Haki za binadamu

Haki za binadamu

Manka leonce

New Member
Joined
Jul 13, 2021
Posts
2
Reaction score
1
HAKI ZA BINADAMU
Hizi ni haki ambazo mtu anazipata mara tu anapozaliwa, na anaendelea kuwa nazo hadi kifo chake. Kwa maneno mengine, kitendo cha kuzaliwa ukiwa mwanadamu na si kiumbe kingine kinakupa moja kwa moja haki fulanifulani ambazo viumbe vingine havina. Kwa hiyo, haki za binadamu zipo tu, hata kama hazijaandikwa popote, tofauti na haki za kisheria ambazo huanza pale sheria husika inapotungwa, na hufika tamati pale ambapo sheria husika imefutwa.

Mifano michache ya haki za binadamu ni pamoja na haki ya kuishi, haki ya kuwa na makazi, haki ya kutoadhibiwa bila kusikilizwa, haki ya mtu kwenda anakotaka, haki ya kutodhalilishwa na kutwezwa kwa utu, haki ya kumiliki mali, nk.

Kutokana na umuhimu wake, katika nchi mbalimbali haki za binadamu zimewekewa mifumo maalum ya kuzilinda na kuhakikisha hazivunjwi hovyovhovyo. Katika nchi ya Tanzania kwa mfano, ipo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo iliundwa mwaka 2001 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kila mtu, awe kiongozi ama raia anaheshimu haki hizo.

Aidha, Haki za Binadamu zimeingizwa rasmi katika Katiba ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania. Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wameeleza kwa ufasaha kwamba Katiba imeingiza vifungu hivyo kwa mkono wa kulia na kuviondoa kwa mkono wa kushoto.

Maana yake ni kwamba katika Katiba hiyo hiyo zipo ibara zinazomhakikishia kila mtu kulindiwa uhai, heshima na utu wake, lakini katika vifungu hivyohivyo, au vingine katika katiba hiyo hiyo vinaweka masharti magumu kwa mtu kuweza kufaidi haki hizo.

Haki za Binadamu zinatambuliwa ulimwenguni kote. Kilichoisukuma Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kunakuwa na mifumo thabiti ya Ulinzi wa Haki za Binadamu ni mateso na uhalifu mkubwa dhidi ya binadamu uliofanyika wakati wa vita vya pili vya Dunia vilivyoanza tarehe 1 Septemba, mwaka 1939 na kumalizika tarehe 2 Septemba, mwaka 1945. Ni vita vilivyoshuhudia unyama wa hali ya juu unaoweza kufanywa na mwanadamu dhidi ya mwanadamu mwingine, hususan yule aliye dhaifu kimamlaka, kinguvu, kiuchumi, kisiasa, nk.

Kwa hiyo, mnamo mwaka 1948 mataifa yapatayo 50 chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa yalikutana na kutengeneza orodha ya mambo ambayo yalikuja kufahamaika kama Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu. Kuanzia wakati huo, kila nchi ikaendelea kuzilinda haki hizo kwa ama kuzitungia sheria, au kuziingiza katika Katiba za nchi zao. Mpaka sasa, Tamko hilo limefasiliwa katika lugha zaidi ya 360 duniani kote.
 
Back
Top Bottom