Fikra zangu juu ya nchi yangu ya Tanzania

Fikra zangu juu ya nchi yangu ya Tanzania

EMMANUEL I NGADAYA

New Member
Joined
Mar 22, 2012
Posts
1
Reaction score
0
1. Akili ya mwanadamu hujengwa na fikra inayotokana na uzoefu wa mazingira yaliyomzunguka, ningeshauri serikali itengeneza sera itakayoweza kuboresha matumizi ya teknolojia ikiwamo utandawazi maana matumizi MABOVU ya teknolojia yanaitafuna nguvu kazi ya taifa letu la Tanzania, hii sheria ya mtandao pekee sidhani kama inatosha na inasaidia sana maana navyoiona imetazama sana taarifa inayowekwa na mtumiaji kwenye mtandao na sio taarifa inayotafutwa na mtumiaji ila tu kwasababu sio mtaalamu sana wa mambo haya ya teknolojia naomba niishie hapa kwenye hili suala.

2. Mkulima mzuri siku zote uandaa mbegu bora, ardhi yenye rutuba ili kuja kupata mazao yaliyo bora katika msimu wa kilimo kinachotegemea mvua yaani masika na sio kiangazi. Hapa namaanisha hakuna kitu kikubwa taifa litakachoweza kufanya kama kuandaa kizazi kitakachojikita katika uzalendo kikiwezeshwa kwa nyenzo bora na imara tayari kwa kulitumikia taifa bila kusahau kuweka nguvu nyingi katika kuwajenga vijana kisaikolojia, kielimu na kimaendeleo nikimaanisha kijamii, kiuchumi, kidini na kisiasa yakifanyika haya naamini miaka mitano ijayo watanzania wote tutazungumza lugha moja ya maendeleo. Tunahitaji maboresho katika mifumo tunayotumia kuwaandaa watoto wa kitanzania, namaanisha ni wakati sasa wa kuwafundisha uzalendo toka mtoto anapokuwa chekechea, kuwafundisha masomo kama uraia na hata vitu vinavyotutambulisha kama Tanzania, naamini hii itawajengea dhamira ya kuipenda na kuitumikia Tanzania watakapokuwa vijana na hata wazee.

3. Maendeleo ya watanzania, yataletwa na watanzania. Ni juhudi kubwa inayofanywa na serikali kulikomboa taifa kiuchumi na ni wazi sote tunapaswa kupongeza juhudi hizi bila unafiki. Maendeleo ni kutoka hali ya chini aliyonayo mtu husika kwenda hali ya juu iliyo bora na inayoweza kumsaidia kukidhi kile anachohitaji ili kuishi lakini tu juhudi hizo zitokane na shughuli halali au kipato kinachotokana na juhudi halali za mtu binafsi, niombe kila mmoja wetu kutazama maendeleo ya Tanzania kwa kila mtanzania kitu ambacho ni kigum kufikiri au hata kutekeleza ila nina imani na tunakoelekea ambako kila mtanzania atasimama kifua mbele kuendelea kujivunia Utanzania

4. Tufikiri dunia ingekuwa vipi kama kusingelikuwa na jua, hivyo ndivyo fikra na akili zetu zitakavyokuwa kama tutakosa ujuzi na elimu juu ya shughuli tuzifanyazo ili kujipatia kipato, ukitaka kuamini maneno haya pitia historia ya jamuhuri ya China utaelewa kwanini wamefika hapa walipo leo. Ni wakati sasa wa kutazama ni jinsi gani tunaweza wapatia ujuzi hii nguvu kazi ya taifa ili kuweza kuboresha shughuli zao katika kujikomboa kiuchumi, ni wakati wa kufungua milango katika kutoa fursa za kielimu zinazoliliwa na wafanya bihashara wadogo wadogo na hata kada nyinginezo, nawapongeza VETA na vyuo vidogo vinavyotoa elimu/ujuzi kwa vijana kwa hatua waliofikia katika kuwapatia elimu/ujuzi vijana na watanzania wote kiujumla lakini bado naamini tunahitaji kuongeza nguvu za ziada katika kuwapatia elimu/ujuzi vijana wa kitanzania ili kuweza kujiajiri na pia kuweza kupanua soko la bidhaa zao kwa ujasiri unaotokana na elimu/ujuzi na hata mbinu za kupambana kiuchumi wanazopatiwa.

