzia gesi katika eneo la Ubungo baada ya kupata vyeti vya tathmini ya athari za Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira. Pamoja na mipango mizuri hapakuwepo na makubaliano ya kisheria kati ya pande hizo juu ya ujenzi wa kituo hicho. Hivyo mnamo tarehe 30 Desemba 2021 ulifanyika mkutano wa pande mbili ambapo Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka walitangaza kujiondoa wakieleza sababu kuwa wameishaingia mkataba wa miaka 12 na kituo cha usambazaji wa mafuta (Diseli) kwa mabasi ya mwendo kasi, hivyo mradi ulisita kuendelea.

Huu ni uzembe usiotarajiwa kufanywa na shirika la umma kama TPDC. Tunaishauri Serikali kuingilia kati jambo hili ili kuunusuru mradi kwa kuzikutanisha pande zote mbili.

iii) Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania kutoweka udhibiti katika uhakiki wa gesi kutoka rasi ya Mnazi
CAG alitembelea mtambo wa kuchakata gesi wa rasi ya Mnazi na kubaini kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania halikuweka udhibiti kwa kufunga mita yake kwa ajili ya kusoma kiasi cha gesi iliyonunuliwa kutoka kampuni ya Maurel na Prom. Aidha Shirika kama mnunuzi linategemea mita za muuzaji ili kuweza kupima gesi inayonunuliwa na shirika.
Pia, Sheria ya wakala wa vipimo (WMA), inahitaji ukaguzi kufanyika kila robo mwaka, nilibaini mita za Maurel na Prom (M&P) mara ya mwisho kukaguliwa ilikuwa Machi 2021 hadi wakati wa ukaguzi (Agosti 2022) hakuna ukaguzi uliofanyika.

Kukosekana kwa mita na mita iliyopo kutokaguliwa kunaweza kusababisha hasara ya mapato kwa wateja kupewa ankara pungufu na kwa pande wa ununuzi wa gesi kuna hatari kupewa ankara zaidi ya kiasi kilichopokelelewa.

ACT Wazalendo ina maoni yetu ni kuwa makosa haya ni mwanya wa ubadhirifu na hivyo haraka TPDC iweke mita yake
7. Hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme nchini.
Katika zama tulizonazo hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme ya uhakika huchochea ukuaji wa uchumi (Uzalishaji viwandani na mashambani) na utoaji wa huduma zingine kama vile elimu, mawasiliano, usafiri na uchukuzi, matibabu na huduma za utawala. Kwa hiyo, umeme una nafasi na mchango mkubwa sana katika maisha yetu kama jamii na nchi kwa ujumla wake.

Pamoja na umuhimu huu tunaona huduma ya umeme nchini bado sio ya uhakika kumekuwa na changamoto ya muda mrefu ya kukatika kwa umeme mara kwa mara. Kwa hali hii ni wazi kuwa kutosimamiwa vyema huduma ya upatikanaji wa umeme unarudisha nyuma uwekezaji mkubwa kwenye viwanda, kuzoretesha mifumo mingine ya huduma kama vile matibabu, uchukuzi na mawasiliano na masuala ya utawala.

Mwenendo wa uwezo wetu wa kuzalisha umeme kwa mujibu wa taarifa za wizara kutoka kwenye hotuba ni kuwa, ongezeko la uzalishaji wa umeme nchini kwa mwaka 2021/22 ni megawati 124.92 ni sawa na asilimia 7.94 kwa kulinganisha na uzalishaji wa mwaka uliopita ambao ulikuwa na jumla MW 1608.46 wakati uzalishaji wa sasa ni 1,733.38. Wakati, mahitaji ya juu ya umeme katika mfumo wa Gridi ya Taifa yameongezeka na kufikia MW 1,335.01 ikilinganishwa na MW1,201.02 zilizokuwa zimefikiwa mwaka 2020/21, sawa na ongezeko la asilimia 11.16.

