Hadithi: Lulu

Wawindaji wale walipiga kelele kama mbwa mwenye shangwe ya kugundua mnyama alipo. Kino akashika kisu chake mkononi barabara akiwa tayari kwa lolote. Alijua alichotakiwa kufanya; kama wawindaji wale wakigundua sehemu aliyofagia nyayo atatakiwa kumrukia mpanda-farasi, kumuua na kuchukua bunduki yake. Hiyo ndiyo nafasi pekee ya kujiokoa aliyokuwa nayo. Walipozidi kukaribia ndivyo Kino alivyozidi kujiweka tayari, akijiandaa kuruka bila wao kutegemea.

Kwenye maficho yao Juana akasikia sauti ya kwato za farasi, na wakati huohuo Koyotito akatoa kelele za kugumia. Haraka Juana akamchukua na kufunga kwa mtandio kisha akampa ziwa anyone, Koyotito akanyamaza.

Wawindaji walipokaribia Kino aliweza kuona miguu yao tu, na miguuu ya farasi. Wawindaji walisimama kwenye lile eneo alilofagia, walilichunguza huku mpanda-farasi akiwa kasimama pembeni. Farasi alipiga kelele kama ya chafya. Wawindaji wakageuka kumuangalia farasi, wakiangalia masikio yake.

Kino akazidi kutulia kimya, alibana pumzi, misuli yake ikazidi kukaza na jasho likamtiririka usoni. Wawindaji wale walisimamam pale kwa muda mrefu, kisha wakaoanza kusogea mbele wakichunguza ardhini. Mpanda-farasi aliwafuata nyuma. Kino alijua kwamba watarudi, watachunguza huku na huko lakini mwishowe watarudi pale alipofagia nyayo.

Alirudi kwenye maficho yao. Safari hii hata hakujihangaisha kuficha alama zake, alikuwa ameacha alama nyingi asizoweza kuzificha. Pale jiwe lilikuwa limeng’oka, hapa matawi yamekatika, kule eneo limevurugwavurugwa. Na zaidi ya yote, alikuwa amehamaki, kitu kilichokuwa kichwani mwake ni kukimbia tu. Alijua kuwa wawindaji wale watayapata mapito yake, na alijua hakuna njia ya kujiokoa zaidi ya kukimbia. Juana alimuangalia mume wangu kwa uso uliojaa maswali.

“Wawindaji, tuondoke haraka.” Alisema Kino.

Lakini ghafla ghafla huzuni na kukata tamaa vikamjaaa Kino. Akasema, “Pengine labda ni vyema nikajipeleka wanikamate.”

Haraka juana akasimama na kusema, “Unafikiri watakurudisha ukiwa hai ukawatuhumu kukupora lulu? Tuondoke haraka.”

Lakini Kino akawa anasita. Juana akasema tena, “Unafikiri wakikukamata wataniacha mimi hai? Unafikiri watamuacha mtoto hai?”

Hoja za Juana zikafanya akili na ujasiri vimrudie. Akauma midomo na macho yake yakawa makali. “Twende. Tutaelekea milimani, pengine tutawapoteza huko.”

Haraka haraka, akakusanya kibuyu, mkoba mdogo walioweka vitu vyao; alivishika kwa mkono wa kushoto huku mkono wa kulia akiwa ameshika kisu chake kikubwa. Alifungua vichaka ili Juana aweze kupita na kisha wakaanza safari kuelekea magharibi, kwenye milima mirefu ya mawe. Walikimbia kidogokidogo kupita kwenye vichaka vifupi. Kino hata hakuhangaika kujaribu kuficha alama za walimopita, walikuwa wamehamaki. Walipokuwa wanakimbia waling’oa mawe hapa na pale na kuangusha majani ya miti. Jua la utosi lilipiga nchi bila huruma. Mbele yao ilikuwepo milima ya mawe, ikiwa na kilele kimesimama wima. Kama wanyama wanaokimbizwa hufanya; Kino alikuwa akikimbia kuelekea kwenye muinuko.

