Akawageukia askari akasema, ‘Haya, mlete hapa; na wewe Skraga, unoe tayari mkuki wako.’ Basi watu wawili wakaja mbele na walipomkaribia Yule mwanamwali, ndipo kwanza alipofahamu ajali yake, akalia sana, akageuka apate kukimbia. Lakini wale askari wawili walimshika wakamleta analia na kujaribu kuwatoka.
Gagula akamuuliza, ‘Jina lako nani, wewe mwali? Je, hutaki kunijibu? Je, mwana wa mfalme afanye kazi yake sasa?
Kusikia hayo, Skraga alionekana kuwa mwovu kupita kiasi, akajongea hatua moja, akainua mkuki wake, na mara niliona mkono wa Bwana Good unashika bastola, na Nuru ya bastola ilimpata machoni Yule mwali, akanyamaza kimya.
Akaacha kushindana, akafumbata mikono yake akasimama anatetemeka toka kichwa hata miguu.
Skraga akacheka, akasema, ‘Tazama anajikunyata kuona mchezo wangu, hata kabla hajaiona.’ Akapapasa mkuki wake. Nikamsikia Bwana Good anasema kimoyomoyo, ‘Lo! Nikipata nafasi utajuta maneno yako, Mbwa we!’
Basi, sasa Gagula akamfanyia dhihaka , akasema, ‘Sasa umekwisha tulia, tuambie jina lako nani? Mpenzi wangu. Haya sema, usiogope.’
Yule mwali akatetemeka, akajibu, ‘’Ewe mama, jina langu naitwa Foulata, na ukoo wangu ni Suko. Ewe mama, kwa nini sina budi kufa? Mimi sikufanya makosa au ubaya wowote!’
Gagula akajibu, ‘Usifadhaike, lazima ufe uwe sadaka kwa Wale Wazee wakaao huko, lakini ni afadhali kulala usiku kuliko kufanya kazi mchana; ni afadhali kulala usiku kuliko kufanya kazi mchana; ni afadhali kufa kuliko kuishi, nawe utakufa kwa mkono wa mwana wa mfalme.’
Yule mwali Foulata akajiuma vidole vyake kwa huzuni akalia, ‘Ole wangu, huu ndio ukatili kweli! Mimi ni kijana! Nimefanya nini nisipate kuona jua likitoka katika giza la usiku huu, nisione tena nyota zikifuata majira ya jioni, nisipate kuchuma maua katika umande wala kusikiliza nyimbo za mteremko wa maji?
Ole wangu, sipati tena kuona nyumba ya baba yangu, wala kuona tena mapenzi ya mama yangu, wala kuchunga wana wa kondoo! Ole wangu, sitapata mwanaume wakunipenda na wala sitazaa wana! Ukatili! Ukatili!’
Tena akajiuma vidole kwa huzuni akageuka akatazama juu na machozi yalionekana yakimtoka machoni, akawa wa kusikitisha kabisa hata kuleta huruma kwa mtu yeyote, ila wale mashetani waliokuwa wamekaa mbele yetu hawakujali kabisa.
Na wala haikuvuta huruma kwa Gagula, wala bwana wa Gagula, ila niliona dalili ya huruma na huzuni katika sura za walinzi wale, na katika sura za wale wakubwa waliokuwapo; na Bwana Good alijizuia kwa shida tu, akafanya kama anakwenda kumsaidia.
Basi kwa akili ya kike, Yule mwali alitambua fikira zake, na mara akaruka akajitupa mbele yake akamshika miguu akalia, ‘Ewe baba mweupe uliyetoka katika nyota, nifunike kwa nguo yako ya ulinzi, nitambae katika kivuli cha nguvu zako nipate kuokoka.
Niokoe katika mikono ya watu waovu hawa wasio na huruma!’ Bwana Good akamshika mkono akasema, ‘Vema, mimi nitakulinda.’ Akainama akamshika mkono akasema, ‘Haya ondoka, mwanangu.’
Twala akageuka akamwashiria mwanawe, naye akajongea mbele ameshika mkuki juu.
Bwana Henry akasema akinong’oneza, ‘Sasa huu ndiyo wakati unaofaa; unangoja nini? Nikajibu kwa sauti ndogo, ‘Mimi nangoja kuona dalili ya mwezi kupatwa kwanza.
Nimeutazama kwa nusu saa hivi, lakini sioni dalili ya kupatwa.’
Akajibu, ‘Sasa lazima tubahatishe au huyu mwanamwali atauawa, maana naona Twala anaanza kuchoka.’
Basi nikatambua kuwa asemavyo ni kweli, nikatazama mwezi mara moja tena nisione hata dalili ya kupatwa, nikajikaza nikasimama mbele, nikajongea katikati ya Skraga na yule mwanamwali, nikasema, ‘Mfalme jambo hili halitakuwa; sisi hatutavumilia jambo hili; mwanamwali na aende zake salama.’
Twala akaghadhibika mno, akasimama katika kushangaa kwake, na askari wake waliokuwapo na wanawali nao walishangaa.
Na mfalme Twala akasema, ‘Halitakuwa! Wewe mbwa mweupe aliaye mbele ya simba katika pango lake; halitakuwa! Wewe una wazimu? Angalia sana usije ukapatwa na ajali ya kifaranga huyo, na wale waliopo pamoja nawe vile vile.
Je, wawezaje kumwokoa au kujiokoa mwenyewe? Nani wewe ujitiaye katikati ya mimi na matakwa yangu? Kaa upande, na wewe Skraga muue!
Haya, askari wangu, washike watu hawa.’ Basi hapo askari wengi wakatoka kwa nyuma ya jumba walikofichwa. Bwana Henry na Bwana Good na Umbopa wakasogea karibu nami, wakaelekeza bunduki zao.
Nikasema kwa sauti kuu lakini moyo wangu haukwepo kabisa, ‘Acheni! Twacheni sisi watu weupe tuliotoka katika nyota, tunasema kuwa halitakuwa.
Mkikaribia hata hatua moja tu, tutauzima mwezi, na sisi tukaao katika nyumba yake tunaweza kufanya hivi, tutaitia nchi yote katika giza tupu, nanyi mtaonja uchungu wa nguvu zetu.’
Basi maneno yangu yaliwastua; watu wakasimama, na Skraga akasimama kimya mbele yetu, ameshika mkuki wake juu.
Gagula akasema, ‘Msikieni! Msikieni! Msikieni asemavyo uwongo. Basi na afanye anavyosema na mwanamwali ataachiliwa. Afanye au auawe pamoja na mwanamwali na wale walio pamoja naye.’
Nikatazama mwezi tena, na sasa: nilifurahi, maana niliona kuwa alama nyeusi inaanza kuonekana katika mwezi.
Ndipo nilipoinua mkono wangu kwa taratibu sana nikaonyesha juu mbinguni, na Bwana Henry na Bwana Good wakafanya vile vile, tukaanza kusema maneno yoyote tuliyoweza kuyakumbuka.
Pole pole na kwa tara-tibu, kivuli kilianza kufunika mwezi, na kilipozidi kuja nikasikia watu wanaanza kuvuta pumzi juu, nikasema,
‘Tazama, Ewe Mfalme! Tazama, Gagula!
Tazameni nyinyi wakubwa, na watu wote, mwone kama watu weupe waliotoka katika nyota wametimiza maneno yao au kama ni uwongo mtupu! Mwezi unafunikwa mbele ya macho yenu; na sasa hivi itakuwa giza tupu.
Mmeomba ishara nasi tumeifanya. Ee mwezi, ufunikwe uwe giza tupu! Uzime mwangaza wako, Ee wewe mtakatifu; ulete ule moyo wa kiburi hata mavumbini, Ee mwezi, ule dunia kwa vivuli vyako.’
Basi watu wote waliguna kwa hofu. Wengine walisimama kama wamegeuka mawe, na wengine walijitupa chini wakapiga magoti wakalia kwa sauti kubwa.
Na mfalme mwenyewe alikaa kimya, uso umembadilika.
Gagula tu hakunyamaza, akasema, ‘Giza litapita, nimeyaona kama haya zamani; hapana mtu anayeweza kuzima mwangaza wa mwezi; msiogope; mkae kimya na giza litapita.’
Nikasema, ‘Ngojeni mtaona. Ee Mwezi!Mwezi! Mwezi!’ na sisi wote watatu tukazidi kusema maneno ya ovyo ovyo tu! na kwa muda wa dakika kumi tukaendelea hivyo hivyo.
Giza likazidi, na watu wote walikodoa macho yao kutazama juu, na walikaa kimya kabisa. Sasa dunia ikaanza kujaa vivuli vya ajabu, na kila kitu kilikuwa kimya kama mauti.
Wakati ulipita na pamoja giza likazidi kushika mwezi. Ikawa ajabu mno, maana kwanza ikawa kama mwezi unakaribia dunia na kuzidi kuwa mkubwa.
Sasa uligeuka rangi ukawa mwekundu kama damu, na halafu tuliona alama zile zilizo katika mwezi zinang’aa katika wekundu wake.
Pole pole giza likatambaa; sasa limefika nusu ya ule wekundu kama damu. Likazidi kuenea hata hatukuweza kuona sura za watu waliokuwa karibu. Sasa kila mtu alikuwa kimya kabisa, nasi hatukusema neno.
Mara Yule kijana Skraga alilia kwa hofu, ‘Mwezi unakufa. Wachawi weupe hawa wameuwa mwezi. Tutaangamia katika giza.’ Naye alishikwa na wazimu kwa hofu akainua mkuki wake akampiga Bwana Henry kwa nguvu zake zote.
Lakini alikuwa amesahau habari za nguo zile za chuma alizotupa mfalme, na mkuki ukapinduka bila kuzipenya.
Kabla hajapata nafasi kupiga tena, Bwana Henry akashika ule mkuki akampiga kifuani. Skraga akaanguka maiti! Basi watu walipoona hivyo, na kwa sababu ya hofu waliyokuwa nayo kufikiri kuwa mwezi unakufa, wakaanza kutawanyika, wakapiga mbio na kulia.
Na hata mfalme na walinzi wake na Gagula wakaondoka mbio wakakimbilia majumbani, na baada ya dakika chache tukajiona tupo peke yetu pamoja na Foulata, Yule mwanamwali tuliyemwokoa, na Infadus, na wakubwa wengine waliotujia usiku, na maiti ya Skraga mwana wa mfalme.
Nikasema, ‘Wakubwa, tumewaonyesha ishara mliyotaka. Kama mmeridhika, basi twendeni upesi mahali mlipotaja. Hatuwezi sasa kukomesha kitendo chetu.
Giza litaendelea kwa muda wa saa moja na nusu. Haya, na tujifiche kwa giza hili.’
Infadus akasema, ‘Twendeni.’ Akageuka akaenda, na wakubwa wale walimfuata, na sisi na yule mwanamwali tulifuatana nao.
Kabla hatujalifia lango la mji, mwezi uliliwa kabisa na nyota nyingi zikaonekana katika mbingu nyeusi. Tukashikana mikono tukajikokota katika giza.