Aidha, ongezeka la watumiaji kutokana na usambazaji wa umeme vijijini linakuwa kwa asilimia 13.54. Ni dhahiri kuwa kasi ya uzalishaji na usambazaji haulingani, jambo linalopelekea kuwa na upungufu wa uwezo wa kuhudumia wananchi, hivyo changamoto za kukatika kwa umeme mara kwa mara hutokea,

Kila mwaka ifikapo Mwezi Oktoba mpaka Disemba, nchi yetu hulazimika kuzima mitambo yake ya umeme wa kutumia maji kwa takribani mwezi mzima kwa kuwa wastani wa maji ya uzalishaji unakuwa chini ya kiwango kinachotakiwa kusukuma mitambo. Katika kipindi hicho, mitambo ya umeme wa maji ambayo huweza kuzalisha hadi megawati 561, hushuka na kuzalisha mpaka megawati 110 pekee, kwa mujibu wa TANESCO.
Hali hii inatokea katika wakati ambao nchi yetu imeshafanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya gesi asilia.

Taifa letu linaweza kuepuka changamoto ya kutokuwa na umeme wa uhakika kwa kuitumia vema fursa ya gesi asilia tuliyonayo.

8. Gharama za kuunganisha umeme zinapaswa kuwa jukumu la serikali.
Katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021 Serikali ilipunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi wa mijini kufikia shilingi 27,000. Hatua hii ilipokelewa kwa furaha na wananchi walijitokeza kwa wingi ili kupata huduma hii muhimu. Katika mwaka wa bajeti 2021/2022 Serikali ilizirejesha gharama za awali za kuunganisha umeme kwa kile kilichoelezwa kuwa ni gharama halisi ya kuunganisha umeme. Hatua hii iliyoleta maumivu kwa wananchi ni matokeo ya Serikali kukimbia wajibu wake wa kutoa huduma muhimu kwa umma.

Hatua ya Serikali kuunda kamati ya kufanya tathmini ya maeneo yenye sifa za vijijini kwa maeneo ya mijini ili kufanya gharama ya umeme kushuka ni kupoteza rasilimali bure. Serikali itekeleze wajibu wake huo.

Hivi sasa kuna mkanganyiko mkubwa ambapo baadhi ya maeneo kama vile Skonge mkoani Tabora kata moja inagawanywa baadhi ya mitaa kuitwa mjini na mingine vijijini. Serikali ijifunze kwa matokeo ya ongezeko la watu walioomba kuunganishiwa umeme bei ilipokuwa shilingi 27,000 na upungufu wa maombi baada ya bei kupandisha.
Maamuzi haya ya Serikali yana akisi kuwa, Serikali inapopata shida ya kiuchumi inaona njia ni kumkandamiza mwananchi.

Hitimisho.
Bajeti ni nyenzo muhimu sana katika kupima vipaumbele vya matumizi ya fedha za umma katika kukabiliana na changamoto za wananchi na upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi. Katika kutazama bajeti ya mwaka huu ya Wizara ya Nishati trilioni 3.01 inaweza kuonekana ni bajeti kubwa Lakini uhalisia wa gharama za miradi katika sekta ya nishati ni dhahiri kwamba bado ni tone dogo sana. Pia, ni muhimu kwa Serikali kuboresha utekelezaji wa bajeti kwa kuhakikisha inatoa fedha zilizotengwa kwa wakati ili kuepusha kulipa gharama za ziada kwa wakandarasi na watoa huduma wengine. Aidha, utendaji wa TANESCO unapaswa kutazamwa upya na kuimarishwa. Ni wakati sasa wa kumaliza mazungumzo na wawekezaji wa Mradi wa Gesi Asilia Lindi, ili kulihakikishia taifa uhakika wa nishati na uendelevu wake.

Ahsanteni sana.

Ndg. Is-haka Mchinjita
Waziri Kivuli wa Nishati
ACT Wazalendo
01 Juni, 20223
 
Back
Top Bottom