Nchi hii ilikuwa ni kame isiyo na maji, ilijaa mimea ya miba ambayo ilikuwa na uwezo wa kutunza maji, ikiwa na mizizi mirefu iliyoweza kwenda chini sana kusaka maji. Ardhi yake ilikuwa si udongo bali mwamba. Nyasi chache dhaifu zilimea kwenye nyufa za mwamba huu. Vyura wadogo walikuwa wakishangaa familia ya Kino ilipokuwa ikipita na mara chache waliona sungura walioshtushwa na ujio wao wakiruka na kujificha. Jua kali lilikuwa likipiga jangwa hili, mbele yao mlima ule ulionekana kama ni eneo salama na baridi..

Kino alizidi kukaza mwendo. Alijua kitakachotokea. Alifahamu kuwa baada ya mwendo kidogo wawindaji watatambua kuwa wamepotea njia, na watarudi wakiitafuta kwa makini. Muda si mrefu watayapata maficho yao, na kutoka hapo haitakuwa kazi tena kuwafuatilia. Mawe yaliyong’olewa barabarani, majani ya miti yaliyoangushw, matawi yaliyoinama na maeneo ambayo yamekwanguliwa baada ya mguu kuteleza yataonyesha kila kitu. Akilini Kino aliweza kuwaona wawindaji wakifuata alama walizopita kwa shauku huku mpanda-farasi akifuata nyuma. Alifahamu kuwa Mpanda-farasi ndiye atakamilisha kazi kwa bunduki yake, hatathubutu kuwarudisha mjini. Muziki wa uovu ukazidi kuimba kwa sauti kubwa masikioni mwa Kino. Uliimba pamoja na sauti za nchi inayopigwa joto na kelele za nyoka wa jangwani.

Muinuko ukazidi kuwa mkali na mawe yakazidi kuwa makubwa. Lakini sasa umbali wake na wa windaji ulikuwa mkubwa hivyo wakapumzika. Alipanda juu ya jiwe kubwa na kuangalia alikotoka. Hakuweza kuwaona wawindaji, hata mpanda-farasi hakuonekana. Juana yeye alikaa kwenye kivuli cha jiwe lile na kuanza kumnywesha Koyotito maji; ambaye kwa kiu aliyokuwa nayo alikunywa kwa pupa. Japo Juana alikuwa amechoka lakini macho yake yalionyesha nuru. Kino akashuka, Juana akamuona akimuangalia miguuni ambapo alikuwa na majeraha kutokana na mawe na vichaka hapa na pale. Alifunika miguu yake kwa sketi yake haraka na kumpatia Kino kibuyu cha maji lakini Kino alitikisa kichwa kukataa na kulamba midomo yake mikavu kwa ulimi.

“Juana,” alianza kusema Kino. “Wewe utajificha. Mimi nitawaongoza, na wakifika mbali kunifuatilia wewe utaondoka kuelekea kaskazini. Nenda Loreto au Santa Rosalia. Kama nikiweza kuwatoroka nitakufuata huko. Hii ndiyo njia pekee ya kuwa salama.”

Juana alimuangalia Kino machoni kama vile anamshangaa, kisha kwa msisitizo akasema, “Hapana, tutakwenda na wewe.”

“Nikiwa peke yangu ninaweza kwenda kasi zaidi. Ukifuatana nami utamuweka mtoto hatarini.”

“Hapana,” aliendelea kukataa Juana.

“Itakubidi ufanye hivyo. Ni jambo la busara na mimi nimeamua hivyo,” akasema Kino

“Hapana,” akajibu Juana.

Kino akamuangalia mke wake usoni lakini alikutana na uso shupavu. Macho ya Juana yaling’aa. Kino akaishia kutingisha mabega tu asijue la kufanya, lakini mke wake alikuwa amempa nguvu. Walipoanza safari tena haikuwa kwa kukimbia kwa hamaki kama hapo mara ya kwanza.

