Fedha husema, za Saudia huimba pia...

Fedha husema, za Saudia huimba pia...

Rubawa

JF-Expert Member
Joined
Dec 25, 2015
Posts
2,055
Reaction score
3,267
BARAZANI KWA RAJAB

Fedha husema, za Saudia huimba pia

Na Ahmed Rajab

WENYE nguvu Saudi Arabia wamekwishaanza kutambua kwamba zama za kutumia fedha kuwa mbadala wa diplomasia huenda zikawa zimekwisha. Diplomasia ya fedha, ya kuzinunua nchi au viongozi wa nchi, ni diplomasia iliyokuwa ikitumiwa sana na wafalme mbalimbali tangu uanzishwe utawala wa ukoo wa al Saud.

Kwa sasa, utajiri wa Saudi Arabia unahodhiwa na Mohammed Bin Salman, mrithi wa ufalme. Lakini tunasikia kwamba baadhi ya ma ami na ma binamu wa Mohammed Bin Salman wamo mbioni kujaribu kumtenga asije akawa mfalme kama alivyopanga baba yake, Mfalme Salman Bin Abdulaziz al Saud.

Dhamira hiyo wanayo pia viongozi wa madola ya nje yenye usemi katika nchi hiyo. Marekani, kwa mfano, inasemekana kwamba inapendelea kiti cha ufalme wa Saudi Arabia kikaliwe na mwana wa mfalme Mohamed Bin Nayef, binamu wa Bin Salman na aliyewahi kuwa mrithi wa ufalme na akaondoshwa.

Na kuna Khalid Bin Salman, mdogo wake Mohammed Bin Salman. Wenye kumtaja wanasema kuwa yeye ni kijana makini na hafanyi mambo kwa kukurupukwa kama kaka yake Mohammed.

Wengine katika aila ya al Saud wanampendelea Ahmed Bin Abdulaziz al Saud, mdogo wake Salman na ami yake Mohammed.

Ahmed aliwahi, kwa muda mfupi mnamo 2012, kuwa waziri wa mambo ya ndani. Siku hizi yuko London, ambako inaonesha anafuatilizia kwa makini yanayoendelea miongoni mwa jamaa zake huko Riyadh.

Katika miaka ya mwanzo ya 1980 alipewa dhamana ya kuleta mageuzi katika jimbo la mashariki la al Hassa wanakoishi wafuasi wengi wa madhehebu ya Shi‘a.

Ahmed al Saud alisema wazi kwamba serikali ililipuuza eneo hilo na iliwabagua Mashi‘a. Akaahidi kuingiza rasilmali nyingi ili kuleta maendeleo.

Mwezi uliopita, saa za usiku alipokuwa anarudi nyumbani kwake London alikabiliwa na waandamanaji waliokuwa wakiulaani ukoo wa al Saud kwa vifo vya watoto nchini Yemen wanaouliwa kwa mabomu ya Saudi Arabia. Aliwaambia waandamanaji wasiulaumu ukoo mzima wa al Saud ila wamlaumu Mfalme Salman na mrithi wake.

Siku ya pili, mbiombio aliikosoa ripoti hiyo akisema alichosema ni kuwa Salman na mrithi wake ndio wenye dhamana ya dola na maamuzi yake.

Na ni kweli kwamba mtu mwenye nguvu kushinda wote Saudi Arabia ni Mohammed Bin Salman. Pamoja na kuwa mrithi wa ufalme, yeye pia ni naibu waziri mkuu (waziri mkuu ni baba yake, Mfalme Salman) na waziri wa ulinzi. Kadhalika, Bin Salman ni mwenyekiti wa Tume ya Shughuli za Uchumi na Maendeleo na mwenyekiti wa Tume ya Shughuli za Kisiasa na Usalama.

Bin Salman amefanya mageuzi makubwa katika wizara ya ulinzi. Kwanza, taasisi za kupambana na ugaidi na za ujasusi wa ndani ya nchi zimewekwa chini ya halmashauri moja ya usalama wa taifa (PSS) inayoripoti kwake.

Halafu amevitanua vitengo vya kiuchumi na vya kibiashara vya sekta za ulinzi na usalama ambazo zote ziko chini yake. Mei 2017 paliundwa Viwanda vya Kijeshi vya Saudi Arabia (SAMI) vikiwa ni tawi la Mfuko wa Uwekezaji wa Umma (PIF), ambao ndio mfuko wa utajiri wa taifa ulio chini ya udhibiti wake Bin Salman pekee.

Miezi mitatu baadaye pakaanzishwa Mamlaka ya Viwanda vya Kijeshi (GAMI) kushugulikia ununuzi wa vifaa vya kijeshi na vya kiusalama. Mamlaka yote hayo mawili, SAMI na GAMI, yako chini yake Bin Salman.

Kwa hivyo, fedha nyingi sana zimehaulishwa kutoka mashirika mengine ya kijeshi na usalama na amekabidhiwa Bin Salman.

Wakati huohuo ameunda kikosi maalum kiitwacho Kikosi cha Chui. Inasemekana kwamba kazi yake ni kuwaua wakosoaji wa serikali ya Saudia walio ndani na nje ya nchi.

Miaka ya nyuma, Saudi Arabia ilikuwa ikiendesha sera zake za mambo ya nje faraghani. Hapakuwa na wengi waliokuwa wakijua jinsi nchi hiyo ilivyokuwa ikizicheza karata za sera yake ya nje.

Lakini daima imekuwa na turufu iliyoitumia mara kwa mara katika sera zake za nje. Turufu yenyewe ni fedha.

Inazitumia fedha hizo kuwanunua viongozi, taasisi au nchi. Mfano mzuri wa karibuni ni dola za Marekani milioni mia sita na ishirini na nane ($628 milioni) zilizokutikana katika akaunti binafsi ya benki ya waziri mkuu wa zamani wa Malaysia, Najib Razak, anayekabiliwa na mashtaka kadhaa ya ufisadi.

Kwa muda mrefu, Razak amekuwa akidai kwamba alipewa fedha hizo na mwana mmoja wa mfalme wa Saudi Arabia wakati wa enzi ya Mfalme Abdullah, aliyefariki dunia 2015.

Alipewa hizo fedha baada ya wimbi la wanaharakati kusaidia kung’olewa madarakani Rais Zine el Abidine Ben Ali (Tunisia), Mu‘ammar Qadhafi (Libya) na Hosni Mubarak (Misri).

Razak alisema alipewa hizo fedha ili alizuie wimbi hilo la mabadiliko lililoanza Tunisia 2011 lisizikumbe nchi nyingine za Kiislamu.

Mara mbili al Jubeir, waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, alikiri kwamba aliyoyasema Razak yalikuwa kweli. Hata hivyo, Jumamosi iliyopita al Jubeir alijikanya mwenyewe akisema si kweli kwamba Razak alipewa fedha hizo na serikali ya Saudi Arabia.

Mkutano mkuu wa uwekezaji uliofanywa majuzi Riyadh umethibitisha kwamba fedha na nguvu, na hasa nguvu za fedha, ndizo zenye kuamua mambo duniani. Makampuni mengi ya nchi za Magharibi yanazirandia hisa za kampuni ya mafuta ya Saudi Aramco zitapoanza kuuziwa wageni. Hisa hizo zitakuwa na thamani ya dola za Marekani bilioni mia moja ($100 bilioni).

Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akipiga kelele kuhusu mauaji ya mwandishi Jamal Khashoggi lakini kilicho muhimu kwake ni fedha na si utetezi wa haki za binadamu.

Zamani Saudi Arabia ikizitumia fedha zake kama chambo lakini sasa Bin Salman atazitumia kama bakora ya kuzichapia nchi zenye kuthubutu kuikosoa nchi yake. Dalili zilianza kuonekana Novemba iliyopita pale Saudi Arabia ilipomrejesha balozi wake wa Ujerumani. Pia ilivunja uhusiano wa kibiashara na baadhi ya kampuni za Kijerumani. Ilichukua hatua hizo baada ya waziri wa mambo ya nje wa siku hizo wa Ujerumani kusema kwamba Saudi Arabia ndiyo iliyomchochea waziri mkuu wa Lebanon Saad al Hariri ajiuzulu.

Halafu kuna kadhia ya 2015 Uhispania ilipokataa kuiuzia Saudi Arabia mabomu 400 yenye kuongozwa na miale ya laser, kwa sababu yakitumiwa kuitwanga Yemen.

Ghafla baadaye Uhispania ilibadili msimamo. Na ilifanya hivyo kwa sababu Saudi Arabia nayo ilitishia kwamba isipouziwa mabomu hayo, itauvunja mkataba wa kununua manowari kutoka Uhispania yenye kugharimu euro bilioni 1.8.

Kufutwa kwa kandarasi hiyo kungeinyima Uhispania fursa ya kuwapatia ajira Wahispania laki sita katika nchi yenye ukosefu mkubwa wa ajira.

Mwaka huohuo wa 2015, Sweden nayo iliingia matatani ilipoishtumu Saudi Arabia kukiuka haki za binadamu. Baadhi ya mikataba ya kibiashara na makampuni ya Sweden ilivunjwa.

Ni wazi kwamba Bin Salman anatumia nguvu zake za kifedha kujaribu kuwanyamazisha wenye kuipinga serikali yake kwa kuziponda haki za binadamu.

Mwezi Agosti mwaka huu, ilikuwa zamu ya Canada kupigwa bakora na Saudia. Canada ilitoa wito kutaka “aachiwe kwa haraka” Samar Badawi, dadake mwanaharakati Raif Badawi, aliye kifungoni Saudi Arabia.

Serikali ya Saudia ilikasirishwa. Miongoni mwa hatua ilizochukua ni kumfukuza balozi wa Canada kutoka Riyadh na kusimamisha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Ilikuwa kama Saudia inajigamba kwamba si nchi ya kuchezewa. Waziri wake wa mambo ya nje, Adel al Jubeiri, alisema: “Ebo! Mnafikiri nani sisi? Jamhuri ya ndizi?”

Bila ya shaka, Saudi Arabia si jamhuri ya ndizi. Kwanza, si jamhuri, ni nchi ya kifalme. Pili, ina utajiri mkubwa wa mafuta. Kwa hivyo haimo katika kaumu ya nchi ziitwazo “jamhuri za ndizi”. Hizo ni nchi maskini zenye kutegemea mauzo ya zao moja la kilimo, kwa mfano ndizi.

Juu ya hayo, ijapokuwa Saudi Arabia ni falme yenye utajiri mkubwa viongozi wake wanajifanyia mambo kama wafanyavyo viongozi wa hizo jamhuri inazozidharau.

Kwa muda mrefu serikali ya Saudi Arabia imekuwa ikichota fedha kutoka Mfuko wa Saudi iliouanzisha 1974, kuzisaidia nchi maskini, hususan za Kiislamu. Misaada yake mingi ya mikopo rahisi ilisaida miradi ya usafiri, nishati na maji.

Si nchi maskini tu ambazo imekuwa ikizisaidia. Nchi hiyo imekuwa ikizifadhili taasisi mbalimbali zenye kuheshimika katika nchi za Magharibi. Imewafadhili pia waandishi na wachambuzi wa siasa za Mashariki ya Kati.


Katika miezi ya karibuni hata waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair alifadhiliwa pauni za Kiingereza milioni tisa. Inasemekana fedha hizo zitaiwezesha Taasisi ya Blair kufanya kazi ya kuleta mageuzi na usasa katika eneo la Mashariki ya Kati. Pia zitasaidia kuleta suluhisho la kikanda katika mchakato wa kuleta amani katika eneo hilo pamoja na kuleta utawala bora Afrika na kuzifanya dini tofauti zivumiliane.


Ajabu ya mambo ni kwamba fedha za nchi isiyovumilia dini nyingine, au hata madhehebu mingine, na isiyo na utawala bora ati zitatumiwa kustawisha utawala bora Afrika na kuzifanya dini tofauti zivumiliane.
 
Siasa za middle East cjawai zielew...too much confusion kyajepo za Western na huku kwetu Kajunjumele (ndisi republic)
 
Back
Top Bottom