Hizi ni fedha za Umma

Kitaja

JF-Expert Member
Jun 14, 2011
2,836
1,382
SHAIRI: HIZI NI FEDHA ZA UMMA
1. Wakubwa wapongezana, kwa vicheko na kwa dansi,
Mafungu wamegawana, lumbesa na sandarusi,
Pongezi wamepeana, ahojiye wametusi,
Hizi ni fedha za umma,ni lazima zirejeshwe.

2. Mwasema sio za umma,benki kuu ni ya nani?
Wachunguzi wamesema,kigugumizi cha nini?
Hata epa mulisema, leo tena kuna nini?
Hizi ni fedha za umma, ni lazima zirejeshwe.

3. Eti mchango wa shule, bilioni kibindoni,
Msiokuwa na shule, maboksi hayo bebeni,
Mliotangulia mbele, gunia zima bebeni,
Hizi ni fedha za umma, ni lazima zirejeshwe.

4. Taifa linjia panda, hosipitali kiama,
Bajeti imeshapinda, wafadhili wamegoma,
Hofu imekwishatanda, miradi imesimama,
Hizi ni fedha za umma, ni lazima zirejeshwe.

5. Wazalendo itikeni, himahima amkeni,
Kwa pamoja simameni, nchi yetu teteeni,
Tuwatie matatani, mafisadi wasosoni,
Hizi ni fedha za umma, ni lazima zirejeshwe.


By Kitaja wa JF.
 
Kitaja nimeelewa,unachotaka kusema
Wengine walibebewa,wao wakibaki nyuma
Wakaanza kutetewa, na kuonewa huruma
Ni fedha za umma

Hakika inauma, kwa sisi walipakodi
Pesa zetu tunachuma,kwa vitendo na ahadi
Halafu twaachwa nyuma,mgao wa makusudi
Ni fedha za umma
 
Back
Top Bottom