5. Kuna neno moja la kiingereza linalosema "ACESS", ukitumia google translater utambiwa kwa kiswahili ni "upatikanaji" , sasa jaribu kukaa chini na kufikiri ni mara ngapi umeshindwa katika mipango yako au umefeli kutimiza malengo yako au hata kukosa kazi au ajira kwa sababu tu ya KUTOPATIKANA KITU FULANI MUHIMU. Binadamu tupo duniani, tunahangaika usiku na mchana ili tu kuweza kupata access ya vitu muhimu maishani mwetu, sijafanya utafiti lakini tu fikra zangu zinanituma kuwa ni idadi kubwa ya watanzania hatuna ACCESS ya vitu muhimu tunavyovihitaji ili kuendelea, inaweza kuwa elimu, inaweza kuwa mtaji, inaweza kuwa fursa, inaweza kuwa chochote kile ambacho kinaweza mkomboa mtanzania kutoka hatua moja kwenda nyingine. Ni wakati sasa wa kutathmini ni nini tunahitaji kufanya ili kila mtanzania angalau aweze kuwa na access na vitu vitakavyomfanya aweze kutoka sehemu alipo na kukua kiuchumi yaani kimaisha na ni wakati wa serikali pia kutangaza au kotoa vipaumbele vya kiuchumi na kimaendeleo kwa watanzania kwanza.

6. Maji ni uhai na afya ni mtaji. Vijana wengi sana nchini, watoto na hata wazee wamejikita au wanaanza kujikita katika matumizi ya vilevi na kula vyakula vinavyo dhohofisha afya zao. Kigezo kimoja cha taifa lililoendelea ni watu wake (nguvu kazi ya taifa) kuwa na afya bora inayowawezesha kufanya kazi katika weledi na maarifa, sitalizungumza kiundani lakini niwaombe tu wananchi wenzangu kuepuka vilevi hasa katika nyakati ambazo zinakuhitaji kulitumikia taifa maana utumiaji wa vilevi hivi madhara yake ni makubwa ingawa itachukua muda na hata mpaka miaka mitano mtu kuweza kuona madhara ya vilezi hivyo mwilini mwake.

Suala lingine katika afya ni upatikanaji wa huduma bora ya afya kwa kila mtanzania, tuliona marekani ObamaCare sasa sijui hapa kwetu tutakuwa na .........Care, kiufupi nishauri tu serikali yangu pendwa kuwa ni kweli kipaumbele kwa sasa ni kulikuza taifa kiuchumi, ila ni wakati sasa wa kuangalia mfumo wetu wa afya nje na ndani kuona ni jinsi gani tunaweza kuboresha ili kuweza kukidhi idadi ya watanzania inayoongezeka kila kukicha. Afya inahusisha vitu vingi sana lakini naamini vikubwa ni rasilimali watu, vitendea kazi na miundombinu bila kusahau rasirimali fedha, ninachomaanisha hapa siku zote idadi ya watu inapoongezeka tunahitajika kuboresha mifumo tuliyonayo kama afya, miundombinu na hata elimu kitu ambacho nawapongeza Waziri Mh. Ummy Mwalimu na mama yetu Prof. Ndalichako, wamekuwa wakionesha juhudi katika uboreshwaji wa mifumo yaani afya na elimu ukizingatia idadi ya watanzania mpaka 22/10/2016 ilikadiriwa kuwa Milion 55.65 wakati 2013 ilikadiriwa kuwa Million 49.25, hivyo ni dhahiri kuwa tunahitaji kuboresha mifumo ili kukidhi haja za idadi ya watu inayoongezeka.

