HADITHI : SWEET PAIN(MAUMIVU MATAMU)

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,743
25,535
SEHEMU YA 03



David Robert, Mtanzania anayeishi Marekani anaingia Marangu, mkoani Kilimanjaro akiwa na wenzake Wilson Johnson na Joel Poulsen ambao ni wazungu, kwa pamoja wanamsaka msichana mrembo ambaye angeweza kuingia kwenye shindano la kumsaka msanii atakayepewa mkataba wa dola milioni mia moja kwa ajili ya kucheza Sinema ya Sweet Pain huko Marekani.

Muda mwingi, wazungu Wilson Johnson na mwenzake Joel Poulsen walikuwa wakilalamika kuwa wamepoteza muda wao bure kwa kuwa hawakuona wasichana wenye viwango walivyohitaji. Wakiwa katika soko maarufu la mazao la Shokoni, mtazamo wao ulibadilika baada ya kumuona msichana mwenye nguo zilizochoka lakini mwenye sura ya kuvutia kuliko kawaida, Manka.

David ndiye aliyemfuata, akazungumza naye kisha baadaye akamkutanisha na wenzake na kukubaliana kwenda kwa mama yake kwanza. Kila kitu kikawa sawa. Matayarisho ya safari yakafanyika, Manka akaondoka kuelekea Dar es Salaam kuwafuata akina David, lakini nyuma akimuacha mpenzi wake Martin ambaye alikuwa anampenda kuliko kawaida.

Dar es Salaam alikutana na akina David ambao walimpeleka madukani kwa ajili ya kununua nguo na baadaye wakampeleka saluni. Akatengenezwa nywele zake na kubadilika. Manka akawa mpya kabisa.

Wakiwa kwenye ndege, safarini kuelekea Los Angeles, Marekani, Manka alimkumbuka mpenzi wake Martin. Alijitahidi sana kujikaza na kuficha hisia zake, lakini akazidiwa, ghafla machozi yakaanza kuchuruzika machoni mwake.

David pekee ndiye aliyegundua kwamba Manka alikuwa akilia. Alipomuuliza, akamjibu kwa kifupi; Martin!
Je, nini kitatokea? SONGA NAYO...

HISIA kali juu ya mpenzi wake Martin ndizo zilizomjia na kumtesa moyoni. Alitamani sana kwenda Marekani na ni kweli tayari alikuwa angani kwenye ndege akielekea huko, lakini alishindwa kuelewa ni kwa namna gani angeweza kukaa mbali na mpenzi wake.

Haikuwa hiyari yake machozi kumwagika machoni mwake, bali mapenzi mazito ambayo yalishindwa kujificha na kutoka hadharani! Alimpenda sana Martin wake.

David hakuelewa kilichompata Manka, lakini hata alipomtajia jina la Martin alibaki na mshangao, hakuelewa maana yake. Akamwangalia Manka machoni, alipogundua hilo, akazidi kulia.
“Manka tafadhali, acha kulia. Enhee huyo Martin ni nani?”
“Martin?”

“Ndiyo ni nani?”
“Mchumba’angu!”
“Amefanyaje sasa? Ndiye anayekusababisha ulie?”
“Ndiyo...nampenda sana. Sijui ni kwa nini nashindwa kuamini kuwa hatachukua mwanamke mwingine! Naona kama anaweza kunisaliti.”

“Hapana Manka, huna sababu ya kuwaza hivyo, kama anakupenda hawezi kufanya hivyo.”
“Najikuta nimepoteza matumaini kabisa, nahisi kama nimefanya uamuzi mbaya kwenda Marekani.”

“Kwani umesahau kwamba unakwenda kwa ajili ya kutengeneza maisha yako? Kumbuka kwamba iwapo utashinda, utapata dola milioni mia moja, ni fedha nyingi sana ambazo zinaweza kubadilisha kabisa maisha yako.

“Hilo ndilo jambo la msingi zaidi unalopaswa kufikiria kwa sasa, mengine yote achana nayo. Kwa nini usimwamini mwenzako? Halafu hutakiwi kuwa na mawazo, maana unakwenda kushindana, lazima akili yako iwe imetulia kabisa!”
“Sawa kaka David, nimekuelewa vizuri!”

“Kama ndivyo, naomba ufute machozi.”
Manka hakubisha, akafuta machozi na kujitahidi kutulia. Machoni hakuwa na machozi kabisa lakini ndani ya moyo wake alikuwa katika wakati mgumu sana wa mawazo dhidi ya Martin wake.

Hata hivyo, hakukuwa na jinsi, aliutuliza moyo wake, akajitahidi kukubaliana na hali halisi. Safari ikaendelea, ilikuwa ni mara yake ya kwanza kusafiri na ndege, lakini furaha yake ilizimwa na Martin.

***
Walipotua katika uwanja wa ndege, David na wenzake wakaongozana na Manka hadi nje ya uwanja ambapo waliwakuta watu waliofika kuwapokea wanawasubiri wao. Walikuwa ni wanaume wawili, Moses na Jackson.

Walipokutanisha macho yao tu na Manka wote wakaonekana kupagawa. Manka alikuwa mwanamke mrembo kuliko kawaida. Haikuwa rahisi kuamini kwamba alitokea kijijini Shokoni akiwa hana hili wala lile.
Siri iliyokuwa nyuma ya mwonekano wake hawakuijua, waliojua yote hayo ni David na wenzake.

