Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
Wajitia kukataa, huna lolote wataka,
Yanini inuka kaa, na jasho kukumwaika?
Sasa wachuchumaa, kama tipa wabinuka,
Zina nitia wazimu, hizo sitaki nataka.
Fahamu nimeshapika, mezani nimeandaa
Qadar zake Rabuka, kila kitu kina njaa,
Tule tupate ridhika, sima isiyo budaa,
Zina nitia wazimu, hizo sitaki nataka.
Pomoja tuzime taa, ya huko tulipotoka,
Tuwashe na mshumaa, wa hapa tulipofika,
Leo ipate kung'aa, na kesho kuimulika,
Zina nitia wazimu, hizo sitaki nataka.
Nilitafuta shufaa, ya moyo unoripuka
Nikapiga na rakaa, nipate wa kuchunuka,
Hichi si bure kichaa, nipe dawa muibaka.
Zina nitia wazimu, hizo sitaki nataka.
Tupia unalotaka, moyo wangu kwako jaa,
Midhali nimekutaka, mwenyewe bila tamaa,
Wallahi sitakuchoka, nitabeba kila baa,
Zina nitia wazimu, hizo sitaki nataka.
Ninaliwacha jukwaa, kikomo ninakiweka,
Sio mwisho wa sanaa, muwache kusikitika,
Nikiupata wasaa, jengine nitaandika,
Zina nitia wazimu, hizo sitaki nataka.
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Call/whatspp 0622845394 Morogoro.