Hadithi ya kusisimua: Mkataba wa siri - 3

Hadithi ya kusisimua: Mkataba wa siri - 3

Joined
Feb 9, 2014
Posts
20
Reaction score
6
MTUNZI: JOSEPH SHALUWA
ILIPOISHIA...
Msisimko alioupata ulikuwa mkubwa sana. Pamoja na kufikisha umri wa miaka 22, akiwa tayari ameshamaliza elimu yake ya kidato cha nne, hakufikiria kabisa suala la kuoa binadamu. Alitamani kuoa jini.
SASA ENDELEA...

Aliamini hao ndiyo wangeweza kuwa na upendo wa dhati, wasingemtesa wala kumnyanyasa. Hapo ndipo kulipokuwa na tatizo. Kwa Mkoa wa Kilimanjaro, tena akiwa anaishi katika Manispaa ya Moshi Mjini, katika kitongoji maarufu cha Njoro, stori za majini hazikuchukua nafasi kubwa sana kwa wakazi wa eneo hilo.
Alikulia mikononi mwa wazazi wake wenye kipato cha kawaida kabisa, tena wakiwa wanaishi nyumba ya kupanga hapo Njoro. Walichoweza kufanya kwake, ilikuwa ni kumsomesha kwa uwezo wao wote. Kwa fedha za kuokoteza kwa kufanya biashara ndogondogo na vijibarua visivyo na uhakika!
Alisoma Shule ya Msingi Njoro na baadaye akachaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari JK Nyerere ambapo kwa bahati mbaya hakufanikiwa kuchaguliwa na elimu ya juu zaidi kwa sababu alipata dalaja la nne!
Kwa namna alivyofundishwa na wazazi wake, kwa Suma maisha hayakuwa magumu sana, kwani aliamua kufanya vibarua mbalimbali ili aweze kujikimu. Hakutaka kujihusisha kabisa na mambo ya wasichana.
Alikuwa na msimamo mkali sana kuhusu mambo ya wasichana. Jambo hilo liliwashangaza wengi wakiwemo wazazi wake, maana hata siku moja, hawakuwahi kusikia Suma alikutwa amesimama na msichana mahali.
Miaka mitatu ilipita baada ya kumaliza kidato cha nne, kwa kudunduliza fedha zake, aliweza kupanga chumba chake na kununua vitu vyake vya ndani kisha akahamia Kitongoji cha Majengo. Wengi waliamini Suma alihama kwa lengo la kukwepa maneno ya watu.
Hilo hakujali.
Aliangalia sana maisha yake na namna alivyotamani yawe. Siri kubwa ilikuwa ndani ya moyo wake. Ni kweli alitamani sana kuoa, lakini si binadamu. Alitaka jini! Angempataje? Hilo lilibaki kuwa swali gumu lililomtesa kichwa chake.
“Yes...even devils loves,” (Ndiyo...hata majini wanaweza kupenda) aliwaza Suma akikumbuka sehemu ya jina la ile sinema aliyoiangalia.
“Kwa nini nisioe jini? Mimi sitaki usumbufu na hawa binadamu wenzangu,” akawaza Suma.
“Halafu maisha magumu niliyonayo, nitawezaje kuogeza mtu mwingine wa kunitegemea ambaye naye atazaa wengine na kunizidishia machungu katika hii dunia yenye ubaguzi?
“Ona wenzangu...mbona wanaishi vizuri. Wana majumba ya kifahari, magari na biashara za uhakika...mimi nitawezaje? Nahitaji msaada hakika na mahali pekee nitakapoweza kupata ni kwa majini. Lazima nitampata tu,” akazidi kuwaza Suma.
Ni mawazo yaliyomtesa sana kichwa chake. Hakutaka mateso wala shida maishani mwake. Alihitaji kustarehe na kutulia. Alihitaji faraja ya moyo hakika. Kwake, hapakuwa na binadamu ambaye angekuwa na uvumilivu kama majini aliowaona kwenye sinema za majini.
“Lazima hilo litimie,” akazidi kuwaza.
***
Walikuwa wanawake wawili tu barabarani, wakitembea kwa miguu, vikapu vikiwa juu ya vichwa vyao. Walitokea kununua mahitaji katika soko maarufu la vyakula mjini Moshi – Mbuyuni. Walishavuka kwenye mto mdogo unaopitisha majitaka maarufu kwa jina la Maji Machafu, wakishika njia pembeni ya kiwanda cha zamani cha Pepsi.
Hawa ni mama Suma na mama Mwaija. Kama kawaida ya wanawake, walizungumza mengi sana. Waliongelea ndoa, wakajadili kuhusu maisha na baadaye wakaanza kuwateta watu. Stori zilipoisha, mama Mwaija akaanza mpya...
“Halafu mwenzangu kuna jambo nimelisikia mitaani limeniuma sana, nimelivumilia sana lakini naona limenifika hapa, siwezi kuacha kukuambia, wewe ni shoga yangu.”
“Nini hicho mama Mwaija?” akauliza mama Suma.
“Ni kuhusu mwanao.”
“Yupi sasa? Mwenyewe unajua nina watoto wanne.”
“Suma.”
“Nini tena?”
“Hivi mtoto wenu mzima kweli?”
“Kivipi yaani?”
“Maneno niliyoyasikia, mbona yanatisha? Inasekana eti hawezi kitu!”
Mshtuko mkubwa ukaingia moyoni mwa mama Suma. Zaidi ya mara tatu neno lile likajirudia kichwani mwake; ‘Hivi mtoto wenu mzima kweli?’. Maumivu yasiyoelezeka yakauvamia moyo wake. Hata hivyo hakujua uzima uliozungumziwa.
Alitaka kufungua kinywa chake aulize, akahisi kama kuna kitu kinamkaba na kumzuia kufanya hivyo.
“Mwanangu anaumwa nini?” akajiuliza mwenyewe.
“Lakini haina maana kuumiza kichwa wakati naweza kuuliza,” akajisemea moyoni.
Ukweli ni kwamba siyo hakuweza kuuliza ila aliogopa na hakuwa tayari kusikia tatizo la mwanaye mpendwa. Ya nini ajitese? Kwa nini abaki na maswali? Akaamua kuvunja ukimya...
“Kivipi yaani?”
“Maneno niliyoyasikia, mbona yanatisha? Inasekana eti hawezi kitu!” mama Mwaija akagongelea msumari.
“Mh!”
“Unaguna nini mwenzangu, ndiyo mambo yanayosemwa huko mitaani.”
“Unadhani ni kwa nini wanasema hivyo?”
“Haya mambo yameanzia mbali, inasemekana kwanza hajawahi kuonekana na mwanamke yeyote wa mtaani, halafu kingine ilifikia hatua Tatu akamwambia wazi kuwa anampenda, mwanao akamtukana sana nusu ampige kwa sababu eti alimwambia mambo ya kijinga!”
Mama Mwaija alikuwa anamzunguzia Tatu, mtoto wa mzee Mvungi ambaye anasifika kwa uzuri mtaa mzima. Watu wenye fedha zao waligongana vikumbo kumgombea msichana huyo bila mafanikio. Leo hii eti Suma anatamkiwa na malkia huyo kuwa anampenda halafu anamkataa!
Lazima ushangae!
“Mh! Lakini labda hajamtaka!” akajibu mama Suma kwa lengo la kujiondolea aibu.
“Sawa ila sasa hata akiwa na wenzake, wakianza kuzungumzia mambo ya wasichana huonekana anakasirika na kuondoka zake.”
“Sina uhakika na hili jambo.”
“Usinitaje, mimi nimekuambia tu kama shoga yangu. Sisi wote ni wazazi.”
“Sawa.”
“Lakini jambo lingine linalowashtua zaidi watu ni tabia yake ya kujipenda kupita kiasi. Muda wote msafi, ananukia marashi, ananyoa vizuri, anavaa nguo nzuri...kwanini ajipende hivyo kama mtoto wa kike? Mchunguze mwanao shoga yangu!”

ITAENDELEA KESHO...
 
JOSEPH SHALUWA ni wewe mshauri na mtunzi wa hadithi kwenye magazeti pendwa/udaku?
 
Last edited by a moderator:
Wee mwamndishi unajuaje ni ya kusisismua? Isiponisisismua nakudai fidia.

Wasomaji ndio wanatakiwa waseme ya kusisismua.

Kama kuna mmoja naye niliona kaweka 'ya kusisismua-mimba ya jini'. Tangu lini mimba ya jini ikasisimua?
 
Mkuu hivi unatuchanganya, hadithi yako iweke sehemu moja yote usiwe unaanzisha thread mpya.
 
Back
Top Bottom