Kila tarehe 23 mwezi Mei ni Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Fistula ya uzazi. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “
TUMAINI, UPONYAJI NA HESHIMA KWA WOTE.”
Kwa Tanzania matibabu ya Fistula ni
BURE kabisa ikijumuisha nauli ya kumtoa mgonjwa alipo hadi hospitali, chakula, upasuaji na nauli ya kumrudisha. Hii ni katika kuhakikisha Fistula ya Uzazi inatokomezwa kabisa nchini ambapo kwa takwimu za mwaka 2014, wanawake takribani 20,000 walikuwa na fistula nchini.
Wanawake 20,000 wana ugonjwa wa fistula Tanzania
FISTULA NI NINI?
Fistula si neno geni kwa wengi wetu ingawa inawezekana tusijue maana halisi ya neno hili. Fistula ni tundu linalounganisha njia mbili za mwili zilizo wazi. Kuna fistula za aina nyingi lakini inayozungumziwa hapa ni Fistula ya Uzazi(Obstetric Fistula).
FISTULA YA UZAZI
Fistula ya uzazi ni tundu lisilo kawaida ambalo halikutakiwa kuwepo kati ya kibofu cha mkojo na njia ya uke(Vesico-Viginal Fistula – VVF) au kati ya njia ya haja kubwa na uke(Recto-Vaginal Fistula – RVF). Wanawake wengi hupata VVF, wachache RVF na wachache zaidi hupata zote kwa pamoja.
SABABU ZA KUTOKEA KWA FISTULA
Uzazi Pingamizi
Fistula mara nyingi hutokana na Uzazi pingamizi(Obstructed labour) wa muda mrefu ambao haukuhudumiwa kwa wakati mwafaka. Hali hii inapotokea kunakuwa na msuguano kati ya mfupa katika nyonga na kichwa cha mtoto unaopelekea jeraha katika njia ya haja kubwa au ndogo ambalo baadaye hugeuka kuwa tundu.
Uzazi au uchungu pingamizi ni uzazi usioendelea aidha kwa sababu mtoto ni mkubwa kuliko njia ya uzazi, nyonga za mama kuwa na tatizo(aidha mama hakuwa na ukuaji mzuri kutokana na utapiamlo utotoni au ajali iliyoathiri nyonga) ama ulalo mbaya wa mtoto tumboni.
Upasuaji
Upasuaji kwa ajili ya uzazi au matibabu mengine katika viungo vilivyopo maeneo ya nyonga huweza kusababisha fistula. Hii hutokea pale daktari ama kwa bahati mbaya ama uzembe anatoboa kuta za njia ya haja kubwa au ndogo ya mgonjwa na kusababisha fistula.
Mionzi
Mionzi kwa ajili ya matibabu ya Saratani ya Shingo ya Uzazi huweza kusababisha fistula kwa kuua seli na kupelekea tundu.
Majeraha/Magonjwa ya Kuambukiza
TB ya Kibofu
Majeraha ukeni
DALILI ZA FISTULA
Dalili kuu ya fistula ni mwanamke kutokwa na haja kubwa au ndogo bila ridhaa yake au bila kujua.
Nyinginezo:-
Vidonda sehemu za siri
Kuchechemea kutokana na maumivu yatokanayo na uzazi pingamizi
MADHARA YA FISTULA
Kimwili
Mwanamke kutokwa na haja ndogo au haja kubwa ama vyote kwa pamoja bila kutambua wala kuwa na uwezo wa kuzuia hali hiyo.
Kuungua au kutokwa na vidonda sehemu za siri vitokanavyo na kemikali zilizopo kwenye mkojo.
Kupoteza uwezo wa kuzaa.
Kupoteza uwezo wa kujamiiana.
Kijamii
Unyanyapaa wa mtu binafsi na jamii kwa ujumla
Kutelekezwa ama kutalikiwa na mume au mwenza
Kushindwa kushiriki shughuli za kijamii
Kisaikolojia
Kushuka moyo (Sonona)
Aibu na Kutojiamini
Kujiua kwa baadhi ya wanawake kwa kukosa tumaini (85% hupoteza watoto wao pia)
Kiuchumi
Kushindwa kufanya shughuli za kiuchumi na kuishi maisha ya dhiki.
MATIBABU
Matibabu ya Fistula ni kwa nja ya Upasuaji wa kuziba tundu/matundu yaliyojitokeza.
Baada ya hapo mwanamke huwekewa mpira wa haja ndogo kwa muda wa siku 14 ili njia iweze kupona na baada ya hapo huangaliwa kama amepona.
Baadhi ya wanawake hufikishwa hospitali wakiwa na kibofu cha mkojo kilichoharibika kabisa hivyo hufanyiwa upasuaji na kutengenezewa kibofu cha bandia katika sehemu ya haja kubwa hivyo hujisaidia haja zote kwa pamoja.
Fistula ni ugonjwa wa aibu na fedheha kwa wanawake na hupelekea waathirika kupoteza maana ya maisha hivyo sambamba na upasuaji, huduma za ushauri wa kisaikolojia hutolewa ili kuweza kuwarudishia thamani yao. Mafunzo ya Ujasiriamali pia hutolewa pia ili kuwawezesha wanawake hawa kujiinua kiuchumi na kumudu maisha yao mapya.
KINGA YA FISTULA
Fistula ni ugonjwa ambao unaweza kutokomezwa kabisa endapo hatua sahihi zitachukuliwa
Kuwahi kwenda kujifungulia kwenye kituo cha kutoa huduma za afya
Mama kuhudhuria kliniki ili kujua hatari zozote zilizopo na kupanga mipango ya kuzikabili
Kuzuia mimba za utotoni(Ni rahisi kwa mtoto kupata fistula kwani maungo hayajakua vizuri)
Serikali kuboresha miundombinu na huduma za afya ya uzazi hasa vijijini. Uwepo wa huduma za dharura kama upasuaji au uwepo wa magari ya wagonjwa na barabara thabiti ndio njia pekee ya kutokomeza janga hili.