SoC03 Elimu ya uraia ikuzwe kuchochea utawala bora na uwajibikaji nchini

Stories of Change - 2023 Competition

Nyakijooga

Senior Member
Dec 9, 2018
123
202
Umewai kujiuliza umuhimu wa elimu ya Uraia kwa umma?

Kwanza kwa tafsiri isiyo rasmi ' ELIMU YA URAIA ' ni aina ya elimu ambayo ulenga kukuza mahusiano ya kijamii kwa lengo la kuimarisha nafasi za kuishi pamoja kijamii.

Elimu ya Uraia uwezesha raia kutambua wajibu wake katika jamii au nafasi aliyonayo kwenye jamii inayomzunguka, elimu hiyo pia umuwezesha raia kutambua haki zake na za wengine...

Licha ya baadhi ya wananchi kuwa na elimu ya uraia ambayo upatikana katika mazingira mbalimbali ambayo hasa hasa sio rasmi, lakini bado elimu hii ni kikwazo kwa wengi licha ya kuwa na umuhimu mkubwa.

NATAKA KUELEZA NINI?

Raia wengi siku hizi wamekuwa wakilalamikia zaidi makosa au changamoto zinazowapata ambazo ni matokeo hasi ya uwajibikaji wa viongozi waliopewa dhamana kwenye nyadhifa mbalimbali, malalamiko hayakomi kila kukicha.

Lakini ikifanyika tathimini inaonesha moja kwa moja kuwa kuwa chanzo kikubwa cha raia kuendelea kuumia na kulalamika ni kutokuwa na elimu ya uraia ya kutosha ambayo inaweza kuwapa mwanga wenye suluhisho.

Tukumbuke elimu ya uraia inatupa fursa ya kushiriki kwa usahihi zoezi zima la uchaguzi, kuanzia kwenye kujitokeza kuwania nafasi, kampeni, kusikiliza sera, kuhoji na kuwauliza maswali wagombea, kushiriki zoezi la kupiga kura, kuchagua au kuchaguliwa.

Kuna raia ambao wanaishia kulalamika juu ya changamoto zinazotokana na changamoto za utawala bora na uwajibikaji lakini kutokana na kukosa elimu ya uraia uenda watu hao wangepata fursa ya kupewa nafasi hizo wangeleta ufumbuzi wa changamoto hizo, wanakosa tu Mtu wa kuwatoa usingizini.


UFINYU WA ELIMU YA URAIA UNAWEZA KUZAA NINI?

Mfano, yamekuwa yakifanyika makosa mengi ya kuchagua viongozi ambao sio wawajibikaji wala hawazingatiii misingi ya utawala bora lakini kiini kikubwa ni kukosekana kwa elimu ya uraia ya kutosha ambayo inatoa fursa kwa raia kung'amua nani anafaa kuwa kiongozi au nani hafai?.

Lakini leo hii jamii zinakumbatia viongozi wanaotoa Rushwa. Hili linatokana na Raia wengi ambao ndio wapiga kura kukosa elimu ya uraia badala yake wanadhani uwezo wa kutoa rushwa sifa ya kiongozi ambaye anaweza kuivusha jamii!, Jamii yenye uelewa wa kutosha kuhusu elimu ya uraia usimama kidete kukemea vitendo hivyo sio mtu anapewa kanga au kijora ili amchague kiongozi, kwa namna hiyo tutanapataje viongozi wawajibikaji na wanazingatia misingi bora ya uwajibikaji?

Ufinyu wa elimu ya uraia kwa raia wengi inapelekea baadhi viongozi washindwe kuwajibika kwa kuwa wanafahamu udhaifu wa wananchi wanaowaongoza, kuna wakati utokea matukio yanye viashiria vya ukiukwaji wa utawala bora, lakini licha ya uwepo wa sheria zinazotoa fursa ya kuwachukulia hatua lakini jamii uishia kwenye minongono. Niseme tu, jamii kukosa elimu ya uraia ni kubariki matukio ya aina hiyo kuendelea.

Matokeo mengine ya kukosekana kwa elimu ya uraia ni wananchi kushindwa kuipa nguvu mijadala inayogusa mstakabali wao na Taifa lao.

Leo hii kwenye Dunia ya utandawazi kupitia mitandao ya kijamii ukifatilia mijadala muhimu inayogusa wananchi inahusisha watu wachache ikilinganishwa na matukio yasiyokuwa na tija ya moja kwa moja kwao na Taifa kwa ujumla. Kwa kuzingatia muktadha huo inaweza huo unaweza kuwa mlango wa viongozi na baadhi ya watu kupitisha mambo ambayo yanafifisha utawala bora pia inaweza kuwa sababu ya baadhi ya watu kwenye nafasi zao washindwe kuwajibika katika misingi inayotakiwa kutokana na namna udhaifu wa raia wao wengi.

Utawala bora na uwajibikaji wa viongozi kwenye nyadhifa mbalimbali pamoja na taasisi zetu nchini msingi wake ni wananchi kuwa na elimu ya uraia inayowawezesha kuona uovu na kuwawajibisha wanaoenda kinyume na taratibu.

Elimu ya uraia uwawezesha wananchi kutojitenga na michakato mbalimbali inayoamua hatma yao, lakini siku hizi ni rahisi kusikia kijana anasema 'sipendi kujihusisha na siasa' ukiuliza kwanini atakwambia hayo mambo yana wenyewe. Lakini inapotokea kijana huyo amekosa ajira au zimepitishwa kodi na tozo zinazombana asikue unasikia akinongona chinichini.

Watu wengi wakipata elimu ya uraia itakuwa rahisi kuondoa mifumo ambayo ni kikwazo cha utawala bora na uwajibikaji badala yake itakuwa chachu ya mageuzi ya mifumo yenye kutanguliza zaidi maslahi ya umma na Taifa kwa ujumla.

Leo hii wapo watu wengi ambao wakisikia mchakato wa mabadiliko ya Katiba wanaona kama ngonjera hii inaweza kuwa ni matokeo ya kukosa elimu ya uraia. Elimu ya uraia inapokosekana mamlaka au kundi la watu wachache kwenye jamii wanapata fursa ya kuamua mambo yaendeje sio wananchi wenyewe kuamua.

Ni mara ngapi tumeshuhudia upigaji kwenye Taasisi zetu za Serikali, ni mara ngapi tumesikia vitendo vya uvunjaji wa sheria kwa viongozi wetu na taasisi zetu, tumechukua hatua gani ? wakati mwingine hata kupaza sauti tumeshindwa. Kushindwa kuchukua ni kubariki vitendo hivyo kuendelea.

Tukiachana na hayo ni lini umeshiriki mkutano wowote kwenye Mtaa wako?, ni vijana wangapi wanajitokeza? Je, ni mara ngapi tumejitokeza kujadili au kuchangia mijadala yenye tija kwetu?.

NINI KIFANYIKE?

Inaitajika jitihada kubwa kueneza elimu ya uraia kwa umma wa watanzania, lakini uwezekano upo.

Inawezekanaje?

Serikali kwa kushirikiana na wadau ikiwemo na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO,s) ambazo ufanya majukumu kwenye maswala yanayogusa Elimu ya Uraia, mfano wadau wa uhuru wa kujieleza, uwajibikaji, Haki za Binadamu, Demokrasia na utawala bora..., watengeneze mpango mkakati wa pamoja kwa kushirikiana na Serikali vyema na TAMISEMI ili kuandaa program mbalimbali ambazo zitawezesha elimu hii kuenea mpaka kwenye ngazi za chini.

Mfano unaweza kuandaliwa mkakati ambao unawezesha wadau hao kupata fursa kwenye vyombo vya habari kutoa elimu ya uraia itasaidia kuwafikia watu wengi, kuna matukio mengi hayaripotiwi kwenye mamlaka za kisheria au yanaripotiwa lakini hayafanyiwi kazi ipasavyo kutokana na raia wengi kutokuwa na elimu ya uraia.

Elimu hiyo inaweza kutolewa kwenye ngazi tofauti, hususani kwenye Serikali za Mitaa. Shule ngazi za primary na sekondari zinaweza kuhamasishwa kuwa na 'clab' maalum zinazoeneza elimu ya uraia tena kwa lugha rafiki, makundi hayo yatachochea elimu ya uraia kuenea zaidi kwenye vichwa vya waliowengi.

NA HILI LINAWEZA KUSAIDIA

Serikali inaweza kuunda taasisi yeye jukumu la kutoa elimu ya uraia lakini baada ya kufanyika tathimini ya gharama ikaonekana kuwa kubwa majukumu hayo yanaweza kukaimishwa kwenye taasisi nyingine mfano Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Ambayo inaweza kubadilishwa kimuundo ili kutekeleza majukumu ya kutoa elimu ya uraia, ikishapewa majukumu hayo inakuwa na matawi sehemu tofauti nchini na wakawa wanaendesha mafunzo kwa wadau mbalimbali hususani watendaji ngazi za mitaa na Kata, Maafisa ustawi, Maasifa Maendeleo ili watumike kama mabalozi.

Kuwa na watu hao kwenye jamii zetu ni rasilimali ambayo inatakiwa kutumiwa vizuri zaidi kuleta tija kwa umma, wanaweza kuwa mabalozi ambao wanaifikia jamii moja kwa moja kuliko utaratibu ambao umezoeleka kipindi uchaguzi ukikaribia baadhi ya wadau kuibukia ghafla kuanza kutoa elimu kisha kupotea.