Kadri walivyokuwa wakizidi kupanda ndivyo nchi nayo ilivyozidi kubadilika, tena haraka. Sasa miamba mikubwa ilichomoza ikiwa na makorongo marefu kati. Kino alijitahidi kutembea juu ya miamba kadri alivyoweza, ilikuwa si rahisi kuacha alama juu ya miamba hivyo alijua hilo litawachelewesha wale wawindaji kuyapata mapito yake. Hakupanda mlima moja kwa moja bali alitembea zigi-zag. Mara nyingine alielekea kusini na kuacha alama na kisha kueleka mlimani tena, akipita juu ya mawe bila kuacha alama. Mlima ulizidi kuwa mkali, alivuta pumzi kwa shida kadri alivyokuwa akipanda.

Jua lilianza kuzama upande mwingine wa mlima ule. Kino akaanza kuelekea kwenye korongo moja lililokuwa limefunga kwa mimea. Alijua kuwa kama kuna sehemu ina maji basi itakuwa ni pale penye mimea iliyofungamana. Na kama kuna njia rahisi ya kuvuka korongo lile basi itakuwa ni pale pia. Kulikuwa na hatari kwa sababu wawindaji nao watatambua hilo, lakini alikuwa ameishiwa maji hivyo wazo hilo hakulizingatia sana. Jua lilipokuwa likizama, Juana na Kino walikuwa wakijikongoja kuelekea kwenye korongo lile kichovu.

Upande wa juu wa korongo lile kulikuwa na chemichemi ndogo ya maji ikibubujika. Chanzo chake ilikuwa ni theluji iliyokuwa sehemu isiyofikiwa na jua mlimani. Ilikuwa ikitoa maji baridi na masafi karibu muda wote, ni muda mfupi tu wa mwaka ilikuwa inakauka. Nyakati za mvua iliweza kuwa mapromoko makubwa ya maji yakishuka korongoni. Ilishuka na kutengeneza kidimbwi; nacho baada ya kujaa maji yakaporomokea kwenye kidimbwi kingine, kijito kilienda kwa mtindo huu kama ngazi hadi kilipopotea kwenye makorongo. Wanyama walitoka kila kona ya nyika ile kuja kunywa maji kwenye kijito hiki. Kondoo mwitu, puma, swala, panya na wengine wengi. Ndege nao walitoka sehemu mbalimbali kuja kweny kijito hiki. Pembeni ya kijito hiki mimea mbalimbali ilijishikiza popote ilipopata nafasi; zabibu-pori, michikichi pori na mingine mingi. Ndani ya vidimbwi walikuwemo vyura, minyooo na viumbe wengine, kitu chochote kilichopenda maji kilikuja mahali hapa. Paka waliwinda mahali hapa, walichafua maji kwa manyoya ya ndege waliowaua na kwa damu. Madimbwi haya madogo yalikuwa sehemu ya uhai sababu ya maji, na sehemu ya kifo sababu ya maji.

Wakati Juana na Kino wanafika sehemu ya maji jua lilikuwa limezama upande wa pili wa milima. Kutoka eneo hilo waliweza kuona sehemu kubwa ya jangwa hadi kwenye ghuba ya bluu iliyokuwa mbali mashariki. Walifika kwenye kidimbwi wakiwa wamechoka sana, Juana alipiga magoti na kumuosha Koyotito uso, kisha akajaza kibuyu maji na kumnywesha. Mtoto alikuwa amechoka sana hivyo alikuwa anasumbua sana, hadi Juana alipompatia ziwa ndipo akatulia. Kino alikunywa maji kidimbwini kwa muda mrefu, kisha akakaa kwa kuridhika akimuangalia Juana akimlisha mtoto. Baada ya kupumzika kidogo akaenda kwenye sehemu ambayo kijito kilikuwa kinaporomoka kwenda chini na kuanza kuangalia uwanda wa chini kwa makini. Macho yake yakaona kitu na akabaki amekikodolea. Mbali bondeni aliweza kuwaona wale wawindaji wawili; walionekana kama nukta tu au sisimizi, na nyuma yao alionekana sisimizi mkubwa zaidi.

Juana alikuwa akimuangalia mume wake na akaona jinsi mgongo wake ulivyojikaza.

“Wako umbali gani?” aliuliza

“Kufika jioni watakuwa hapa,” alijibu Kino.

