Hadithi: Rais Anampenda Mke Wangu

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,447
CHAPTER 1
ILIKUWA ni asubuhi tulivu, anga lilifunikwa na mawingu mepesi baada ya wiki nzima ya mvua za vuli . Angalau sasa wakazi wa mji waliweza kutoka majumbani mwao kwenda makazini na maeneo mengine kujitafutia ridhiki bila usumbufu uliotokana na mvua za mfululizo. Jua lilikuwa likichomoza na kuanza kuibadilisha hali ya hewa kutoka kwenye baridi na kuileta kwenye hali ya wastani ambayo haikuleta usumbufu kwa wakazi.

***********

Derrick alikuwa ndani ya gari lake aina ya Land Rover 109 akiwa amefunga mkanda sawasawa kuepuka ajali kwasababu barabara ilikuwa na mashimo mengi. Wakati huo gari za aina hiyo ndizo zilikuwa zinatamba nchini na watu binafsi wachache sana walikuwa nazo. Hizi ndizo zilizoonekana gari za maana sana, na mara nyingi zilikuwa zikitumiwa na watumishi wa serikali. Derrick alikuwa safarini kuelekea kijijini kwa babu yake sehemu ya Nyehungi wilayani Senga.

*************

Safari yake ya siku mbili kutoka jijini Shuntown kupitia Singada, hadi Moroni ilikuwa imemchosha kupita kiasi. Alitamani afike kijijini kwa ili amueleze babu yake kilichokuwa kikimpeleka. Alikuwa ameyachoka maisha ya upweke na alitaka aoe mwanamke kutoka kijijini kama alivyomuahidi mama yake. Derick aliamini mke wake angetoka kijijini ingawa wakati huo hakujua mwanamke huyo mwenye bahati angekuwa nani. Alijua wanawake wazuri ambao hawajaguswa kabisa walikuwepo kijijini ambao wangeweza kuishi na mwanaume na kujenga masha.

*************

Wakati Derrick anakimaliza kijijini cha kalebenzi ili aanze kukitafuta kijiji cha Nyehungi gafla aliona kitu ambacho hakutegemea kukutana nacho pale. Alifikiri labda yupo Mjini ! alishindwa kuendelea ikabidi apunguze mwendo wa gari na kusimama kabisa. Alikuwa amemuona msichana mmoja mrembo sana . Akashusha kiyoo cha gari lake na kuanza kumuita mrembo huyo.

************

Hakutegemea kumuona msichana mzuri kama yule kijijini pale . Alikuwa ni mrefu na mwenye weusi wa asili, ngozi yake ilikuwa line mno pamoja na kuwa ilikuwa imepauka sababu ya kukosa mafuta!

Nywele zake fupi zilimfanya aonekane mzuri na wa kuvutia zaidi. Alikuwa mwembamba na mwenye umbilie la kimitindo! Derrick alishindwa kuendelea . Ndani ya moyo wake alihisi ndiye mwanamke aliyekuwa akimujitaji.

****************

"Wewe msichana hebu njoo hapa" Derrick aliita kwa sauti ya chini lakini msichana yule hakusimama wala kugeuka nyuma kumwangalia. Ikamlazimu Derrick ateremke garini na kuanza kutembea taratibu akimfuata kwa nyuma. "Simama basi!"

Badala ya kusimama msichana yule alitupa mzigo wa kuni aliokuwa ameubeba kichwani na kuanza kukimbia kuingia vuchakani!

Derrick alicheka na kuanza kutembea taratibu kurudi kwenye gari ambako aliwasha gari lake na kuondoka zake kwa kasi. Mbele kidogo alikutana na kundi la vijana walioonekana kama wanatoka porini kukata miti ya kujengea nyumba.

************

Derrick alipunguza tena mwendo wa gari lake na baadae alisimama na kumuita mmoja wa vijana wale na kumsalimia, lakini alionekana kutoelewa Kiswahili vzuri. Baada ya salamu alianza kumtupia maswali.

