Hadithi ya kusisimua: Mkataba wa siri - 4

Hadithi ya kusisimua: Mkataba wa siri - 4

Joined
Feb 9, 2014
Posts
20
Reaction score
6
SEHEMU YA NNE


MTUNZI: JOSEPH SHALUWA
ILIPOISHIA...
“Lakini jambo lingine linalowashtua zaidi watu ni tabia yake ya kujipenda kupita kiasi. Muda wote msafi, ananukia marashi, ananyoa vizuri, anavaa nguo nzuri...kwanini ajipende hivyo kama mtoto wa kike? Mchunguze mwanao shoga yangu!”
SASA ENDELEA...

Mama Suma alikuwa kimya kabisa, hakuwa na la kujibu, tayari walikuwa wameshaingia mtaani kwao. Mama Mwaija akaagana na mama Suma ambaye nyumbani kwake ilikuwa mtaa wa pili.
***
Siku nzima mama Suma alishinda na mawazo. Maneno aliyoambiwa na mama Mwaija yalimuumiza sana. Hayakuwa mambo mapya kwake, ila alishtuka baada ya kugundua kwamba kumbe yanajulikana na watu walishaanza kuyajadili!
Hata yeye mwenyewe alikuwa na mawazo sana juu ya tabia ya mwanaye kujipenda kupita kiasi. Jambo lingine lililomtesa ni kutokana na tabia yake ya kutopenda kabisa kuwa karibu na wanawake.
“Mwanangu jamani, hivi inawezekana ni kweli anafanya huo mchezo?” akawaza mama Suma.
“Lakini ngoja nitazungumza na baba yake, lazima nitafute ukweli wa hili jambo, ni aibu sana kwa familia yangu,” akaendelea kuwaza.
Jioni mumewe alivyorejea kutoka kazini, jambo la kwanza kuzungumza naye lilikuwa ni juu ya Suma.
“Kuna nini tena mke wangu?”
“Zungumza na mtoto, Suma anapotea.”
“Kivipi? Bado una yale mambo tu?”
“Siyo ninayo? Hata mtaani sasa wameanza kuyazungumza.”
“Mtaani?”
“Ndiyo.”
“Kivipi?”
Mama Suma akamsimulia mumewe kila kitu jinsi alivyozungumza na mama Mwaija. Baba Suma alishtuka sana, hakutegemea kama mwanaye angekuwa akisemwa hivyo mitaani.
“Ngoja nitakwenda kuzungumza naye.”
“Ndiyo maana alivyoamua kujitegemea amekwenda kupanga Majengo, hataki kukaa hapa mtaani kwa sababu wameshajua tabia yake.”
“Mke wangu acha kumhukumu mtoto kabla hujawa na uhakika, Jumapili nitakwenda kwake, nitajua huko huko.”
“Rajabu ameshaoa, Elibariki ana mchumba, Meshack ndoa yake ilikuwa Jumamosi iliyopita, wote hawa amemaliza nao shule, mbona yeye hana hata mtoto wa kusingiziwa mitaani? Lazima kuna kitu,” akasisitiza mama Suma.
“Nimesema nipe muda nikazungumze naye, ukweli utajulikana mke wangu,” akasema baba Suma.
“Sawa.”
***
Alichelewa sana kutoka kazini siku hiyo, tayari ilikuwa imeshatimu saa moja na dakika zake za jioni. Alikuwa amechoka sana lakini pia alikuwa na hamu ya kujua mengi zaidi kuhusu majini.
Alikuwa amesimama kwenye duka maarufu la viatu mjini Moshi liitwalo Bora, akakumbuka kwamba katika jengo lilelile kuna ukumbi wa sinema wa Plaza. Asingeweza kwenda hadi Majengo akawahi kuangalia kwenye vibanda vya mitaani wakati ukumbi ulikuwa pale pale.
“Tatizo watakuwa na hiyo filamu?” akawaza.
“Ngoja nijaribu,” akajisemea.
Akapandisha juu haraka, ambapo alipita mbele ya duka la vifaa vya ujenzi la Njiwa Hardware, akapanda hadi kwenye ubao wa matangazo ya filamu katika Ukumbi wa Plaza Cinema.