“Inabidi tuelekee magharibi,” alisema Kino huku akiangalia upande ule yanakotokea maji. Aliona mapango yaliyotengenezwa na maji. Alivua ndala zake na kupamba kuyaelekea, alipoyafikia aliona kuwa yana ukubwa wa futi kadhaa tu, yakiwa na mteremko kidogo kuelekea ndani. Kino aliingia kwenye pango kubwa, aliona kuwa mtu akiwa nje hataweza kumuona. Alirudi haraka kwa Juana.

“Tukajifiche mule pangoni. Pengine hawatatuona.” Alimwambia mkewe.
 
Juana hakubisha wala kuhoji, akajaza kibuyu chake maji hadi juu, Kino akamsaidia kupanda kwenda kwenye lile pango, kisha akakusanya mizigo yao na kumpatia. Juana akakaa mule pangoni akimuangalia mume wake, alimuona kuwa hakujiahangaisha kufuta alama walizoacha mchangani kando ya kidimbwi, badala yake alipanda upande wa pili wa kingo ya kijito kama umbali wa futi mia moja, akivuruga vichaka kutengeneza njia. Aliporudi akaanza kuchunguza vizuri sehemu ya kupandia kwenye pango kuona kama hakuna alama yoyote kisha naye akapanda pangoni na kukaa pembeni ya Juana.

“Wakipita kuelekea juu sisi tutatoroka kushuka chini tena. Wasiwasi wangu ni kuwa pengine mtoto atalia. Jitahidi kuhakikisha halii.”

“Hatalia,” alisema Juana huku akimuinua mtoto na kumtazama machoni, Koyotito naye alimkodolea macho. “Anafahamu tunachopitia.”

Kino akalala karibu na muingilio wa pango, kidevu amekiweka juu ya mikono aliyoikunja umbo la X. alikuwa akiangalia kivuli cha mlima kilivyokuwa kikiongezeka urefu polepole hadi kikafika kwenye ghuba.

Wawindaji hawakuonekana kabisa, ilionekana walipata tabu kugundua mapito ya Kino. Walipofika kwenye kidimbwi jua lilikuwa linamalizia kuzama. Wote walikuwa wanatembea kwa miguu sababu farasi hakuweza kupita mteremko mkali kuelekea kidimbwini. Wale wawindaji wawili walichunguza kwa makini mchanga pale pembeni ya kidimbwi na wakaona alama zikivuka upande wa pili kisha wakaanza kunywa maji. Mpanda-farasi akakaa kupumzika, na wawindaji wakachuchumaa karibu yake. Moto wa sigara zao ulionekana ukiwaka na kupungua. Kino akaona kuwa walianza kula, akasikia minong’ono ya sauti zao.

Giza zito likatanda kwenye korongo lile. Wanyama waliozoea kuja kunywa maji walifika, lakini waliponusa harufu ya binadamu waliondoka zao.

Nyuma yake Kino alimsikia Juana akinong’ona, “Koyotito. “ akijaribu kumnyamazisha mtoto. Kwa jinsi sauti ilivyotoka alitambua kuwa Juana alikuwa amemziba mtoto mdomo kwa mtandio.

Chini yake kwenye ufukwe wa kidimbwi aliona njiti ikiwashwa, na katika huo mwanga aliona kuwa wawili kati ya wale watu walikuwa wamelala, wamejikunyata kama mbwa. Mtu wa tatu alikuwa akilinda, na aliona mng’ao wa bunduki. Mwanga wa njiti ukazima lakini uliacha picha machoni mwa Kino. Wanaume wawili walikuwa wamelala kwa kujikunyata, na mmoja amechuchumaa mchangani, bunduki ikiwa kati ya miguu yake.

Polepole Kino alirudi pangoni. Alisogea karibu ya Juana na Kumnong’oneza sikioni.

“Kuna namna ya kuwashambulia.’

“Watakuua,” alisema Juana

“Kama nikifanikiwa kumshambulia yule mwenye bunduki nitakuwa salama,” alisema Kino. “Wengine wamelala.”

Juana akamshika mkono Kino na kumwambia. “Wataona nguo zako nyeupe kwenye mwanga wa nyota.”

“Hawawezi, na natakiwa kwenda kabla mwezi haujatoka.”

Kino akafikiria kwa muda akitafuta maneno ya faraja lakini hakuyapata. Mwishowe akasema, “Kama wakiniua lala kimya kabisa. Wakishaondoka elekea Loreto.”

Mikono ya Juana ikatetemeka kwa hofu.

“Hakuna njia nyingine, bila hivyo asubuhi watatupata,” alisema Kino.

Kwa sauti ya kutetemeka Juana akasema. “Mungu awe nawe.”

Kino alimuangalia mke wake usoni. Akamshika mtoto wake kichwani. Kisha akamshika shavuni.

Kwa kuangalia uelekeo wa muingilio wa pango Juana aliweza kumuona kino akivua nguo zake. Japo zilikuwa ni nguo chafu lakini zingeweza kuonekana kwenye giza. Ngozi yake ya kahawia ndiyo ilikuwa ulinzi wake bora zaidi. Kisha akamuona akichomeka kisu chake kwenye kamba yake ya shingoni. Kisu kilining’inia kifuani mwake na kuacha mikono yake yote huru. Hakurudi kumuaga, kimyakimya akatokomea.

Juana alisogea karibu na muingilio wa pango na kutazama nje. Alikuwa kama bundi kwenye kiota chake mlimani. Mtoto wake alikuwa amelala mgongoni mwake, akihisi pumzi yake ya moto shingoni mwake. Juana akasema sala zake kwa kunong’ona, sala ya salamu Maria na sala za mababu zake.

Giza halikuwa zito sana, upande wa mashariki radi ilionekana, alipotizama chini aliona mwanga wa sigara ya mlinzi wa zamu.

Kino alishuka ule mwamba polepole kama mjusi. Alikuwa amegeuza kamba yake hivyo kisu kilinig’inia mgongoni mwake, ilifanya hivyo ili kisiweze kugongana na mawe. Alishuka polepole akijishikiza kwa vidole vya mikono na miguu mwambani. Alikuwa kama ameukumbatia mwamba ule. Alifahamu kuwa kelele yoyote, kujikwaruza, kuteleza, kupumua kwa nguvu, jiwe kuporomoka au sauti yoyote isiyoendana na sauti za usiku kutamshtua mlizi wa zamu. Lakini usiku haukuwa kimya kabisa; vyura walioishi karibu na kijito walipiga kelele na nyenze walipiga kelele kali zilizosikika bondeni kote. Kichwani kwa Kino kulikuwa na muziki wa aina yake, muziki wa adui ukipiga kwa sauti ya chini ukiwa umechanganyikana na muziki wa familia uliopiga kwa sauti ya juu na kali, kali kama mlio wa hasira wa puma jike. Muziki wa familia ndiyo uliokuwa ukimsukuma kumshukia adui. Ilionekana kama nyenze na vyura waliimba pamoja naye.

Kama kivuli, Kino alishuka mpaka chini kwenye mchanga wa fukwe ya kidimbwi. Alishuka kwa tahadhari bila kupiga kelele. Alitambua kuwa japo ni usiku lakini mlinzi akiangalia upande aliopo anaweza kuona umbo lake kwenye mwamba. Ilimchukua muda mrefu sana kufika chini.

Sasa umbali wake na adui ulikuwa kama futi ishirini tu. Alijaribu kukumbuka ardhi ya eneo lile ilikuwa namna gani; je kuna jiwe lolote linaloweza mfanya ajikwae? Alipotazma mashariki aliona ishara za mwezi kuandama muda wowote, na anatakiwa kushambulia kabla ya mwezi kutoka. Aliweza kuona umbo la mlinzi lakini hakuweza kuwaona wale waliolala, alifahamu kuwa mtu wa muhimu kabisa ni mlinzi. Polepole alifungua kisu chake kutoka kwenye kamba ya shingoni. Lakini tayari akawa amechelewa.

Alipoinuka tayari mwezi ukawa umeshotoka pande za mashariki. Akarudi haraka kichakani.

Mwezi ulitoa mwanga mkali na kutengeneza vivuli korongoni pote. Sasa Kino aliweza kumuona mlinzi waziwazi; alikuwa amekaa karibu na kidimbwi. Mlinzi aliuangalia mwezi na kisha akawasha sigara yake, mwanga wa njiti ulimulika uso wake kwa sekunde kadhaa. Kino aliwaza kuwa hatakiwi kusubiri zaidi. Mara tu mlinzi atakapogeuka amrukie. Miguu yake ilikaza kujiandaa na shambulio.

Ghafla kilio kilisikika kutoka kule juu pangoni. Mlinzi aligeuka kusikiliza kisha akasimama. Mmoja kati ya waliolala akatikisika, akaamka na kwa sauti ya usingizi akauliza, “Ni nini?”

“Sifahamu,” alijibu mlinzi. “Ni kama kilio cha mtu-kilio cha mtoto.”

Yule aliyeamka akasema, “Atakuwa mbweha mwenye watoto. Nimewahi sikia mtoto wa mbweha akilia kama mtoto wa binadamu.”

Jasho lilimtoka Kino kwenye paji la uso. Kilio kikasikika tena na mlinzi akaangalia ule upande wenye pango. “Pengine ni mbweha kweli,” alijisemea. Hapo Kino akasikia bunduki ikiwekwa tayari kupiga.

“Kama ni mbweha hii itamnyamazisha,” alisema mlinzi huku akilenga bunduki yake kuelekea juu pangoni.
 
Kino aliruka! Akiwa hewani mlio mkubwa wa bunduki ulisikika. Kisu chake kikazama shingoni, hadi ndani kabisa kifuani mwa mlinzi yule. Kino akawa kama mbogo mwenye hasira. Haraka alikamata bunduki huku anachomoa kisu chake. Nguvu zake na kasi yake vilikuwa kama vya mashine. Alimponda muwindaji aliyefuatia kichwa kwa bunduki kama vile anaponda tikiti maji. Mtu wa tatu alitambaa kama mdudu kaa; aliingia dimbwini na kuanza kupanda upande wa pili akiwa amehamaki, akiparamia mimea ya ukingoni huku akihema kwa kasi na kuongea maneno yasiyoeleweka. Kino alikuwa amekuwa hatari na asiye na huruma kama chuma. Alimnyooshea bunduki na kupiga. Alimuona adui yake akiangukia ndani ya kidimbwi, Kino akaingia ndani ya maji. Kwa mwanga wa mwezi akamuona adui yake akiwa na macho yaliyojaa hofu kuu. Akamlenga na kumpiga risasi kwenye paji la uso.

Sasa Kino akabaki amesimama hajielewi. Kuna kitu aliona hakiko sawa, kuna ishara ilikuwa inataka kumwambia kitu. Wakati huu nyenze na vyura walikuwa kimya kabisa. Hapo akili ikamjia Kino, aliijua sauti aliyoisikia, kilio kikali cha uchungu kilisikika kutoka pangoni, kilio cha mauti.

Kila mtu katika mji wa La Paz anakumbuka kurudi kwa familia ya Kino; wapo wazee wachache ambao walishuhudia, lakini hata wale waliosimuliwa na na baba au babu zao wanakumbuka vyema. Ni tukio lililomgusa kila mtu.

Ilikuwa ni karibu na jioni ambapo wavulana walikimbia kwa shauku mjini wakisambaza habari kwamba Kino na Juana wanarudi. Kila mtu alifanya haraka kwenda kuwaona. Jua lilikuwa linazama kwenye milima ya magharibi, na vivuli virefu vilitokea ardhini. Pengine hilo ndilo linalofanya wale waliowashuhudia wakumbuke mpaka leo.