"Unamfahamu yule msichana mrefu niliyekutana nae pale?" Derrick aliuliza.
" Bing'we alihaya kinehe uyu shi?" (Nyie anasemaje huyu naye") . Kijana yule aliwageukia wenzake na kuwauliza swali katika lugha ya Kisukuma. Bahati mbaya pamoja na wazazi wa Derrick kuwa Wasukuma, yeye kakuelewa kabila hiyo, hivyo hakuelewa kijana yule aliongea nini!.

**************

Mmoja wa vijana katika kundi lile alisogea mbele na kumuuliza Derrick shida yake. Naye aliekeza vizuri nia ya kutaka kumfahamu msichana aliyekutana nae.

"Yule ni motto wa Ng'walimu wetu !" Alijibu kijana yule katika kiswahili chenye lafudhi ya kisukuma.
"Anaitwa nani?"
"La nyumbani anaitwa Kabula, la kanisani anaitwa Diana. "
"Anaishi wapi?"
"Yeye na wazazi wake wanakaa shuleni !"

**************

Tayari Derrick alishapata alichokitaka kutoka kwa vijana wale. Alichukua kitabu kidogo na kuandika kila kitu kwa kumbumbu kumbu zake. Baada ya hilo aliingiza mkono mfukoni akatoa noti ya shilingi kumi na kuwakabidhi wale vijana!. Walishangaa sana hawakutegemea kama wangepata kiasi hicho cha pesa siku hiyo, pesa ambayo kwa siku hizo ilikuwa na thamani sana. Wakashangilia na kuanza kukimbizana kuelekea vichakani, naye akawasha gari na kuandoka.

**************

Ulikuwa umepita mda mrefu sana bila Derrick kufika jijijini kwao. . Mara ya mwisho alifika wakati was mazishi ya baba yake, baada ya hapo hakurudi tena kwakua majukumu ya kuendesha kampuni na mali za baba yake yalimzidi.

*************

Waliongea mengi sana kakini Derrick hakugusia kabisa suala la kutafuta mchumba kijijini ingawa baada ya chakula cha usiku ilibidi amueleze jambo hilo babu yake. Mzee Masalu, kama alivyoitwa babu yake Derrick, alishangaa sana kusikia Derrick alitaka kuoa mwanamke kijijini!. Hakuna mtu aliyetegemea safari hiyo ya Derrick ilikuwa na lengo la kwenda kutafuta mchumba.

**************

"Huko mjini umekosa mchumba mjukuu wangu?"
"Sio hivyo babu ni lazima nifanye kitu nilichomuahudi mama kabla hajafa! Nakumbuka nikishawahi kumwambia sitaoa mwanamke tajiri Bali nitaoa masikini ili nimsaidie maisha na hicho ndicho kimenileta hapa kijini."
"Huyo mwanamke wa kukupa wewe na huo umaridadi wako tutampata wapi?"
"Hilo lisikusumbue baba mimi tayari
nimekwishamuona mwanamke anayefaa kuwa mke wangu!"
"Umemuona wapi?"
"Kijiji cha nyuma sijui kinaitwa Kalebenzi!"
"Ni mtoto wa nani?"
"Mtoto wa mwalimu mkuu wa pale!"

****************

Babu aliinamisha kichwa na kuanza kumfikiria mwanamke huyo yukoje, lakini hakufanikiwa kuoata kumbukumbu yeyote juu ya mwanamke anayezungumziwa . Alimfahamu mwalimu mkuu wa shule ya Kalebenzi lakini hakuwafahamu watoto wake.

