Hatujarogwa... tunajiroga wenyewe!

IsangulaKG

JF-Expert Member
Oct 14, 2010
706
385
Kila siku iendayo kwa Mungu, maisha nchini Tanzania yanabadilika. Nasema yanabadilika kwa kuwa , wakati kwa wengine yanakuwa mepesi zaidi, kuna wengine ambao yanakuwa magumu zaidi.

Ukweli usiopingika ni kuwa, hawa ambao maisha yao yanakuwa magumu zaidi kila kukicha, ndiyo hao hao wanaowapa nafasi hawa wenye maisha 'mepesi' kuendelea kuwa na maisha mepesi zaidi. Kwa maana nyingine, kama ni ufisadi, masikini ndio wanaochangia kuongezeka kwa ufisadi Nchini Tanzania. Najua hapo waweza kubisha lakini mojawapo ya sifa yangu kuu, kama lilivyo jina langu 'Mlosi' 'Mtulutumbi' siku zote najitahidi kufikiria zaidi ya kutumia common sense:

Watanzania masikini, ni chanzo cha ufisadi
Kwa kutokuwa makini, kura zao wazinadi
Wakati wa kampeni, hupokoea vizawadi
Kuweka madarakani, viongozi mafisadi

Watanzania masikini kama chanzo cha Ufisadi

Toka tupate Uhuru tumekuwa na Chaguzi kadhaa za Viongozi mbalimbali wa kisiasa. Kama ilivyo maana ya kiongozi, ni 'mtu ambaye anaongoza walio chini yake ili kuifikia dira ya pamoja iliyowekwa" .Zaidi ya asilimia 80 ya watanzania ni Masikini na wengi wao wanakaa vijijini. Hata hivyo , watanzania hawa wa vijijini, ndiyo wanaomiliki asilimia kubwa katika kundi la masikini wa Nchi hii, bahati nzuri , masikini hawa hawa ndio walio na nafasi kubwa ya kuwaweka viongozi madarakani. Hali hii inathibitishwa na Uchaguzi wa Urais wa mwaka 2005 ambapo Chadema ilishinda zaidi sehemu za mijini, huku CCM ikikomba kura nyingi sana vijijini;

Swali kuu hapa ni kuwa
Huko huko vijijini,
Kuna wengi masikini,
Miaka kama hamsini,
CCM Madarakani
Baada ya kampeni
CCM INAWINI...
Unadhani kwa nini?


Kuna Tatizo Gani?
Hebu turudi nyuma kati ya Themanini na mwanzoni mwa mwaka wa Tisini, wakati Mwl. Nyerere anaamua kuwepo na vyama vingi Nchini, zaidi ya asilimia themanini ya wananchi walikuwa wametoa maoni kuwa tuendelee na mfumo wa chama kimoja... Kwa ufupi mwalimu Nyerere alikiuka Demokrasia! Alienda kinyume na matakwa ya walio wengi! Hebu tafakari, kwa nini Mwl.Nyerere alikiuka Demmokrasi?
Je, ni kwa sababu huo ndiyo mfumo wa chama chake wa kukiuka maamuzi ya wengi?
Je, ni utashi wake Binafsi kwa kuona kuwa Nchi hii inahitaji harakati mpya za kutukomboa kifikra?
Je, aliwaona watanzania 'mazuzu' kwamba hata akikiuka demokrasia hawatahoji?
Je, aliogopa kuwa asilimia 20 waliotaka vyama vingi watamsumbua katika Uongozi?
Kwa nini alipindisha Maamuzi ya wengi ili kuwaridhisha wachache?

Kimsingi, majibu ya maswali haya si rahisi hata kidogo kwani ukweli halisi anaujua Mwalimu Nyerere mwenyewe japo kuna sababu nyingi sana za 'juu juu' zilitolewa!.
Jambo la kujifunza hapa ni kwamba, hata wakati ambao kulikuwa na mwamko wa kidemokrasia Afrika na duniani kote...bado watanzania walitaka chama kimoja. Bado walitaka kutawaliwa na Chama kimoja....Hadi leo, zaidi ya MIONGO KADHAA ya vyama vingi nchini, Watanzania BADO wanataka KUTAWALIWA NA CHAMA KIMOJA!

Ingekuwa watu hawazeeki, ningesema watanzania wengi wanapenda kutawaliwa na chama kimoja kwa kuwa Wanaenzi jinsi ambavyo Chama hiki (Ambacho kimsingi kiliundwa baada ya Uhuru) kilivyowaongoza miaka ya awali baada ya shida za ukoloni Lakini ukweli ni kwamba kizazi cha wazee kimepungua sana Nchini Tanzania. Takwimu za Mwaka 2010 Zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wana miaka chini ya 40. (Age distribution in Tanzania statistics - NationMaster.com). Kwa maana kuwa walizaliwa baada ya Uhuru, hawayajui machungu ya Ukoloni wala harakati za Uhuru au miaka ya mwanzoni ya kujipanga kiaendeleo baada ya uhuru. Lakini je kwa nini bado wanataka kutawaliwa na Chama kimoja? Naweza kutoa majibu mepesi tu kwa haya maswali Magumu; HOFU, UOGA NA UBINAFSI (Wimbo wangu wa Kila siku)

Kama wewe ni mfuatiliaji wa Makala zangu, utagundua kuwa kila mara nasisitiza Ujumbe huu; kwamba 'MOJAWAPO YA KITU AMBACHO CHAMA TAWALA KIMEFANIKIWA KATIKA NCHI HII NI KUWAJENGEA WANANCHI UOGA WA KUCHUKUA HATUA'
Acha nithibitishe hili;
1: Mojawapo ya sababu kubwa ya wananchi wengi kutaka kuendelea na mfumo wa Chama kimoja, ni kwa sababu 'walitishwa' kuwa vyama vingi vitaleta vita na kuvuruga amani.
2: Huko vijijini wakati wa kampeni, vyama vya Upinzani uhubiriwa kama chanzo Cha vita nchini na Mvurugiko wa Amani
3: Wakati Vyama vingi vimeanza wananchi 'walitishwa' kuwa vyama vya upinzani vinampinga Nyerere hivyo kuvichagua ni 'kumpinga' Nyerere
4: Watu wanaojaribu kuwaamusha wananchi 'hukamatwa kamatwa' na polisi, hutishwa na wengine hupigwa
5: Watetezi wa haki za wanyonge hutishiwa maisha..Mwakembe na wengine
6: Wakati wa Mgomo wa Madaktari, madaktari 'walitishwa' kuwa watafukuzwa kazi na ili kuthibitisha hoja yangu ya Uoga na ubinafsi; madaktari hao hao (wa meno) wakatoa TUZO kwa Rais kikwete wakati wenzao (Medical Doctors) wakidai kuboreshwa kwa huduma ya Afya Tanzania.

Kwa hii 'image' ambayo imejengeka kwa wananchi ya KUWAJENGEA UOGA, imewafanya wadumae akili zao kuchukua maamuzi mazito hasa wakati wa Uchaguzi ambao wana nafsi kubwa ya kufanya Mabadiliko. Hali hii imewadumaza hata uwezo wa kufikiri hasa wakati wakiwa katika Chumba cha kupiga kura ambacho mtu yuko peke yake!


Sababu ya Pili ni kukosekana kwa Maono!
Watanzania wengi hawana maono ya Mbali. Japo neno hili si zuri ila naomba nilitumie hapa kwamba watanzania wengi masikini "Cannot think Beyond their Pants" Nirudie tena kuomba samahani kwa kulitumia neno hili kwani nalenga tu kujenga hoja yangu; Nalithibitisha Hili:
Chama tawala kimeongoza kwa zaidi ya miaka 50, na hadi leo Uchumi wa Nchi unaporomoka. Tanzania imeendelea kubaki katika nafasi ya Tatu ya umasikini duniani mbali na kuwa na rasilimali nyingi kuliko nchi zote za Afrika mashariki na nchi Nyingi sana duniani;
Mbali na Hili;

Hapa ndipo niliposema , kuna wananchi who cannot think beyond their Pants!

