Hii ndio sababu kuu vita haitakuja kuisha Palestina vs Israeli

george aloyce

JF-Expert Member
Aug 22, 2017
1,177
1,822
MGOGORO PALESTINA, ISRAEL: UTAKATIFU JERUSALEM KIKWAZO CHA AMANI

KISIASA na kihistoria kwa marejeo ya miaka 500 hadi milenia moja iliyopita, Israel ni wavamizi, waliingia kwenye miliki ya Palestina na kuunda taifa lao ndani ya ardhi ya Wapalestina.

Miaka 76 iliyopita (mwaka 1947), hakukuwa na nchi inayoitwa Israel. Mei 14, 1948, Kiongozi wa Mamlaka ya Kiyahuudi, David Ben-Gurion, aliitangaza Israel kuwa dola huru na kamili.

Ben-Gurion, katika azimio lake la uhuru, alitangaza kuwa kuanzishwa kwa dola ya Israel ni ufunguo wa milango kwa kila Myahahudi popote alipo uhamishoni, kurejea nyumbani kwao.

Aliyekuwa Rais wa Marekani, Harry Truman, haraka sana alitangaza kuitambua dola ya Israel. Yalikuwa mafanikio makubwa ya Wayahudi, yaliyoanza kupitia harakati za uhamaji wa Aliyah miaka takriban 150 iliyopita.

Tafsiri ya Aliyah ni uhamaji wa Wayahudi kutoka uhamishoni na kurejea kwenye ardhi yao ya kihistoria, kijiografia na hatima yao. Ardhi hiyo ni Palestina. Aliyah ya kwanza ilikuwa mwaka 1882 – 1903, ingawa rekodi zinaonesha kuwa Wayahudi walianza kuweka maskani Palestina mwaka 1878.

Historia haiwezi kusomeka vizuri kama haigusi mateso ya Wayahudi Ulaya. Watawala wengi barani Ulaya waliyafanya maisha ya Wayahudi kujaa mateso. Wayahudi walihitaji mahali salama, wapaite nyumbani.

Mathalan, Aliyah ya kwanza chanzo chake ni Urusi. Wayahudi waliona mateso makali Urusi chini ya utawala wa Alexander III. Aliyah ya pili, mwaka 1904 – 1914, ni matokeo ya Wayahudi kukwepa chuki dhidi yao Ulaya. Vilevile mlipuko wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, ulichochea mashambulizi dhidi ya Wayahudi Ulaya.

Aliyah ya tatu, mwaka 1919 – 1923, ilichagizwa na matumaini makubwa ya Wayahudi baada ya Azimio la Balfour. Novemba 2, 1917, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa UK, Arthur Balfour, alimwandikia Kiongozi wa Wayahudi wa UK, Walter Rothschild, kuhusu mpango wa UK, kuunga mkono kuanzishwa kwa taifa la Israel ndani ya Palestina.

Azimio la Balfour, liliwasha taa ya kijani kwa Wayahudi. Wimbi kubwa lilihamia Palestina kwa matumaini ya kujenga taifa lao. Aliyah ya nne mwaka 1924 – 1928, ilisababishwa na mateso ya kiuchumi ya Wayahudi Poland. Waliwekewa ugumu wa kuishi, wakatozwa viwango vikubwa vya kodi. Wayahudi wakatafsiri “akufukuzaye” hakwambii toka.

Aliyah ya tano 1929 – 1939, ilianza na sababu za kiuchumi, halafu Adolf Hitler alipoibuka Ujerumani, mamia elfu ya Wayahudi walikimbia kukwepa sera za Nazi. Wayahudi wengi waliuawa. Vita ya Pili vya Dunia ilipoanza mwaka 1938, iliongeza hatari kwa Wayahudi ambao walikimbilia Palestina na Yemen.

NJIAPANDA JERUSALEM

Vita ya Palestina mwaka 1947 – 1949 ni sehemu muhimu ya mgogoro wa Mashariki ya Kati, sio tu Palestina na Wayahudi, bali pia jumuiya ya Waarabu dhidi ya Israel.

