Hatari ya kuhangaikia urembo

Pi Network

JF-Expert Member
Mar 22, 2016
273
500
Urembo wa kweli hutegemea nini? Watu fulani husema urembo hutegemea maoni ya mtazamaji. Isitoshe, maoni ya watu wengi kuhusu urembo yametofautiana sana katika utamaduni na enzi mbalimbali.

Jeffery Sobal, mtaalamu wa sayansi ya lishe katika Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani, anasema hivi: “Katika karne ya kumi na tisa, jamii nyingi ziliwaona watu wanene kuwa watu wanaoheshimika. Watu wanene walionwa kuwa watu wenye afya na ufanisi, huku watu wembamba wakionwa kuwa maskini hohehahe ambao hawawezi kununua chakula cha kutosha.” Sanaa nyingi za kipindi hicho zinaonyesha maoni hayo. Mara nyingi sanaa hizo zilionyesha wanawake wenye mikono mikubwa, miguu minene, mgongo mpana, na mapaja manene. Baadhi ya sanaa hizo zilikuwa picha za watu halisi walioonwa kuwa warembo zaidi.

Ingawa urembo unahusisha mengi zaidi ya kuwa mnene au mwembamba, watu fulani wangali na maoni hayo. Jamii fulani zinazoishi kwenye visiwa vya Pasifiki Kusini hupenda sana unene. Katika maeneo fulani ya Afrika, wasichana wanaotarajia kuolewa hupelekwa kwenye makao ya pekee ambako wanalishwa vyakula vingi vyenye mafuta mengi ili wanenepe na kuvutia zaidi. Mtu mmoja anayemiliki klabu ya usiku huko Nigeria anasema hivi: “Kwa kawaida, wanawake Waafrika ni wanene . . . Huo ndio urembo wao. Huo ndio utamaduni wetu.” Katika jamii nyingi za Hispania, unene huonwa kuwa ishara ya utajiri na ya mafanikio.

Lakini katika maeneo mengine mengi, watu wanene hawaonwi kuwa warembo. Kwa nini? Watu fulani husema kwamba biashara zilipoongezeka na viwanda kuenea, chakula kilizalishwa kwa wingi na kusambazwa katika maeneo mengi, hivyo kuwawezesha watu maskini kupata vyakula ambavyo hapo awali vililiwa na matajiri tu. Hivyo, pole kwa pole watu wanene wakaacha kuonwa kuwa warembo. Kwa upande mwingine, dini fulani huwaona watu walionenepa kupita kiasi kuwa walafi, na hilo limewafanya watu wawe na maoni mabaya kuhusu unene. Pia, mavumbuzi ya kisayansi kuhusu magonjwa yanayosababishwa na kunenepa kupita kiasi yameathiri maoni ya watu. Mambo hayo na mengineyo yamewafanya watu wabadili maoni yao kuhusu urembo. Kwa miaka mingi sasa, watu wengi ulimwenguni wamesema kwamba watu wembamba ndio warembo.

Vyombo vya habari vimechangia sana maoni hayo. Watu wanaoonyeshwa katika matangazo ya biashara kwenye mabango na televisheni huwa wembamba na wenye misuli. Watu wenye maumbo hayo hutumiwa katika matangazo hayo ili kuonyesha kwamba mtu atakayetumia bidhaa zinazotangazwa atakuwa mwenye uhakika na atafanikiwa. Pia, waigizaji maarufu wa sinema na vipindi vya televisheni huwa na maumbo kama hayo.

Maoni hayo huwaathirije watu wa kawaida, kutia ndani vijana? Makala moja ya hivi karibuni iliyozungumzia maoni ya watu kuhusu umbo lao ilionyesha kwamba “kufikia wakati msichana Mmarekani anapomaliza shule ya sekondari, yeye huwa ametazama televisheni kwa zaidi ya saa 22,000.” Wakati mwingi, wasichana hao huwatazama wanawake warembo wanaoonwa kuwa wenye maumbo bora. Makala hiyo inaongeza hivi: “Wanawake wanapotazama maumbo hayo tena na tena, wao huyahusianisha na umashuhuri, furaha, upendo, na mafanikio.” Basi si ajabu kwamba baada ya kutazama picha za wanamitindo katika gazeti fulani, asilimia 47 ya wasichana waliohusishwa katika uchunguzi mmoja walitamani sana kupunguza uzito, ingawa ni asilimia 29 tu kati yao waliokuwa wanene sana.

Vilevile, maoni ya watu kuhusu urembo huathiriwa sana na biashara ya mitindo. Jennifer, mwanamitindo anayetoka Venezuela, ambaye hufanya kazi huko Mexico City, anasema: “Ni lazima mwanamitindo awe mrembo, na siku hizi ni lazima uwe mwembamba ili uwe mrembo.” Mwanamitindo mmoja Mfaransa, anayeitwa Vanessa, anasema: “Hakuna anayekulazimisha kuwa mwembamba, bali ni wewe unayejilazimisha mwenyewe. Hilo ni zoea lililoenea ulimwenguni pote.” Wasichana fulani walipochunguzwa, asilimia 69 kati yao walikubali kwamba wanamitindo wanaoonyeshwa katika magazeti wameathiri maoni yao kuhusu umbo lenye kupendeza.

Lakini sio wanawake tu ambao huathiriwa na maoni yanayotolewa kuhusu umbo bora. Gazeti El Universal la Mexico linasema: “Bidhaa zinazokusudiwa kuboresha umbo la wanaume zinapatikana kwa wingi kuliko wakati mwingine wowote.”
397ff705312be782dcf0bfa5be334e8a.jpg


Je, Jitihada za Kupata Umbo Bora Zimefanikiwa?

Watu wengi huamua kufanyiwa upasuaji wa kubadili maumbile ili wawe na umbo bora au wapendeze zaidi. Kuna matibabu mbalimbali ya aina hiyo na gharama zake zinazidi kupungua. Matibabu hayo yalianzaje?

Kulingana na kitabu Encyclopædia Britannica, mbinu za kisasa za upasuaji wa kubadili maumbile zilianza baada ya Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, wakati ambapo watu waliojeruhiwa vitani walitibiwa majeraha yao. Tangu wakati huo, mbinu hizo zimetumiwa sana kutibu majeraha makubwa yanayosababishwa na moto au misiba na kurekebisha kasoro za kuzaliwa. Hata hivyo, kama vile kitabu Britannica kinavyosema, mara nyingi upasuaji wa kubadili maumbile “hufanywa hasa ili kuboresha sura za watu wenye afya.” Kwa mfano, umbo la pua linaweza kubadilishwa, ngozi inaweza kupunguzwa usoni na shingoni, ukubwa wa masikio unaweza kupunguzwa, mafuta yanaweza kuondolewa kiunoni na mapajani, sehemu fulani za mwili zinaweza kuongezwa ukubwa, na kitovu pia kinaweza kurekebishwa kupatana na mapendezi ya mtu.

Lakini, vipi watu wenye afya ambao huhatarisha afya yao ili kuboresha umbo lao? Wao hukabili hatari gani?

Angel Papadopulos, katibu wa Chama cha Upasuaji wa Kubadili na Kuboresha Maumbile cha Mexico, anasema kwamba nyakati nyingine watu ambao hawajazoezwa ifaavyo hufanya upasuaji huo na kusababisha madhara makubwa. Kliniki nyingine hutumia vitu fulani hatari ili kuboresha umbo la mtu. Mapema katika mwaka wa 2013, gazeti moja liliripoti kwamba hali zisizofaa katika saluni fulani zilisababisha kashfa kwenye Visiwa vya Canary, ambako mamia ya wanawake walikuwa wamefanyiwa upasuaji hatari.*

Hata wanaume hujitahidi kupata umbo bora. Baadhi yao hutumia saa nyingi wakifanya mazoezi ili kuboresha umbo lao na kuongeza misuli yao. Gazeti Milenio linasema: “Hatimaye wao hupoteza marafiki, na mahusiano yao na watu wengine huharibika kwa sababu ya kujishughulisha sana na mazoezi ya mwili.” Kwa sababu ya kutamani sana kuwa na misuli, wengi wao hutumia vitu vinavyoweza kudhuru mwili, kama vile dawa za steroidi.

Wasichana fulani hujinyima chakula au hula sana na kujitapisha kwa sababu ya kuhangaikia sana umbo lao. Baadhi yao hutumia dawa za kupunguza uzito haraka ambazo hazijaidhinishwa na taasisi za afya zenye kuheshimika. Dawa hizo zinaweza kusababisha madhara makubwa.

Zaidi ya madhara ya kimwili, kuna hatari nyingine zinazosababishwa na kuhangaikia sura kupita kiasi. Dakt. Katherine Phillips wa Chuo Kikuu cha Brown, Marekani, anasema kwamba watu wanaohangaikia umbo lao kupita kiasi hupata ugonjwa fulani unaowafanya wadhanie kwamba wana kasoro za mwili, ijapokuwa hazipo. Inakadiriwa kwamba watu 2 kati ya kila watu 5 wana ugonjwa huo. Pia anasema kwamba watu wenye ugonjwa huo “huamini kuwa wana sura mbovu sana hivi kwamba wao hujitenga na marafiki na wapendwa wao. Wanaweza kushuka moyo na kutaka kujiua.” Phillips anataja kisa cha msichana mmoja mrembo aliyedhania kwamba uso wake umejaa makovu, ijapokuwa alikuwa na vipele vidogo tu usoni. Msichana huyo aliacha shule alipokuwa katika darasa la nane kwa sababu hakutaka kuonekana na watu.

Je, sura ya mtu ni muhimu sana hivi kwamba ahatarishe afya yake ya kiakili na ya kimwili ili kupata umbo bora?

Je, kuna urembo ulio bora zaidi ambao mtu anapaswa kuuhangaikia?
a00d0facad1e202f5cc76a434518180f.jpg
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom