Esther Malleko: Uchafuzi wa Mazingira ni Changamoto kwa Taifa

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,897
941
MHE. ESTHER MALLEKO - UCHAFUZI WA MAZINGIRA NI CHANGAMOTO KWA TAIFA​

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Esther Edward Malleko leo tarehe 24 Aprili 2023 amechangia hotuba ya Bajeti Wizara ya Mazingira na Muungano ambayo ipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 bajeti yake ni Shilingi Bilioni 54.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mazingira na Muungano Mhe. Malleko amempongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya katika juhudi za Utunzaji wa Mazingira nchi nzima

Mhe. Malleko amesema Wizara ya Mazingira na Muungano ina bajeti finyu sana katika Wizara, huku akiiomba Serikali kuiangalia bajeti ya Wizara ya Mazingira na Muungano na kuiongeza ili kuongeza ufanisi katika utendaji kwani imebeba Wizara zingine katika Utunzaji wa Mazingira

Mhe. Malleko amesema moto unaotokea katika Mlima Kilimanjaro unasababisha uharibifu wa Mazingira, Serikali kutumia fedha nyingi kuuzima moto, husababisha vifo kwa watu wanapoenda kuuzima moto na kiwango cha barafu kinazidi kupungua.

Mhe. Malleko amesema Serikali ione umuhimu wa kutoa elimu kwa Wananchi wa chini katika kutunza mazingira pia wajue namna ya kufaidika kuuza hewa ukaa

"Wilaya ya Tanganyika kuna Vijiji 8 vimepata takribani Milioni 380 kwa uuzaji wa hewa ya Kaboni, Serikali ione umuhimu kutoa elimu kwa wananchi hao hasa katika upandaji wa miti ili kuzidi kuvuna kwa wingi hewa ukaa" - Mhe. Malleko

"Tanzania kwa mwaka mmoja inazalisha taka takribani tani Milioni saba (7), kiasi kinachoweza kukusanywa/kuzolewa ni asilimia 35 tu katika miji, majiji na Halmashauri."

"Asilimia 30.7 ya utupaji taka nchini ni holela, watu wanatupa taka katika maeneo ambayo hayajatengwa katika mifereji na mito na mvua zinaponyesha takataka zinaziba mifereji ya maji ambapo hupelekea mafuriko na kipindupindu"

"Asilimia 38.4 ya maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kutupa taka miundombinu yake haikidhi utupaji taka. Asilimia 27.8 ni maeneo yametengwa kwa utupaji taka lakini hayahudumiwi kwa sababu ya ufinyu wa bajeti"

"Asilimia 5.3 ya utupaji taka nchini ndiyo inahusisha utupaji taka sahihi na salama, Asilimia 90 ya utupaji taka nchini sio salama"

Mhe. Malleko amesema kwa Mkoa wa Dodoma wananchi wanaweza kukaa na takataka ndani ya nyumba zaidi ya wiki mbili, zikija kuzolewa taka gari linalozoa taka na lenyewe ni takataka, wanaozoa zile taka hawana vifaa vya kuwakinga

Mwisho, Mhe. Malleko ameiomba Serikali kuiongezea bajeti Wizara ya Mazingira na Muungano ili iweze kufanya kazi zake kwa unafuu zaidi huku akiunga mkono hoja ya Bajeti ya Wizara ya Mazingira na Muungano

WhatsApp Image 2023-04-24 at 17.30.04.jpeg
 
Back
Top Bottom