SERIKALI imesema kuwa gharama za kumtibu mgonjwa mmoja wa Kifua kikuu (TB) sugu ni Sh. milioni 35 ambapo matibabu yake ni kati ya miezi tisa hadi 12.
Kiasi hicho cha fedha kinatosha kununua magari aina ya Toyota Noah manne kwa soko la madalali la jijini Dar es Salaam.
Gharama hizo zilibainishwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy alikuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya kilele cha maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu duniani inayofanyika kila mwaka Machi 24.
Alisema matibabu ya ugonjwa huo ni makubwa na kuwasisitiza wananchi kuwa TB inatibika na dawa zake zinatolewa bure.
Aidha, Waziri Ummy alisema mgonjwa wa kifua kikuu cha kawaida matibabu yake ni wastani wa Sh. milioni mbili na kipindi cha matibabu yake ni miezi sita.
Alibainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), watu milioni 10.4 huugua kifua kikuu kila mwaka duniani na kati ya hao wagonjwa milioni moja ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15.
Kifua kikuu ni ugonjwa pekee wa kuambukiza ambao unasababisha vifo vingi duniani, alisema waziri huyo, ambapo kwa mwaka 2016 takribani watu milioni 1.3 walifariki dunia.
"Hapa nchini kwetu jumla ya vifo vilivyotokea miongoni mwa hao vilikuwa 28,000 sawa na vifo 77 vinavyotokana na TB peke yake kila siku," alisema Mwalimu.
Aidha, Mwalimu alisema jumla ya watu 60,000 nchini kila mwaka wanakadiriwa kuwa na ugonjwa huo ambapo 2016 watu 65,908 waligundulika na kuwekwa kwenye matibabu.
"Wakati huohuo, takwimu hizi zinaonyesha kuwa wagonjwa wapatao 94,000 (asilimia 59) nchini hawakuweza kugundulika hivyo kukosa kupewa matibabu ya TB," alisema.
Alisema kuwa takwimu hizo zinadhihirisha kuwa ugonjwa huo bado ni janga la kitaifa hivyo serikali pamoja na wadau wengine wanatakiwa kuongeza juhudi kumfikia kila mhitaji kabla ya kuchelewa kukatiza mnyororo wa maambukizi.
Alitaja mkoa ambao umeonekana kuwa kinara wa wagonjwa wa kifua kikuu ni Dar es salaam, ukiwa na asilimia 20 ukifuatiwa na Mwanza wenye asilimia sita, Mbeya, Arusha, Dodoma na Moogoro zenye asilimia tano na Geita, Tanga, Manyara na Kilimanjaro zote zenye asilimia nne.
Alisema sababu kubwa ya mikoa inayoongoza ni kutokana na msongamano wa watu.
Alisema katika kuhakikisha kuwa ugonjwa wa kifua kikuu unakomeshwa serikali imeweka mikakati yake kabambe ambayo itasaidia kudhibiti maambukizi ya TB katika maeneo mbalimbali.
Mwalimu alisema moja ya mikakati hiyo ni matumizi ya mashine za kupima sampuri ya makohozi ya mgonjwa wa kifua kikuu yenye uwezo mkubwa tofauti na ile iliyokuwa inatumika zamani.
Chanzo: Nipashe