Enyi waume wapendeni wake zenu

Ushuhuda wa Injili

JF-Expert Member
Nov 12, 2012
427
160
Amani iwe nawe mwana wa Mungu. Nichukue nafasi hii kukushukuru wewe ambaye umefanyika kuwa baraka kwetu katika kuineza injili pamoja nasi.

Mungu aliye hai awabariki nyote ambao mnajitoa kwa ajili yetu kutufanya kuwa hewani. Mbarikiwe nyote mnaotuombea, mnaotutakia mema na mnaotubariki kwa namna iwayo yote. Mbarikiwe sana.

Mbarikiwe nyote mnaotubariki kwa baraka za mwilini. Kama ambavyo tumekuwa tukiwabariki kwa baraka za rohoni nanyi mwatubariki kwa baraka za mwilini, hatuna cha kuwalipa ila tunashukuru sana. Mungu mwaminifu yeye mwenyewe audhihirishe uaminifu wake kwenu.

Aziponye familia zenu, ndoa zenu, kazi zenu, utafutaji wenu, masomo yenu, watoto wenu, wazazi wenu, n.k. Tunaomba sana kwa ajili yenu nyote mnaotufuatilia kwenye social networks zetu zote tunazozitumia. Mungu ametupa neema ya kutumika, nasi tunaomba hekima, nguvu, busara na maarifa toka kwake kila siku.

Nirudi kwenye somo la leo.

Nilipokuwa nikianza maisha ya ndoa Mungu alianza kunifundisha namna ya kuishi na mke ili kutokuingia katika migongano isiyokuwa ya maana. Mambo mawili ya msingi Mungu alinifundisha; kwanza ni kujifunza kuwa kimya mbele za mke wangu tunapokuwa tumetofautiana. Lakini pili alinifundisha kumpenda mke wangu katika utofauti huo huo tunaokuwa naye. Nikawa najiuliza kumpendaje? Kwani simpendi?

Mnapotofautiana katika mapenzi kila mtu huwa anajiona yu na haki kuliko mwenziwe. Mwanamke anajiona ana haki vile vile mwanaume anajiona ana haki. Huwa iko hivyo maana tumerithi jambo hili toka kwa mababu zetu Adamu na Eva.

Adamu alivyoulizwa na Mungu kwanini umekula matunda ya mti niliokukataza alimsukumizia Eva kosa hilo. Akasema yule mwanamke uliyenipa!. Mwanamke alivyoulizwa naye akasema sio mimi ni nyoka ndiye aliyenidanganya!. Hakuwepo aliyekuwa tayari kuchukua jukumu la anguko lile.

Mungu alinifundisha nimpende mke wangu. Kuanzia hapo nikaanza kujifunza kumpenda mke wangu. Nikajifunza mambo mengi katika hili. Kwanza nikajifunza kwamba mwanamke ni ‘kiumbe kisicho na nguvu' ambaye maandiko yanasema ‘KADHALIKA NINYI WAUME, KAENI NA WAKE ZENU KWA AKILI; NA KUMPA MKE HESHIMA, KAMA CHOMBO KISICHO NA NGUVU; NA KAMA WARITHI PAMOJA WA NEEMA YA UZIMA, KUSUDI KUOMBA KWENU KUSIZUILIWE' #1Petro 3:7

Roho mtakatifu alinishangaza sana kwa neno hili. Ni neno ambalo nilizoea kulisoma lakini siku hiyo likaja na msukumo wa aina yake. Ukweli ni kwamba wanawake ni dhaifu. Kuna mazingira mengi yanayowafanya waingie katika udhaifu huo. Ukiacha maumbile yao yalivyo, kuzaa, kunyonyesha n.k yanawafanya wawe dhaifu. Wanazingirwa na mambo mengi.

Moja ya jambo linalozuia maombi yetu ni dhambi. Na kama tukiruhusu hasira kutawala katika mahusiano ya ndoa twatenda dhambi na hii lazima izuie maombi yetu wanaume. Mpendwa wangu, wanaume tunachangia kwa asilimia kubwa amani ya familia.

Tunachangia kwa asilimia kubwa amani ya ndoa zetu. Kama hatutaweza kukaa kwa akili na wake zetu, ndoa zetu lazima zitaingia katika matatizo. Ni lazima tujifunze kuwa na akili na maarifa namna ya kuwatunza wake zetu tusiingie katika kuvurugana ndani ya ndoa. Amani ya ndoa iko mikononi mwa wanaume.

Ikiwa mwanamke hapendi utokapo kazini ukifika nyumba unakuwa busy na laptop ukifanya kazi za ofisini, basi ni bora ubaki ofisini uhakikishe umemaliza kazi zako ili ukifika nyumbani uwe na muda mzuri naye.

Ikiwa mwanamke hapendi urudi nyumbani ukiwa umelewa, ni vema ukafanya hivyo kwani walevi kwanza hawana fungu katika ufalme wa mbinguni sasa kwann wewe ung'ang'anie ulevi wakati mke na hata Mungu wako hapendi.

Ikiwa mke wako hapendi siku za weekend unamuacha peke yake nawe unakuwa busy na marafiki zako basi ni vema ukawa na muda naye kwani ni siku za mapumziko hivyo anastahili kupata nafasi hyo.

Nilikuwa nikiwashauri watu fulani kwa ajili ya ndoa yao ambayo ilikuwa imeingiliwa na ‘mdudu'. Mwanamke anataka kuondoka akaanzishe familia yake. Analalamika mumewe ni mlevi sana. Na akilewa ni tatizo kwenye mabaa. Wahudumu wa kike wa baa wote ni halali yake!! Nikamwambia mwanaume kwamba amani ya familia iko mikononi mwake.

