Nyota 14 wa Eritrea watowekea Kenya
na Mwandishi Wetu
WACHEZAJI 14 wa timu ya taifa ya Elitrea, wametoroka katika hoteli waliyokuwa wamefikia mjini Nairobi kwa ajili ya michuano ya Kombe la Chalenji iliyofikia tamati juzi.
Kwa mujibu wa Katibu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicolas Musonye, wachezaji hao wametoweka huku wenzao wanane wakirejea kwao Eritrea.
Musonye alisema wao Cecafa tayari wamearifiwa kuhusu tukio hilo na watashirikiana na vyombo vinavyohusika kuhakikisha wachezaji hao wanakamatwa.
Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jana jioni, Musonye alisema hiyo si mara ya kwanza kwa wachezaji wa timu hiyo kuingia mitini baada ya mashindano.
Wachezaji wa Eritrea wamekuwa na tatizo hili, wamewahi kufanya hivyo nchini Tanzania na Uganda, siwezi kujua kuna tatizo gani nchini kwao, alisema Musonye.
Musonye alisema watafanya kila wawezalo kuhakikisha nyota wote 14 wanakamatwa na kurejeshwa kwao kwani wana uhakika hadi kufikia jana jioni, walikuwa bado wako nchini humo.
Katika michuano ya safari hii, Eritrea ilifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali, lakini ikangolewa na Kilimanjaro Stars kwa kufungwa mabao 4-0.