Vita ilipokwisha, Israel ilibaki na kipande chake, Jordan walichukua West Bank, Misri walimiliki Ukanda wa Gaza. Palestina ikagawanywa mara tatu.

Mwaka 1967, Israel ilifanya mashambulizi ya kushitukiza, ikafanikiwa kuzipiga Misri, Jordan na Syria, ikatwaa West Bank na Gaza, Palestina, Peninsula ya Sinai, Misri na Golan, Syria.

Mgawanyo wa ramani ya mwaka 1967, ulibakisha Ukanda wa Gaza na West Bank kuwa maeneo pekee ya Palestina, ukiacha Israel ikiwa na eneo kubwa. Kutoka Gaza hadi West Bank, lazima kwanza upite Israel. Hata hivyo, hilo sio tatizo sugu.

Vyama vikuu vya siasa Palestina, Fatah na Hamas, vyote malengo yake ni kuunda taifa la Palestina kwa kuheshimu ramani ya mwaka 1967. Japokuwa Hamas hawatambui uwepo wa Israel, Fatah wanaitambua, shabaha zao zinafanana kuelekea kuunda dola huru ya Palestina.

Mfupa mgumu wa mgogoro wa Israel na Palestina ni mji wa Jerusalem. Hakuna upande unakubali kuuacha. Sababu kubwa ni imani inayokutanisha dini tatu; Uislam, Uyahudi na Ukristo.

Wayahudi huamini Myahudi wa kwanza ni Ibrahim, kupitia matembezi yake Nchi ya Ahadi, Karne 1800 Kabla ya Kristo. Eneo ambalo Ibrahim alikaribia kumtoa sadaka mwanaye Isaka, ndio Jerusalem.

Wana wa Israel waliporejea Nchi ya Ahadi baada ya kukombolewa na Musa Misri, Mfalme wa Tatu wa Waisrael, Daud, aliufanya Jerusalem kuwa Mji Mkuu. Halafu, mtoto wa Daud, Mfalme Suleiman, alijenga Hekalu Takatifu na kulifanya kuwa kitovu cha ibada za Wayahudi.

Wana wa Israel walihiji mara tatu kwa mwaka kwenye Hekalu hilo. Walioshindwa kufika hekaluni, walipaswa kufanya ibada kwa kuelekeza nyuso zao usawa wa Jerusalem.

Kwa kutii masharti hayo, mahekalu (synagogues) ya Wayahudi, yalijengwa kwa wingi kwa uelekeo wa Jerusalem. Hadi leo, mahekalu ya Wayahudi, popote yanapojengwa, huelekezwa Jerusalem.

Wayahudi hawapo tayari kuacha Jerusalem itwaliwe na Palestina kwa sababu ni mji wao mtakatifu. Ni sehemu yao ya hija. Wanaita ardhi ya baba yao wa kwanza, Ibrahim. Usahihi wa wao kuimiliki Jerusalem wanaamini ni maandiko ya Musa, Torati na Daud, Zaburi.

Wakristo, Yesu alizaliwa Bethlehem, alikulia Nazareth. Pamoja na hivyo, Jerusalem ina historia na utukufu wa kipekee kwa sababu ndipo Yesu alifundisha, akala chakula cha jioni kwa mara ya mwisho, akakamatwa, akahukumiwa, akatembezwa kwa mateso hadi Golgotha (Calvary), alikowambwa msalabani.

Yesu alizikwa Jerusalem na siku tatu baadaye, kaburi lake lilikutwa tupu. Yesu aliwatokea mashuhuda wa kaburi lake Jerusalem, kisha alipaa kwenda mbinguni. Kuna Kanisa la Ufufuo (Church of Holy Sepulchre), lililopo Jerusalem. Nalo ni sehemu muhimu ya Ukristo.

Utamaduni wa kiimani kwa Wakristo kwenda kuhiji Jerusalem, hutembea Via Dolorosa – Njia ya Simanzi, na vituo vyake 14 hadi Golgotha, kufuata nyayo za Yesu. Pamoja na kuwepo ubishani wa madhehebu wa Kikristo kuhusu Via Dolorosa, kutoka Wakatoliki hadi Waorthodox, ukweli unabaki huu, Jerusalem ni historia ya Wakristo.

Waislam, wanauita Jerusalem ni mji mtakatifu. Zaidi, Jerusalem ni uthibitisho wa juu kuwa Uislam ulikuwepo kabla ya Mtume Muhammad (S.A.W). Awali, uelekeo wa sala kwa Waislam (qibla), ulikuwa Jerusalem. Baadaye, qibla ikawa Ka’ba, Makkah. Ushahidi ni Quran, Sura Baqara (sura ya pili), aya ya 142 mpaka 152.

Jerusalem kuna Msikiti wa Aqsa ambao ni nyumba ya tatu kwa utakatifu, baada ya Makkah na Madina. Miraj ni safari ya Mtume Muhammad, iliyoanzia Msikiti wa Makkah, kituo cha pili kilikuwa Msikiti wa Aqsa, Jerusalem. Kisha, Muhammad akiwa na Malaika Jibril, walipaa hadi mbingu ya saba kutokea Aqsa.

Lengo la Miraj lilikuwa kumdhihirishia Muhammad uwepo wa Mungu. Kumwonesha ukweli wa mafundisho aliyohubiri, ikiwemo uwepo wa pepo na moto. Muhammad aliongoza sala ya mitume akiwa Aqsa.

Jerusalem kwa Waislam ndio palipo na historia ya Nabii Ibrahim. Mtume mwenye hadhi kubwa kwenye Uislam. Ndipo Ibrahim alitaka kumchinja mwanaye wa uzeeni, Ismail, kutimiza amri ya Mungu, lakini alipewa kondoo kama mbadala. Ni sababu Waislam ni suna kuchinja sikukuu ya Eid al Adha, kumwenzi Ibrahim.

Yesu, ndio Nabii Issa (A.S) kwa Waislam. Alama zake ni muhimu kwao. Mwanazuoni Al Ghazal, ni sehemu ya historia ya Usilam, alikuwa mkazi wa Jerusalem. Kwa kifupi, Jerusalem ni mji wa kiimani na kiutawala kwa Waislam. Kuanzia milenia ya kwanza na kwa karne 12 baadaye, Jerusalem ilitawaliwa na Waislam.

UHUSIKA WA UK, MAREKANI

Dola ya Ottoman (Uturuki), iliitawala Palestina kwa kipindi kirefu. Ujio wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, uliamsha vuguvugu za Waarabu dhidi ya Ottoman. UK, walikuwa wachochezi wakuu wa vuguvugu ili kuiangusha Dola ya Ottoman kwa ahadi ya kuwawezesha kupata uhuru.

UK ilifanya makubaliano na Sharifu wa Makkah, Saudi Arabia, katika mfululizo wa mazungumzo ya barua yaliyoitwa McMahon-Hussein Correspondence, kuhusu kuwaondoa Ottoman. Wakati huohuo, UK ilisaini na Ufaransa Mkataba wa Sykes-Picot, uliohusu kugawanya mara mbili miliki zote chini ya Ottoman.

Waarabu walipigana vita ya matumaini ya kupata uhuru. Baada ya kuishinda Ottoman, UK na Ufaransa waligawana nchi. Mwaka 1917, UK waliwachanganya zaidi Waarabu kupitia Azimio la Balfour. Halafu mwaka 1920, UK walianzisha Mamlaka ya Palestina.