Ni muhimu sana kutambua kuwa elimu ya uraia haina ukomo na faida yake sio kwenye uchaguzi pekee!, kuishi kwa kuamini hivyo ni kujidanganya.

FAIDA ZIPI ZINAWEZA KUPATIKANA?

Zipo faida nyingi ambazo Taifa linaweza kunufaika nazo baada ya raia wake kuwa na elimu ya uraia. Tutamulika chache kulingana hasa zinazoweza kuchochea utawala bora na uwajibikaji.

Mosi, iawezesha raia wengi kuwa katika nafasi nzuri ya kutambua wajibu wao, kama nilivyogusia mwanzo wa andiko kwenye kuelezea maana ya elimu ya uraia, lilijitokeza neno ''raia kutambua wajibu wake", bila shaka hiko hivyo.

Wapo watanzania wengi ambao hawatambui umuhimu wa kulipa kodi kwa Nchi yao, lakini wengi wao hawaoni umuhimu kwa sababu hakuna ambaye amewagusa kuwafungua macho kuona umuhimu uliopo. Hivyo elimu hii inaweza kuchochea walipaji kodi kwa hiari.

Pili, kuwezesha wananchi kushiriki kuwachagua viongozi bora wanaoheshimu utawala bora na wawajibikaji, elimu ya uraia ikikolea kwenye vichwa vya wananchi itachochea mazingira ya kuwapata viongozi bora sio bora viongozi.

Inawezekanaje?, Elimu hii inaweza kusaidia wapiga kura wengi kuchagua viongozi wanaozingatia misingi ya uongozi, ambao sio watoa rushwa wala wapokea rushwa, viongozi wenye kuwajibika ipasavyo kwa manufaa ya umma.

Tatu, Elimu hii itawezesha raia kuiwajibisha Serikali na baadhi ya watu au taasisi zinapoenda kinyume, Serikali na wadau wakiwa wanatekeleza majukumu yao wakitambua presha iliyoko nyuma yao kutoka kwa wananchi itachochea uwajibikaji lakini inapotokea hakuna msukumo nyuma Serikali na baadhi ya wadau wanakuwa katika nafasi ambayo inawafanya wasiwajibike ipasavyo ikilinganishwa na presha inayokuwa nyuma yao.

Mfano, kwenye timu zetu za Simba na Yanga, nadhani kuna wakati viongozi wanaweza hata kutokulala usingizi kutokana na presha za mashabiki, lakini hilo kwenye taasisi zetu au Serikalini uenda likawa swala hadhimu kutokea!. Kuna wakati yanatokea mambo ambayo sio rafiki lakini yanaisha wahusika kuwajibika au kuwajibishwa.

Nne, Elimu ya Uraia itasaidia kukuza uhuru wa kujieleza, raia wakitambua kuwa wanayo haki ya kutoa maoni kuhusu masuala mbalimbali bila kuvunja sheria ya Nchi itakuwa hatua ambayo inachochea uwajibikaji na utawala bora, raia wataelewa kuwa umuhimu wa kutoa maoni na namna rafiki ya kutoa maoni bila hofu.

Tano, Itasaidia wananchi kuwa tayari kushiriki katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, hatua hiyo itawafanya raia kuongeza kasi ya uwajibikaji na kuwa tayari kushiriki katika michakato mbalimbali ambayo inagusa hatma ya maisha yao.

Wananchi wanaposhiriki kwenye michakato muhimu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inawezesha kupatikana kwa miongozo rafiki kwa wananchi ambayo wanashiriki katika mchakato wa kuipata, mfano wananchi wanaposhiriki katika michakato ya kupitisha sheria mpya au kufanya maboresho ya sheria inatoa fursa ya kuondoa malalamiko mengi pia inaongeza uwezekano wa wananchi kutii sheria bila shuruti hali ni nyenzo muhimu katika utawala bora na uwajibikaji.

Sanjali na faida hizo elimu ya uraia itawezesha raia kuondoa mtazamo ambao umekuwa ukijenga hofu kwa baadhi ya raia kushindwa kutoa maoni kwa baadhi ya mambo ya msingi kwa sababu ya hofu, lakini pia itasaidia kuwezesha viongozi na wadau wengine wanaopewa dhamana mbalimbali kutambua kuondoka kwenye mawazo hasi ambayo baadhi yao udhania kuwa wanaotoa maoni yanayoenda kinyume na mtazamo wao wanastaili kutendewa visivyo. ELIMU YA URAIA UPELEKEA KUWA NA JAMII ILIYOSTAHARABIKA
 
Back
Top Bottom