Fr.Karugendo: Tupande mbegu za Uzalendo | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Fr.Karugendo: Tupande mbegu za Uzalendo

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Sumaku, Jun 18, 2009.

 1. S

  Sumaku Member

  #1
  Jun 18, 2009
  Joined: Feb 17, 2009
  Messages: 53
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Tupande mbegu za uzalendo

  Na Padri Privatus Karugendo

  Mnamo mwaka 1976, Kule Soweto, Afrika ya kusini, maelfu ya watoto weusi wa shule waliingia mitaani na kufanya maandamano ya zaidi ya nusu kilomita, wakipinga elimu duni waliyokuwa wakiipata na kudai kufundishwa kwa lugha yao. Walifanya maandamano ya amani kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa serikali ya makaburu.

  Ujumbe huu ulikuwa mchungu kwa wakubwa na hawakuwa tayari kuusikiliza. Kama kichaa anavyoweza kutumia bunduki kuua mbu, ndivyo makaburu walivyofanya kwa wanafunzi hao. Mamia ya wasichana na wavulana walipigwa risasi na kupoteza maisha yao. Kwa vile bunduki inaua mwili, lakini fikra na roho vinaendelea kuishi, maandamano hayo hayakuzimwa kwa risasi! Machafuko yaliyofuatia tukio hili yalipoteza maisha ya mamia ya watu na kuacha majeruhi kadhaa.

  Viongozi wa nchi huru za Afrika OAU, waliamua kuweka kumbukumbu ya mashujaa waliopoteza maisha yao kule Soweto, na wale wote walioshiriki maandamano hayo. Ingawa uamuzi wa kuikumbuka siku hii ulichelewa sana, bado ni jambo la kupongezwa. Kumbukumbu hii imepewa jina la Siku ya Mtoto wa Afrika. Imeanza kusherehekewa tarehe 16.6.1991. Tangia tarehe hiyo kila mwaka inakumbukwa. Mbali na kuwakumbuka mashujaa wa Soweto, siku hii imekuwa ni ya kukumbuka matatizo mengi yanayowazunguka watoto wa Afrika. Kauli mbiu ya mwaka huu ni kwamba Afrika imfaayo mtoto- Himiza na endeleza haki yake ya kuishi. Mtoto asitelekezwe!

  Hapa Tanzania, siku hii inasherehekewa kwa michezo, nyimbo, ngoma na shughuli mbalimbali za kuwakumbusha watanzania matatizo ya mtoto wa Afrika/Mtanzania. Mashaka yaliyopo ni kama watoto wanakumbushwa “Ushujaa” wa watoto wa Soweto. Je watoto wa Tanzania, wanakumbushwa jinsi watoto wa Soweto, walivyokubali kujitoa Muhanga kwa ajili ya kuandaa Soweto ya kesho. Damu iliyomwangika Soweto, ni kati ya mchago ulioisaidia Afrika ya Kusini kupata Uhuru wake na kufanikiwa kuufukuza ubaguzi wa rangi. Haya yanakumbushwa au tunabakia kwenye michezo na ngoma?

  Ukweli ni kwamba watoto wa Afrika, wana matatizo mengi. Matatizo ya kutopata elimu, matatizo ya kiafya, matatizo ya lishe, matatizo ya kufanyishwa kazi ngumu, matatizo ya kulazimishwa kuolewa kwenye umri mdogo, matatizo ya kukeketwa, matatizo ya kubakwa na matatizo ya kulazimishwa kuishi kwenye mazingira magumu. Mtoto wa Afrika anatelekezwa! Tunashindwa kulinda uhai wa mtoto wa Afrika.

  Tunaposema kumtelekeza mtoto, hatumaniishi kumzaa mtoto na kumtupa, kumzaa mtoto na kumkana, tunamaanisha pia kumzaa mtoto na kushindwa kumpatia mahitaji muhimu kama elimu, chakula bora, malazi bora, upendo na maadili bora. Bila mifumo inayoeleweka ya kuwafundisha watoto wetu maadili bora, ni kuwatelekeza! Bila kumpatia mtoto mwongozo wa maisha ni kumtelekeza!

  Familia hazina mifumo mizuri ya kufundisha maadili. Baadhi wameamua kuwaacha watoto wao wafundishwe maadili na televisheni, wengine wanawaacha watoto wao wafundishwe na dunia! Matokeo yake tunayafahamu sote. Viongozi wa dini nao hawana mfumo unaoeleweka wa kufundisha watoto maadili bora.

  Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshuhudia matatizo mengi ya watoto. Tumewatelekeza watoto wetu. Tunashuhudia watoto wetu wanavyosukumwa kila siku kwenye daladala, watoto wanavyosoma kwa shida, shule za msingi wengine wanakaa chini, sekondari wanasoma bila kuwa na walimu wa kutosha, matokeo yake wanafanya vibaya na kushindwa kuendelea na masomo ya juu. Tunashuhudia watoto wetu wakikoswa ajira, tunashuhudia watoto wetu wakibugia madawa ya kulevya.

  Lakini pia idadi ya watoto yatima inaongezeka kila kukicha, idadi ya watoto wa mitaani inaongezeka, idadi ya watoto wanaofanya kazi ngumu kama vile kwenye machimbo, kwenye mashamba makubwa ya chai na mkonge, inaongezeka kwa idadi ya kutisha, idadi ya machangudoa inaongezeka, idadi ya wapiga debe inaongezeka na inatisha, machinga nao wanaongezeka kwa idadi kubwa nk. Na hawa wote hawana mfumo wa kuwafundisha maadili bora. Wanafundishwa na dunia!

  Wapiga debe na machinga, kama kungekuwa na mipango mizuri wangeweza kufanya kazi nyingine za kuzalisha na kulijenga taifa letu, wengi wao ni vijana wenye nguvu na akili nzuri. Ila ndo hivyo mipango si mizuri. Kuna mambo mengi ya kuandika juu ya watoto wa Tanzania. Kuna mambo mengi ya kufanya juu ya watoto wa Tanzania. Sehemu kubwa ya Bajeti yetu ingeelekezwa kwa mtoto wa Tanzania, ili kuaandaa Tanzania ya kesho yenye utulivu na amani!

  Mbali na matatizo yote hayo ya mtoto wa Tanzania, kuna hali ya kutisha, inayoonyesha jinsi kizazi cha watu wazima kinavyojishughulisha na Tanzania ya leo, bila kuaangalia Tanzania ya kesho. Hii inajionyesha kwa mambo mengi. Jinsi bajeti inavyoandaliwa, jinsi ya kupanga vipaumbele- magari mazuri- majumba mazuri- mishahara minono- matibabu ya nje na mengine mengine yanayofanana na hayo niliyoyata hapo juu. Mtoto anayekulia kwenye mazingira ya rushwa, ufisadi, ulevi, kushabikia ngono,uzembe, udanganyifu, majungu, “ubongo”, ujambazi, anakuwa ametelekezwa kimalezi! Hakuna dalili za watu wazima kukazana kutengeneza mifumo ya kuwapatia watoto maadili bora. Mtoto aliyelelewa na maadili bora ndiye anajengeka kizalendo kimwili na kiroho. Hatuwezi kuijenga Tanzania ya leo na kesho bila kukazana kupandikiza “roho” ya kizelendo kwa watoto wetu.

  Chanzo cha siku ya mtoto wa Afrika, ni maasi yaliyofanywa na watoto wa Soweto, kwa kukataa kunyanyaswa. Walikuwa wakipata elimu duni ukilinganisha na ile ya wazungu. Pia, walitaka elimu itolewa kwa lugha yao. Kule Soweto, watoto waliaanza kutambua kwamba wale waliokuwa wakifundishwa katika shule nzuri ndio waliokuwa wakipata kazi nzuri na vyeo vya juu katika serikali. Hali ya kutamani hali bora ya maisha kwa siku za mbele, hali ya kutaka kuwa na vyeo na nafasi nzuri za kazi, iliwafanya wanafunzi kukataa elimu duni waliyokuwa wakiipata.

  Hawakuogopa nguvu za jeshi la Makaburu. Walikuwa tayari kupambana bila silaha – na kweli wengi wao walipoteza maisha. Watoto wa Soweto, walitambua kwamba kujifunza kwa lugha za kigeni wasingepata maarifa yenyewe. Walitaka wafundishwe kwa lugha ya kwao, lugha inayofanana mazingira yao, lugha inayogusa maisha halisi, lugha inayoweza kuharakisha maendeleo. Hoja yangu ni kwamba Bila kuwa waangalifu, inawezekana na sisi hapa Tanzania, tunaandaa Tanzania ya kesho yenye maasi kama ya Soweto. Kinachoweza kutusaidia, katika hali kama hii ni kuwajengea watoto wetu maadili bora.

  Kwanini ninasema hivyo, ukiachia mbali sekondari za kata ambazo tutake tusitake zinaanzisha pengo kubwa kati ya elimu duni na elimu bora, kuna sekondari za binafsi zinazoaanzishwa, ambazo karo ni kubwa, na wanaoweza kupeleka watoto ni wale wenye pesa, na ambao baadhi yao wana vyeo vya juu serikalini. Hivyo elimu bora na nzuri itabaki kwa matajiri na wenye vyeo. Kwa maana hiyo watakao pata kazi nzuri na kupata vyeo vya juu serikalini ni wale waliosomea kwenye shule bora.

  Kule Soweto, watoto weusi walifanya maasi kupinga ubaguzi uliokuwa ukifanywa na wazungu kwenye elimu. Hapa Tanzania maasi yatakuwa kati ya watoto wa maskini na watoto wa matajiri. Hili liko wazi, kulifumbia macho, ni kuiandaa Tanzania ya kesho yenye maasi na kumwaga damu. Mtu anayelipenda taifa letu la Tanzania, ni lazima alitupie macho na kutafuta jibu la haraka. Na njia ya kufanikisha hili ni kuwa na mfumo wa maadili bora kwa watoto wote wa Tanzania.


  CHANZO: kwanzajamii.com
   
Loading...