Saa 12:00 jioni – Game in Forest (Billy Blanks)
Saa 2:00 usiku – Vampire’s With True Love (Sarafina Hollins)
Saa 4:00 – Shamba Kubwa - Kiswahili (Mzimuni Theatre Group)
Wengi walikuwa wakifurahia sana kuona kwamba kuna Filamu ya Shamba Kubwa ambayo ni ya Kiswahili. Ilikuwa filamu ya kwanza ya Kiswahili kuoneshwa katika ukumbi huo. Ingawa ratiba ilionesha kwamba ingeoneshwa saa 4:00 usiku, walikuwa tayari kusubiri!
Kwa Suma ilikuwa tofauti kabisa, alirukaruka juu kwa furaha alipoona Filamu ya Saa 2:00 usiku – Vampire’s With True Love, pamoja na elimu yake ya kawaida ya kidato cha nne, aliweza kupata tafsiri rahisi kuwa, sinema ile ilikuwa juu ya majini wenye upendo wa kweli.
“Haya ndiyo mambo ninayoyataka sasa,” akasema moyoni mwake kisha akatoka na kuvuka barabara.
Moja kwa moja aliingia kwenye Mgahawa wa Shaonaro kwa lengo la kupata chakula ili kuvuta muda wa kuingia kwenye sinema. Alikula kijeshi, robo saa kabla ya sinema kuanza tayari alikuwa dirishani akikata tiketi – alichosubiri ilikuwa ni muda tu!
Dakika zilikwenda taratibu sana, lakini hatimaye akaona watu walioingia saa 12 wakitoka, haraka akatupa macho yake kwenye saa yake ya mkononi, zilibaki dakika tano tu. Watu walipoisha, akaingia zake ukumbini na kukaa siti za mbele kabisa akisubiri muda ufike.
Saa 2:00!
Sinema ikaanza!
***
“Majengo Polisi....” sauti ya konda ilisikika akiuliza abiria wake.
“Shusha!” Suma akasema kwa sauti kubwa kwa kuwa alikuwa amekaa siti ya nyuma.
“Polisi?!!!”akauliza tena.
“Amesema shusha....tatizo nyie makonda huwa mnauliza abiria halafu mnatoa vichwa nje, mtasikiaje?” abiria mmoja akadakia.
“Tuliza mzuka, nimesikia.”
Daladala ile iliyotokea Mbuyuni kuelekea Kiboriloni ilisimama kwenye makutano ya barabara ya kuelekea Kituo cha Polisi Majengo. Suma akalipa nauli na kushuka zake, akavuka barabara na kuanza kutembea taratibu.
Akiwa anakaribia kufika Posta, akakutana na msichana mrembo sana. Alikuwa mweupe, mrefu, mwenye tabasamu pana, aliyevalia gauni aina ya dira. Suma alivutiwa naye sana, akamwangalia kwa muda mrefu sana bila kupepesa macho. Alivyokutana naye kabisa, akajifanya kuangalia pembeni.
Walivyopishana, Suma akageuza shingo; akakutana uso kwa uso na yule msichana. Alikuwa na tabasamu pana sana. Wote wakasimama.
“Si vibaya tukisalimiana,” yule msichana akasema akitabasamu.
Suma hakuwahi kupata mshtuko wa moyo kama wakati huo. Alihisi moyo wake kama umepigwa shoti ya umeme baada ya kusikia sauti tamu ya yule dada. Hakukumbuka kama hakumjibu ila naye aliendelea kutabasamu.
“Mambo vipi?” yule dada akasalimia.
“Poa, mzima?” akaitikia Suma.
“Wa afya.”
Wakapeana mikono.
“Mimi naitwa Zakhia, sijui mwenzangu?”
“Suma.”
“Unaishi mitaa gani?”
“Hapo chini, jirani na Makando Bar.”
“Sawa.”
“Wewe je?”
“Nakaa nyuma ya nyumba ya Kishamba Dispensary.”