“Sijapata kuona msichana mzuri kama huyu, bila shaka ndiye atakayeshinda!” Jackson akamwambia Moses.
“Ni kweli, kule kuna wasichana wengi wazuri, lakini huyu amewazidi wote. Kwa hakika ni mwanamke mrembo sana!”

Walikuwa wakizungumza wakati akina David na Manka wakiwa wanawakaribia kabisa.
“Poleni sana na safari,” akasema Moses akiwaangalia akina David.
“Ahsante sana!”
“Naona mmekuja na malkia?”

“Ndiyo hivyo, tuna imani anaweza kubahatika!”
“Hongereni sana kwa kazi nzuri!”
“Tunashukuru sana, vipi huku wameshakuja wote?”
“Wengi waliokuwa bado, wameingia juzi, jana na leo, mpaka sasa hivi bado nchi tatu tu; Ghana, Zimbabwe na Malawi, wengine wote tayari.”
“Ok! Basi twendeni hotelini.”

“Karibuni sana...Tanzania ndiyo ina warembo kiasi hicho? Kuna haja ya kwenda kutembea huko siku moja, unaweza kujikuta unaoa Mtanzania...” Moses akatania.
Bila kupoteza muda, wakaingia kwenye magari, safari ya kwenda hotelini ilipo kambi ya warembo hao ikaanza. Njia nzima Manka alikuwa akishangaa jinsi Los Angeles lilivyo katika mpangilio mzuri wa kuvutia.

Kila kitu kilikuwa kipya kwake, hakutegemea kama kuna siku angefika kwenye jimbo kubwa na la kupendeza kiasi kile. Kuna wakati alikuwa akidhani yupo ndotoni, lakini fikra hizo zilikatishwa na matukio yote kufanyika kwa uhalisia.
Isingekuwa rahisi kuwa amelala kwa siku zote hizo, hivyo akaamini kwamba ni kweli alikuwa amekanyaga nchi ya Marekani bila kutegemea.

“Mh! Pazuri sana huku kaka David.”
“Ni kweli, huku wenzetu wameendelea sana, kila kitu ni mipango, kama nasi tukiweka mipango ya muda mrefu, tunaweza kuibadilisha Tanzania yetu!”
“Ni kweli kabisa!”

Safari iliendelea, gari walilopanda David na Manka likiwa limetangulia na lingine lililowabeba Wilson na Joel likiwafuata kwa nyuma. Ni kama Manka alikuwa ameingia kwenye dunia mpya kabisa. Mazingira ya Los Angeles yalimtamanisha sana.
“Belair Hotel!” Manka alisoma maandishi hayo juu ya bango lililokuwa katika lango kubwa la kuingilia katika hoteli hiyo.

Dereva akaendesha taratibu hadi kwenye maegesho, akaegesha. Wote wakashuka, nyuma yao gari lingine likaingia na kuegesha, wakashuka na kuungana na wenzao, kisha wakaongozana kuingia mapokezi.

Manka akafanyiwa usajili kisha akaoneshwa chumba chake ndani ya hoteli hiyo. Alitakiwa kupumzika kwanza, hadi jioni ambapo angekutanishwa na washiriki wengine. Ndivyo ilivyokuwa jioni walikutana kwenye chumba cha mkutano kwa ajili ya kufahamiana.
Kulikuwa na wasichana wengi warembo kutoka nchi mbalimbali za Bara la Afrika, ambao kila mmoja alikuwa anatamani kushinda mkataba huo ambao ungebadilisha kabisa maisha yao.

Siku hiyo waliingia wasichana wawili tu kambini hapo, Manka aliyetokea Kilimanjaro, Tanzania na Wambui aliyetokea Nairobi, Kenya. Kwa kawaida, huanza kuingia wenyeji kwanza kisha wageni kuingia mwishoni.

Wa kwanza kuingia alikuwa ni Wambui ambaye alishangiliwa lakini si kwa kiwango kikubwa. Hatimaye zamu ya Manka ikafika, alipoingia tu kwenye chumba cha mkutano, watu wote wakamtolea macho!

Manka akaogopa sana. Akasita kutembea, akasimama na kujiangalia kama alikuwa amevaa vizuri, aliamini walikuwa wakimshangaa kutokana na kukosea kitu fulani katika mpangilio wa mavazi yake.

Hakujua kwamba, alikuwa kivutio kikubwa kwao! Bila kuelewa kilichotokea, Manka alikuwa akikaribia kunyakua kitita cha dola milioni mia moja!

Je, manka atafanikish ndto ya kuish maisha ya kifahari na martin???
 
mkuu hii si ndo ile ya shigongo kipindi flan alikuwa anaweka kwenye gazeti lake sijui Risasi au Ijumaa??

kama ni yake.. mkuu unaruhusa??
 
mkuu hii si ndo ile ya shigongo kipindi flan alikuwa anaweka kwenye gazeti lake sijui Risasi au Ijumaa??

kama ni yake.. mkuu unaruhusa??
Huyu dogo anamatatizo flani,juzi kaiba makala ya member flani inahusu kifo cha J F Kennedy,then kaja na hadithi sijui yakuitwa Gamboshi leo kaiba na hii tena.
Dogo ni wa kupuuzwa kapata smartphone majuzi.
 
Anatakiwa ajueanachofanya ni kosa kisheria..
Huyu dogo anamatatizo flani,juzi kaiba makala ya member flani inahusu kifo cha J F Kennedy,then kaja na hadithi sijui yakuitwa Gamboshi leo kaiba na hii tena.
Dogo ni wa kupuuzwa kapata smartphone majuzi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom