Jabali la Siasa
JF-Expert Member
- Jul 10, 2020
- 3,579
- 2,906
==
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ukaguzi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya tatu katika eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam na kutoa maagizo ya kuharakisha maandalizi ili huduma ianze mapema.
Katika ziara hiyo, Majaliwa alikagua barabara kuu za mradi, vituo vya abiria, pamoja na karakana za kuhifadhi na kufanyia matengenezo mabasi. Alisisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuona huduma inaanza haraka kwa kuwa ni mkombozi wa wakazi zaidi ya milioni moja wa Mbagala wanaosafiri kila siku kwenda katikati ya jiji.
“Mabasi haya tayari yameanza kuwasili nchini tangu Agosti 5 kutoka China. Ni jukumu letu kuhakikisha hayakai tu bandarini au kwenye maegesho bila kuanza kazi. Wananchi wanahitaji huduma hii sasa,” alisema Majaliwa.
Mradi wa awamu ya tatu wa BRT unaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 550 unafadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia. Utekelezaji wake unahusisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 23.6 kuanzia kituo cha Gerezani hadi Mbagala Rangitatu.
Kwa mujibu wa taarifa za Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), kati ya mabasi mapya 250 yaliyotengenezwa nchini China, tayari mabasi 99 yamewasili yaliyo chini ya Ubia, na mengine yanatarajiwa kuendelea kuwasili kwa awamu. Baada ya kukamilika, mradi huu unakadiriwa kusafirisha zaidi ya abiria 400,000 kwa siku, ukipunguza kwa kiasi kikubwa msongamano katika barabara ya Kilwa.
Majaliwa ametoa onyo kali kwa wakandarasi na watendaji wa DART kuhakikisha viwango vya ubora vinazingatiwa, akibainisha kuwa Serikali haitavumilia ucheleweshaji au uzembe unaoweza kuongeza gharama za mradi.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa DART alisema maandalizi ya kuingiza mabasi hayo katika mfumo yamefikia hatua ya mwisho na majaribio yataanza wiki chache zijazo. Aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi kutarahisisha usafiri, kuokoa muda wa safari kwa zaidi ya dakika 45 kila siku, kuongeza tija ya kiuchumi na kupunguza matumizi ya mafuta kwa wananchi.
Wananchi wa Mbagala wamepokea kwa matumaini makubwa taarifa za kuanza kwa huduma hiyo, wakisema itawaondolea changamoto za foleni na muda mrefu wanaopoteza barabarani kila siku.