Haya ndiyo mabadiliko 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
3,575
13,261
KATIBA YA KUDUMU YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA 1977

Katiba hii iliitwa Katiba ya Kudumu na ilikuwa ni Katiba ya tatu ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania. Katiba hii ilipatikana kupitia Tume ya Rais iliyokuwa na wajumbe 20 (10 toka kila upande wa Muungano) ikiongozwa na Sheikh Thabit Kombo na Katibu wake akiwa Ndugu Pius Msekwa. Tume hii ilianza na kazi ya kutunga Katiba ya CCM ambayo ilizaliwa baada ya kuunganisha vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP) tarehe 5 Februari, 1977.

Katiba yenyewe ilijikita katika misingi mikuu mitatu ambayo ni Urais wa kifalme, mfumo wa chama kimoja cha siasa na muundo wa serikali mbili. Katiba hii ilipitishwa na bunge maalum lililoteuliwa na Rais kutokana na bunge la kawaida. Katiba hii ilipitishwa ndani ya masaa matatu tu. Kwa ujumla Katiba ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko mara 6 14 tangu ilipopatikana. Watu wengi wamezungumzia marekebisho hayo mengi kama ni “viraka”.

Hata hivyo mengi ya mabadiliko hayo yamewakwepa wananchi isipokuwa yale ya 1983-1984 ambayo angalau yaliwashirikisha wananchi kwa kiasi fulani. Katika marekebisho hayo, NEC ilianzisha mjadala wa wananchi uliodumu kwa mwaka mmoja badala ya kufanya maamuzi yenyewe. Baada ya hapo, chama kiliiagiza serikali kutekeleza yaliyotokana na maoni ya wananchi. Baadhi ya mapendekezo ya wananchi yalipelekea kuingizwa kwa tamko la haki za binadamu.

Pia, mapendekezo kadhaa yaligusia maswala ya Zanzibar na uhuru wake ambayo yote hayakuwa sehemu ya mapendekezo ya chama. Mwaka 1991 Rais Ali Hassan Mwinyi aliteua Tume ya kuangalia mfumo bora wa siasa nchini ikiongozwa na Marehemu Jaji Mkuu Francis Nyalali. Tume hiyo ilifanya kazi nzuri sana ikisafiri nchi nzima kukusanya maoni ya wananchi. Kutokana na kazi yake Tume ilipendekeza mambo kadhaa ikiwemo haja ya kufutwa kwa sheria 40 kandamizi. Aidha, Tume ilipendekeza kuzifanyia mabadiliko makubwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar.

Mengi ya mapendekezo ya Tume hii hayakukubaliwa na Serikali isipokuwa pendekezo kuu la kuachana na mfumo wa utawala wa chama kimoja cha siasa kwenda kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa. Kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapo Julai, 1992 kulifanyika bila mabadiliko makubwa ya Katiba. Hivyo, Katiba ile ile ya Chama Kimoja ililazimishwa kwa kuwekewa “viraka” na “mapengo” kuubeba mfumo mpya wa siasa. Matatizo ya uamuzi huu wa serikali bado yanaonekana hadi leo. Baadaye kulikuwa na Kamati ya White Paper iliyoongozwa na Jaji Robert Kisanga ya mwaka 1998. Kamati hii ilifanya kazi ya kusifiwa na kukabidhi taarifa yake kwa Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa.

Kwa bahati mbaya, serikali ilitupilia mbali mengi kati ya mapendekezo yake na kuendelea na utaratibu maoni ya serikali. Kuanzia mwaka 1977 hadi sasa Mabadiliko yalifanyika katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ni haya yafuatayo:

(i) Mabadiliko ya Kwanza 1979 Yalikuja miaka miwili tu baada ya kuandikwa kwa Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Jambo kuu katika mabadiliko haya ni kuanzishwa kwa Mahakama ya Rufani inayofanya kazi katika Jamhuri yote ya Muungano.

(ii) Mabadiliko ya Pili 1980 Mabadiliko haya yalikuja kama sehemu ya kujaribu kushughulikia kero mbalimbali za muungano. Lengo lilikuwa kujibu baadhi ya maswali yaliyokuwa yakiibuka toka Zanzibar. Ilitarajiwa kuwa marekebisho haya ya pili ya Katiba yangesaidia kuimarisha muungano jambo ambalo kwa bahati mbaya halikutokea na kupelekea marekebisho mengine mwaka huohuo.

(iii) Mabadiliko ya Tatu 1980 Mabadiliko haya ni ya pili katika mwaka huohuo wa 1980. Kitaaluma, hii huwa ni dalili ya Katiba mbovu. Mabadiliko haya yalikuja kuweka sawa mfumo wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, mfumo wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na muundo wa Baraza la Wawakilishi.

(iv) Mabadiliko ya Nne 1982 Mabadiliko haya yalilenga kuboresha utaratibu wa uteuzi wa wakuu wa mikoa. Hata hivyo, mabadiliko hayo bado yaliendelea kulalamikiwa kwa kutoweka bayana uwajibikaji wa viongozi hao wa mikoa na wilaya.

(v) Mabadiliko ya Tano 1984 Mabadiliko haya yalikuja kufuatia madai ya muda mrefu ya kutaka kuwepo kwa uhuru mpana zaidi pamoja na haki za binadamu katika Katiba. Hatimaye mabadiliko haya yaliingiza tamko la haki za binaadamu kwenye Katiba ya nchi sehemu nzima ya tatu.

(vi) Mabadiliko ya Sita 1990 Mabadiliko haya yalianzisha rasmi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) yakiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 1995. Kabla ya hapo maswala ya uchaguzi yalisimamiwa na chama. Hata hivyo kiu ya wananchi kutaka demokrasia halisi ya uchaguzi haikumalizwa na mabadiliko haya.

(vii) Mabadiliko ya Saba 1990 Katika mwaka huohuo yalikuja mabadiliko ya saba ya Katiba ya Tanzania ambayo yaliweka utaratibu wa kupata mgombea mmoja wa Urais kwa Zanzibar. Mfumo uliotangulia ulikosa uwazi wa namna ya kumpata mgombea wa urais kwa upande wa Zanzibar.

(viii) Mabadiliko ya Nane 1992 Mabadiliko haya yalikuja wakati kukiwa na vuguvugu la mabadiliko kidunia kuelekea demokrasia ya vyama vingi. Mabadiliko ya nane yalifuta rasmi mfumo wa chama kimoja nchini na kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa. Aidha muundo wa bunge la muungano ulibadilika na kuanzisha viti maalumu vya wanawake kufikia asilimia 15 na viti vitano (5) toka Baraza la wawakilishi. Uandikishaji wa vyama vya siasa na uteuzi wa wagombea kupitia vyama vya siasa ulianzishwa na mabadiliko haya. Hata hivyo, nafasi ya wagombea huru au binafsi bado iliendelea kubanwa.

(ix) Mabadiliko ya Tisa 1992 Miezi sita baada ya mabadiliko ya nane, mabadiliko mengine yalifanywa kurekebisha utaratibu wa uchaguzi wa Rais wa Muungano, kutamka kuwa Rais anaweza kuondolewa kwa kura ya bunge kutokuwa na imani naye, kuanzisha nafasi ya Waziri Mkuu kikatiba na namna ya kumwondoa kwa kura ya kutokuwa na imani naye pia. Mabadiliko haya yaliweka masharti magumu kwa Rais kuweza kulivunja bunge.

(x) Mabadiliko ya Kumi 1993 Mabadiliko haya yalikuja kuhamisha chaguzi za madiwani kuweza kufanyika pamoja na uchaguzi wa Rais na Wabunge. Pia, mabadiliko haya yaliipa mamlaka Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) kusimamia chaguzi hizo.

(xi) Mabadiliko ya Kumi na Moja 1994 Mabadiliko haya yalikuja wakati nchi ikijitayarisha kwenda kwenye Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi vya siasa hapa mwaka 1995. Mapendekezo ya mabadiliko haya yalitokana na ushauri wa Tume ya Jaji Mark Bomani ambayo ilipendekeza kuwepo kwa mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano. Mgombea mwenza huyo angekuwa ndiye Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuanzia hapo, Rais wa Zanzibar aliacha kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano lakini alibaki kwenye Baraza la Mawaziri kama mjumbe tu. Hii nayo imelalamikiwa sana na upande wa Zanzibar. Hii ni kwa sababu mabadiliko haya yalibadilisha kabisa msingi wa Muungano kwa kuondoa uhusiano wa moja kwa moja kati ya Serikali ya Jamhuri ya 9 Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vile vile Wazanzibari wengi hawakupenda Raisi waliyemchagua kugeuzwa kuwa waziri tu.

(xii) Mabadiliko ya Kumi na Mbili 1995 Mabadiliko haya yalipitishwa mwishoni mwa mwaka 1995 kabla ya bunge kuvunjwa rasmi na kuruhusu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi. Aidha mabadiliko haya pia yaliweka kiapo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Makamu wake, Waziri Mkuu na Rais wa Zanzibar kula kiapo cha kulinda muungano. Mabadiliko haya pia yaliweka ukomo wa Rais kuwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.

(xiii) Mabadiliko ya Kumi na Tatu 2000 Mabadiliko haya yalikuja baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini Tanzania na baada ya baadhi ya mapendekezo ya Tume ya Jaji Robert Kisanga kukataliwa na Serikali. Kwa kiasi kikubwa mabadiliko haya yalionekana kuwa yalikuja kukandamiza demokrasia nchini. Kwanza, kwa mara ya kwanza Rais anaweza kuchaguliwa na kutangazwa mshindi kwa kupata kura zozote zile ili mradi awazidi wengine. Kabla mabadiliko haya, Mgombea urais asingeweza kutangazwa bila kupata angalau asilimia 51% ya kura zote zilizopigwa. Kwa sasa, hoja ni wingi wa kura tu na hivyo kuondoa uwezekano wa kura kurudiwa. Pia, mabadiliko hayo yalimpa Rais uwezo kuteua watanzania 10 kuwa wabunge wa Jamhuri ya Muungano. Hakuna mwongozo maalum wa namna ya kuteua wabunge hao. Aidha, mabadiliko hayo pia yaliongeza viti maalum vya wanawake toka 15% hadi 20%, jambo pekee lililosifiwa kuwa jema katika mabadiliko haya.

