Hili la kodi, tujihadhari na chachu ya wapotoshaji

Ngaliwe

Senior Member
Dec 30, 2015
161
364
BWANA Yesu katika moja ya mafundisho yake, aliwaambia wanafunzi wake kujilinda na upotoshaji wa mafundisho na maneno ya aina ya watu ambao wao hakuna kitu wanafanya kwa ajili ya jamii hiyo isipokuwa kila kitu wanachosema ni kwa ajili ya manufaa yao binafsi au kushindana na kupingana na watu walio kinyume chao bila kujali sana kile wanachokisema kina athari gani kwa jamii husika.

“Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaonyeshe ishara itokayo mbinguni. Akajibu, akawaambia, [Kukiwa jioni, mwasema, Kutakuwa na kianga; kwa maana mbingu ni nyekundu. Na asubuhi, mwasema, Leo kutakuwa na dhoruba; kwa maana mbingu ni nyekundu, tena kumetanda. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa mbingu; lakini, je! Ishara za zamani hizi hamwezi kuzitambua?] Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake. Nao wanafunzi wakaenda hata ng’ambo, wakasahau kuchukua mikate. Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo. Wakabishana wao kwa wao, wakisema, Ni kwa sababu hatukuchukua mikate…..Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.” Mathayo 6: 1-7, 12.

Katika Tanzania ya leo kumejaa mafundisho ya Mafarisayo na Msadukayo wa kisiasa. Hawa ndiyo ambao kila uchao wanaipigia kelele serikali kwa kuhusu haki fulani fulani za huduma kwa raia, wanataka dawa lakini wakati huo huo hawataki serikali itimize wajibu wake katika kuyatekeleza hayo, ilimradi wao kazi ya kubwa ni kutaka kupinga kila kitu kinachofanywa na serikali kwa kuwa kwa kufanya hivyo kunawafanya waishi aina ya maisha wanayoishi, bila kujali kupinga na kupotosha huko kuna athari gani kwa wananchi.

Moja wa wajibu mkubwa wa serikali ni kutoa huduma kwa wananchi wake, za afya, elimu, miundombinu, ulinzi na usalama wa raia wake kwa kutaja machache kati ya mengi. Serikali katika hili haiwezi kutimiza wajibu huo bila kukusanya kodi kutoka kwa raia, ndiyo maana ni wajibu wa serikali kuweka mfumo rafiki wa utozaji wa kodi ambao pia siyo kero kwa wananchi.

Wanaharakati wetu ambao wamejipambanua kuwa kinyume na serikali kwa kila kitu wamekuwa mstari wa mbele kuishambulia serikali kwamba inategemea vyanzo vya kodi vile vile mwaka hadi mwaka, kwamba haina ubunifu wa kupanua wigo wa kodi ili iweze kukusanywa kwa wingi kukidhi mahitaji yanayoipasa serikali katika kutoa huduma kwa watu wake.

Kwa hakika ukitazama mwenendo wa mfumo wa kodi zetu hapa nchini ulikuwa unaona umuhimu wa kupanua wigo wa kodi ili kwanza kupunguza mzigo wa kodi kwa wananchi wachache hasa wafanyakazi na wafanyabiasahara ambao ndiyo wanabeba mzigo mkubwa wa kodi, lakini pia hoja ilikuwa kwamba kupanuliwe wigo wa kodi ili kuwahusisha wananchi wote kushiriki wajibu wao wa msingi, kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe.

Kwa kulitazama hili ni kweli kwamba kulikuwa na haja ya kupanua wigo wa kodi kwa sababu kwanza ili kuwashirikisha wananchi katika wajibu na jukumu lao la msingi kabisa katika ujenzi wa taifa lakini muhimu sana kuipa uwezo serikali kutimiza wajibu wake wa kuhudumia wananchi kikamilifu.

Kwa nia njema kabisa na kwa kuonyesha ilivyo sikivu, Serikali ikasikiliza hoja hizo na ikawakalisha wataalamu wake kitako ili kuchakata hili na hatimaye wamekuja na kodi hii ya tozo kwenye mitandao ya simu ambayo kwayo inamhusisha kila mmoja kushiriki katika ujenzi wa taifa lao.

Kelele zimeanaza tena, serikali inalaumiwa kwa kutimiza wajibu wake, hawa ni aina ya watu ambao Maandiko Matakatifu yanawaweka kwenye kundi la wanafiki, yaani jamii za Mafarisayo na Masadukayo ambao wamesimama kwenye miimo ya milango ya Ufalme wa Mbinguni lakini wao wenyewe hawaingii lakini wanawazuia watu wengine wenye nia ya kuingia.

Watu hawa wanataka serikali itoze kodi kutoka kwa nani? Kilio kwamba kuna kundi dogo tu la wananachi wanaobebeshwa wigo wa kodi umepanuliwa unamhusisha kila mwananchi, wameanza ushawishi wa kuichonganisha serikali na wananchi, wanataka kodi itozwe kwa nani? Nani hasa mwenye wajibu wa kulipa kodi katika taifa kuliko mwingine? Tukiutazama ukweli halisi kama alivyoeleza Rais Samia Suluhu Hassan, kodi itarekebishwa viwango lakini itendelea kutozwa, ndiyo hasa msingi wa wajibu wa wananchi kwa taifa lao.

Lakini kulikuwa na kilio kikubwa kuhusu mbinu za ukusanyaji wa kodi na namna ya kuzifanya rafiki, serikali ikasikiliza ikaitazama kodi ya majengo ambayo imekuwa kwa miaka kadhaa lakini haikuwa inakusanywa kikamilifu, imekuja na ubunifu mzuri kabisa wa kukusanya kodi hii ambao hauna usumbufu kwa serikali na kwa wananachi, lakini ambao unahakikisha ukusanyaji wenye tija wa kodi hii. Kama kawaida Mafarisayo na Masadukayo wetu wa kisiasa wameanza kelele na kejeli kuhusu mfumo huu. Hata baada ya Mamlaka ya Mapato kufafanua aina ya nyumba ambazo hazitatozwa kodi hii na msamaha kwa nyumba za wazee wanaostahili kusamehewa kodi hii, bado wameendelea kufanya uhasidi wao, eti wanahoji Luku itatambuaje nyumba hizo, hili ni swali kweli la kuhoji kuhusu utambuzi wa nyumba kwenye zama hizi za Sayansi na Teknolojia?

Watanzania tunao wajibu wa kulijenga taifa letu, Tanzania itajengwa na watanzania wote kwa umoja wao, wajibu na kazi ya ujenzi wa Taifa siyo lelemama, ni kazi kubwa ya jasho na inahitaji bidii kubwa bila kuchoka. Kama tunalalamika deni la serikali kuongezeka, tunadai huduma bora za kijamii hakuna muujiza zaidi ya sisi wenyewe kuutambua wajibu wetu kwa Mama Tanzania na kuubeba wajibu huo kikamilifu.

Wanaharakati wanaopinga hizo kodi hawawatakii mema Watanzania wenzao lakini pia hata hatma ya Taifa letu. Huko Ulaya ambako wengi wa wanaharakati wanaopinga kodi hizi wanapahusudu kwa kila kitu, wana mfumo wa kodi ambao unahakikisha kuwa kipato cha raia anachokipata kinakamuliwa vilivyo kiasi kwamba mtu anabakiwa na hela ya kula tu. Lakini husikii wanawalalamikia huko wanapiga porojo za kinafiki hapa kwetu ili tuendelee kudidimia.

Wito kwa kila mwenye mapenzi mema kwa Taifa letu, bila shaka atakuwa mjumbe mzuri kwa jirani rafiki na ndugu yake kwamba Taifa linahitaji nguvu, juhudi na machango wa kila mmoja wetu katika ujenzi wake, na ili tufanikiwe kwenye hili ni lazima tujikinge na mafundisho na chachu za wanaharakati wasiolitakia mema taifa letu na sisi wenyewe kwa kisingizio cha kututetea kumbe wanatetea maslhi yao na mawakala wa uaharibifu waliowatuma kubomoa taifa letu.
 
Habari ya ushawishi wako ndefu mno imechanganya siasa na dini!Umesahau mpe Kaisari yaliyo ya Kaisari,na mpe Mungu yaliyo ya Mungu.
 
Kama kanisani kwako kuna waumini kama wewe basi kamwe siwezi kuja kujumuika na kondoo kama wewe.
 
Mbona amenena vyema. Tulipe kodi kila mtu na alipe kodi tutazoea tuu
 
Back
Top Bottom