"Eti nyie wajukuu mnamfahamu Hugo msichana anayeongelewa?"
"Hapo kwa Mwalimu kuna msichana mmoja tu"
"Anaitwa nani?"
"Anaitwa Kabula au Diana!"
"Anafaa kuolewa na kwenda kuishi mjini kwa mnavyoiona tabia yake?"
"Ah anafaa lakini nwembamba mno, halafu ni mweusi! mimi nafikiri anatakiwa mwanamke mweupe"
"Mimi namtaka huyohuyo babu..! sitaki Mwanamke mnene au mweupe. Huko mjini sio chati kabisa!"
"Sio nini?". Babu aliuliza.
" Sio chati"
"Ndio nini?"
"Yaani hawapendwi kabisa! Babu naomba unisaidue nimuoe msichana Hugo. Sijui nitashukuru vipi babu yangu"
"Kweli unamtaka msichana huyo?"
"Ndio babu na nitafurahi sana!"

*************

Siku iliyofuata bila kuchelewa wazee watatu waliokuwa marafiki wakubwa wa mzee Masalu walitumwa kwenda Kalebenzi.

Waliporudi jioni walikuwa na jibu lililomfurahisha sana Derrick na kumfanya ahisi ushindi moyoni mwake. Alitaka akirudi jijini aende na mwanamke ambaye angebadilisha akili za watu walioamini kuwa wanawake wazuri walikuwa mjini pekee.

"Baba yake amekubali ila ameomba kijana wetu aende akaonane naye na pia akaonane na mwenzaje anayeonekana bado anaogopa kuolewa mjini!" Walisema wazee waliotumwa kwao Kabula.
"Unasikia Derrick ? Kwahiyo ujiandae kesho utaondoka na wenzako wawili mwende huko Kalebenzi mkaonane na Mzee na pamoja na mwanamke unayemtaka....! ila nina wasiwasi kama utamuweza mwanamke wa kijijini!"
" Ndiye ninayemtaka babu"
"Haya kesho nendeni!"

***************

Siku iliyofuata Derrick na wajukuu wenzake wakiume wawili waliondoka kwenda Kalebenzi kwa gari lake. Walipofika walipokekewa vizuri na kukaribishwa ndani! Sekunde chache tuu baada ya kuingia ndani makundi ya watu walijaa nyumbani kwa Mwalimu kuishangaa gari ya Derrick.

"Yee! Yee ! yee! yee! Lolagi!" ( jamani! jamani ! jamani! . Hebu angalieni) .Walizidi kushangaa akinamama wa kisukuma.

Derrick na wenzake walikuwa ndani wakiongea na mzee Cosmas, baba mzazi wa Kabula. Alikuwa akimshangaa sana Derrick. Alimfahamu vizuri marehemu babu yake kwasababu walisoma wote shule ya msingi.

*************

" Ulipokuja kwenye mazishi ya baba yako ulikuwa bado mdogo sana, hivi sasa umeongezeka mwili na urefu"
"Tunakuwa baba sisi si watoto tena! "
"Kweli nyie ndio mnataka mchukue nafasi zetu ! "
Wote walocheka na muda mfupi baadae walikaribishwa chakula. Derrick alitegemea Kabula ndiye angekwenda kutenga chakula mezani na kula nao, lakini haikuwa hivyo!
Walitengewa chakula na wasichana wengine wawili waliokula pamoja nao hadi mwisho.

**************

"Mbona msichana mwenyewe hatumuoni" aliwauliza wenzake.
"Huwezi kumuona sasa hivi mpaka wakati wa kuondoka!" Mmoja wao alijibu.
Na hivyo ndivyo ilivyokuwa . Kabula ndiye aliyewasindikiza Derrick na wenzake kwenda kwenye gari lao wakati wa kuondoka!"

Waliongea maneno mengi na Derrick aliyetumia muda wake mwingi kumueleza Kabula juu ya uzuri wake na kwamba kama angefika mjini angeishi maisha mazuri akiwa mke wake.

****************

"Hujui tu kuwa wewe ni mzuri. Ungekuwa mjini wewe ungeweza kuwa hata mrembo wa nchi yetu na baadae kuwa mrembo wa dunia!"
"Ulenimela!" ( unanitania!" ) Kabula alijibu kwa Kisukuma kiswahili kilionekana kumpa tabu kiasi Fulani.
Derrick alimwangalia Kabula kuanzia kichwani hadi miguuni. Alishindwa kuumaliza uzuri wa msichana yule. Hakutegemea kabisa kukutana na mwanamke mzuri kiasi kile kijijini!.

Waliporudi nyumbani siku hivyo mipango ya kulipa mahari ilifanyika. Babu yake Derrick alitoa ng'ombe 20 kama mahari ya kumuoa Kabula na mipango ya ndoa ikaanza kufanyika na tarehe ikapangwa!. Derrick aliamua kufanya harusi ndogo kijijini, lakini alipanga kufanya kubwa zaidi akifika jijini shuntown . Alitaka kudhibitishia ulimwengu kuwa wanawake wazuri hawakuwa mjini peke yake.

*************

Harusi za vijijini ni tofauti sana na za minni, kijijini hakuna kadi na watu hualikana wenyewe kwenda kwenye harusi . Kinachotakiwa ni kuwepo chakula cha kutosha watu wote, wale wanywe pombe za kienyeji na kushangilia.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Derrick . Mamia ya watu walikusanyika kwa mzee Masalu kushuhudia Derrick akimuoa Kabula. Wazazi wa pande zote mbili waliamua kufanya harusi sehemu moja!. Derrick akawa amemuoa Kabula kama mchezo tuu wa kuigiza, kumbe ndio ulikuwa kweli.

***************

"Naingia 'tauni' na kitu kikali ambacho hakijaguswa wao wenyewe watazima zao. Kwanza nikimfikisha namfungia ndani, saluni humohumo, bi chau humohumo! Kila kitu losheni humohumo ndani. Atakuwa akitoka nje wakati wa kwenda kujifunza gari tu!" Derrick aliwaza.

Alikuwa na hamu sana ya kufika mjini ili awaonyeshe watu mwanamke mzuri aliyemtoa kijijini.
"Najua hawataamini!" Aliendelea kuwaza Derrick.

*************

Baada ya ndoa yao iliyofungwa kienyeji, Derrick na Kabula walikaa nyumbani kwa mzee Masalu kwa muda wa wiki mbili kabla hawajaondoka kwenda Shuntown! Ilitakiwa kuwa safari ya wiki mbili , lakini Derrick, kwa kutumia gari yake hivyo mpya, alisafiri kwa siku moja na nusu tu wakawa wameinga jijini.

Walitakiwa kuingia Shuntown, mji wa Sokomoni SAA 10:00 jioni , lakini Derrick aliamua kupaki gari lake kwa muda maeneo ya Mlandizi akisubiri giza liingie. Hakutaka kabisa mtu amuone Kabula katika hali aliyokuwa nayo.
Alitaka akae ndani kwa muda wa wiki kama tatu hivi akifanyiwa ukarabati wa mwili. Wakati huo Derrick angekuwa akifanya mipango yote ya harusi. Hakutaka mtu yeyote atoe hata senti tano katika harusi hivyo na alikuwa amepania kufanya kila alichiweza mpaka Raisi wa Jamuhuri ya sokomoni ahudhurie harusi yake.

****************
Saa mbili usiku aliingia nyumbani kwake na kumpeleka Kabula moja kwa moja hadi ndani. Walilala mpaka asubuhi. Alichokifanya asubuhi hiyo hakikuwa kingine zaidi ya kutafuta saluni moja ya kupamba mabibi harusi na kuwakodisha kwa ajili ya kazi ya kumremba na kumkarabati Kabula kabla hajatokeza nje.

Siku hiyohiyo alianza kuwatangazia Rafiki zake kuhusu nia yake ya kufunga ndoa. Walipomuuliza ni mwanamke gani alitaka kuoa aliwaambia wasubiri na wangemuona siku ya harusi yenyewe.

*******************

Watu wa kuremba waliendelea na kazi yao kila siku. Nywele za Kabula zilipakwa dawa ya kuzilaiinisha, kucha zilinyooshwa na midomo yake ilipakwa rangi ! Hata Derrick mwenyewe hakuamini kuwa yule alikuwa ni Kabula aliyekutana nae akiwa na mzigo wa kuni kichwani mwake.

****************

"Mtoto anatisha jamani utafikiri Naomi Campbell" Derrick aliwaza baada ya kumuangalia Kabula akiendelea kurembwa.
"Kaka Derrick nakupongeza kwakweli unajua kuchagua! " Mmoja wa warembaji alishindwa kuvumilia na kujikuta akimwambia Derrick maneno hayo.

"Ahsante Dada! "
Derrick alinunua gari ndogo aina ya Peugeot 404 ambayo kila siku jioni dereva maalumu aliyeajiriwa na Derrick akimfundisha Kabula kuendesha gari hiyo! Wakati huo gari hizo ndio zilikuwa maarufu sana kwa ajili ya starehe, tena zilikuwa za kisasa zaidi.

Kwa Kabula mambo yote aliyokuwa akiyaona yalikuwa kama ndogo na yalikuwa yakija gafla mno , kwa wiki chache kabla alikuwa mchafu akihangaija na kuni kijijini, lakini pale alikuwa akishughulikiwa kama Malikia!.

Kila kilichofanyika ndani ilibidi afundishwe na Derrick. Hata kuwasha jiko la umeme Kabula hakuelewa. Ilikuwa ni kazi ngumu kwa Derrick kumfundisha kila kitu, lakini hakuchoka kwasababu alikuwa ameamua kuoa mwanamke wa aina hiyo. Aliamini siku moja angekuwa mtaalamu wa kila kitu ndani ya nyumba yao.

****************

Siku ya harusi yao mamia ya watu walifurika katika ukumbi wa Garden Inn ulikuwa katika jiji la Shuntown, na kama alivyokuwa amepania Derrick , miongoni mwa watu hao alikuwa ni Raisi wa Jamuhuri ya Sokomoni bwana Gabriel Mtomoko!. Idadi kubwa ya mawaziri, maafisa na wafanyabiashara mbalimbali walikuwepo katika harusi hiyo!
Kila mtu aliyekuwa ukumbini alishindwa kuelewa Derrick alimtoa wapi msichana yule.

Uzuri wa Kabula ulimchanganya kila mmoja aliyekuwemo ndani ya ukumbi huo . Hata Raisi mwenyewe ambae mara kwa mara aligeuka kumuuliza mtu aliyekuwa karibu yake habari juu ya Kabula!

****************

"Katika tembea yangu yote sijawahi kuona mwanamke mzuri kama huyu hapa nchini! " alisema Raisi.
Kwa furaha aliyoipata katika harusi hiyo Raisi Gabriel alitangaza kuligaramikia fungate la Derrick na Kabula katika visiwa vya Shelisheli kwa muda wa mwezi mmoja! Na watu wote walishangilia.

Raisi alikuwa amevutiwa waziwazi na uzuri wa Kabula. Alikuwa na sifa zote za kuwa mwanamke aliyetamani kumuoa maishani mwake , lakini hakufanikiwa kumpata! Kiufupi alimtamani na alitaka Kabula awe wake, lakini alishindwa angeanzia wapi kumchukua.

Aliyaogopa yaliyompata Mfalme Daudi, ambae kwa kumtamani Balsheba, mke mzuri sana wa mmoja wa askari wake aliyeitwa Uria, aliamua kumtuma mstari wa mbele kulikokuwa na mapigano makali ili afe na mfalme akamchukua mke wake na kumwoa. Kwa kosa hilo mfalme Daudi alipaya alipata adhabu mbaya kutoka kwa Mungu.

***************

"Adhabu iliyompata mfalme Daudi ilikuwa ni kubwa. Lakini si katika tendo hilo ndipo Mfalme Suleiman akazaliwa!" Aliwaza Raisi Gabriel huku akimuangalia Kabula aliyekuwa mbele yake.

