Haki ikikosekana, Amani ipo Mashakani

Haki ikikosekana, Amani ipo Mashakani

Nyendo

JF-Expert Member
Joined
Jun 4, 2017
Posts
1,362
Reaction score
4,816
1. Amani pasipo haki, Ni wapi umeiona?,
Kwa hadithi sikumbuki, Ajabu'li kuliona,
Walo juu mishikaki, wa chini hakuna dona,
Haki Ikikosekana, Amani I Mashakani

2. Wanahubiri Usawa, wanaiba wakigawa,
Mifumo imepagawa, Dhoofu yataka dawa,
Wamewajaza machawa, waimbe nchi I Sawa,
Haki Ikikosekana, Amani I Mashakani

3. Amani wanayosema, ya wasiojulikana
Imegeuka kiama, kuna hofu kila kona
Nani alie salama, wote tunaulizana
Haki ikikosekana, amani i mashakani

5. Twatakiwa kuongea? Au tubakie kimya?
Ni swali nawatengea, mwapaswa kulimumunya
Maana tukitembea, watuo wanatuminya
Haki ikikosekana, amani i mashakani

6. Wanakuja na mitutu, kuitangaza amani
Unatekewa Kisutu, haupo magerezani
Hauwaambii kitu, wanakana asilani
Haki ikikosekana, Amani I mashakani

7. Wanatupwa mashambani, huku wengine mitoni
Wanatekwa mabasini, wauawa maporini
Wanavamiwa makanisani, I wapi hiyo amani?
Haki ikikosekana, Amani i mashakani

8. Na Mtuambie leo, Kipi mwataka tunene
Mnatunyima upeo, kuwasifu tufanane
Wakoloni mamboleo, yu wapi Beni sanane
Haki ikikosekana, Amani i mashakani.

9. Kuongea yetu haki, yaturuhusu Katiba,
Hatutaki unafiki, maovu kimya kubeba,
Msitupige fataki, maoni yakiwakaba,
Haki ikikosekana, Amani i mashakani.

10. Haki huzaa amani, muimbayo jukwaani,
Katu hazitengamani, vinginevyo maafani,
Haraka Badilikeni, ubinafsi uacheni
Haki Ikikosekana, Amani I Mashakani

11. Utaifa hushamiri, Haki ikisimamiwa,
Nchi hali huwa shwari, chaguzi zenye usawa,
Furaha iso mithiri, hakuna wa kutugawa,
Haki ikikosekana, amani i mashakani,
 
  • Thanks
Reactions: 004
Back
Top Bottom