Enzi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Enzi

Discussion in 'Jukwaa la Lugha' started by X-PASTER, Apr 3, 2009.

 1. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #1
  Apr 3, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Bure mnazuzuka, enzi ni kama maua,
  Hayakawi kunyauka, hili ninachanganua,
  Chini yakapukutika, mwisho wake hivyo hua,
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.

  Maua hunawirika, vizuri yakachanua,
  Lakini kubadilika, kupo likawaka jua,
  Mwisho yakaja toweka, kana kwamba hayakua,
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.

  Msije kughafirika, kudhani zake hatua,
  Ni za kudumu miaka, sivyo hivyo nachambua,
  Mara hali hugeuka, yakesha nafafanua,
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.

  Ole kwenye mamlaka, msije kujifutua,
  Enzi mliyoishika, yaweza kujifungua,
  Juu mkaporomoka, hadi chini mkatua,
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.

  Kijiweni hekaheka, mambo mmeyatibua,
  Watu mlivyowafyeka, utadhania mabua,
  Bado Udi mwamsaka, ni mambo ya kushtua!
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.

  Itakuja kufutika, enzi mliyochukua,
  Nyinyi zidini mahoka, tutakuja washushua,
  Mtu cho huanguka, kufumba na kufumbua,
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.

  Mpanda ngazi hushuka, usemi huu murua,
  Kiingiacho hutoka, mzima huja ugua,
  Enzi huja huondoka, jueni msiojua,
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.


  From: Udii (Mnyongee).
   
 2. M

  Maamuma JF-Expert Member

  #2
  Apr 8, 2009
  Joined: Dec 22, 2008
  Messages: 856
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 35
  Bure mnazuzuka, enzi ni kama maua,
  Hayakawi kunyauka, hili ninachanganua,
  Chini yakapukutika, mwisho wake hivyo hua,
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.


  Ni lazima tuzuzuke, mana twajua yapita,
  Aheri turukeruke, kabla hatujajuta,
  Mwisho wetu tuufike, raha tumeshazipata,
  Wakati wako ni huu, ponda raha kufa kwaja.


  Maua hunawirika, vizuri yakachanua,
  Lakini kubadilika, kupo likawaka jua,
  Mwisho yakaja toweka, kana kwamba hayakua,
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.


  Mtu unaponawiri, hapohapo shikamana,
  Ujana ukisafiri, tubaki kutazamana,
  Mana mwisho umejiri, kikiri zote hakuna,
  Wakati wako ni huu, ponda raha kufa kwaja.


  Msije kughafirika, kudhani zake hatua,
  Ni za kudumu miaka, sivyo hivyo nachambua,
  Mara hali hugeuka, yakesha nafafanua,
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.


  Tunajua yana mwisho, ndo mana twakimbizana,
  Tunafanya maonesho, badae hutoyaona,
  Tutakuwa wa michosho, na wala hamu hatuna,
  Wakati wako ni huu, ponda raha kufa kwaja.


  Ole kwenye mamlaka, msije kujifutua,
  Enzi mliyoishika, yaweza kujifungua,
  Juu mkaporomoka, hadi chini mkatua,
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka


  Hayo yote twayajua, tumeshaimbiwa sana,
  Mashehe wanaugua, eti tunapotezana,
  Wachungaji watujua, walia wakituona,
  Wakati wako ni huu, ponda raha kufa kwaja.


  Kijiweni hekaheka, mambo mmeyatibua,
  Watu mlivyowafyeka, utadhania mabua,
  Bado Udi mwamsaka, ni mambo ya kushtua!
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka


  Tumefyeka wengi sana, na wengine twawasaka,
  Mradi vyetu vyafana, utu kwetu umetoka,
  Pesa twahesabiana, twavuna kama ukoka,
  Wakati wako ni huu, ponda raha kufa kwaja.


  Itakuja kufutika, enzi mliyochukua,
  Nyinyi zidini mahoka, tutakuja washushua,
  Mtu cho huanguka, kufumba na kufumbua,
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.


  Enzi itapofutika, ‘tajua mbele kwa mbele,
  Gereza likinifika, ntaenda kwa upole,
  Raha nilishazikoka, sasa zamu ya upele,
  Wakati wako ni huu, ponda raha kufa kwaja.


  Mpanda ngazi hushuka, usemi huu murua,
  Kiingiacho hutoka, mzima huja ugua,
  Enzi huja huondoka, jueni msiojua,
  Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka


  Usemi nautambua, wauma kama surua,
  Raha nilizotumbua, ziko tu kwenye barua,
  Enzi imeniumbua, shetani kaniparua
  Majuto ni mjukuu, mwishowe huja kinyume.


  Eh mafisadi wenzangu, ujumbe mnasikia?
  Na tumrudie Mungu, muda hautobakia,
  Tujiswafi ndugu zangu, safari imewadia,
  Majuto ni mjukuu, mwishowe huja kinyume.


  Tulisema ponda mali, eti kufa kunakuja,
  Hatukupima akili, kufanya yalo na tija,
  Tutabaki na maswali, majibu hayatokuja,
  Majuto ni mjukuu, mwishowe huja kinyume.
   
Loading...