Katika Kampeni za Uchaguzi kule Arumeru. Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa akawaambia wana Arumeru kuwa:

Atamshauri Rais, Kitatua kero zao,
Alishakuwa Rais, Tena kwa kura zao
Matatizo yao , hakuyaona?
Shida zao, hakuziona?

Swali la kujiuliza, hivi kama ukiwa umekaa kwenye ghala la Chakula ukashindwa kumpa mtu mwenye njaa Chakula, unaweza kumshawishi Mkulima alime shamba kisha ampe mavuno mwenye njaa?

Lakini usije kustaajabu..kweli wana ARUMERU wanakubaliana na ahadi hii na Kumpa Mkapa nafasi ya 'KUMSHAURI' Rais- INABILITY TO THINK BEYOND THEIR PANTS!

Tena, Ubinafsi pia umetawala ati utakuta wanamuuliza mgombea, 'nikupigie Kura umenipa nini" badala ya kuangalia faida ya Pamoja " collective benefits' watakayoipata kwa kumchagua kiongozi fulani

Twafanya makosa sana, wakati wa uchaguzi
Badala sema Hapana, na kuleta Mapinduzi
Mafisadi kuwabana, Kuwataa kwa uwazi
Wale wale twachagua, wenye tuhuma za wizi
Wasafi twawabagua,twawaona hawawezi!

Nimewahi kuhudhuria semina moja ya kisiasa nje ya nchi. Katika baadhi ya presentation zilizofanyika, moja iliongelea hali ya maendeleo ya Nchi za Afrika toka zipate Uhuru. Jambo lililodhihirika ni kuwa wakati wa ukoloni, Nchi nyingi za Africa zilikuwa zinapata maendeleo kwa kasi kuliko baada ya Uhuru. Wengi tuliotoka Nchi za Afrika tulibisha sana hoja hii lakini mtoa mada alijitetea: Nyingi kati ya Nchi ambazo wakoloni walichelewa kuondoka zina maendeleo makubwa kuliko Nchi ambazo zilipata Uhuru mapema. Moja wapo ya Nchi zilizo pata uhuru mapema ni Tanzania. Nchi zilizopata Uhuru mwanzoni kama vile DRC, Benin, Burkina faso,Tanzania, zinajikongoja kimaendeleo kuliko nchi ambazo wakoloni walichelewa kutoka kama vile Africa Kusini, Namibia (Isipokuwa Zimbabwe ambayo tunajua nini kinachoendelea huko). Mtoa mada alitumia vipimo kadhaa vya kiuchumi kuthibitisha point yake. Mfano rahisi ni Kenya na Tanzania, Kenya Ambayo imepata uhuru miaka miwili baada ya Tanzania ina maendeleo zaidi ya Tanzania. Mada hii ilinistua akili yangu na nikalazimika kujiuliza masali kadhaa:

1: Je Hatuwezi kujiletea maendeleo wenyewe bila kuwategememea Wazungu? Swali hili linajibiwa na Tabia ya Rais wetu kutembeza 'BAKULI' la kuomba misaada Nje ya Nchi hasa kwa Wazungu. Katika mada mbali mbali hapa JF, tumeshuhudia Rais anavyokosolewa kwa kuomba omba misaada nje ya Nchi hali iliyopelekea kupata 'critisism' nyingi sana. Iwapo Rais anayetegemewa na wananchi kuongoza harakati za kuleta maendeleo nchini anategemea 'misaada' ya wazungu ili kuwakomboa wanachi wake, je huu si ushahidi kuwa hatuwezi kujiletea maendeleo wenyewe?

2:Swali jingine ni kuwa je MISAADA YA WAHISANI Ndiyo itakayo tuondolea Umasikini WETU?

Binafsi siamini kuwa Umasikini wa watanzania unaweza kuondolewa kwa Misaada ya wahisani. Hasa kwa sababu fedha nyingi zinazo tolewa na wahisani kimsingi asilimia kubwa inarudi kwao na majirani zao; Zinarudi kwao kwa mfumo ufutao:
Ukipata fedha ya kuendesha mradi wa kilimo kwa mfano:
  • Bado hauna uwezo wa kuzalisha vifaa vya mradi hivyo utanunua toka China, india au huko huko kwa wahisani
  • Wataalamu washauri (Consultants) Wanaokuja kushauri mradi hutumia fedha hizo kwanzakusafiri katika ndege zao wenyewe, kustarehe katika mahoteli yao yaliyojengwa Nchini mwetu, kutembelea magari tuliyonunua kwao yanayotumia mafuta tuliyonunua kwao. Utatayarisha ripoti na computer zao n.k
  • Tena katika Miradi ya Afya ndo mbaya zaid kwani utanunua dawa kama ARV kwao, vifaaa vya hospitali utanunua kwao na kadhalika... SOMA kitabu cha WHITE MAN'S BURDEN
HAKUNA NCHI YOYOTE DUNIANI ILIYOPATA MAENDELEO KUTOKANA NA FEDHA ZA WAHISANI!

NINI KIFANYIKE

Watanzania wana nafasi ya kuleta mabadiliko nchini kwa kutumia kura!

Kama kilivyo kilio Changu cha kila siku, hatua ya Kwanza ni kubadilika kifikra
Kila mmoja popote alipo anawajibu wa kuwafumbua fikra wananchi.
Vita yetu ni vita ya fikra mbovu
Kwa amani, watu waone uovu
Kwa kura, Wawakatae wabovu!

Vita hii si yangu pekee, vita hii ni yangu mimi, wewe na yule! Ni vita isiyotumia siraha za moto! Ni vita ambayo siraha kubwa ni Hoja. Hoja za kuwafanya wananchi masikini watambue kuwa;
Umasikini, si haki yao
Wasidanganyike, kwa vizawadi vya Kampeni!
Na kwamba ukitaka kuligeuza shamba lako ili liwe bustani ya Maua mazuri, Lazima ung'oe visiki!

@Mlosi K. Mtulutumbi . Haki zote zimehifadhiwa!
 
Mtaji wa CCM ni umasikini wa Watanzania. CCM haiwezi kufanya jitihada za kuwapunguzia umaskini Watanzania kwani kwa kufanya hivyo watatuwa wanapunguza mtaji wao.

Bado wanapata kura (za kweli na za kuiba) kwa mtaji wa umasikini wetu. Msimamizi wa uchaguzi anapewa laki moja anauza utu wake. Baada ya week moja laki hana na mtu anakula miaka 5
 
Mlosi na Wana JF,

Tunashukuru kwa mada yako uliyotufumbua na kutuelimisha wajibu wetu.

Ya kwangu ni haya, Watanzania wa leo sio Watanzania wa miaka ya nyuma, Watanzania wa sasa wameamka haswa kasi hii imeshika mjini na sasa inahamia Vijijini.

Tatizo kubwa letu ni Woga kama ulivyosema, tunaogopa na kushindwa kuhoji na kukataa pale tunapoona mambo hayaendi vyema.
Lingine ni watanzania wengi kama sio wachache hatujui Wajibu na haki zetu za msingi.

Elimu ya uraia nayo ni chanzo cha haya hasa wa vijijini, Bill Gates alisema Kuzaliwa Masikini si kosa lako ila Kufa masikini ni kosa lako.
Tukirudi kwa Viongozi au Serikali yetu, wameshindwa kama wanafanya ni kidogo sana kufuata Utawala wa sheria hili siitaji kulitolea ufafanuzi.

Rai yangu:
Sheria ziendelee kubadilishwa kutokana na wakati hasa hasa Katiba yetu, na Mwisho wa yote tukimweka MUNGU kwanza aka mbele hakuna linaloshindikana.
 
Watanzania wengi hawana elimu! Siyo mjini wala kijijini, uelewa wa mambo ni mdogo mno. Ndiyo maana utakuta watu wamejikita kusoma habari za kiudaku badala ya kusoma zile constructive articles. Wengi tunapenda vitu visivyojenga uwezo wa kufikiri au kuchambua mambo, matokeo yake ideas mbovu kama za udini, ukabila, khanga na kofia, ukanda na kubebwa kwenye malori vinakuwa vinafanya kazi na kuwasaidia hawa jamaa wa CCM. Lakini kama wamethubutu kuwapeleka vijana wetu hata hizo shule za kata, basi ndiyo chimbuko la mabadiliko litakakotoka!!
 
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom