barafu
JF-Expert Member
- Apr 28, 2013
- 6,739
- 32,866
Anaandika Ezekiel Kamwaga.
Wazungu 'wametuharibu' waandishi !
Rais John Magufuli alitembelea Rwanda kwenye ziara yake ya kwanza ya kigeni. Kulikuwa na mambo matatu makubwa yaliyoelezwa na vyombo vya habari kuhusu ziara ile; kwamba ni ya kwanza kwa JPM, alizindua daraja pale Rusumo na kuhudhuria maadhimisho ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Zote hizo ni habari nzuri.
Tatizo ni kwamba tukaacha, sote, kuandika kuhusu tukio moja muhimu; la Rais Magufuli kupewa zawadi ya ng'ombe watano na Rais Paul Kagame.
Tulitumia ile picha na kuweka 'caption' lakini hatukufanya uchambuzi wa nini maana ya tukio lile. Hapa ndipo tulipopotea, maana sisi ndiyo tunakaa Afrika na tungeweza kueleza hili vizuri.
Kwamba kwanza JPM na Kagame wanatoka katika makabila ambayo yanaheshimu ufugaji na mifugo. Kwamba Kagame, ingawa ana ng'ombe wa aina nyingi; alimpa Magufuli ng'ombe wa asili kabisa wanaoitwa Inyambo (samahani kwa watani zangu Wanyambo). Hawa ni ng'ombe maarufu, wa aina yake na maziwa yao yanadaiwa kutokuwa na chembe ya cholestrol.
Kwamba zawadi ya ng'ombe ni ishara ya kujenga uhusiano wa kudumu. Kwenye makabila mengi, mahari kwa anayetaka kuoa ilikuwa inahesabiwa kwa idadi ya ng'ombe. Kama kulikuwa na matatizo yoyote huko nyuma, zawadi ile ya ng'ombe imeyafuta (sote tunajua kwamba uhusiano wetu na Rwanda ulikuwa umevurugika katika kipindi cha miaka mitano iliyopita).
Na zawadi ile ilitoka nyumbani kwa Kagame ambako ni wazi marais hawa wawili walikuwa na muda mzuri wa kuzungumza mambo na ndoto zao kwa wananchi wao katika namna ya uwazi na ukweli.
Kwanini hatuandiki vitu kama hivi ? Ni kwa sababu mafunzo ya darasani kwenye vyuo vyetu yanatokana na vitabu vilivyoandikwa na watu wa Magharibi. Uandishi wetu sasa unakwenda na vigezo vya Magharibi.
Tunaangalia vile ambavyo Wamarekani au Waingereza wangeandika.
Hatuandiki kuhusu unyonyaji bali tunaandika kuhusu ufisadi kwa sababu ndiyo ajenda ya Magharibi hivi sasa. Ingawa tunajua tatizo kubwa la nchi zetu hizi ni unyonyaji na si ufisadi.
Unyonyaji wa kulipa watu mishahara midogo, unyonyaji wa kuwakopa wakulima, unyonyaji wa makampuni makubwa kukwepa KISHERIA kulipa kodi, unyonyaji wa kutangaza hasara wakati wamepata faida, unyonyaji wa kutaka kununua bidhaa ghafi kutoka kwetu kwa bei nafuu na kuja kutuuzia bidhaa iliyokamilika ya malighafi hiyohiyo kwa gharama ya juu na kadhalika.
Hivi ndivyo namna wenzetu walivyotuharibu.
Hata kwenye michezo uandishi unabadilika. Tunahesabu 'assists' na kilomita alizokimbia mchezaji uwanjani. Tunashawishi timu kuwa na academies wakati tunajua hatuna uwezo huo kwa sasa.
Wakati tukiwa na timu bora viwanjani, wachezaji walikuwa wakipatikana kwenye shule na timu za mitaani. Mpira hauchezwi tena mitaani na shuleni michezo inakufa.
Wakati hali halisi ikiwa hivyo, miezi michache iliyopita, Arsene Wenger amekiri kwamba siku hizi washambuliaji hakuna. Kama unataka mshambuliaji mzuri inabidi uende Amerika Kusini kwa sababu kule soka liko mtaani.
Mtoto anacheza kwenye viwanja vibovu na watu waliomzidi umri. Anapigwa ngwara, vipepsi, vichwa, ngumi na vibao tangu akiwa na miaka 12. Na ili acheze, anatakiwa kuvumilia yote hayo.
Akiwa mkubwa, ndiyo anakuwa Luis Suarez (akizidiwa anang'ata), Alexis Sanchez (hata akiumia analazimisha acheze), Carlos Bacca (akipigwa kiatu ananyanyuka fasta na kuendelea halafu baadaye atalipiza, Diego Simeone (mwone anavyohaha wakati timu yake ikicheza). Hawa hapatikani kwenye 'academies'.
Na tazama kwenye lakabu (nick names)... Siku hizi kuna Vidic, Cannavaro, Benteke, Messi, Diego etc. Zamani dunia ilikuwa na masuspataa pia. Walikuwepo akina Pele, Beckenbauer, Platini, Scirea, Baresi etc.
Lakini huku waandishi walitengeneza lakabu za kuvutia kwa wachezaji; Malota Soma 'Ball Juggler', Hamis Gaga (Gagarino), David Mjanja 'Kazi Bure', Mwinda Ramadhani 'Maajabu', Abdallah Kibadeni 'King Mputa', Chogo Chemba, Master, etc.
Nakumbuka kuna siku Abubakar Liongo alikuwa anatangaza mojawapo ya mechi za Coastal Union na akamtaja Mohamed Mwameja kama kijana wa aliyekulia eneo la Mwakidila. Nakumbuka mpaka leo hilo neno.
Now, we are talking formations...Distance covered, that La Masia is the example for our clubs etc.. In Tanzania !
Our Western folks are taking us all to the cleaners !