7. Tusikate tamaa na tusikubali kukwamishwa. Kuna misemo mingi juu ya ukataji tamaa katika shughuli zetu za kila siku, ila werevu waliwahi kusema ukiona umeanza kuchoka au unajisikia kukata tamaa ujue umekaribia mafanikio hivyo inakubidi kuongeza juhudi zaidi na sio kukata tamaa. Kuna watu ni mabingwa wa kuridhika na hali waliyonayo na mabingwa wa kutotaka kujaribu kitu kipya au kuchukua RISK, kiufupi hiyo ndiyo tofauti ya tajiri na masikini kwangu mimi, tajiri haogopi kujikita katika kuchapa kazi hata ikionekana faida au hasara za kazi husika, matajiri wengi wamegeuza matatizo kuwa fursa za kimaendeleo kwao. Kama taifa linalohitaji kusonga mbele kimaendeleo ni hatari sana kama kutakuwa na watu ambao ni wepesi kukata tamaa au kutotaka maboresho au marekebisho katika shughuli zetu za kila siku za kujipatia maendeleo, ni wakati sasa wa kufunguka kifikra katika kutumia fursa za kiuchumi kila siku tuamkapo asubuhi naamini taifa litasonga mbele

8. Mh. Rais wangu mpendwa ambae ki ukweli anaiishi kauli mbiu ya hapa kazi tu, kipaumbele kikubwa katika uongozi ni viwanda yaani "Tanzania ya Viwanda" niombe tu kitu kimoja, tumekuwa tukishuhudia wawekezaji wakija na nguvu kazi zao yaani watendaji wa viwanda au miradi kutoka nchi zao au hata nchi jirani, sifahamu kiundani mikataba ya uwekezaji au miradi inasema nini juu ya kuajiri wafanyakazi hasa pale mwekezaji anapoingia nchini kwetu kuwekeza ila niombe tu tuanze sasa kufikiria watanzania wetu wenye ujuzi na ikiwezekana iwekwe sheria itakayomtaka mwekezaji kuajiri watanzania katika miradi yake au kiwanda chake, naomba nichukue mfano wa wahandisi wa barabara au hata majengo na hata wataalamu wengine wengi tulionao, unaweza kuona mgeni kapata tenda ya mradi fulani na akaishia kuajiri wageni wenzake na baadhi tu ya watanzania watakuwa wakifanya shughuli kama udereva au kazi ndogo ndogo na ukijaribu kuwahesabu ni wachache sana kwenye kila mradi na ukichunguza kiundani wanalipwa kidogo sana kulinganisha na kazi wanazofanya. Ni wakati sasa wa kutengeneza sheria au mikakati itakayowawezesha watanzania kuwa wanufaika wa kwanza katika miradi itakayokuwa ikiendeshwa hapa nchini iwe na wageni au wawekezaji wa nje, serikali na hata wawekezaji wa ndani lakini ikumbukwe kuwa hii itawezekana endapo kile kipengele cha kuwapatia elimu/ujuzi watanzania kitawezekana maana bila elimu/ujuzi tutabaki kuwa wafanyakazi wa shughuli ndogo ndogo na kulipwa kipato kidogo

9. Viwanda vidogo vidogo viwe nguzo ya Maendeleo ya VIWANDA Tanzania. Katika vitu ambavyo huwa najisikia amani ni pale ambapo unakuta Mtanzania ana tengeneza bidhaa kama viatu akiwa kijiweni nikimaanisha kwenye kibanda kidogo ambacho anajipatia kipato kila siku, ukifika kwa bwana huyu fundi wa kutengeneza viatu atakupima na atakutengenezea kiatu ambacho ukivalia suti huwezi amini kama kimetengenezwa hapa hapa Tanzania na mtanzania. Sasa basi, hapa ni katika kutengeneza kiatu tu naamini hata wewe unaesoma hapa umewahi kukutana na mtu mwenye ujuzi wa kutengeneza kitu fulani ambacho unaamini kama angepata vitendea kazi sahihi angeweza kutengeneza bidhaa ambazo zingeuzwa hata nje ya nchi, hivyo naamini utakubaliana na mimi ninaposema ni wakati sasa wa kuwawezesha wabunifu vya bidhaa mbalimbali nchini iwe kielimu, kiujuzi au hata kimtaji ili waweze kumudu bihashara zao na kupanua soko lao, jaribu kufikiri bidhaa za kimasai zinavyowavutia watalii wanapofika kutembelea vivutio vya utalii nchini kwetu hapa, kwa hiyo kwa kuwawezesha watu hawa nao watapata nguvu ya kuboresha shughuli zao, watapata nguvu ya kufundisha wenzao na hata kuajiri vijana wawili au watatu na hivyo kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo na kuepusha vijana kujiingiza katika shughuli zisizo halali katika kujipatia kipato. Tunapaswa kuendelea na hata kufikia hatua ya kuwa na modern shoe repair centres ambazo vijana wetu watajipatia kipato hapo. Kama kweli tunahitaji kusonga mbele katika suala la viwanda, watu hawa sio wa kuwasahau kabisa, tunaposema viwanda tusifikirie tu yale majengo makubwa yenye bomba kubwa za kutolea moshi na yanayosababisha uchafuzi wa mazingira, tuweke matazamio yetu na tuelekeze nguvu zetu katika kuwawezesha washonaji nguo, mafundi baiskeli/pikipiki/gari, mafundi viatu, wauza nyanya ambao wamekuwa wakitupa nyanya zao ambazo zimekuwa zikiharibika wakati zingeweza kutengenezewa tomato juice na wakapata kipato zaidi, na nyininezo nyingi tunazozifahamu. Hivyo ni wakati sasa wa kuwekeza katika watanzania wanao jishughulisha na utengenezaji wa bidhaa ndogo ndogo na ikiwezekana ile hoja ya kuzuia bidhaa zilizopo nchini kuingizwa kutoka mataifa mengine itiliwe maanani pia maana haiwezekani nchi yenye ng'ombe wengi kama Tanzania tuagize maziwa kutoka nje au hata viatu na mikoba wakati wapo watu ambao wakiwezeshwa kielimu/kiujuzi wanaweza tengeneza bidhaa hizo hizo tunazonunua kutoka nje.

10. Kipato halali ni msingi wa Amani katika familia na hata taifa kiujumla. Kuna watu wengi wametajirika kihalali kupitia bihashara halali au shughuli halali na wengine kupitia bihashara haram na hata kwa kupitia migongo ya masikini labda kwa kuwadhulumu au hata kuwanyang'anya haki zao. Niombe tu ikiwa ndio namalizia point ya mwisho kuzungumza hapa, ni wakati sasa wa kutengeneza mfumo ambao utaiwezesha serikali kutambua ni jinsi gani kila mwananchi anajipatia kipato na kuweka wazi kuwa kulingana na shughuli anayofanya alipaswa kuwa na hali fulani ya kimaisha/kiuchumi. Mfumo huu hautamzuia mtu kutajirika wala kumiliki mali ila tu utazingatia misingi ya juhudi za mtu binafsi na shughuli halali anazofanya ila itakapoonekana mtu huyu anatumia njia au shughuli ambazo si halali kujipatia kipato basi moja kwa moja mfumo huu utamuwajibisha kulingana na taratibu na sheria zitakazowekwa wazi. Hii itasaidia kujenga upendo na heshima makazini na hata baina ya watanzia wenyewe, itarudisha uaminifu na mapatano baina ya watanzania na itamruhusu kila mtanzania awe kijana au mzee kuamini kuwa endapo ataweka juhudi kwa shughuli anazofanya basi ni dhahiri kuwa atanufaika na ataweza kumudu gharama na mahitaji ya kila siku maishani. Ni kweli kuwa kwenye kila mafanikio huwa zipo chembechembe za dhuluma ila sitaki kuamini maana wapo waliofanikiwa bila dhuluma na wamefanikiwa kutokana na juhudi zao binafsi katika kazi, hivyo ni sahihi kama mfumo utakaowekwa utaweza kumtambua kila mtanzania na kutambua shughuli anayofanya ili kujiingizia kipato, naamini inawezekana na itasaidia kwatika kuboresha mapato serikalini na hata kujenga taifa lenye watu wazalendo na wapenda kazi.

Asanteni sana na Mwenyezi awabariki na kumjalia kila mmoja haja ya moyo wake!
Ni tafakari yangu ya leo.
 
Back
Top Bottom