Pamoja na kwamba maandiko yanasema ‘mke mpumbavu huiharibu nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe nami nakuambia mwanaume mwenye busara huijenga ndoa yake kwa mikono yake mwenyewe. Nikamwambia msikilize mke wako anasema nini? Kama umedhamiria kuivunja ndoa basi, lakini kama unataka kuleta amani msikilize mke wako. Acha ulevi, acha uzinzi rudi utulie na mkeo mjenge familia na future ya mtoto wenu.

Imeandikwa ‘Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.

Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake.

Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa. Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe' #Efeso 5:25-33

Ndugu yangu kama unataka kuleta amani katika ndoa yako hebu kwanza mpe heshima yake mkeo anayostahili. Kuna watu hawawapi wake zao heshima. Hata kama ni wakristo lakini hawawapi wake zao heshima. Kila mara yeye ni kugombana na mkewe tu. Tena wakati mwingine mbele hata za majirani.

Wanawadharau wake zao hata wakiwapo nyumbani mbele za watoto!! Au mbele za ndugu na jamaa na marafiki! Wako tayari kumtakia lunch njema mwanamke mwingine rafiki yake kuliko mkewe. Wako tayari kuwaletea zawadi marafiki zao wa kike kuliko wake zao. Wako tayari kujishughulisha na mambo ya marafiki zao wa kike kuliko wake zao. Hawana hata muda wa kuwaombea wake zao katika shida zao. Heshima ya mke iko wapi hapo?

Lakini jambo lingine ni habari ya kumpenda mke wako kuliko mtu mwingine yeyote. Ndugu yangu unapoingia kwenye ndoa wewe umekuwa mtumwa wa mkeo. Ninyi meshaunganishwa na kuwa mwili mmoja. Unamtumikia mkeo maisha yako yote mpaka Bwana atakapowatenganisha.

Hivyo uwe tayari kumtumikia kwa kila kitu na kumpendeza mkeo kwa kila jambo. Imeandikwa ‘yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe' #1Kor 7:33.

Jifunze kumpendeza mkeo kila siku. Haya si mambo ya kujifunza siku moja kwani wewe na mkeo ni watu mliokulia katika tamaduni mbili tofauti. Ni lazima kujipa muda wa kusomana na kufundishana.

Yote tisa, kumi fanya jambo hili katika ndoa yako. Kwanza ewe mwanaume uwe na muda binafsi wa kuomba kwa ajili ya mke wako na familia yako. Wewe ndiwe kichwa cha familia. Una wajibika kwa ajili ya kila mtu na kila kitu katika familia. Wewe ndiwe kichwa cha familia.

Kichwa ni kiongozi wa mwili. Ni kichwa ndicho kinachopangilia mambo na kuuongoza mwili ufanye. Kila unachokifanya kichwa ndicho kinachoplan.

Sasa kama kichwa hakina mawasiliano na mwili basi hapo ni matatizo. Kama Kristo alivyo kichwa cha Kanisa ndivyo mwanaume ni kichwa cha mkeo na familia nzima. Kama Kristo hawezi kujishughulisha kwa ajili ya kanisa hafai kuwa Bwana na Mwokozi wetu.

Pata muda wako binafsi kumuombea mkeo. Mkeo ana mahitaji mengi. Ukiacha kukua na kumjua Mungu, ana mahitaji mbali mbali ya kimwili na ya kiroho.

Yamkini anahitaji kupata kitega uchumi kwa ajili ya kukupunguzia wewe mwanaume makali ya maisha. Yamkini ana mahitaji fulani fulani ambayo amekuwa akikushirikisha. Hebu chukua muda wako binafsi kumuombea.

Na pia upate muda wa kuomba pamoja naye mkiwa na familia nzima. Maombi ya familia ukiwa na mkeo huponya mianya mingi ambayo adui anaipenyeza. Mtapata muda wa kujifunza neno la Mungu pamoja na kusikia nini Roho Mtakatifu anasema nanyi kuhusu maisha yenu. Mpendwa wangu ndoa ni taasisi ya kwanza kuasisiwa hapa duniani.

Ni taasisi ambayo shetani anaipiga vita kwa nguvu zake zote isiwe na amani maana anajua ndoa ikiwa na amani watoto watakaoibuka hapo watakua na nguvu za rohoni hivyo watamshughulikia ipasavyo. Paulo anasema ‘Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao'!!

Nawe mwanamke imeandikwa "Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana"
Neema ya Bwana wangu Yesu Kristo iwe pamoja nawe. Ungana nami kuieneza Injili kwa kushare ujumbe huu na Mungu atakubariki kwa tendo lako hilo jema.

Kwa ajili ya maombi wasiliana nasi kwenye whatsapp tu kwa namba hii 0758 443 873. Ikiwa unataka kunipigia au kunitumia sms ya kawaida basi tumia namba 0712 204 937. Au wasiliana nasi kupitia :
info@nenolauzima.org
www.facebook.com/UshuhudawaInjili
 
Haya ni maneno tuombe Mungu atupe roho wake maana kimsingi huwa tuanelezwa na kufikiri tumeelewa lakini tatizo linapokuja sasa inakuwa kama ukipenda unaonewa na ukitii sana inakuwa kama unaonewa vile. Peke yetu hatuwezi ila katika yeye atutiaye nguvu.
 
Back
Top Bottom