Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,809
- 34,193
Leo tuangalie tatizo la upungufu wa damu mwilini. Anaemia ni jina la jumla linalotumiwa kubainisha aina mbalimbali za upungufu wa damu mwilini.
Kiwango cha kawaida cha chembe nyekundu za damu (Haemoglobin-Hb) katika mwili wa binadamu ni kati ya gramu 12 mpaka 14 kwa kila mililita ya damu na zikiwa pungufu ya hapo mtu huyo anakuwa na tatizo la upungufu wa damu.
Upungufu wa damu mwilini hutokea iwapo mkusanyiko wa pamoja wa chembe nyekundu za damu zinapopungua kupita kiwango cha kawaida kinachotakiwa kwenye mwili wa binadamu.
Tatizo hili linaweza kumpata mtu yeyote ingawa visababishi vinaweza kutofautiana.
Licha ya utofauti huo mara nyingi tatizo hili husababishwa na mambo makuu matatu ambayo ni kupoteza damu mfano wakati wa hedhi kwa wanawake hasa wanaotokwa na damu nyingi au kuvuja damu kunakosababishwa na vidonda vya tumbo.
Sababu nyingine ni uzalishwaji duni wa chembe nyekundu za damu unaosababishwa na upungufu wa vitamini au lishe duni pamoja na magonjwa sugu. Pia magonjwa ya kurithi.
Iwapo mtu atapungukiwa kiasi cha madini, ulaji wa madini ya chuma katika mlo wa kawaida wa mtu hauwezi kufidia kiwango cha madini kilichopotea na kiasi hicho kinachokuwa kimebaki hutumika mara moja.
Aina za upungufu wa damu mwilini
Zipo aina mbalimbali za upungufu wa damu ikiwemo Haemolytic Anaemia. Hali hii ya upungufu wa damu, chembe nyekundu za damu huharibiwa haraka kuliko mwili unavyoweza kuzalisha chembe nyingine.
Upungufu huu husababishwa na mambo mengi ikiwemo kansa aina ya Lymphoma au utumiaji wa baadhi ya dawa ambazo huweza kuangamiza chembe nyekundu za damu kwa mfano dawa aina ya Methylodopa inayotibu matatizo ya presha ya kupanda.
Mtu mwenye aina hii ya upungufu wa damu anaweza kupatwa na homa, kutetemeka kwa mwili, maumivu ya tumbo na mgongo na mapigo ya moyo kushuka ghafla.
Pernicious Anaemia. Huu ni upungufu wa damu unaotokana na ukosefu wa kutosha wa asidi aina ya Folic (Folate) katika chakula.
Asidi aina ya Folate hupatikana katika mbogamboga za rangi ya kijani, matunda na nyama.Aplastica Anaemia. Huu ni upungufu wa damu unaotokea wakati chembe nyekundu za damu zinaposhindwa kuzalishwa ipasavyo.
Sickle cell Anaemia. Ni aina nyingine ya upungufu wa damu ambao chembe nyekundu za damu huwa na muundo usio wa kawaida unaozuia na kuathiri mishipa midogo ya damu na hivyo kusababisha kuziba kwa mishipa hiyo ya damu.
Dalili za upungufu wa damu mwilini (anaemia)
Mtu mwenye tatizo la upungufu wa damu mara nyingi huwa amepauka mwili na hujisikia kuchoka, udhaifu na huwa na mwendo kasi wa damu (yaani high pulse rate). Mgonjwa kuhisi kiu, kizunguzungu wakati akisimama, moyo kwenda kasi wakati akitumia nguvu kufanya jambo lolote, kuhema mfululizo na kupumua haraka haraka.
Dalili nyingine ni mapigo ya moyo kwenda kwa kasi, kuhisi uchovu sana au hata kuishiwa kabisa na nguvu. Wakati mwingine mgonjwa anaweza kuhisi maumivu ya kifua pamoja na kuchanganyikiwa anaposhughulikia jambo fulani.
Kuvimba kwa tumbo au sehemu za chini yake, kupoteza nguvu na macho kukosa nuru ya kuona vizuri ni dalili nyingine za mtu mwenye tatizo hili.
Matibabu yake
Matibabu ya upungufu wa damu aina yoyote yanategemea aina ya upungufu wa damu inayomkabili mgonjwa.
Upungufu wa damu hutibiwa mapema kwa kubadili lishe pamoja na kuongeza lishe yenye vitamini C na B12 pamoja na madini ya chuma kutokana na visababishi vya tatizo.
Matibabu ya lishe yanaweza kutumika kwa ushauri wa daktari ingawa yanaweza yasitoshe hadi pale mgonjwa atakapoongezewa damu.
Mara nyingine vidonge na sindano zenye lishe hizo huweza kutumiwa na madaktari hospitalini sambamba na matibabu ya tatizo linalosababisha na iwapo mgonjwa yuko mahututi huweza kuongezewa damu. Ushauri, ukiona dalili hizo, muone daktari haraka.chanzo.GBP