“Ahsante, nimefurahi kukutana na wewe.”
“Hata mimi pia, ingawa nataka kukuambia jambo litakalokushangaza kidogo,” akasema Zakhia.
“Jambo gani hilo la kushangaza?”
“Samahani lakini, usinielewe vibaya.”
“Niambie.”
“Suma mimi ni mwanamke, najua sina haki ya kueleza hisia zangu kwa mwanaume kwa sababu wengi wanachukulia kama ni tabia mbaya, lakini naogopa kuacha kufanya hivi kwa muda huu maana sina uhakika wa kukutana tena na wewe...” akasema Zakhia kisha akatulia kwa muda.
Pumzi ndefu zilivutwa puani mwa Zakhia, kisha akaanza kuzishusha taratibu kabisa. Suma alikuwa kimya akimsikiliza. Alishahisi jambo lililokuwa njiani kumfikia...
“Hisia? Hisia gani hizo Zakhia?”
“Nakupenda sana!”
Suma akakunja uso.
“Samahani Suma, usinielewe vibaya tafadhali, ni hisia za moyo wangu. Nilijua ungenifikiria vibaya, lakini sina namna ya kuficha hisia hizi wakati ni kweli ninakupenda kutoka ndani ya moyo wangu.”
“Samahani sana Zakhia.”
“Niambie tu!”
“Wewe ni mwanamke mrembo sana, lakini hatuwezi kuwa wapenzi.”
“Kwanini?”
“Basi tu!”
“Au una mtu wako?”
“Sina.”
“Hujanipenda?”
“Hapana.”
“Bali tatizo ni nini sasa?”
“Tatizo ni msimamo wa maisha.”
“Unamaanisha nini?”
“Katika maisha yangu sijapanga kumuoa mwanamke na kumuoa.”
“Kwanini?”
“Ni utaratibu tu.”
“Kwahiyo hutaoa?”
“Hapana...natarajia kuoa lakini siyo bi....” Suma akakatiza sentesi yake baada ya kujisahau na kutoka kumponyoka neno ambalo hakutaka lisikike.
Zakhia akashtuka sana. Hakuelewa alichokuwa akimaanisha Suma. Haraka neno likamponyoka: “Sijakuelewa.”
“Samahani, kwaheri,” akasema Suma kwa sauti ya ukali kidogo kisha akaondoka zake.
“Watu wengine kwa kuingilia maisha ya wenzao bwana...sijui balaa gani hili?” akawaza kichwani mwake Suma.
Zakhia alibaki amesimama kwa mshangao akimsindikiza Suma kwa macho hadi alivyoishilia. Hakuwa na jibu sahihi juu ya yale yaliyotokea.
***
Mtu aliyekuwa akigonga mlangoni asubuhi hiyo ndiye aliyemshtua Suma usingizi. Ilikuwa Jumapili, saa 2:30 za asubuhi. Muda ambao kwa siku ya mapumziko kama hiyo huwa yupo kitandani hadi saa 4. Akatoka kitandani na kusogea hadi mlangoni, akafungua.
Alikuwa ni baba yake mzazi.
“Kumbe baba, karibu sana baba...” akasema Suma kwa furaha.
“Ahsante.”
“Shikamoo mzee.”
“Marhaba,” akaitikia akionekana hana furaha kabisa usoni mwake.
“Vipi baba, mbona kama haupo sawa? Kuna tatizo gani?”
“Tatizo lipo Suma mwanangu, tena tatizo kubwa sana lakini leo nahitaji hili tatizo liishe.”
“Ni nini baba?”
“Matusi tunayotukanwa sasa yanatosha. Njoro nzima inatutusi kwa sababu yako. Umetuvua nguo mwanetu.”
“Ni juu ya nini baba?”
“Wewe una tatizo gani?”
“Kuhusu nini baba?”
“Kwanini hutaki kuoa?”

ITAENDELEA KESHO...
 
MKATABA1.jpg

kitabu cha hiyo hadithi kimeshakamilika, ukitaka kusoma chote mwanzo mpaka mwisho, weka oda yako kupitia namba 0713 165690 nikupe maelekezo ya namna ya kukipata.
 
Back
Top Bottom