Fedha zakwamisha kesi kigogo Takukuru

Fedha zakwamisha kesi kigogo Takukuru

Kurzweil

JF-Expert Member
Joined
May 25, 2011
Posts
6,622
Reaction score
8,427
MHASIBU TAKUKURU.jpg

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imeshindwa kusikiliza ushahidi wa Jamhuri katika kesi ya kutakatisha fedha inayomkabili Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai, kutokana na mtendaji wa mhimili huo kukosa fungu la kuita mashahidi.

Aidha, mashahidi wanaotakiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo wanatoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam na kwamba wameshindwa kufika kwa sababu mahakama haina fedha za kuwalipa.

Madai hayo yaliyotolewa jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Pius Hila, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, anayesikiliza kesi hiyo.

"Mheshimiwa hakimu kesi hii ilipangwa leo (jana) kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri, lakini hatuna shahidi kwa sababu mashahidi wote wanatoka nje ya Jiji la Dar es Salaam na mtendaji hana fedha za kuwaita mashahidi hao," alidai.

"Mtendaji wa Mahakama ametoa kibali kwamba malipo yatasubiri fedha zitakapoingia. Tunaomba muda kwa sababu mashahidi wameshindwa kuja kwa gharama zao wenyewe," alidai Hila.

Wakili wa Utetezi, Alex Mgongolwa, akisaidiana na Semi Malimi, waliutaka upande wa Jamhuri kuleta mashahidi wengine ambao hawahitaji kuombewa kibali au hawatoki nje ya Dar es Salaam ili kesi hiyo iendelee.

Aliomba Jamhuri ifanye juhudi za kuwapata mashahidi wa nje ya Dar es Salaam, pia wapelekwe mashahidi ambao hawahitaji kuombewa nauli.

Hakimu Simba alisema mahakama itazungumza na mtendaji ili kutafuta fedha sehemu yoyote kwa ajili mashahidi hao wafike na kutoa ushahidi.

"Kesi hii ni ya muda mrefu mahakama itaongea na mtendaji wake atafute fedha popote, ili mashahidi waje kutoa ushahidi kila upande upate haki yake," alisema Hakimu Simba.

Alisema washtakiwa wapelekwe mahabusu kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Oktoba 15 na 16, mwaka huu.

Awali, Ofisa Utumishi Mkuu wa Takukuru Ayoub Akida(52) alitoa ushahidi wake dhidi ya Gugai na wenzake.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Katika kesi ya msingi, Gugai na mwenzake, wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, katika mahakama hiyo.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo alitenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

Ilidaiwa kuwa akiwa jijini Dar es Salaam kama mwajiriwa wa Takukuru alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh. bilioni 3.6 ambazo hazilingani na kipato chake cha awali na cha sasa cha zaidi ya Sh. milioni 800, huku akishindwa kuzitolea maelezo.

Chanzo: IPP
 
Back
Top Bottom