Siye wengine zama zetu hakukuwa na video. Nakumbuka Video ya kwanza kuiona ilikuwa pale Milano Hotel Magomeni mwaka 1983, ambapo watoto walikuwa wanaingia kwa shilingi tatu, kumbuka wakati huo soda ilikuwa inauzwa kwa shilingi saba. Bahati ya kuishi uswahilini inaleta tafakari ya kina na kuyaona maisha kama yalivyo, uswahilini hakuna maisha bandia.
Nakumbuka mwishoni mwa miaka ya 70 na mwanzoni mwa miaka ya 80 mpaka 1984 Chuo Kikuu cha Dar walikuwa na chakula kizuri sana na maji safi kuliko sehemu nyingi wanaowazunguka. Wakati huo sinza ilikuwa ni porini tu. Watoto wa uswazi walipaita chuo kikuu USA sijui kwa nini.
Watoto wengi wa uswazi ya Ubungo, Manzese, Mabibo, Magomeni walikuwa wanakwenda USA kuchukua makombo ya chakula kwa kisingizio cha kupelekea mbwa wakati walikuwa wanakula wenyewe. Makombo hayo walikuwa wanayaita "makombo's".
Kurusha vishada kwa kuokota mabunda ya nyuzi yaliyotupwa toka kiwanda cha Urafiki nao pia ulikuwa ni mchezo maarufu sana zama hizo. Mchezo mwingine ulikuwa ni "sago" ya korosho. maeneo ya Mabibo mpaka Kisukuru yalikuwa ni mapori makubwa sana ya mikorosho. Tabata wakati huo ni kijijini.
Pale chini ya Tabata dampo kulikuwa na bwawa lililokuwa maarufu kwa jina la "deiwaka" na pale Mabibo External kulikuwa na lingine linaitwa "kijiwe samli" Deiwaka lilikuwa ni bwawa wanaogelea vijana wakubwa wavuta bangi wakati lile la kijiwe samli wagoeleaji wake walikuwa ni vijana chini ya miaka 15 tena wacheza sarakasi.
Kitu kingine kilichokuwa kinatuvutia ni Skauti. Mimi skauti yangu tulikuwa tunafanyanyia pale Shule ya msingi Magomeni turiani. kwa kweli tuliinjoi sana hasa wakati wa kuweka kambi Morogoro ambapo wazazi walichangia shilingi 100. Uswazi kwetu kulikuwa na mchezo wa kukata picha kwenye magazeti na kutengeneza "vitambulisho" ambavyo ukikutana na watoto wenzio "mgambo" unawaonyesha nao wanakuruhusu kuendelea na safari.
Mitaani tulikuwa na mchezo wa "korokoro" yaani mnagonga visoda vinakuwa kama chapati (shilingi tano) maganda ya pakti za SM (shilingi 20) na la Sport (shilingi mia) halafu mnacheza kamari. Dah mambo mengi ya uswazi nikiyakumbuka natamani kuyatungia kitabu.