Harufu ya ufisadi ofisi za wabunge

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
270
Matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali kuhudumia ofisi za wabunge majimboni yameonekana kugubikwa na harufu ya ufisadi kutokana na baadhi ya ofisi hizo kutengewa fedha, lakini hazikununua mali zozote huku maofisa wa serikali wakitoa kauli zinazokinzana.
Utata umebainika katika fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuhudumia ofisi ya Mbunge wa Mbeya Mjini baada ya kubainika kuwa katika mwaka wa fedha wa 2004/2005, Halmashauri ya Jiji la Mbeya ilitumia Sh. 2,870,360 kununulia samani za ofisi hiyo ambazo hata hivyo, hazipo.
Kwa mujibu wa nyaraka zilizopelekwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya kipindi hicho wakati huo ikiwa Manispaa kwenda katika ofisi ya Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya, zinaonyesha kuwa fedha hizo zilitumika kununulia samani za ofisi ya mbunge wa Mbeya Mjini pamoja na kuikarabati, kazi ambayo haikufanyika.
Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya, Damson Ntangu, aliliambia NIPASHE kuwa ingawa bado haijawekwa wazi jukumu la kuzihudumia ofisi za wabunge ni la nani, lakini Halmashauri ya Manispaa ya Mbeya (sasa Jiji), mwaka 2004/2005 ilitumia Sh. 2,870,360 kununulia viti sita, sofa kochi seti moja, meza kubwa moja na zuria lenye ukubwa wa mita 15.
Ntangu alisema aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, mwaka 2004 alitoa waraka kuzitaka halmashauri zote nchini kuzihudumia ofisi za wabunge, hadi sasa ndio waraka unaofanya kazi.
Ntangu alisema kutokana na hali hiyo madai yanayotolewa kwamba ofisi ya Mbunge wa Mbeya Mjini haina samani wanaopaswa kulitolea maelezo ni Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambayo kwa mujibu wa nyaraka za barua ilieleza kuwa imetumia kiasi hicho cha fedha kununulia samani za ofisi hiyo.
Uchunguzi zaidi wa NIPASHE umebaini kuwa katika kipindi hicho pia Sh. 3,165,000 zilitolewa na Serikali Kuu ili zisaidie kuhudumia ofisi ya mbunge wa Mbeya Mjini ambazo zilikabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya na pia nyaraka hizo zinaonyesha kuwa katika mwaka wa fedha 2006/2007, hakuna fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuhudumia ofisi ya mbunge.
Wakati utata ukigubika ofisi ya Mbunge wa Mbeya Mjini, kwa upande wa ofisi ya Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Mchungaji Luckison Mwanjale, ofisi yake haina dosari zozote.
Kulingana na nyaraka zilizopo, mwaka 2004/2005 Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini ilitumia Sh. 10,300,000 kwa ajili ya kutengeneza na kununulia samani za ofisi hiyo, kazi ambayo imefanyika kwa umakini mkubwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Juma Rashid Idd, alisema kimsingi, ofisi za wabunge zipo chini ya Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya ambao ndio wanapaswa kutolea maelezo na kwamba Halmashauri inachokifanya ni kutoa ofisi hizo, lakini huduma zote kwa maana ya kununua samani siyo jukumu la halmashauri.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), alisema hadi sasa hajakabidhiwa ofisi kwa sababu ofisi iliyokuwa ikitumiwa na aliyekuwa mbunge, Benson Mpesya (CCM), haina samani hata moja.
Ofisi hiyo ilibainika kwamba haina samani zinazotakiwa baada ya mbunge huyo kwenda kwa Mkurugenzi wa Jiji kwa lengo la kukabidhiwa.
Ofisi hiyo ya mbunge ambayo ipo katika majengo ya zamani ya Halmashauri ya Jiji yaliyopo karibu na kituo Kikuu cha Polisi Mbeya mjini, mbali na kukosa samani muhimu, lakini pia hakukuwepo na makabrasha ambayo hutumika kuhifadhi nyaraka mbalimbali za kiofisi.
RAS, DAS Iringa watofautiana
Kuhusu madai kwamba samani zimeondolewa katika ofisi ya mbunge wa Iringa Mjini, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa (RAS), Getrude Mpaka, amesema ofisi yake inahudumia ofisi za wabunge wa viti maalum wa mkoa na si ofisi za wabunge wa majimbo kama baadhi ya watu wanavyodhani.
Hata hivyo, amethibitisha kuwa fedha za ofisi za wabunge wa majimbo kutoka Serikali Kuu hupitia ofisini kwake na kwamba yeye huzipeleka kwenye ofisi za Makatibu Tawala wa wilaya (DAS) kwa ajili ya utekelezaji.
Mbunge mpya wa jimbo hilo ni Mchungaji Peter Msigwa (Chadema). Alimshinda Monica Mbega (CCM) na alipoanza kazi katika ofisi hiyo hakukuta kitu chochote ofisini.
Mpaka aliliambia gazeti hili jana kuwa kama ofisi hiyo haikukutwa na baadhi ya samani, basi anayepaswa kujibu ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa, Gideon Mwinami, ambaye alisema hajui lolote.
“Kama Katibu Tawala wa wilaya naye anasema hajui chochote, basi nitakaa naye ili tujue nini hasa kimetokea na nitawapeni taarifa baadaye,” alisema Mpaka.
