Mikoba inashughuli nyingi; usione imebebwa tu... Ooh!
Kwa mfano kwa kina mama ukiacha vitu muhimu kama vile Khanga, pamoja na zile kinga zao za mzunguko wa kila mwezi, utakuta pia kuna uturi, podari, sare za kazini... Wapo wanaobeba kwa nia njema kama vile viji zawadi vya watoto wakati wakitoka kazini au matembezini.... Usishangae kukuta ndani ya mkoba kumefichwa visheti, kaimati, sikirimu au ramba ramba na bagia.... Ukipekua sana utakuta tooth pick... vipande vya toilet paper na wakati mwingine hubeba biashara ndogondogo za kuuziana maofisini.
Wale wanaobeba vipodozi hawa wako wengi tu na ikifika wakati utashangaa kwani hata kama yuko ofisini hujisahau kabisa akidhani yuko chumbani kwake jinsi anavyojiremba na na kujipodoa inafurahisha anapokosa kioo cha kujiangalia utamuona akitumia kompyuta bila shaka... au atakuuliza vipi XP nipo poa eeh!?
Kuna mshairi mmoja ameandika haya:
Mkoba wa mkononi, kwa kina mama hadaa
ukimuona njiani, mbwembwezake ni balaa
Akiufungua ndani, wallahi utashangaa
Wale wendao kazini, yanini kuuchukua
Nauli imkononi, imevunyangwa sawia
Mkoba wa kazigani, mahangasha kujitia
Akijapita mahali, alivyoukumbatia
Utadhani muna mali, aogopa kuibiwa
Kumbe muna miambili, na wanja kujipodoa
Harusini kiwaona, kilamtu pekepeke
Ni aina kwa aina, kwa kila mtu na wake
Aringa na kujiona, ati ni mzuri wake
Ata kama ana begi, safari akimbilia
Na huku ana mashungi, mwilini yaning'inia
Ni lazima handbegi, nayo kijipachikia
Hebu siri nambieni, enyi mnaoibeba
Mikoba ya mkononi, kwa nini mna mahaba
Ijapo mwendasokoni,kununua ngogo miba
Ukweli nielezeni, wala msifiche kitu
Mkoba wa mkononi, ni lazima kila mtu
Uutundike kwapani, japo ndani hakuna kitu
Tamati sasa naona, Kalamu naweka chini
Kina mama wasichana,na mtie akilini
Kama hakuna la maana, mkoba wacha nyumbani.