Lycaon pictus
JF-Expert Member
- Jan 31, 2021
- 7,206
- 12,706
Haditi hii ni tafsiri ya hadithi inayoitwa The Pearl iliyoandikwa na John Steinbeck.
Unaweza kusoma hadithi hii na nyingine nyingi kwenye app yetu. huu uzi una maelezo zaidi.
LULU
Sura ya Kwanza
Kino aliamka alfajiri na mapema kabla hata ya giza kuisha. Nyota bado zilikuwa zinaonekana angani na mwanga wa jua ulionekana kwa mbali upande wa mashariki. Jogoo walikuwa wameanza kuwika na nguruwe walikuwa wakitafutiza-tafutiza kwenye mabaki waliyokula jana. Nje ya nyumba yake ya fito kwenye mti wa mituna, kulikuwa na kundi la ndege wadogo waliokuwa wakiruka na kupiga kelele huku na kule.
Kino alifumbua macho, kitu cha kwanza kukiona ulikuwa ni mlango, mwanga ulikuwa umetengeneza umbo la mstatili kufuata umbo la mlango, kisha akaangalia kitanda cha kubembea ambacho Koyotito, mwanawe alikuwa amelala. Akageuza kichwa upande wa pili na kumuangalia mke wake Juana aliyekuwa pembeni yake mkekani. Alikuwa kajifunika mtandio wake wa bluu kuzunguka kichwa, ukifunika pua na kufika hadi kifuani.
Juana alikuwa ameshaamka. Kino hakumbuki ni lini amewahi amka na kukuta mke wake hajaamka. Macho meusi ya Juana yalikuwa yaking'aa. Yalikuwa yakimtazama Kino kama ambavyo humtazama siku zote aamkapo.
Kino akasikia sauti ya mawimbi dhaifu yakipiga ufukweni. Ilikuwa ni sauti nzuri sana masikioni mwake. Akafumba macho kuisikiliza vizuri, ilikuwa kama kusikiliza muziki. Pengine ni yeye pekee hufanya hivi, au pengine watu wote wa jamii yake hufanya hivi. Hapo kale watu wa jamii yake walikuwa ni wanamuziki hodari, hivyo kila walichoona, kufikiri au kusikia walikibadilisha kuwa nyimbo. Lakini sasa nyimbo zote zilikuwa ni za zamani, Kino alizifahamu zote lakini hakuna nyimbo mpya zilioongezwa. Hilo halimaanishi kuwa watu hawakuwa na nyimbo zao binafsi. Ndani ya kichwa cha Kino kulikuwa na wimbo, wimbo laini. Na kama angeweza kuipa jina basi angesema ni Wimbo wa Familia.
Akajifunika blanketi hadi kuziba pua ili kujilinda na hewa yenye unyevunyevu ya asubuhi. Pembeni yake Juana aliamka polepole bila kupiga kelele. Akiwa pekupeku akatembea hadi kwenye kitanda cha bembea alichokuwa amelala Koyotito. Akamuinamia na kunong'ona maneno kadhaa. Koyotito akafumbua macho kumuangalia, kisha akayafumba na kuendelea kulala.
Juana alienda sehemu ya kuwashia moto na kutoa kipande cha mkaa kinachowaka. Kipande hicho alikifukia kwenye majivu jana usiku. Alikipuliza huku akikichochea kwa vipande vidogovidogo vya kuni.
Kino naye akasimama na kujifunika blanketi akiacha macho tu. Akavaa makubazi na kuelekea. Alipofika mlangoni akainama na kukusanya blanketi ili lisiburuzike chini, akatoka kwenda kuangalia mapambazuko.
Alipofika nje mbuzi mmoja akamsogelea, akamnusa na kuanza kumkodolea macho. Nyuma yake moto ulikuwa umeshakolea na kutoa mwanga uliopita huku na kule.
Sasa muziki wa familia ukawa unasikika nyuma ya Kino, na ala yake ilikuwa ni sauti ya jiwe la kusaga; Juana alipokuwa anasaga mahindi ili kuoka keki za asubuhi.
Sasa mapambazuko yakaja haraka na mwanga wa jua ukashuka kwenye ghuba ile kama mlipuko. Kino akainamisha macho chini kujikinga na mwanga mkali. Alikuwa akisikia keki zikikandwa na harufu yake tamu zilipokuwa zikiokwa.
Siafu nao walikuwa na harakati nyingi ardhini, siafu wakubwa weusi na wadogo wa kahawia. Kino alimtazama siafu mdogo aliyekuwa anahangaika kujitoa kwenye mtego wa fukufuku, aliangalia kama vile yeye ni Mungu juu yao. Mbwa mmoja aliyekondeana na muoga akaja karibu yake, maneno laini ya Kino yakamfanya ajikunje na kulala miguuni mwake. Alikuwa ni mbwa mweusi akiwa na mabaka ya njano sehemu aliyotakiwa kuwa na nyusi. Kiujumla ilikuwa ni asubuhi kama asubuhi zingine, asubuhi njema.
Kino akasikia sauti ya kitanda cha kubembea cha Koyotito. Juana alikuwa amemchukua ili kumsafisha na kisha akamfunga na kumbeba kifuani mwake. Kino aliweza kuona yote hayo bila ya kuangalia. Juana akaanza kuimba moja ya nyimbo za kale, sehemu ya wimbo wa familia.
Nje ya nyumba yao kulikuwa na nyumba zingine za miti. Moshi ulionekana ukitoka kwenye nyumba hizo. Hizi zilikuwa na nyimbo zao, mambo yao, na wake tofauti na Juana.
Kino alikuwa ni kijana mwenye nguvu, nywele zake nyeusi zikifunika na kuning'inia kwenye paji lake la uso, macho yake yalikuwa makali sana. Mustachi wake mwembamba ulimkaa vema. Sasa baada ya hewa yenye unyevu kuisha, alikuwa ameshusha blanketi lake kufika usoni. Pembeni aliona jogoo wakijiandaa kupigana na juu aliona njiwa pori wakiruka. Dunia ilikuwa imeshaamka, hapo akasimama na kurudi ndani.
Alipofika ndani, Juana akasimama na kumrudisha Koyotito kwenye kitanda chake kisha akabana nywele zake kwa utepe wa kijani. Kino akachuchumaa karibu na moto, akachukua keki ya mahindi akaichovya kwenye mchuzi na kuanza kula. Ukiacha kile cha siku za sikukuu, hiki ndicho kifungua kinywa pekee alichikijua. Kino alipomaliza kula, Juana naye akapata kifungua kinywa. Walikuwa wamezungumza mara moja tu, hakukuwa na haja ya kuzungumza sababu kila kitu kilizoeleka. Mazungumzo yenyewe ni pale kino alipovuta pumzi kuashiria kuwa ameshiba.
Mwanga wa jua ukaanza kuingia ndani na baadhi ya miale ikatua na kuangaza kitanda cha Koyotito. Ghafla wakatulia kama waliopigwa na bumbuwazi. Kuna kitu kilikuwa kinatembea kwenye kitanda cha Koyotito. Kilikuwa kwenye kamba iliyofungwa kwenye paa kushikilia kitanda, na kilikuwa kikishuka kuelekea kwenye kitanda cha bembea cha Koyotito. Alikuwa ni nge aliyekuwa akishuka polepole huku mkia amesimamisha, akiwa tayari kushambulia muda wowote.
Pumzi ilimtoka Kino kwa kasi hadi akaacha mdomo wazi. Wimbo mpya ukawa umeingia kwenye familia, wimbo wa uovu, muziki wa adui.
Nge aliendelea kushuka polepole kwenye ile kamba. Juana akaanza kusema maneno; sala za kujilinda dhidi ya hatari kama ile kulingana na desturi zao, akaongezea kwa kusali sala ya bikira Maria. Kino yeye akaanza kusogelea kitanda cha Koyotito polepole na bila kufanya kelele. Alikuwa kanyoosha mikono mbele kama mtu anayetaka kupiga makofi au kudaka kitu, macho yote yakiwa kwa yule nge.
Ndani ya kitanda Koyotito alikuwa akicheka na kuinua mkono amshike nge yule. Kino alipozidi kusogea, nge yule akahisi hatari, alisimama na kuinua mkia wake juu mgongoni. Mwiba ulio mwisho wa mkia wake uling'aa.
Kino akasimama kimya, Juana yeye aliendelea kunong'ona sala zake, muziki wa adui ulisikika. Kino akapeleka mikono yake mbele taratibu sana. Mkia wa nge ukasimama wima zaidi, wakati huohuo Koyotito alikuwa akicheka, akatingisha kamba na nge akamuangukia.
Kino akawahi amdake lakini akapita na kuanguka kwenye bega la Koyotito. Akamdunga. Kino akamkamata nge yule na kumsaga katikati ya vidole vyake. Akamtupa chini na kuanza kumponda kwa ngumi yake. Koyotito alilia kwa maumivu makali lakini Kino akaendelea kumponda nge yule mpaka akasagika na kuwa alama ya majimaji sakafuni. Alikuwa kapandwa na hasira huku macho yamemuiva.
Juana akambeba mtoto na kuona alipochomwa, tayari palikuwa pameanza kuweka wekundu. Akaweka mdomo wake hapo, akanyonya na kutema, akanyonya tena na kutema. Koyotito alilia kwa sauti kubwa sana. Kino alizungukazunguka asijue la kufanya.
Kilio cha mtoto kiliwaleta majirani, wakakusanyika nje ya nyumba yao. Juan Tomasi, kaka yake Kino na mke wake mnene; Apolonia na watoto wao wanne walijazana mlangoni hadi kuziba njia. Nyuma yao majirani wengine walikuwa wakijitahidi kuchungulia ndani. Wale waliombele waliwataarifu wale wa nyuma; "Nge, mtoto ameumwa na nge."
Juana akawa ameacha kunyonya sumu, tobo alipochomwa mtoto lilikuwa limetanuka na kuwa jeupe pembeni kwa kunyonywa. Lakini uvimbe mwekundu ukawa umesambaa sehemu kubwa zaidi.
Watu wote walikuwa wanajua kuhusu nge. Mtu mzima anaweza kuwa mgonjwa sana akidungwa, lakini mtoto anaweza kufa kirahisi. Walijua kuwa mwanzo huanza uvimbe, homa na koo kubana, baadaye tumbo huanza kunyonga na mwishowe, kama sumu iliyoingia na nyingi, Koyotito anaweza kufa. Sasa maumivu ya kudungwa yakianza kupungua na kilio cha Koyotito kikawa cha kugugumia tu.
Mara zote Kino alishangazwa na tabia ya mke wake, alikuwa ni mtu mwenye subira na kwa muonekano alionekana ni dhaifu, lakini kwa ndani alikuwa ni mtu jasiri sana. Juana aliyekuwa na subira na, mchangamfu, mwenye heshima na mtii aliyeweza kujikunyata kwa maumivu bila kulia kwa sauti. Aliweza kuvumilia kuchoka na njaa kuliko hata Kino. Walipokuwa ndani ya mtumbwi, Juana alifanya mambo kama mwanaume mwenye nguvu. Na hata sasa alifanya jambo la kushangaza sana.
“Daktari,” alisema Juana. “Nenda kamwite daktari.”
Habari zikasambaa kuwafikia majirani waliokuwa wamebanana nje ya uzio wa nyumba yao. Nao walikuwa wakiongea kati yao.
“Juana anamtaka daktari.”
Lilikuwa jambo la kustaajabisha kumtaka daktari. Daktari hajawahi kuja huku kwenye nyumba za miti. Kwanini aje huku wakati alikuwa anapata pesa za kutosha kuwahudumia matajiri walioishi kwenye nyumba za mawe zilizopigwa chokaa mjini!
“Hawezi kuja,” walisema watu waliokuwa uwanjani.
“Hawezi kuja,” walisema watu waliokuwa mlangoni kumwambia Kino.
“Daktari hawezi kuja,” alisema Kino akimwambia Juana
Juana alimuangalia Kino. Macho yake yalikuwa makali kama simba jike. Koyotito ndiye alikuwa mtoto wa kwanza wa Juana. Alikuwa ndiyo kila kitu kwake. Na kino aliona uso wa mkewe ulioonyesha nia isiyotetereka kwenye lengo lake,na sauti ya muziki wa familia ukalia kichwani mwake.
“Basi tutamfuata,” alisema Juana, na kwa mkono mmoja alijitanda mtandio wake wa bluu kichwani, na upande mwingine akatengeneza bembea ya kumbebea mtoto aliyekuwa akigugumia, kisha akamfunika macho kwa sehemu iliyobakia ili kumkinga na jua. Watu waliokuwa mlangoni waliwasukuma walio nyuma yao ili kumpisha apite. Kino alifuata nyuma, wakatoka hadi nje ya geti, na majirani wakaanza kuwafuata. Suala hilo likawa suala la mtaa mzima sasa. Walitembea haraka haraka kuelekea mjini. Juana alikuwa mbele, alifuatia Kino, na nyuma yao, Juan Tomas na Apolonia. Tumbo kubwa la Apolonia lilichezacheza sababu ya mwendo wa kasi. Kisha walifuatia majirani zao, huku watoto wakikimbia pembeni ya msafara.

SOFTWARE - Jisomee vitabu vya Kiswahili bure ndani ya App hii?
Sasa ndani ya App yetu ya maktaba unaweza kujisomea vitabu vyote vilivyomo bure kabisa. Ingia playstore na install Maktaba by pictuss APP. Unaweza kusoma vitabu hata ukiwa offline. Link ya app inapatikana katika post no 16. Vitabu vilivyopo mpaka sasa. 1. Hekaya za Abunuwasi na hadithi...
www.jamiiforums.com