Alisema fedha ambazo hupitia ofisi ya Katibu Tawala kwa ajili ya ofisi za wabunge hutumika kuweka samani na vifaa vya kuendeshea ofisi hizo kama karatasi, notibuku, kalamu na vifaa vingine.
“Tatizo wabunge wenyewe walioingia hivi sasa wanataka vitu modern (vitu vya kisasa) mno …wanataka laptop, sijui wanataka meza za kisasa;” alisema na kuhoji: “Jamani hela zitatoka wapi labda wasubiri bajeti ijayo?”
DC, DAS Nyamagana wamtetea Masha
Wakati Chadema mkoa wa Mwanza kikidai kuwa kinajiandaa kujadili madai kuwa aliyekuwa mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha (CCM), kuwa aling'oa vitasa na kuondoa samani katika ofisi ya ubunge baada ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana imesikitishwa na madai hayo na kusema kuwa tuhuma dhidi ya Masha ni uzushi mtupu.
Mbunge wa sasa wa Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema) alikaririwa hivi karibuni akidai kuwa Masha aling'oa vitasa na kuondoa samani zilizomo katika ofisi hiyo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dorith Mwanyika, alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, alimtaka mwandishi kuwatafuta Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana au Katibu Tawala wa Wilaya hiyo kwa maelezo kuwa ndio wazungumzaji wa suala hilo.
“Hilo waulizwe Mkuu wa Wilaya au Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana wenyewe ndio wanaweza kulizungumzia kwa uzuri,” alisema RAS aliyesema yuko jijini Dar es Salaam kikazi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Said Kamanzi, alisema jana jijini hapa kuwa anashangazwa na madai ya Wenje kwani hakuna kitasa wala samani zilizoondolewa na kusisitiza kuwa kila kitu kipo sawa.
“Namshangaa sana Wenje, yeye alipokuja ofisini badala ya kuripoti kwa wahusika anakurupuka na kukimbilia katika vyombo vya habari na waandishi nao wanaandika bila kuwasiliana na Mkuu wa Wilaya wala Katibu Tawala, ambao ndio wazungumzaji wa hilo na tunapatikana wakati wowote tunapohitajika,” alisema DC huyo.
Kamanzi alisema kuwa taarifa alizonazo ni kwamba kulikuwa na samani za kawaida katika ofisi hiyo wakati Masha alipoanza kuitumia ofisi hiyo, lakini aliamua kuzibadilisha na kuongeza vitu kama kompyta baada ya kutoridhika na zile zilizokuwepo.
Alisema baada ya kushindwa katika uchaguzi, Masha aliamua kuziondoa samani hizo mchana kweupe baada ya kutoa taarifa kuwa anaziondoa na akaamua kuzirejesha zile za zamani.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana, Elius Mgole, alisema kuwa vitasa vipo na havijang'olewa kama ilivyodaiwa na Wenje.
Alisema kuwa kitasa cha mlango wa nje kipo na kile cha chumba cha ndani kiliwekwa baada ya kukitenga chumba kwa mbao ndicho kilichoharibika, lakini hakijatolewa.
Alisema kuwa samani alizoondoa Masha zilikuwa za kwake ambazo alizinunua kwa fedha zake tofauti na inavyodaiwa kuwa zilikuwa za ofisi.
“Alipoingia ofisini, Masha alikuta samani, lakini hakuridhika nazo hivyo aliamua kununua zake na kuziweka,” alisema DAS na kuhoji: “Sasa kuna ubaya gani kuondoka na samani zake na kubakiza zile za awali?”
Uchunguzi wa NIPASHE umebaini kuwa ofisi nyingi za wabunge katika majimbo hazina thamani za kutosha na nyingi hazifikii viwango, hali inayowalazimisha wabunge kuingiza samani zao binafsi.
Hivi karibuni NIPASHE ilizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu, Sera na Bunge, William Lukuvi, kupata maelezo yake juu ya hali za ofisi za wabunge.
Lukuvi alisema kuwa kimsingi serikali hutoa fedha kwa ajili ya kuendeshea ofisi hizo ambazo hupitia ofisi za RAS na kisha kwa DAS.
“Unajua watu wana taste (ladha) tofauti, mtu anaweza kukuta samani ambazo si za hali ya juu na akaamua kuweka zake kwa gharama zake,” alisema Lukuvi.
“Sasa huyu akiamua kuzindoa ni mali yake huwezi kumzuia, lakini nachojua mimi mali ya serikali haichukuliwi kienyeji tu, kuna utaratibu wa mnada. Ni lazima mhakiki mali wa serikali ajue nini kinauzwa na ni lazima kiuzwe kwa mnada wa wazi.”
Hata hivyo, Lukuvi alipoulizwa juu ya mtu kung’oa kitasa hata kama alikiweka alisema: “Unajua vitu vingine vinategemea na ustaarabu wa mtu, kwa hiyo ni suala la mtu na mtu.”
Kutoka mjini Moshi, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, alisema mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndeasmburo, alipoingia kwenye ofisi hizo mara ya kwanza mwaka 2000, alikuta ikiwa na hali mbaya, ingawa kulikuwa na samani lakini zilikuwa duni sana.
Lema alisema walikarabati ofisi hizo na kuweka samani, lakini baadaye serikali nayo iliongeza samani nyingine.
“Kwa kweli katika ofisi hizi kuna samani za serikali na za mbunge binafsi,” alisema.
Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe (Mbeya), Mawazo Malembeka (Iringa) na Cosmas Mlekani (Mwanza).
CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom