kbm
JF-Expert Member
- Oct 5, 2012
- 5,224
- 1,676
Wapenzi wa mchezo wa pool table nchini, watalazimika kusubiri hadi saa 10 jioni kucheza mchezo huo au kukubali kutozwa faini isiyopungua Sh300,000 wakikutwa wanacheza kabla ya muda uliopangwa.
Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, Abbas Tarimba amesema wametayarisha barua zitakazotumwa kwa wakuu wa mikoa ili kuwasaidia kuelekeza wananchi kuhusu kanuni, sheria na taratibu za mchezo huo.
Alisema barua hizo pamoja na matangazo yatakayotoka katika vyombo vya habari, vitatoa mwongozo wa muda wa kuanza mchezo huo ambao utakuwa ni saa 10.00 jioni na kumaliza saa 5.00 usiku kwa siku za kazi, huku siku za mapumziko utaanza saa 8.00 mchana na kumalizika saa 6.00 usiku.
Tarimba alisema Sheria ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), kifungu cha 52 katika kifungu kidogo cha kwanza sura ya 42, inaeleza asiye na kibali cha kuchezesha au atakayekiuka kanuni za mchezo huo, atashtakiwa na akikutwa na hatia atalazimika kulipa faini isiyopungua Sh300,000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote viwili.
“Kila shughuli hapa nchini ina taratibu zake, watakaokiuka kwa kisingizio cha kuwa hiyo ndiyo ajira yao, watakaokutwa wanautumia mchezo huo kinyume cha sheria na kuugeuza kamari, watachukuliwa hatua za kinidhamu,”alisema.
Wakati Tarimba akisema hayo kuunga mkono kauli ya Rais John Magufuli ya kupiga marufuku vijana kuucheza mchezo huo muda wa kazi, katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam bado unaendelea kuchezwa.
Mwananchi lilifanya uchunguzi katika maeneo ya Buguruni, Mabibo, Vingunguti na Ilala na kukuta vijana wakiendelea kucheza mchezo huo asubuhi, huku baadhi yao wakidai hawajui kama imepigwa marufuku.
Teophili Lyaka aliyekutwa akicheza katika baraza ya nyumba eneo la Mabibo, alisema hajui kama kuna katazo la kucheza mchana na pia analipa fedha mwenyewe na hana kazi ya kufanya.
Leonard Rupia aliyekutwa akicheza katika eneo la Ilala, alisema anatambua Rais amekataza na kusema watu wafanye kazi, lakini amesahau vijana wengi hawana kazi.
Alishauri kwamba vijana watafutiwe kazi kwanza kabla ya kulazimishwa kuacha kufanya vit vinavyowapotezea mawazo.
“Sijui hajui kama hatuna kazi, maisha magumu, mawazo kila kukicha,”alisema.
Cassian Gama anayechezesha mchezo huo eneo la Vingunguti, alisema hiyo ndiyo ajira yake na ametekeleza kilichokuwa kinasemwa na viongozi mbalimbali kuwa vijana watafute fursa za kujiajiri.
“Hapo awali nilikuwa naingiza hadi Sh100,000 kwa sababu ‘token’ ilikuwa inauzwa Sh500. Watu wakijaa wanaotaka kucheza haraka wanapanda dau hadi Sh1,000, lakini sasa yapo mengi. Nauza bei ya zamani na ninapata kati ya Sh20,000 hadi Sh22,000 ukiniambia niache unataka nifanye kazi gani,”alisema.
Miraji Ramadhani aliyekutwa akicheza eneo la Buguruni ambaye ni mchezeshaji pia, alisema hana mpango wa kuacha kucheza, kuchezesha hadi akamatwe ‘akapumzike’ kwa kuwa hana cha kufanya.
Chanzo: Mwananchi