Hakimu Kisutu azuia waandishi kesi ya EPA | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hakimu Kisutu azuia waandishi kesi ya EPA

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Pdidy, Jan 21, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Jan 21, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,376
  Likes Received: 5,663
  Trophy Points: 280
  Hakimu Kisutu azuia waandishi kesi ya EPA

  *Awazuia waandishi kuandika ndani ya mahakama


  Nora Damian


  KATIKA siku ya kwanza kwa kesi ya tuhuma za wizi kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), inayomkabili kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda na wafanyakazi watatu wa Benki Kuu (BoT), waandishi wa habari wamejikuta wakizuiwa kuripoti mwenendo wa kesi hiyo.


  Kizaazaa hicho kilitokea jana saa 8:42 mchana wakati shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Peter Noni, ambaye ni mkuu wa mipango kazi wa BOT alipokuwa anataka kuanza kutoa ushahidi.


  Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali waliokuwepo mahakamani hapo tangu kesi hiyo ilipoanza asubuhi, walijikuta wakizuiwa kuripoti kesi hiyo kabla Noni kuanza kutoa ushahidi wakati hakimu mkuu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Addy Lyamuya alipotangaza amri hiyo.


  Hakimu Lyamuya alisema waandishi hawawezi kuripoti kesi hiyo kwa kuwa hawana kibali cha kuandika mahakamani. “Watu wote wanaoandika waache kwa sababu kabla ya kuingia humu ndani kuandika unatakiwa uwe na kibali,” alisema Lyamuya.


  Hatua hiyo ilisababisha wanahabari kuweka kalamu zao chini na kutoka nje ya mahakama. Kabla ya amri hiyo, waandishi walikuwemo ndani ya chumba cha mahakama tangu asubuhi wakati kesi hiyo ilipoanza kuunguruma na kuahirishwa mara tatu hadi ilipoanza tena majira ya saa 8:00 mchana. Wakati watuhumiwa wa kesi za EPA wanafikishwa mahakamani mwezi Novemba mwaka jana, Lyamuya alikuwa nje ya nchi kwa matibabu na aliporejea kazini alidaiwa kuhitisha majalada yote ya EPA, lakini alipoulizwa na waandishi wa habari alikana.


  Kesi hiyo ilianza kuunguruma asubuhi huku Lyamuya akiwa anasaidiana na Hakimu Ignas Kitusi (Katibu wa Jaji Mkuu) na John Utamwa (Naibu Msajili wa Mahakama Kuu). Pia kulikuwa na makarani waliokuwa wakirekodi mwenendo wa kesi kwa kutumia kompyuta ya mkononi, kama ilivyokuwa kwa naibu msajili wa Mahakama Kuu, Utamwa. Kabla ya kuanza kuunguruma kwa kesi hiyo, upande wa mashitaka ulilazimika kubadilisha hati ya mashitaka baada ya kuwa na mapungufu.


  Hatua hiyo ilitokana na Utamwa kuwasilisha hoja kwa upande wa mashitaka akitaka ufafanue juu ya shitaka la 5 ambalo upande wa mashitaka ulisema kuwa ni mbadala wa shitaka la 3 kwa washitakiwa wa pili, tatu na nne.


  Washitakiwa hao wa ni wafanyakazi watatu wa BoT, Imani Mwaposya, aliyekuwa mkuu wa kitengo cha madeni ya biashara, Esther Komu (kaimu makamu mkurugenzi wa Idara ya Madeni) na Bosco Kimela (kaimu katibu wa BoT). Akijibu hoja hiyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa serikali, Boniface Stanslaus alisema msingi wa mashitaka yao ni wizi na kupotea kwa fedha.


  Naye wakili wa upande wa utetezi, Mabere Marando alisema shitaka la tano si mbadala kwa shitaka la tatu kwa sababu washitakiwa wa pili, tatu na nne hawakushitakiwa kwenye kosa hilo la tatu. Baada ya kubadilishwa kwa hati ya mashitaka, Wakili wa Serikali Stanslaus aliwasomea upya mashitaka yanayowakabili.


  Katika shitaka la kwanza washitakiwa wote wanadaiwa kuwa kati ya Septemba 8 mwaka 2003 na Agosti 18 mwaka 2005 walikula njama na kutenda kosa la wizi wa fedha kutoka BoT.


  Shitaka la pili linamuhusu mshitakiwa wa kwanza Maranda, ambaye anadaiwa kuwa Julai 12 mwaka 2004 jijini Dar es Salaam aligushi hati ya uhamishaji mali kati ya kampuni ya Russia T Ltd ya Tanzania na kampuni ya General Marketing ya India akidanganya kwamba imepewa deni la Sh 207,284,391.44.


  Katika shitaka la nne washitakiwa wote wanadaiwa kuwa Agosti 18 mwaka 2005 waliiba kutoka BoT Sh207,284,391.44. Katika shitaka la sita Mwakosya, Komu na Ndimbo wanadaiwa kuwa wakiwa waajiriwa wa BoT walifanya uzembe uliosababisha benki hiyo kupata hasara ya kiasi hicho cha fedha. Mwisho.
   
 2. Mpita Njia

  Mpita Njia JF-Expert Member

  #2
  Jan 21, 2009
  Joined: Mar 3, 2008
  Messages: 7,012
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Hivi hao waandishi kweli hawaidfahamu sheria inayokataza mtu yeyote kunakili chochote wakati kesi inaendelea bila ruhusa ya mahakama?
   
Loading...