UK, waliandika Azimio la Balfour, Waziri Mkuu alikuwa David George. Msimamo wa UK kuwasaidia Wayahudi ulikuwa na unyoofu mpaka mwaka 1945, alipoingia madarakani, Waziri Mkuu, Clement Attlee. Kipindi cha Attlee, alitaka kufanya mabadiliko ya Azimio la Balfour, lakini alichelewa. Tayari Wayahudi walishajizatiti na waliungwa mkono na Marekani.

Rais wa 32 wa Marekani, Franklin Roosevelt, aliiahidi jumuiya ya Waarabu kuwa taifa la Israel lisingeundwa bila mashauriano na Wapalestina. Roosevelt alipofariki dunia, mrithi wake, Truman, aliunga mkono taifa la Israel pasipo kuzungumza na Wapalestina.

Kwa miaka mingi, Marekani walikwepa kuutambua Jerusalem kama mji wa Israel kutokana na historia yake inavyogonganisha dini tatu. Rais wa 45, Donald Trump, mwaka 2017, aliutambua Jerusalem kama Mji Mkuu wa Israel na akatangaza kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem.

Wazungu, hasa mataifa ya Ulaya, hawakutaka kuishi na Wayahudi. Waliwatesa na waliwaua. Hata hivyo, nchi za Ulaya ndizo zinazoongoza kuitambua dola ya Israel na kuwafanya Wapalestina kuwa watu wasio na dola yao.

MAPIGANO NA HATIMA

Baada ya Israel kuzipiga Misri na Jordan mwaka 1967, iliikalia Palestina jumla. Mwaka 2005, Israel ilijiondoa Gaza, ila bado ipo West Bank. Siasa za Palestina zimegawa miliki hiyo mara mbili, West Bank inaongozwa na Fatah, Gaza ipo chini ya Hamas.

Oktoba 7, 2023, Hamas walifanya mashambulizi ya ghafla kuelekea Israel na kuua watu 1,400. Hamas waliweza kuizidi ujanja mitambo ya ulinzi ya Iron Dome, Israel, ambayo hudhibiti majiji ya Tel Aviv na Jerusalem kushambuliwa. Israel walijibu mapigo na kuua Wapalestina zaidi 3,478. Hii ni ripoti ya Al Jazeera, Alhamisi (Oktoba 19, 2023).

Kiongozi wa Kijeshi wa Hamas, Muhammad Deif, alituma ujumbe wa sauti kuelezea uamuzi wa kuishambulia Israel kuwa ni kuendelea kuikalia West Bank, kushikilia maelfu ya Wapalestina na uvamivi wa hivi karibuni wa polisi wa Israel kwenye Msikiti wa Aqsa.

Wapalestina, hasa Gaza, wamezoea ziara za makombora, kuona damu na kubeba maiti. Ni sehemu ya maisha yao kwa sababu ufumbuzi wa kudumu haupatikani. Waisraeli, hasa wa Tel Aviv na Jerusalem, shambulizi la Oktoba 7, lilikuwa jipya. Hawajazoea.

Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ilitoa hukumu mwaka 2004, ilitambulisha West Bank, ikiwemo Jerusalem Mashariki na Ukanda wa Gaza, kuwa maeneo ya Palestina. Hilo ni gumu kwa Israel kukubali. Jerusalem Mashariki ndipo palipo na Hekalu Takatifu. Wayahudi hawapo tayari eneo lao la ibada takatifu liwe chini ya Wapalestina.

Wapalestina wanapigania ardhi yao na wanaungwa mkono na nchi nyingi za Kiarabu. Mathalan Msikiti wa Aqsa unahudumiwa na Jordan kupitia Wakf wa Jerusalem. Wapalestina na jumuiya ya Waarabu, hawapo tayari kuona maeneo yao matakatifu yakikaliwa na Wayahudi.
1697795586601.jpg
 
mnacopy wapi haya mambo,hii ni nakala ya pili kwa watu wawili tofaut naona mnaleta kuna mdau mwingine ameshacopy na sehem amekuja kipaste humu na ww naona umeileta vile vile

Sent from my SM-J337W using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom