Geita: Mgodi waua watatu, tisa wanusurika

Geita: Mgodi waua watatu, tisa wanusurika

kirerenya

JF-Expert Member
Joined
Aug 27, 2013
Posts
1,698
Reaction score
2,262
xz.jpg

​
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, ajali hiyo ilitokea majira ya saa 5:45 usiku wa kuamkia juzi kwenye shimo namba 131, wakati wachimbaji hao wakiendelea na shughuli za ukarabati wa shimo hilo.

Akithibitisha tukio hilo, Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Injinia Gabriel Baruti alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwamba wa mawe kuporomoka wakati wachimbaji hao wakifanya ukarabati kwenye shimo hilo.

Injinia Baruti aliwataja waliofariki kuwa ni Shida Shija (34), mkazi wa Nyarugusu wilayani Geita, Leonard Kusekwa, mkazi wa Lwamgasa na Lameck Enos ambaye umri na makazi yake hayajafahamika mara moja.

Aidha, Baruti alisema jumla ya watu 12 walikuwa ndani ya shimo hilo ambapo tisa wamenusurika kifo.

Meneja wa mgodi wa Bingwa, Ludelph Zabron, alisema ajali hiyo ilitokea wakati wachimbaji wakifanya ukarabati kwenye shimo hilo.

Alisema kwa bahati mbaya wakati wakifunga mwamba shimoni, kifusi kiliporomoka na kuwafunika.

Naye Yohana Wiliam ambaye alikuwa akiendelea na uchimbaji katika shimo jirani namba 665 aliiambia Nipashe kuwa alisikia kishindo kikubwa na kelele za kuomba msaada.

Alisema alipofika kwenye shimo namba 131 alikuta mlango umezibwa na kifusi hivyo kulazimika kutumia njia ya mlango wa shimo jirani ambapo alifanikiwa

kuwaokoa "watu kadhaa".

Alisema baada ya wachimbaji hao kutoka salama, alikwenda kutoa taarifa kwa uongozi wa mgodi huo.

“Nilijitahidi kadri ya uwezo wangu kuokoa maisha ya wachimbaji wenzangu na kufanikiwa kuwaokoa sita wakiwa hai, pengine pangekuwapo na kitengo cha uokoaji hapa mgodini wote wangetoka hai,” alisema Yohana.

Richard Paulo ambaye ni manusura wa ajali hiyo alisema walikuwa wachimbaji 11 wakifanya kazi ya ukarabati wa shimo na ghafla kifusi kiliporomoka na kuziba mlango.

Alisema ndipo walipopiga kelele za kuomba msaada kwa wenzao na kwamba walikuwa wamepoteza matumaini ya kuiona dunia tena wakati huo.

Mpaka juzi saa 7:00 mchana Nipashe ilipofika eneo la mgodi huo ilikuta shughuli za uopoaji miili zikiendelea kwa wachimbaji kushirikiana na kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa, wakitumia

zana duni hata hivyo kufukua miili ya marehemu hao.


WACHINA WAWILI

Matukio ya maafa kwenye migodi midogo si haba nchini, hata hivyo. Machi 29, mgodi wa dhahabu katika Kijiji cha Nyamitondo wilaya na mkoani Geita ulifungwa baada ya raia wawili wa China kufariki ndani ya shimo lenye urefu wa zaidi ya mita 100 kwa kulipukiwa na baruti wakati wakivunja miamba.

Wachina hao, imeelezwa, walikuwa wakivunja miamba ya dhahabu katika mgodi huo bila ya kuwa na vyeti vya kulipua baruti.

Mgodi huo unamilikiwa kwa ubia baina ya Mayala Ngweso na kampuni ya kichina ya Taichangain Tanzania Group.

Akitoa tamko la kufunga mgodi zaidi ya miezi miwili iliyopita, Ofisa Madini mkazi Mkoa wa Geita, Alli Maganga alisema hatua hiyo inalenga kupisha uchunguzi wa kina.

Pia, alisema Maganga, hatua hiyo itashinikiza mgodi huo kutekeleza masharti na maelekezo uliopewa na serikali ili kuhakiksha sheria na kanuni za madini zinazingatiwa na kufuatwa.

Maganga alisema raia wawili wa China waliotambuliwa kwa majina ya Li Shaobin (44) na Qian Zhaorang (49)waliojitambulisha kuwa mafundi michundo walifariki dunia baada ya kujeruhiwa vibaya na baruti ndani ya shimo katika mgodi huo wakilipua miamba ya dhahabu.

Alisema uchunguzi wa awali ulibaini marehemu hao hawakuwa na vyeti vinavyowaruhusu kulipua baruti, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria ya nchi.

Aidha Oktoba 10, mwaka jana, mchimbaji mmoja alifariki dunia na mwingine kunusurika baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo katika mgodi huo huo wa Bingwa.

Aliyefariki ni Fikiri Paulo (27), mkazi wa kijiji cha Mlanda wilayani Chato ambaye mwili wake ulitolewa shimoni akiwa ameshaaga dunia.

Mwili huo ulitolewa shimoni na wachimbaji wadogo ambao walikesha wakiendesha zoezi la kuufukua mwili wa marehemu kuanzia saa 5:00 usiku ajali ilipotokea hadi saa moja asubuhi.

Manusura wa ajali hiyo ni Musa Evarist (19), mkazi wa kijiji cha Mpomvu.

Chanzo cha ajali hiyo kilidaiwa kuwa ni kukatika kwa gema la udongo wa mwamba wa mawe katika shimo walimokuwa wakichimba vijana hao.

Baada ya gema kukatika, imeelezwa, kifusi kilifukia wachimbaji hao

Chanzo: Nipashe
 
Wapumzike kwa Amani marehemu wote wa Tz na wachina wawili.
 
Back
Top Bottom