Hali ya Usalama Nchini
Ndugu Wananchi;
Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila miaka mitano tunafanya uchaguzi wa kuchagua viongozi wetu. Uchaguzi wa mwisho tumefanya tarehe 31 Oktoba, 2010. Kabla ya hapo tulikuwa na kampeni zilizochukua karibu miezi mwili na nusu. Kila chama kilielezea jinsi kitakavyokabiliana na matatizo yanayowakabili wananchi wa nchi yetu ikiwa ni pamoja na haya wanayoyazungumza sasa. Hatimaye siku ya uchaguzi wananchi walifanya uamuzi wa kuchagua chama walichokiamini, nacho ni Chama cha Mapinduzi. Iweje leo, miezi mitatu baadae kwa mtu au chama cha siasa kufanya maandamano kwa masuala yale yale waliyoyasema kwenye kampeni. Siyo sawa hata kidogo. Kuchochea ghasia ati kwa nia ya kuiondoa Serikali madarakani ni kinyume cha Katiba na ni kuiingiza nchi katika mgogoro usiokuwa wa lazima. Tutasababisha umwagaji wa damu, watu kupoteza maisha na mali zao kuharibiwa bila sababu yoyote ya msingi.