Juana na Kino waliingia mjini wakitembea bega kwa bega, si kama ilivyo kawaida; Kino mbele, Juana nyuma. Jua lilikuwa mgongoni mwao hivyo vivuli vyao virefu viliwatangulia mbele, walionekana kama wamebeba minara miwili ya mashaka. Kino amebeba bunduki mkononi, na Juana alikuwa amebeba mtandio begani mwake kama furushi. Ndani yake kulikuwa na mzigo mdogo. Mtandio ulikuwa umekakamaa kwa damu iliyokauka, na ulitikisika huku na huko alivyokuwa akienda. Uso wake ulikuwa mzito na uliochoka, na wakati huo huo ukiwa umekaza kwa jinsi alivyopambana na uchovu. Macho yake makubwa yalionekana kama yanamtazama yeye mwenyewe. Alikuwa mbali kama mbingu ilivyo mbali. Midomo ya Kino ilikuwa imekaza, na watu wanasema alikuwa na utisho ndani yake, kwamba alikuwa hatari kama tufani inayojiandaa. Watu wanasema kuwa wawili hawa hawakuwa kama watu; kwamba walipita katikati ya uchungu na kutokea upande wa pili; kwamba ni kama kulikuwa na kitu kisicho cha kawaida kikiwazunguka. Watu waliokimbia kwenda kuwaona, walirudi nyuma na kukaa pembeni haraka kuwaacha wapite. Hakuna aliyethubutu kuwaongelesha.

Kino na Juana walipita kwenye mji kama vile ulikuwa haupo. Hawakuangalia kulia wala kushoto, juu wala chini, walikaza macho mbele tu. Miguu yao ilitembea kwa kukakamaa, na utisho mweusi ulikuwa pamoja nao. Walipokuwa wanapita mjini walanguzi waliwachungulia kupitia madirishani, vijakazi walichungulia kupitia magetini, na wamama walificha nyuso za watoto wao kwenye sketi zao. Kino na Juana walitembea bega kwa bega kupita mjini hadi kule kwenye nyumba za miti, majirani zao walisimama pembeni wakiwapisha wapite. Juan Tomas aliinua mkono kuwasalimu lakini hakusema salamu yenyewe, kwa sekunde kadhaa aliacha mkono hewani akiwa ameduwaa.

Ndani ya masikio ya Kino wimbo wa familia ulikuwa mkali kama kilio. Hakujali kitu, wimbo wa familia uligeuka wimbo wa vita. Walipita kwenye eneo ambalo nyumba yao ilikuwapo bila hata kupaangalia. Walipita vichaka vya pembeni ya fukwe na kuelekea baharini. Wala hawakuangalia mtumbwi wa Kino ulioharibiwa.

Walipofika kando ya maji walisimama na kuangalia ghuba ile. Kino akaweka bunduki chini, kisha akaingiza mkono mfukoni na kutoa lulu yake. Aliiangalia na ilionekana kama ni ya kijivu na yenye kasoro. Sura ovu zilionekana ndani yake, na aliona mwanga wa moto. Aliona pia sura ya mtu aliyejaa uoga ndani ya kidimbwi. Alimuona pia Koyotito akiwa amelala pangoni, nusu ya kichwa chake imeondolewa kwa risasi. Lulu ilionekana mbaya kabisa ilikuwa ya kijivu, ilikuwa kama kansa. Alisikia muziki wa lulu, mbaya na wa ukichaa. Mikono ilimtetemeka, akageuka kumpatia Juana lulu. Juana alisimama pembeni yake, bado akiwa amebeba maiti begani. Aliingalia lulu kwa sekunde kadhaa, kisha akamuangalia Kino machoni na kwa sauti ya upole akasema, “Hapana.”

Kino akajianza na kurusha lulu ile kwa nguvu zake zote. Waliitazama ikienda, ikingaa kwa kupigwa na jua. Waliona ikipiga maji kwa mbali, walisimama pale wakiangalia eneo lile kwa muda mrefu.

Lulu ilipiga maji ya kijani na kuzama hadi sakafuni. Mwani uliiita na kuikaribisha. Ilionekana ikiwa na mg’ao wa kijani. Ikatwama kwenye sakafu ya mchanga kati ya mimea iliyokuwa kama mifeni. Juu yake, uso wa bahari ulikuwa kama kioo cha kijani. Lulu ikiwa imetulia sakafuni. Pembeni yake kaa alitibua mchanga na kuchafua maji, mchanga ulipotua lulu haikuonekana tena.

Muziki wa lulu ukafifia kuwa mno’ngono, na mwishowe kuzimika kabisa.

MWISHO
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom