Fikra sahihi huanza na Mungu

Tutor B

JF-Expert Member
Jun 11, 2011
9,025
6,555
Salaam kwa wote!

Nianze kwa kuwaweka vizuri wasomaji wangu kwamba mada ya leo ina lugha ya falsafa kidogo, hivyo, wasome polepole kila nukta ili kupata uelewa sahihi wa kile kinachojadiliwa. Mwanafikra makini na mkubwa sio yule anayeanza safari ya kufikiri ndani ya ubongo wake. Safari sahihi ya fikra inapaswa kuanzia nje ya Ubongo. Nani aliyeumba ubongo unaojenga akili ya kufikiri, hili ndilo liwe jambo la kwanza. Japo fikra inazaliwa ndani ya ubongo lakini safari ya kufikiri ianzie nje.


Mtu anayetaka kuufikiria ubongo kama kipande cha nyama na kisha afanye safari yake ya kufikiri hadi kufikia mwisho na kutoa hitimisho kwa msingi wa kipande hicho cha nyama ambacho kikitolewa nje ya fuvu la kichwa hakina tofauti yoyote na ‘uji wa madida’ usioweza kuzaa fikra yoyote, huyo atakuwa amepotea njia kwani ameianza vibaya safari yake ya kufikiri!

Hawezi kupata njia sahihi ya kumfikisha kwenye hitimisho sahihi la madhumuni halisi ya kufikiri. Kilichomsibu msomi yoyote yule ‘asiyemwamini Mungu’ (educated atheist) kimetokana na ukweli huo kwamba aliianza vibaya safari yake ya kusomea kile alichokisoma. Alianza na akili yake badala ya kuanza na Muumba wa akili yake.

Katika mfumo sahihi wa elimu, mwanafunzi huanza kusoma kwa Jina la Mwenyezi Mungu. Kusoma kwa Jina la Mwenyezi Mungu kuna falsafa pana sana.
Kwanza ndio mwanzo sahihi wa safari ya kufikiri kwani unamtaka mtu aanze mchakato wa kufikiri nje ya ubongo wake. Huo ndio mwanzo sahihi wa kusoma ambao ndio, hatimaye, utakaozalisha mwanafikra sahihi. Ubongo una udhaifu wa kughafilika na kukumbwa na bumbuwazi la mazoea au ugonjwa wa kupooza akili (mental paralysis).
Mtu anayesoma kwa shauku tu ya nije kuwa nani katika maisha yangu; bosi, Mbunge, Waziri, Daktari, Rais bila dhana ya usomi wake kuakisi falsafa sahihi ya lengo la kuumbwa kwake, huyo lazima apatwe na kiharusi cha kiakili au pumbao la kisomi (intellectual foolishness)! Kwa maneno mengine, huu ni ujinga uliokwenda shule!


Na mtu anayeianza asubuhi yake kwa fikra ya chai itapatikanaje, au anayeielekeza akili yake yote katika swali la chakula cha mchana kitapatikanaje, na anayemaliza jioni yake kwa kufikiria tu Simba au Yanga imeshinda au kufungwa goli ngapi bila kujirudi kiakili maisha yake yana lengo gani katika dunia hii, huyo lazima apatwe na kiharusi cha akili. Akili yake hupoozea katika yale anayoyafikiria kila kukicha!

Bila amsha-amsha ya Ufunuo wa Mungu unaouchagiza ubongo kuzitazama ishara za Muumba, basi ubongo wenyewe tu pekee unaweza kupumbaa usiwe na wazo kabisa la Muumba! Na unaweza hata kulazimishwa kumkataa Muumba!

Kabla ya kufikiwa na Ufunuo, wanadamu huwa wazito wa kumfikiria Mungu. Matope ya kufuru na ushirikina yanayonasa akili zao ni matokeo ya ubongo kushindwa kujenga picha sahihi ya Mungu.
Mara nyingi, kwa uzoefu wa kihistoria, mwanadamu akiachwa bila ufunuo, haangukii peupe bali huangukia kwenye giza la ujinga.

Ujinga ni zao la ubongo wake mwenyewe pale unapotoa majibu yasiyo sahihi juu ya kitendawili cha maisha yake. Walioleta upinzani dhidi ya Manabii na Mitume walioleta ufunuo wa kuzisaidia akili zao, walikuwa mateka wa ujinga uliozalishwa na ubongo wao. Msaada wa ufunuo uliletwa kwa kuzingatia udhaifu huo wa akili ya mwanadamu.


Hiyo ni kwa sababu hakuna Picha yoyote ya kiumbile inayoweza kuvutwa au kujengwa na Ubongo huo kuliakisi “Umbile” la Muumba. Chochote kinachofikiriwa au kujengewa picha ya Mungu sicho.
Ndani ya Akili ya mwanadamu, Mungu hayupo kabisa kiumbile. Kwa hakika, hakuna kitu kinachoitwa “Umbile la Muumba” bali kuna “Muumba tu wa Umbile.” Umbile ni kazi ya Muumba.
Hakuna kazi ya kuumba nyuma ya Muumba. Na kwa usahihi zaidi tuseme, ‘hakuna “nyuma” ya Muumba bali kuna Muumba nyuma ya kila kiumbe. Sasa, baada ya kuona kumbe akili inahitaji msaada wa nje pale linapokuja suala la kumjua Muumba, kwamba lazima mtu aletewe au arejee ufunuo ndipo akili yake imtambue vizuri Muumba, basi si sahihi kwake kuianza fikra yake yoyote ndani ya akili yake.
Mathalani, unapomuona kuku anadokoa punje, akili yako isianze wala kuishia na kuku kama kuku. Bali, punde unapomuona kiumbe huyo, akili yako ijiulize, nyuma ya kuku huyu yupo Nani aliyesanifu umbile lake la miguu miwili na kumpamba manyoya mwilini?
Hapo, moja kwa moja, unaanza na Muumba wa kuku badala ya kuanza na kuku kama kuku. Kwa maneno mengine, dhima ya umbile la kuku ni kumuakisi Muumba wa kuku papo kwa hapo.
Hapo sasa, utaanza kukitafakari kila alichonacho kuku kwa msingi huo. Utayatafakari macho yake mawili na kumuona ‘Fundi’ aliyeweka sawasawa jicho la kulia na la kushoto.
‘Bahati nasibu’ ya maumbile isingeweza kurudia macho mawili; Jicho la kwanza na la pili yote yamefanana na yamekaa pamoja, na utendaji kazi wao unahitaji yakae hivyo ili kuku aone kotekote kwa wakati mmoja.
Hapo unapata yakini kuwa, kwa hakika, hapa pana Muumba aliyesanifu kichwa kidogo cha kuku, kisha akakiwekea macho madogo, si makubwa kama ya ng’ombe!
Halafu unayatafakari manyoya yaliyompamba kuku. Yana rangi mbalimbali; meupe, meusi, kijivu, mekundu na kadhalika. Nani aliyechagua kila kuku awe na manyoya ya rangi fulani?
Ngozi tupu ya ndani ya kuku isingekuwa salama bila manyoya. Imefunikwa vizuri na manyoya sio tu kumuhifadhi kuku bali kukiweka salama kitoweo chako. Kisha unatazama mdomo wa kuku ulivyochongwa kwa namna ya kumwezesha kudokoa punje.
Ulaji pekee anaoutegemea kuku ni wa kudokoa. Hana mikono ya kumsaidia kuingiza chakula mdomoni. Hivyo, amehitaji mdomo uliochongoka.

Nani aliyesanifu na kuuchonga mdomo huu? Kwa kifupi, tafakuri inaanza, inatawala na kuhitimishwa na wazo la Mungu. Kama mtu anasoma sayansi ya umbile la kuku ili kujua kibaiolojia kuku yukoje, atanufaika sana kama atamsoma kwa nidhamu hii.

Lakini akiufumbia macho ukweli ulio nje ya akili yake japo hoja zake zipo ndani ya akili hiyo, na kisha kumsoma kuku kama kuku, basi akili yake italala na kufumbika, na hivyo, kuukwaa upofu wa kushindwa kumuona Muumba anayeonekana katika umbile la kuku.

Haya ndiyo makosa makusudi ambayo mifumo ya elimu imeyafanya kwa kuzigeuza maabara za sayansi kuwa vyumba vya kusomea viungo tu vya viumbe bila kumuhusisha Muumba.

Matokeo yake, ulimwengu wa wasomi uliopaswa kuwa kinanara wa Imani ya kumkubali Mungu, umekuwa nyuma na ‘mvivu’ wa kumfikiria Mungu. Ndio ulimwengu unaothubutu kutoa ufafanuzi wa kuitupilia mbali imani ya Mungu, na kuelekeza vipawa vya akili na kiwiliwili katika kutumia rasilimali za dunia ili kula na kunywa na kisha kusubiri kifo baada ya kitambo cha maisha.

Maisha yamekumbwa na ‘uzembe’ wa kutomjali Mungu Muumba na matakwa Yake kwa sababu ya msingi mbovu wa fikra na elimu. “kumtanguliza Mungu” sio wimbo wa kisiasa bali ndio ukweli wa kimaumbile ambao kama mwanadamu angeuzingatia katika tafakuri yake ya kila siku angeishi maisha ya utii, uadilifu na unyenyekevu mkubwa.

Ni msiba wa kiimani kuwa dunia imejenga mazoea ya kukitazama kila kiumbe na kisha kukiacha kama kilivyo bila kukaribisha wazo la Mungu. Jua linachomoza Mashariki na kuzama Magharibi huku macho yakiona bila akili kuzinduka kuwa ni Nani aliyeliwekea utaratibu huo wa kila siku?

Kila mmoja amekuwa akiyaona mawio na machweo kama majira tu ya dunia lakini sio kama ishara za Nani anayeuleta Usiku na Mchana kwa masaa yanayolingana, 12 kwa 12. Ni mwanamahesabu gani aliyezigawa saa za usiku na mchana?
Ulimwengu umeendelea kuwa na kitendawili cha Mungu yupo au hayupo ilihali elimu ya mwanadamu ya kusoma ishara za maumbile imekuwa kubwa mno kuliko wakati mwingine wowote ule wa historia ya mwanadamu.
Dhima ya elimu zote ni kuisaidia akili kusoma ishara za Muumba japo wakati huo huo mwanadamu anaweza kupata kazi au vyeo vya kidunia kwa elimu hiyo.

Wanadamu wangekuwa viumbe wema mno kama, kwa wakati mmoja, wangeifanya elimu kuwa nyenzo ya kusomea ishara za Muumba na hivyo wakamjua barabara na kumtii, na wakati huo huo kuitumia elimu hiyo kupata mkate wao wa dunia.
Mkate huo ungezingatia mipaka ya Muumba huyo katika kupatikana na kutumiwa kwake. Ufisadi na isirafu ambao umeikumba dunia ni matokeo ya usomi mkavu usiotimiza dhima yake kuiangazia akili ishara za Muumba.
Waliosoma ndio wamekuwa vinara wa ufisadi, na waliogizani ndio wanaojaribu kuipapasa imani ya Mungu kwa tabu na mashaka! Wamo hata wanadini ambao wanafunikwa na utamaduni wa imani bila imani.
Nikutakie mapumziko mema ya Pasaka.
 
Umenena jambo la msingi sana Mkuu, ubarikiwe sana.
Hakuna kitu pasipo Mungu muumbaji maana yote yaliyopo ni matokeo ya uumbaji
 
Back
Top Bottom