(xiv) Mabadiliko ya Kumi na Nne 2005 Kwa mara ya pili tangu mwaka 1984, mabadiliko ya mwaka 2005 yalionekana kuwa na mambo mengi mazuri. Kutoka 20%, mabadiliko yaliongeza viti maalumu vya wanawake hadi 30%. Kwa mfano, mabadiliko haya yaliweka bayana zaidi uhuru wa kuabudu, uhuru wa kushiriki na watu wengine, uhuru wa maoni na kujieleza na kuondoa vizuizi vyote (clawback clauses) vilivyokuwepo kwenye Katiba. Pia, mabadiliko yaliweka utaratibu wa kuteua wabunge wa viti maalum vya wanawake kutegemeana na uwiano wa ushindi wa kila chama katika kura za ubunge majimboni.
 
Pamoja na marekebisho yote, badi Katiba iliyopo haijazingatia kwa upana haki za binadamu, hasa haki za mwanamke. Wenzetu Mwanamke akijifungua wanampa Likizo ya Miezi 10 aleemwanaye.

Tuwe na Katiba inayo ainishe kwa ufasaha misingi yote ya haki za binadamu, yaani kisiasa, kiuchumi na kijamii ili kuleta maendeleo na kuweka ulinzi madhubuti wa haki hizo. Mfano watu wanapotea wanatekwa na Katiba haisemi chochote. Tumuulize nani kuhusu Ben saanane. Katiba mpya ndio Suruhisho.
 
Mkuu asante sana kwa Makala haya Binafsi nimepata kujua baadhi ya vitu nlivyokuwa sivijui awali,

Kwakweli mchakato wa mabadiliko wa Katiba umeanzia mbali sana. Jambo nililojifunza katika mchakato huu wa mabadiliko ni kwamba viongozi wetu wengi hawapo tayari kuruhusu mabadiliko ya Katiba ambayo yatabana maslahi yao. Mathalani, katika mabadiliko ya katiba ya Mwaka 1992 inaonesha wazi namna viongozi walivyo wagumu wa kukubali mabadiloko kwa kulazimisha katiba ya chama kimoja iendelee kutumika wakati nchi imeingia katika mfumo wa vyama vingi.

Kimsingi, kuna baadhi ya mabadiliko ya katiba ambayo yamenivutia kiasi. Mfano, mbabadiliko yaliyohusiha kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini. Mabadiliko haya yalikuwa ni hatua ya msingi ya kuzaliwa kwa demokrasia nchini japo naamini wapo viongozi wanaojutia mabadiliko haya kutokana na kuchukia uwapo wa vyama pinzani nchini kwa sasa (wanatamani vipotee kabisa).

kadhalika, mabadiliko yaliyonivutia katika katiba ni yale ya mwaka 2005 yaliyoonekana kutambua uwapo wa uwakilishi wa wanawake bungeni pamoja na kuondoa baadhi ya vikwazo. Kwa mfano, suala la kutambua uhuru wa kuabudu na uhuru wa kutoa maoni zilikuwa ni hatua za msingi za utekelezaji wa haki za binadamu. Jambo la kusikitisha katika mambo hayo mawili uhuru wa kujieleza au kutoa maoni bado umefinywa sana kiasi ambacho Watanzania wengi wanapata uzito kutoa maoni mbalimbali kuhusu masuala yanayoendelea katika taifa lao isipokuwa kwa kutumia vyombo vichache kama hapa JF (where we dare to talk openly) I appreciate this.

Kwa ujumla, natamani sana kushuhudia mabadiliko ya Katiba ambayo yatakuwa wazi na tija katika kutetea haki za wananchi na taifa kwa ujumla kuliko mabadiliko yanayolinda maslahi ya upande mmoja.
 
Katiba iliyopo inampa manufaa makubwa Rais kutimiza ndoto zake na jaribio la kutaka kuwa na Katiba ya wananchi lilizimwa na Bunge linalojiita kuwa linatuwakilisha wananchi
 
Roving Journalist umeweka vizuri hayo mbadiliko ya katiba, lakini tuletee sisi walalahoi wa nanjilinji kiunaga ubaga, hayo mabadiliko ya katiba yanaleta kitu gani kwa mwananchi. Ikumbukwe! kwenye hili fuvu la demokrasia, mwananchi hana nguvu juu ya yanayoendelea ktk nchi yake.

Mabadiliko yote ya katiba uliyoyaainisha yanawafaa wao waliobadili, Henceforth mabadiliko ya katiba kisiasa hayana maana kama hayatoweka misingi ya maendeleo katika falsafa na itikadi kama nchi kwanza.

Itabadilishwa zaidi na zaidi, lakini haitakuwa na cha msingi kama katiba yenyewe haina target zaidi ya kuwaangalia group la watu wachache wanaotawala(Oligarchy)
 
Back
Top Bottom