Urefu wake na mwanya uliokuwepo katikati ya meno yake ulimchanganganya Mheshimiwa Raisi na kujikuta akiapa waziwazi kuwa ni lazima angemchukua Kabula hata kama ni kwa garama kubwa kiasi gani.

"Haiwezekani mtu kama Derrick tu aoe mwanamke mzuri kiasi hiki , ni lazima nimchukue atake asitake ! Raisi aliwaza kichwani mwake.

**************

Majira kama ya saa kumi hivi usiku Raisi aliaga na kuruhisiwa kuondoka ukumbini kurejea Ikulu kupumzika . Watu wote ukumbini walisimama wima kumuaga wakati anaondoka . Tofauti na wengi walivyotegemea kuwa Raisi angetoka moja kwa moja nje, lakini baada ya kunyanyuka kutoka mahali alipokuwa amekaa, alitembea kwenda mbele na kuanza kuwakumbatia watu waliokaa viti vya mbele pamoja na bwana harusi.

" Hongera Derrick , umtunze vizuri mtoto wawatu huyu atakuwa mke mzuri sana kwako sawa? Na umenifurahisha sana maana nimesikia umewaacha wote hapa mjini na kutafuta mwenyewe Shamba!" Raisi alimtania kabla ya kumkumbatia Derrick.

*************

Alipomalizana na Derrick kilichofuata kikawa kukumbatiana na Kabula. Mwili wake ulilitetemeka ! Nyota ya Kabula kimapenzi ilimzidi Raisi, jasho jembamba lilimtoka mishipa yote ya fahamu ilikaa tayari kuhisi joto la mwili wa Kabula! Raisi alijishangaa ni kwanini siku hiyo alijisikia hivyo.

Alipomtia Kabula mikononi, Raisi alihisi vinyweleo mwilini mwake vikisimama wima na alianza kusikia baridi!
Alizungusha mikono yake taratibu kukizunguka kiuno cha bibi harusi kisha akasogeza mdomo wake karibu kabisa na sikio la Kabula na kuanza kuongea maneno kwa sauti ya chinichini huku pumzi yake ikipenya taratibu ndani ya sikio la Kabula na kumfanya ahisi uvuguvugu wa kusisimua.

*************

Kabula hakuyaamini macho yake . Katika maisha yake hakuwahi kufikiri kuwa ipo siku angekuja kukumbatiana na Raisi wa nchi yao. Mara nyingi alimuona katika televisheni na magazeti peke yake. Mambo haya yote yaliyokuwa yakitokea katika maisha yake yalikuwa ya gafla mno! Ilikuwa ni kama ndoto kwake na alijisikia yupo juu ya dunia akiangalia kila kitu kwa chini!

" Wewe ni msichana mzuri sana Kabula!"
"Ahsante Mheshimiwa Rahisi" alisema Kabula katika kiswahili chenye lafudhi ya Kisukuma, lakini kabla hajaendekea na shukrani zake Rais akiwa bado amemkumbatia, aliusikia ulimi wa Raisi ukipenya ndani ya sikio lake! Akasikia kitu kama shoti ya umeme ikapita ndani ya sikio lake na kusambaa mwili mzima!"

***********

"Nakupenda sana wewe msichana na ni lazima siku moja uwe mke wangu" Raisi alisema kwa sauti ya chini bila kusikika. Kabula alishindwa ajibu kitu gani kwa suala hilo. Watu walikuwa wamesimama wima wakijaribu kutafakari kilichokuwa kimiendelea mbele ya Raisi na bibi harusi bila kupata majibu .
ITAENDELEA
 
Habari mambo naitwa Mr Equator Nimeandika ujumbe huu kuku omba swala moja tu!
Mimi nimetengeza website ya ku share story ambayo ni http://www.equatorstory.com/
Je umekuwa ukipata tabu kupost story zako hapa?
Hili ndo suluhisho lako.
Mimi nataka nkupe nafasi ya kuwa mmoja wapo wa kwanza kutumia hii website
unda account yako na uweze kupost story yako mpya.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom